Teolojia ya Kiroho
Teolojia ya maisha ya kiroho ni tawi la teolojia linalohusu utekelezaji wa teolojia ya dogma na ya teolojia ya maadili katika kuongoza watu kuelekea muungano na Mungu ulio wa dhati zaidi na zaidi, likifafanua muungano huo ni nini na njia za kuufikia ni zipi. Hivyo linafafanua taratibu za ustawi wa uzima wa Kiroho kwa misingi ya teolojia (kwanza Biblia, lakini pia Mapokeo na Ualimu wa Kanisa) likiilinganisha na mang'amuzi ya watakatifu.
Kitengo hicho cha teolojia ni muhimu hasa kwa Wakatoliki na Waorthodoksi, ambao kwao muungano na Mungu ndio lengo la ufunuo wake kwa binadamu.
Madhehebu mengine ya Kikristo yana mtazamo tofauti kuhusu kumfuata Yesu Kristo kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.
Mafundisho ya imani na mang’amuzi ya watakatifu
haririTeolojia hiyo inahitaji kuchambua mang'amuzi hayo kitaalamu, ikibainisha taratibu zake kadiri ya saikolojia (k.mf. ukavu unaotakasa unavyohusiana na muungano na Mungu). Somo hilo ni la kiteolojia pale ambapo uchambuzi huo unapotegemea mafundisho ya imani pia. Ikiwa elimunafsia ni ya lazima kwa maadilidini, ni ya lazima zaidi kwa maisha ya Kiroho ambayo yanachunguza ndani ya mtu hatua zake hadi muungano kamili.
Katika fani hii ni lazima tukwepe aina mbili za upotovu ambazo ni rahisi zitupate: moja kwa kuzingatia mafundisho ya imani na kupuuzia mang'amuzi, nyingine kwa kuzingatia mang'amuzi na kupuuzia mafundisho ya imani. Tunapaswa kuzungumzia maisha ya Kiroho kwa mwanga wa teolojia kuhusu neema inayotia utakatifu, maadili ya kumiminiwa na vipaji saba; la sivyo tungekusanya tu dalili za hali za Kiroho za juu, pasipo kuelewa kanuni za msingi za ustawi wa uzima wa Kimungu ambao haung'amuliki kwa kuwa si wa kimaumbile. Pia tungetia maanani mno uhaba wa watu wanaofikia muungano wa ndani na Mungu: hapo tungedhani walio wengi hawaitwi hata kwa mbali na kwa jumla wafikie hatua hiyo; tungesahau maneno ya Yesu yanayokumbushwa na [[walimu wa Kiroho kuhusu suala hilo: “Waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache” (Math 22:14).
Upande wa pili tunapaswa kuzingatia maelezo ya watakatifu kuhusu hatua mbalimbali za maisha ya Kiroho, tukiyaangaza kwa imani ili kutambua katika mang'amuzi yao yapi ni ya pekee tu na yapi ni ya juu, lakini yanakusudiwa kuwa ya kawaida. Upande huo hatari nyingine ni kudhani neema ya kuzama katika sala ni ya wengi, tukiichanganya na sala sahili ya mapendo ambayo ni utangulizi wake tu. Kufuatana na aina hizo mbili za upotovu, kuna makosa mawili ya kuepwa katika kuongoza watu: kuwaachisha njia ya juhudi mapema mno au baadaye mno.
Basi, tunapaswa kuchimba ukamilifu wa Kikristo ili kuona wazi lengo ambalo Mwokozi amewawekea watu tusilipunguze. Halafu kuchambua mang'amuzi ili tutofautishe yaliyo ya lazima na yaliyo ya ziada. Hatimaye kujumlisha hayo mawili ili kuona yaliyo ya lazima au ya kufaa na ya kutamaniwa kusudi tuufikie ukamilifu, na yale ambayo ni ya pekee tu na hayahitajiki kufikia utakatifu mkuu.
Kutokana na hatari hizo mbalimbali, kusoma maisha ya Kiroho kunadai ujuzi wa teolojia (hasa juu ya neema, maadili ya kumiminiwa, na vipaji vya Roho Mtakatifu kuhusiana na mafumbo makuu ya Utatu, umwilisho, ukombozi na ekaristi) pamoja na ujuzi wa walimu wa Kiroho, hasa wale ambao Kanisa limewatambua kuwa viongozi katika masuala hayo.
