Hatua tatu za maisha ya kiroho
Hatua tatu za maisha ya Kiroho ni kati ya masuala makuu ya Teolojia ya Kiroho. Hatua hizo zinaitwa za wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika; au za utakaso, mwanga na muungano.
Tofauti na wanateolojia kadhaa wa karne za mwishomwisho, walimu wakuu wa maisha hayo waliamini watu wowote wanaweza kutamani na kujiombea kwa unyenyekevu neema ya kuzama katika mafumbo ya imani, ambayo yote yanadhihirisha wema wa Mungu usio na mipaka. Waliona hiyo sala ya kumiminiwa ni sharti la muungano wa dhati na Mungu ulio ukamilifu wa Kikristo. Kwa msingi huo walifafanua kila hatua ya maisha ya Kiroho.
Katika Biblia
haririKatika Injili, hasa katika Heri Nane, tunaona ukuu wa ukamilifu wa Kikristo tusioweza kuupata tusipofisha yale yote yasiyofaa ndani mwetu, tusipobeba msalaba kwa uvumilivu, tusipomuomba Baba aliyefichika moyoni mwetu, tusipomsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu kila anapotuangaza, ili kwa msaada wake wa pekee tuzame kwa upendo katika mafumbo ya wokovu na hivyo tuungane na Mungu.
Mtume Paulo aliandika: “Iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu… twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu... Mambo ambayo jicho halikuyaona, wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao… ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu” (1Kor 2:6-10). Ndiyo yanayotazamwa na waliokamilika wanaposali. “Kwa hiyo nampigia Baba magoti… awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef 3:14-19).
Katika maisha ya mitume, waliolelewa na Bwana mwenyewe, kuna hatua tatu tofauti zinazolingana na zile za maisha ya Kiroho. Hatua ya kwanza, ile ya wanaoanza, ilichukua tangu waongoke hadi Mateso ya Bwana, walipopitia dhiki kubwa hata Mtume Petro akamkana Mwalimu wake. Halafu akajuta, na ndio uongofu wake wa pili, katika ule utakaso wa Kimungu uliokuwa kama usiku wa giza na mateso. Kitu cha namna hiyo kiliwatokea mitume wengine pia walipojaliwa kughairi baada ya kukimbia. Hatua ya pili, ile ya wanaoendelea, ilichukua kuanzia Mateso hadi Pentekoste. Kipindi hicho walikuwa bado waoga, imani yao ilihitaji kuangazwa, tumaini lao lilihitaji kuimarishwa, na upendo wao haukuwa bado na ari uliyopaswa kuwa nayo. Hatua hiyo ilitimia kwa kuondolewa uwepo wa kimwili wa Bwana alipopaa mbinguni. Hapo walipaswa kuendelea kwa imani tupu, wakikabili dhuluma walizotabiriwa. Hatua ya tatu iliwaanzia Pentekoste, ambayo ikawa kwao kama uongofu wa tatu, utakaso halisi wa Kimungu na mageuzo yaliyowaingiza katika maisha makamilifu. Iliangaza akili yao na kuimarisha utashi wao ili wamhubiri popote Yesu msulubiwa. Sifa maalumu ya hatua hiyo ni kuzidi kuungana kwa ndani na Mungu, kujitoa sadaka kikamilifu hadi kufia dini. Hatua zao hizo, kila moja ilianza na uongofu au mageuzo ya roho: tukizitafakari zitaangaza kweli hatua tatu za maisha ya Kiroho.
Katika Mapokeo
haririMaelekezo ya Maandiko yamethibitishwa na Mababu wa Kanisa.
Ukristo wa Mashariki
haririTuone kwanza ushuhuda wa wale wa Ukristo wa Mashariki.