Uhusiano na maadilidini
haririKatika ngazi ya chini, maadilidini yanatakiwa kuzungumzia si tu madhambi ambayo tuyaepe, bali pia maadili ambayo tuwe nayo na usikivu katika kumfuata Roho Mtakatifu.
Maisha ya Kiroho hayana upana wa maadilidini, lakini ni tawi la juu yake kwa jinsi linavyolenga kufikisha hadi muungano wa dhati na Mungu: kwa njia yake teolojia inarudi ilipoanzia na kudumisha umoja wake. Kwa hiyo linatakiwa kufuata mwanga wa ufunuo wa Kimungu uliomo katika Biblia na Mapokeo, ambao peke yake unaweza kutujulisha uzima wa Kimungu na muungano na Mungu ambao unapita maumbile.
Maisha ya Kiroho yanatumia mawazo ya maadilidini, lakini kuhusiana zaidi na ustawi wa uzima wa Kimungu rohoni.
Utekelezaji wake, ambao ndio lengo la maisha ya Kiroho kupitia uongozi wa mtu mmojammoja, una pande mbili: juhudi na mafumbo. Upande wa juhudi maisha ya Kiroho yanazungumzia hasa namna ya kufisha vilema na kutekeleza maadili. Upande wa mafumbo yanazungumzia hasa usikivu kwa Roho Mtakatifu, neema ya kuzama katika mafumbo ya imani, na muungano unaotokana na neema hiyo, halafu karama ambazo pengine zinaongozana nayo.
Upande wa juhudi na ule wa mafumbo: tofauti na uhusiano kati ya hizo mbili
haririKadiri ya Thoma wa Akwino, Yohane wa Msalaba na Fransisko wa Sales upande wa juhudi maisha ya Kiroho yanazungumzia hatua ya utakaso wa wanaoanza; hao, wakijua kwamba hawatakiwi kubaki nyuma na kupooza, wanajitahidi kutekeleza maadili, lakini kwa namna ya kibinadamu, yaani kwa nguvu zao zikisaidiwa na neema za kawaida.
Kumbe upande wa mafumbo unaanza katika hatua ya mwanga ambapo wanaoendelea, wakiangazwa na Roho Mtakatifu, wanatenda mara nyingi na waziwazi kwa vipaji vyake saba; kwa uongozi maalumu wa huyo mlezi wa ndani wanatenda kwa namna ipitayo maumbile ambayo kabla ya hapo ilikuwa imefichika au kujitokeza mara mojamoja tu.
Kwa walimu hao mambo yanayopatikana upande wa mafumbo ni ya juu katika njia ya kawaida ya utakatifu, ila si ya pekee hasa (kama njozi). Ni hivyo hata kwa wale wanaoitiwa utakatifu katika utendaji mwingi. Basi, kujua upande wa mafumbo hakufai tu kwa uongozi wa watu wachache wanaoitwa kufuata njia za pekee, bali kwa watu wote wanaolenga ukamilifu na muungano na Mungu katika maisha ya kila siku.
Ujinga wa kiongozi wa Kiroho kuhusu mambo hayo unaweza ukazuia wale anaowaongoza: kwa kuwa hapaswi kudhani kila huzuni ya mtu aliyechoka kiakili ni takaso la Kimungu, lakini pia asidhani kuwa hilo likipatikana ni huzuni ya kinafsi tu.
Kutokana na hayo yote, ni wazi kwamba upande wa juhudi unalenga upande wa mafumbo. Vilevile upande wa mafumbo usipotanguliwa na juhudi za kufaa ni uongo mtupu. Tukitazama njia ya utakatifu kuanzia umbile letu, mafundisho haya yataonekana yamezidisha. Lakini tukiitazama kuanzia mafumbo yapitayo maumbile (uwemo wa Utatu mtakatifu ndani mwetu, umwilisho ulioleta ukombozi na ekaristi), hapo tutaiona kwa hekima, yaani kutoka juu, badala ya kupima yote kutoka chini unavyofanya upumbavu. Ikiwa kweli Utatu mtakatifu unaishi ndani mwetu, ikiwa kweli Neno alifanyika mwili akafa kwa ajili yetu, yumo katika sakramenti kuu na kila siku anajitoa kwa ajili yetu, basi hapo watakatifu tu, wanaoishi kwa kujua na kama kung'amua mara nyingi mafumbo hayo, na kwa kuyapenda zaidi na zaidi katika giza na matatizo maishani, ndio waliopo panapotakiwa. Hapo maisha ya muungano wa ndani na Mungu yanaonekana kuwa peke yake ya kawaida kweli.