Inyasi wa Antiokia aliandika mara nyingi juu ya uwepo wa Kiroho wa Mwokozi ndani ya waamini, akawahimiza hivi, “Tufanye tendo letu lolote kwa kuzingatia kwamba Mungu anaishi ndani mwetu; hivyo tutakuwa mahekalu yake, naye atakuwa Mungu wetu mwenye kukaa ndani mwetu”. Mwenyewe alitaka kuishi kwa kuungana na Kristo zaidi na zaidi, na kufa ili kuungana naye milele. Alitamani kusagwa na meno ya simba awe unga wa ngano wa Kristo, kama vile Yesu alivyosagwa awe mkate wetu wa ekaristi. Barua zake zimejaa ujuzi wa juu wa Kristo, imani hai yenye kupenya ambayo ni sala ya kumiminiwa na ambayo inafurika katika utume wenye matunda mengi kutokana na upendo mkubwa. Ili kufikia muungano huo wa dhati ni lazima kujidharau pamoja na yale yote ambayo hayafai na yanafisha uzima wa Kimungu ndani mwetu.
Irenei alisisitiza binadamu akubali kuundwa na Mungu kama udongo mikononi mwa mfinyanzi. Badala ya kupinga au kukwepa kazi hiyo, azidi kujionyesha mtulivu kwa Roho Mtakatifu katika sala na hivyo atafikia kupima mambo yote Kiroho na kuishi kwa upendo wa Mungu tu.
Klementi wa Aleksandria alieleza roho inavyopanda juu kupitia hali zifuatazo: kwanza uchaji wa Mungu, halafu imani na tumaini, hatimaye upendo na hekima. Waliokamilika wana amani na kutawaliwa na upendo; wamejaliwa hekima ya siri ya Mungu, ujuzi wa dini ambao unatokana na mwanga wa Roho Mtakatifu kwa watu wasikivu na kugeuza maisha yao ya ndani kwa kuwafanya marafiki wa Mungu.
Sawa naye, mwanafunzi wake Origenes alisema mtu aliyekamilika anaishi hasa kwa upendo na kwa kawaida anapokea kwa Roho Mtakatifu hekima ya kumiminiwa, ujuzi wa dhati wa fumbo la Utatu Mtakatifu. Kuhusu Injili ya Yohane aliandika, “Hakuna anayeweza kuelewa maana ya Injili kama hajaegama kifuani pa Yesu wala hajapokea kutoka kwake mama Maria awe mama yake pia”. Neno ndiye anayejifunua kwa waliokamilika na kuwaunda kama alivyowaunda mitume. Mwenyewe alibainisha hatua tatu: ile ya wanaoanza, ambao ndani mwao maono yasiyofaa yanapungukiwa nguvu; ile ya wanaoendelea, ambao ndani mwao maono hayo yanaanza kuzimishwa na wingi wa neema; hatimaye ile ya waliokamilika. Alihimiza usikivu kwa Roho Mtakatifu, ambaye kwa njia yake tunaweza kumuendea Kristo na kupanda juu kwa Baba, katika sala ya kumiminiwa inayosaidiwa na upweke.
Didimo Kipofu alimualika kila Mkristo kuungana kikamilifu na Kristo, Bwana arusi wa roho iliyotakata.
Bazili Mkuu katika Kanuni zake alipanga maisha imara ya Kiroho yanayoandaa kwa sala ya kumiminiwa na muungano na Mungu. Ni sharti kutakata zaidi na zaidi: “Jicho la roho, kisha kuwa safi pasipo kivuli, linatazama mambo ya Mungu kwa mwanga ambao unatoka juu na kuijaza kwa wingi usiishibishe… Kisha kustahimili mapigano yenye tabu na kufaulu kuiokoa roho - iliyoambatana sana na mwili - katika mchanganyiko wa maono, roho inakuwa ya kufaa kwa kuongea na Mungu… Aliyefikia hali hiyo hatakiwi tena kukubali mvuke wa maono ya kidunia uchafue na kufunika kwa ushungi macho ya roho yake na hivyo kuifanya ikose sala ya kumiminiwa ya Kiroho na ya Kimungu”.
Gregori wa Nazianzo alisema Mungu ni mwanga halisi tunaoweza kuupata tu tukiwa wenyewe mwanga na tumetakata ili tupande toka uchaji wa Mungu hadi hekima. Katika waandishi hao wote tunakuta majina haya matatu: utakaso, mwanga na muungano.
Gregori wa Nisa alionyesha tunavyopaswa kujitenga na viumbe na kuishi na Kristo ili tukaribishwe kutazama umungu na kuungana nao. Ushindi huo juu ya adui unapatikana kwa njia ya msalaba tu, na kwa kutakasa zaidi na zaidi akili katika mambo yote ya hisi. Ukamilifu unaifanya roho iwe bibi arusi wa Kristo.