Kabla hatujafikia maisha hayo, tuko bado kama watu waliosinzia, wasioishi vya kutosha kwa hazina ile kuu tuliyokabidhiwa na Mungu. Utakatifu ni muungano wa ndani na Mungu, yaani ukamilifu wa upendo kwake na kwa jirani. Ukamilifu huo unapatikana katika njia ya kawaida, kwa sababu amri ya upendo inayowapasa wote haina mipaka. Utakatifu huo hauhitaji elimu ya juu, wala utendaji mwingi wa nje, bali kuishi kwa ndani na Mungu kwa kutekeleza kwa namna bora maadili na vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyoongozana nayo.
Ndio utangulizi wa kawaida wa uzima wa milele, nao unafanyika duniani au toharani, mpaka roho iwe imetakata kabisa iweze kukaribishwa kwenye heri ya kumuona Mungu. Tukisema kuzama katika mafumbo ya imani ni sharti la kufikia utakatifu, maana yake ni kwamba pasipo hilo kwa kawaida hatufikii utakatifu.
Mhimili na umoja wa maisha ya kiroho
haririTeolojia ya maisha ya Kiroho inategemea mafundisho kuhusu maadili ya Kikristo na vipaji vya Roho Mtakatifu, halafu inachimba taratibu na masharti ya ustawi wake kwa lengo la kufikia ukamilifu wa Kikristo. Kweli mojawapo ya msingi ni kwamba imani, tumaini na upendo ndio mhimili wa maisha ya Kiroho. Kutotambua ukweli huo ni kosa kubwa linalothibitisha kuwa mtu haelewi Ukristo. Lakini umuhimu wake katika maisha ya Kiroho unategemea msimamo kuhusu tofauti iliyopo kati ya upande wa juhudi na upande wa mafumbo.
Neno juhudi linamaanisha utekelezaji wa ufishaji, ibada na maadili: upande huo maisha ya Kiroho yanaongoza watu kupambana na dhambi na kuendelea katika uadilifu. Kumbe upande wa pili unahusu mafumbo, yaani muungano wa dhati wa roho na Mungu, matukio ya muda yanayoweza yakaendana na ngazi za muungano huo (k.mf. kutoka nje ya nafsi) na hatimaye neema za pekee (k.mf. mafunuo ya binafsi).
Upande wa juhudi unatokeza hasa namna ya kibinadamu ya maadili ya Kikristo, kumbe upande wa mafumbo mara nyingi unatawaliwa wazi na namna ya Kimungu ya vipaji vya Roho Mtakatifu (ambavyo waadilifu wote wanavyo). Katika mtazamo huo, uliosahauliwa na wengi kati ya karne XVII na karne XX, tunaona umoja wa maisha ya Kiroho katika hatua zake tatu zilizoainishwa na mapokeo.
Inatosha kusoma vitabu vya Mt. Fransisko wa Sales kuhusu maisha ya Kiroho upande wa juhudi ili kuhakikisha alivyoyawekea mhimili wa maadili ya Kimungu. Humo alisema ufishaji wa ndani na wa nje ni njia kubwa ya kujivutia fadhili toka mbinguni, mradi ufanyike kwa upendo. Kwake malipizi makali siyo bora, kwa kuwa ufishaji wa kawaida, ambao kila siku unapata nafasi bila ya kuzitafuta, unazaa matunda mengi zaidi na kulinganisha matakwa yetu na yale ya Mungu. Alisema ufishaji bila ya sala ni kama mwili usio na roho, na sala bila ya ufishaji ni kama roho isiyo na mwili. Alieleza ustawi wa maadili ya Kimungu si tu kinadharia bali kiutekelezaji.