Efrem pia aliona kuwa sala ya kumiminiwa, tunayojaliwa kwa kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ndiyo fadhili ya maisha makamilifu. “Tutakapokuwa tumeshinda maono yetu, na kuangamiza ndani mwetu mapenzi yoyote ya kimaumbile, na kuondoa kabisa rohoni mwetu hangaiko lolote lisilosaidia wokovu, ndipo Roho Mtakatifu, kwa kuikuta roho yetu katika utulivu, na kuishirikisha akili yetu uwezo mpya, atakapotia mwanga mioyoni mwetu, kama inavyowashwa taa iliyo na utambi na mafuta tayari … Basi, kabla ya yote, tuandae roho zetu kupokea mwanga wa Kimungu, ili tustahili zawadi za Mungu”.
Kwa Denis utakaso unaandaa kumjua Mungu kwa dhati; mwanga unashirikisha ujuzi huo; hatimaye utakatifu unafanya uchanue kikamilifu. Hatua ya muungano inahusu mafumbo na ni utangulizi wa uzima wa milele.
Masimo Muungamadini alibainisha hatua tatu za sala kuhusiana na hatua tatu za upendo. “Sala ya kawaida ni kama mkate: inawatia nguvu wanaoanza; ikiongezewa neema ya kuzama kidogo katika mafumbo, inakuwa kama mafuta tunayojipaka; hatimaye, tukizama kabisa ni kama divai tamu mno inayolevya wanaoinywa hata wakajisahau… Kuzama katika sala kunatokana na mwanga wa Roho Mtakatifu… Aliyetakata anaangazwa na kustahili kuingia ndani kabisa mwa hekalu na kufurahia muungano na Neno”. Mwenyewe alionyesha majaribu makali ambayo wanasala wanapaswa kuyapitia ili kutakaswa moja kwa moja na kuthibitishwa katika upendo wa Mungu.
Hatimaye Yohane wa Damasko aliandika, “Aliyefikia kiwango cha juu kabisa cha upendo, kama kwa kutoka nje ya nafsi yake, anamvumbua Yule asiyeonekana, akiruka juu ya wingu lile la hisi linalozuia macho ya roho yasione. Akidumu katika amani, anamkazia macho Jua la Haki na kufurahia tamasha hilo asiloweza kulikinai… Kufikia kumtazama Mungu, kisha kutekeleza kwa bidii maadili, ni hazina isiyonyang’anyika kamwe”.
Basi, kadiri ya Mababu wa mashariki, kuzama katika mafumbo ya Kimungu ni kwenye njia ya utakatifu: mwanzo wake ni hatua ya wanaoendelea, halafu kunaendana kwa kawaida na upendo wa waliokamilika.
Ukristo wa Magharibi
haririMababu wa Kilatini wametuachia mafundisho hayohayo.
Augustino alitofautisha ngazi mbalimbali, akisisitiza vita dhidi ya dhambi (vilivyo kazi ngumu ya utakaso), vinavyofuatwa na mwanga kwa waliotakata, na hatimaye na muungano na Mungu. Halafu akaelekeza safari ya kupanda kwa Mungu kufuatana na vipaji vya Roho Mtakatifu: uchaji wa Mungu ndio kidato cha kwanza, na hekima ndiyo kilele. Katikati alibainisha vipindi viwili vya maandalizi yenye kutakasa. Alikiita kile cha mbali maisha ya utendaji, yaani utekelezaji wa maadili ya kiutu yanayohusiana na vipaji vya ibada, nguvu, elimu, shauri; halafu kipindi cha karibu maisha ya kumiminiwa sala, yaani utekelezaji bora wa maadili ya Kimungu na wa vipaji vya akili na hekima katika roho zilizo tulivu na sikivu kwa neema. Hapo imani ni chanzo cha kuzama katika mafumbo, na upendo motomoto unaunganisha na Mungu kwa dhati.
Yohane Kasiano alionyesha maisha ya Kiroho yanavyolenga kumtazama Mungu, ambako upendo wake unatekelezwa kikamilifu. Tunapaswa kujiandaa tufikie huko kwa kusali tusamehewe dhambi, kutekeleza maadili na kutamani upendo wa kuwaka zaidi. Hapo sala inakuwa “yote ya moto” kutokana na “kumtazama Mungu tu na kuwaka kwa upendo motomoto… Hivyo roho katika chungu cha udongo inaanza kuonja malimbuko ya utukufu inaotumainia mbinguni”.
Gregori Mkuu alikubali kugawa maisha ya Kiroho katika ngazi tatu: mapambano na dhambi, maisha ya utendaji au utekelezaji wa maadili, na maisha ya kumiminiwa sala yanayohitajiwa na wahubiri wa Neno la Mungu na wale wanaotaka kuufikia ukamilifu. Kwake matendo yote yanakosa ukamilifu mpaka roho ziwe zimeangazwa na sala ya kumiminiwa kutoka juu. Ndiyo kikomo cha juhudi, tunda la neema maalumu na utekelezaji wa kipaji cha hekima. Ni hali ya kujaliwa kuzama katika mafumbo ambayo mtu ajiandae kuipokea kwa unyenyekevu, usafi wa moyo na kukusanya mawazo karibu mfululizo. Mwenyewe alionyesha matakaso machungu ambayo “yanakausha ndani mwetu kila pendo la kihisi” na kutuandaa tuzame katika sala na kuungana na Mungu, ambapo tunakuta nguvu kubwa katika majaribu na upendo motomoto.
Hatua tatu za maisha ya kiroho na za maisha ya kimwili
haririThoma wa Akwino alifananisha hatua tatu za maisha ya Kiroho na zile za maisha ya kimwili: utoto, ujana na utu uzima. Ni mfano unaostahili tuuzingatie pamoja na kuangalia vipindi vya mpito kati ya hatua moja na nyingine.
Inakubalika kuwa sehemu ya kwanza ya utoto inakwisha akili inapochangamka kwenye umri wa miaka saba hivi, halafu inafuata sehemu ya pili inayodumu mpaka ubalehe, kwenye miaka kumi na nne hivi. Ujana unaenea kati ya miaka hiyo na ishirini. Halafu unafuata utu uzima, ambamo tunatofautisha kipindi kinachotangulia ukomavu kamili na kile kinachoufuata kwenye miaka thelatini na tano hivi, kabla ya kuanza mteremko wa uzee.
Namna ya kuwaza inabadilika pamoja na mwili. Mtoto anafuata ubunifu na hisi; hajajua kupambanua na kupanga, na hata akili inapoanza kuchangamka inaendelea kutegemea mno hisi. Mtu anapobalehe anabadilika si upande wa mwili tu, bali pia wa nafsi, akili na maadili: haridhiki tena na ubunifu, bali anaanza kutafakari maisha na haja ya kujiandaa afanye kazi fulani. Kipindi hicho cha mpito, kinachoitwa pengine umri usio na shukrani, hakikosi matatizo; ndipo tabia adili inapoundika au kuharibika; pengine mtu anabaki nyuma, bila msimamo. Mfano huo unaangaza maisha ya Kiroho ambamo aliyeanza asipokuwa kwa wakati wake mtu anayeendelea, basi ama anaelekea maovu ama anabaki nyuma na kuwa vuguvugu, aina ya mbilikimo upande wa roho. “Kutotaka kusonga mbele ni kurudi nyuma” (Bernardo), kumbe kulenga ukamilifu moja kwa moja ni kuwa nao tayari kwa namna fulani.
Ikiwa ubalehe ni kipindi kigumu, ni kigumu pia kile cha uhuru wa kwanza kinachomuingiza kijana kwenye utu uzima. Akimaliza kukomaa kimwili anapaswa kuanza kushika nafasi yake katika jamii. Sawa na mwana mpotevu, wengi wanapita vibaya kipindi hicho, wakitafsiri uhuru wanaoachiwa kuwa idhini ya kutenda lolote. Kinyume chake, anayekomaa inavyotakiwa, anajihusisha na mambo yake binafsi, ya familia na ya jamii kwa namna bora kuliko kijana, akiyazingatia kwa upana zaidi. Inatokea karibu hivyo katika maisha ya Kiroho kwa mtu anayeendelea: namna yake ya kuwaza inainuka na kuwa ya Kiroho zaidi na zaidi, akiona vizuri mambo ya Mungu au maisha ya Kanisa kuhusiana na uzima wa milele.