Teolojia hiyo safi kuhusu juhudi, badala ya kuishia mawaidha yanayosahau ukuu wa maadili ya Kimungu, inahuishwa nayo daima na kuelekeza maisha ya juu zaidi. Hatupotoshi maisha ya Kiroho tunapoonyesha maadili ya kiutu yanavyotakiwa kutumikia imani, tumaini na upendo. Vilevile hatuyapotoshi wala hatuzidishi nafasi ya vipaji vya Roho Mtakatifu dhidi ya maadili ya Kimungu, tunapofundisha ustawi wa imani, tumaini na upendo unavyotakiwa kuwa katika hatua ya mwanga, wala tunapokumbusha maadili hayo matatu yanavyotakaswa katika usiku wa roho, wala tunapoonyesha ushujaa wa maadili hayo katika hatua ya muungano. Hatupunguzi hata kidogo nafasi ya imani tunapofafanua ngazi zake za juu kwa kusema juu ya namna ya Kimungu ya vipaji vinavyotufanya tupenye na kuonja mafumbo tuliyofunuliwa. “Sala ya kumiminiwa ni tendo ambalo kimsingi linatokana na imani hai na kwa namna yake ya Kimungu linatokana na vipaji vya hekima na akili” (Gaetano na Yosefu wa Roho Mtakatifu). Hatuwezi kuwaza tendo la vipaji hivyo lisilotokana na imani kama mzizi wake. Maadili ya Kimungu yanabaki bora kuliko vipaji, ingawa yanakamilishwa navyo, kama vile mti ulivyo bora kuliko matunda yake, lakini ukiwa nayo ni kamili kuliko usipokuwa nayo.
D. Banyez, aliyewahi kumuongoza Teresa wa Yesu, alisema inawafaa wanateolojia, kisha kutumia miaka katika masomo, wawasiliane na mtu mwenye maisha ya Kiroho, kwa sababu wasipofanya juhudi za kudumu wala kuwa na maisha ya sala ya dhati, hawawezi kutambua utajiri wa Kiroho wa masomo wanayoyafafanua. Wanaishia kwenye ganda wasifikie kiini chake: tena wako katika hatari ya kuzingatia historia au mantiki tu wakizungumzia kwa mtazamo wa chini mafumbo makuu ya Kimungu. Roho ya teolojia ina uhai mdogo kadiri tunavyoishia hapo badala ya kujiweka tayari “kuelewa mafumbo kwa faida kubwa” (Mtaguso wa kwanza wa Vatikano) kwa mtazamo wa juu unaotawaliwa na vipaji vya akili na hekima.
Hayo yanathibitisha kwamba mhimili wa maisha ya Kiroho ni maadili ya Kimungu, ambayo ni bora kuliko vipaji, lakini yanakamilishwa navyo. Kwa mfumo wake imani inapita maumbile isiweze kukosa, lakini ni kamili zaidi inapopenya na kuonja mafumbo yote kwa uvuvio wa vipaji vya akili na hekima.
Lugha ya walimu wa kiroho na ile ya wanateolojia
haririLugha ya maisha ya Kiroho, yenye msingi katika Biblia, imepata muundo maalumu kwa njia ya walimu wa Kiroho. Polepole misamiati waliyoitumia kutokana na mang’amuzi yao imepenya teolojia ya maisha ya Kiroho, lakini inahitaji kulinganishwa na ile ya teolojia ya kawaida ili kukwepa makosa kadhaa, kama yale aliyoyaangukia Eckart akitamka kwa maana ya kifalsafa maneno yaliyo kweli kwa maana ya Kiroho tu.
Lugha ya walimu wa Kiroho inaonekana na wanateolojia wengi kuwa inatumia mno mifano, tena inapita kiasi. Shida ni kwamba pengine mwenye akili anadai kumsahihisha anayemzidi akili, kama vile kinda angedai kumfundisha tai namna ya kuruka! Wanateolojia hao hawaelewi kuwa “lugha ya Kiroho haina budi kutofautiana na ile ya falsafa; humo mifano ya kuzidisha inatumika si kama pambo la usemi, bali ni namna inayotakiwa kabisa ili kumaanisha mambo kwa usahihi, kwa sababu kazi yake ni kutokeza mang’amuzi, tena mang’amuzi ya hali ya juu, yaliyo magumu kutokezwa kuliko mengine yote… Akili inavuka toka misamiati ya aina moja hadi ya aina nyingine, kama vile kutoka Kilatini kwenda Kichina au Kiarabu. Lakini haiwezi kutumia sarufi ya lugha mojawapo kwa nyingine” (Yakobo Maritain).