Katika hatua tatu za maisha ya Kiroho “kuna viwango mbalimbali vya upendo kulingana na majukumu mbalimbali ambayo ustawi wa upendo unamdai mtu ayachukue. La kwanza ni kukwepa dhambi na kushinda mivuto ya tabia mbovu inayopingana na mivuto ya upendo: ndilo jukumu la wanaoanza, ambao ndani mwao upendo unahitaji kulishwa na kutunzwa usije ukapotea. Linafuata jukumu la pili: mtu anapaswa zaidi kukesha na kukua katika uadilifu, jambo linalowafaa wanaoendelea ambao kazi yao hasa inalenga upendo uimarike kwa kustawi ndani mwao. Jukumu la tatu la mtu ni kujitahidi kwa namna ya pekee kuungana na Mungu na kumfurahia: ndilo linalowafaa waliokamilika, wanaotamani kwenda zao wakae na Kristo” (Thoma wa Akwino).
Kama kuna kipindi kigumu cha ubalehe kati ya utoto na ujana, vilevile kuna kipindi cha namna hiyo katika kuvuka toka hatua ya utakaso ya wanaoanza kwenda hatua ya mwanga ya wanaoendelea. Hapo mtu aliyeanza kwa bidii anakabili hatari ya kukwama katika kasoro kadhaa asizozitambua, hasa ya kuishia faraja za kihisi katika sala. Basi anaachishwa hizo ili aingizwe katika njia ya Kiroho isiyotegemea hisi, ambapo katika ukavu anaanza kumiminiwa sala ili asonge mbele.
Ndivyo alivyoeleza Yohane wa Msalaba, “Usiku au utakaso wa Kimungu wa hisi unampatia mtu usafi wake ukimvua upande wa hisi na kuulinganisha na upande wa roho… Ni jambo la kawaida, linalowatokea wengi kati ya wanaoanza”. Hapo wanakuja kutambua kwamba, ili wakue katika upendo, wanapaswa kuwa maskini rohoni, kujinyima aina zote za upuuzi, majivuno, kiburi na ulafi wa roho. “Hayo makao ya hisi yanapopata kutulia hivyo, kwa maono kuratibiwa, tamaa mbaya kuzimwa, hamu kutulizwa na kulala usingizi katika usiku wa utakaso, ndipo roho inapoweza kutoroka iwajibike katika njia ya Kiroho. Mtu anaanza kuwa miongoni mwa wanaoendelea, na kujikuta katika hatua inayoitwa ya mwanga. Ndipo Mungu anapomlisha na kumuimarisha kadiri anavyopenda kwa sala ya kumiminiwa, pasipo huyo kuichangia kwa mifuatano ya mawazo, kwa utendaji au kwa kushiriki katika kazi hiyo” (walau kwa kawaida).
Mbele zaidi alieleza kasoro maalumu za wanaoendelea: ushamba wa kimaumbile, haja ya kujitokeza, kujiamini kipumbavu na kiburi cha chinichini. Hizo zinaonyesha wanavyohitaji utakaso wa Kimungu wa roho ili kuingia hatua ya waliokamilika. Jaribu hilo ni kipindi kigumu kama kile kinachotokea katika maisha ya kawaida, kijana anapoanza kutumia uhuru, pengine kwa hasara yake mwenyewe.
Yohane wa Msalaba ametufafanulia sheria za juu za uzima wa neema zinazotimia kwa wale wanaosonga mbele kwa bidii wasigeuke nyuma. Tukisoma kwa makini maisha ya watumishi wa Mungu, tunaona katika matatizo yao utakaso huo wa kina wa hisi na wa roho ambao hatimaye uliweka utu wao wote chini ya Mungu. Mtakatifu huyo alieleza vizuri kuliko wote vipindi hivyo viwili vigumu vya mpito kutoka hatua moja hadi nyingine, alivyoviita kwa usahihi matakaso ya Kimungu ya hisi na roho. Hayo yanalingana na umbile la binadamu (lenye pande mbili, yaani mwili na roho), tena yanalingana na mfumo wa neema inayotia utakatifu, inayotakiwa kuhuisha zaidi na zaidi vipawa vyetu vyote na matendo yetu yote mpaka undani wa nafsi uwe kweli wa Mungu tu kwa kutakata umimi wowote (yaani kujipendea kwa kujitambua au la).
Kwa ufupi ni kwamba katika wale wanaoanza, pamoja na kiwango cha kwanza cha upendo, yanaonekana maadili chipukizi. Kujishinda kwa ndani na kwa nje kunazidi kuwaepusha na dhambi nyepesi za makusudi, au kuwainua mara wakiangukia dhambi ya mauti. Sala yao ni ya midomo na ya kutafakari kwa mifuatano ya mawazo kunakoelekea kugeuka sala sahili ya mapendo. Ndani mwao vipaji vya Roho Mtakatifu vinafichikafichika bado: mara mojamoja wanapata miangaza yake ya pekee, lakini hawajawa tayari kufaidika nayo. Usikivu kwa Roho Mtakatifu unaendelea kuwa dhaifu; mtu anatambua zaidi utendaji wake mwenyewe na kulazimika mara nyingi kukiri umaskini wake katika kipindi kigumu cha ukavu wa hisi, utakaso mchungu wa Kimungu ambao unastahimiliwa vizuri au kiasi na unaashiria kuvukia hatua ya mwanga.
Katika wale wanaoendelea, pamoja na kiwango cha pili cha upendo, yanaonekana maadili imara, hasa upole, subira, unyenyekevu halisi zaidi unaowaelekeza wawe wema kwa jirani, na roho ya mashauri matatu ya Kiinjili. Vipaji vya Roho Mtakatifu vinaanza kujitokeza, hasa vitatu vya chini, yaani uchaji, elimu na ibada. Wanazidi kuwa wasikivu kwake na kufaidika na mianga ya ndani. Hapo wakijitahidi kweli, kwa kawaida sala ya kumiminiwa inaanza kwa tendo mojamoja la kuzama katika sala wakati wa kukusanya mawazo kwa hiari; halafu, wakiwa waaminifu, zinafuata polepole sala ya kujaliwa kukusanya mawazo, sala ya utulivu (ama mkavu ama wenye nderemo), ambapo ni wazi mchango wa kipaji cha ibada kinachowafanya walie, “Aba! Yaani, Baba!” (Rom 8:15; Gal 4:6). Ndipo maongezi na nafsi yao yanapogeuka kuwa maongezi na Mungu. Hapo wanaanza kuona ndani mwao kiburi kinachofichika, utovu wa wema kwa jirani, pengine ukali, utovu wa ari kwa wokovu wa wengi wanaopotea; kasoro hizo zote zinahitaji utakaso mwingine wa Kimungu, ule wa roho.
Katika wale waliokamilika, pamoja na kasoro kadhaa zisizo za hiari kabisa, tunashuhudia kiwango cha tatu cha upendo na maadili ya hali ya juu (pengine ya kishujaa): upole mkubwa, subira inayoyumbishwa kwa nadra tu, unyenyekevu mkuu ambao hauogopi dharau bali unapenda kudhalilishwa, imani kubwa inayofanya waone mambo yote kutoka juu, tumaini kubwa kwa Mungu, moyo mkuu unaolenga kutenda makuu ingawa yanaendana na vipingamizi, halafu kujiachilia kikamilifu katika matakwa ya Mungu ambayo hali yetu ya kesho na ya milele inayategemea. Roho ni kama inatawaliwa na Roho Mtakatifu anayeiongoza kutekeleza maadili kikamilifu zaidi. Vipaji vya akili na hekima vinaonekana kwa namna wazi na mara nyingi zaidi. Kwa kawaida ndipo inapopatikana sala ya kumiminiwa ya muungano. Hatimaye undani wa roho umetakata, na vipawa vyote vya umbile vipo moja kwa moja chini ya Mungu aliyemo katika hekalu la ndani kama utangulizi wa heri isiyo na mwisho kamwe.
Viungo vya nje
hariri- "Ascetical Theology". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Mystical Theology". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Christian and Religious Perfection". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Beatific Vision". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Asceticism". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "State or Way (Purgative, Illuminative, Unitive)". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- "Sanctifying Grace". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
- Ascetic theology from 1902 Catholic dictionary