Kwa mfano, Yohane wa Msalaba anaeleza hali ya kuzama katika sala kuwa ni kutotenda, kumbe Thoma wa Akwino anaiita “utendaji bora kuliko wowote”. Wa pili anatazama upande wa falsafa, wa kwanza upande wa mang’amuzi ya mafumbo, ambamo kusimama kwa utendaji wa kibinadamu kunaonekana kama kutotenda.
Vilevile, neno “maumbile”, maana yake katika falsafa ni ya kinadharia: ni jinsi yalivyokusudiwa na Muumba, pasipo ubaya; kumbe maana ya Kiroho inategemea mang’amuzi ya dhambi ya asili, yaani kwamba madonda yaliyotokana nayo hayajapona kikamilifu hata ndani ya Wakristo, yakiathiri umbile na kujitokeza kama umimi mkubwa unaozidishwa na dhambi za binafsi. Hivyo mafundisho ya lugha hizo mbili hayapingani.
Misingi ya kiteolojia ya lugha ya walimu wa kiroho
haririKila fani ina misamiati yake maalumu isiyoeleweka vizuri kwa wasioijua. Maneno yanatokeza mawazo, kama vile mawazo yanavyotokeza ukweli wa mambo. Mawazo ya sayansi ni sahihi kuliko yale ya kawaida, hivyo pengine yanadai misamiati mipya kuyatokeza. Ikiwa hivyo kwa sayansi, kwa nini isiwe hivyo kwa maisha ya Kiroho?
Teolojia ikitetea lugha ya walimu wa Kiroho inafundisha kwamba tunaweza kusema juu ya Mungu na juu ya maisha ya Kiroho kwa kutumia ama maneno yenye maana halisi ama mifano. Hivyo tunasema kwa maana halisi, “Mungu ni mwema na mwenye hekima: ndiye wema na hekima yenyewe”. Kwa kuwa hizo sifa hazina kasoro, Mungu anazo kuliko viumbe. Kumbe kwa mfano tu tunaweza kusema, “Mungu anaghadhibika”: kwa kuwa hasira ni ono la hisi, haiwezi kuwemo ndani ya Mungu aliye roho tu; hivyo “ghadhabu ya Mungu” ni mfano tu wa haki yake.
Tuongeze kwamba kati ya maneno yenye maana halisi yanayotumika kumhusu Mungu, yale ya kukanusha (k.mf. “asiyebadilika”) ni sahihi kuliko yale ya kukiri, kwa sababu sisi tunajua zaidi Mungu asivyo kuliko alivyo. Yaani tunajua vizuri kwamba hana mwili, wala mwendo, wala mipaka; kumbe hatuwezi kujua namna ambayo sifa za Kimungu zimo ndani mwake na zilivyo kitu kimoja tu katika ukuu wa Umungu ambao uko wazi kwa wenye heri wa mbinguni tu, wanaouona moja kwa moja. Ndiyo sababu waliozama katika mafumbo wakimzungumzia Mungu wanatumia zaidi maneno ya kukanusha (k.mf. “asiyeeleweka”), tena wanasema kumtazama hivyo ni bora kuliko kuelewa, kwa sababu kwa namna yake kunafikia juu zaidi, hadi ukuu wa Umungu na maisha yake ya ndani.
Halafu, kati ya majina ya kukiri yanayotumika kwa maana halisi, yale yasiyobainisha na yale ya kawaida ndiyo yanayomtokeza Mungu vizuri zaidi. Kwa hiyo jina YHWH ndilo lake kuliko yote, kwa kuwa fumbo la jina lenyewe linadokeza bahari isiyo na mipaka ya Umungu. Kinyume chake, majina yaliyo wazi (k.mf. “Mwenye akili”) hayatokezi inavyofaa ukuu wa Mungu. Ndiyo sababu waliozama katika mafumbo wanasema sala ya kumiminiwa si wazi wala haielezeki, hata hivyo ni bora kuliko maneno wazi ya njozi. Hatimaye, maneno ya mifano yanahitajika panapokosekana yale yenye maana halisi. Ndiyo sababu waliozama katika mafumbo wanasema juu ya kuposwa na kuolewa Kiroho ili kumaanisha muungano na Mungu ambao unaigeuza roho. Haja ya kutumia mifano ya namna hiyo inatokana na sisi kujua mambo ya Kiroho kwa njia tu ya vitu vinavyoonekana, pamoja na ugumu wa kupata maneno ya kufaa kuyatokeza.
Msamiati muhimu zaidi wa walimu wa kiroho
haririMsamiati wa kawaida wa Maandiko matakatifu na wa teolojia unaweza ukatosha kufundishia maisha ya Kiroho; lakini walimu wa maisha hayo, ili kuepa sentensi ndefu mno, walitumia msamiati maalumu au kuupa maana mpya ule wa zamani, kiasi kwamba hausemi ukweli ukitumika upande wa falsafa au wa teolojia ya kawaida. Kwa mfano, wakisisitiza udogo wa kiumbe chochote, ambao mwanateolojia angeutokeza kwa sentensi tano, wanatamka kifupi, “kiumbe si kitu”. Usemi huo si uongo, isipokuwa tukiuelewa kwa maana halisi ya maneno (hapo ungesema Mungu hajaumba chochote; lakini hilo halihitaji maelezo). Kwa mtazamo wake mwanateolojia angeuongezea msemo huo walau “peke yake” aweze kuukubali.
Msamiati wa kupinganisha unatokeza jambo kuu kwa njia ya matokeo yake ndani mwetu yaliyo kama kinyume chake. Kwa mfano, “giza kuu” maana yake ni “mwanga usiofikiwa anamokaa Mungu” ambao unatupofusha macho. Vilevile hekima ya Mungu inaitwa “upumbavu” kwa kuwa ndivyo inavyoonekana na wapumbavu: “upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu” (1Kor 1:25).
Msamiati wa kuzidisha unataka kudokeza ukuu usio na mipaka wa Mungu (k.mf. “wema mkuu”) au udogo wa kiumbe mbele yake. Msamiati huo haupiti ukweli, bali dhana za watu, kwa kuwa Mungu ni mkuu kuliko tunavyoweza kuwaza, na adhabu zake zinapita ubunifu wetu. Katika maandishi ya kibinadamu, pengine vipimo vinazidishwa ili kumgusa msomaji (k.mf. kwa kusema mtu mrefu ni jitu). Kumbe waliozama katika mafumbo wanatumia msamiati wa kuzidisha kwa sababu wanashindwa kueleza kwa namna tofauti ukuu wa Kimungu; kuzidisha kwao hakuna kosa wala udanganyifu. Mfano wa aina hiyo ni maneno ya Yesu: “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe… Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe…” (Math 5:29-30). Si suala la kujikata, ila ni usemi unaofaa kuonyesha ukuu wa hatari na haja ya kuikwepa haraka.
Yohane wa Msalaba alipochora ukurasa wa kwanza wa kitabu chake “Kupanda Mlima Karmeli” aliandika juu ya mapito membamba ya ukamilifu, “kutokuwa na chochote, chochote, chochote, chochote”. Ingawa anaonekana kudai mtu ajikane mno, kusudi lake ni kumpandisha kwa njia ya mkato. Juu ya hayo aliandika, “Kwa kuwa sitaki tena kitu kwa kujipendea, napewa vyote pasipo kuvitafuta”. Hapo mbele akaeleza, “Kujitenga na viumbe kunaleta furaha na faraja kuliko kutamani kwa moyo kuvimiliki… Mtu akijitenga na vitu anakuja kuvifahamu wazi zaidi, upande wa maumbile na upitao maumbile, na hivyo anavifurahia sana kuliko yule anayeambatana navyo. Anavifurahia kadiri ya ukweli wake, si kadiri ya udanganyifu wake. Hisi zinafikia maumbo tu ya vitu, kumbe roho inapenya ukweli na thamani yake. Kwa sababu hiyo, furaha za hisi zinaitia giza akili yetu… Kuikataa na kuitakasa furaha hiyo kunaiwezesha akili ione vizuri, kama vile hewa inavyong’aa moshi ukiondoka. Aliyejitenga na viumbe anavifurahia vyote kama kwa kuvimiliki, kumbe yule anayetafuta tu kuvimiliki anavikinai bila ya kukifurahia hata kimoja”. Mtume Paulo aliwahi kusema, “… kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote” (2Kor 6:10). Fransisko wa Asizi alifurahia mandhari nzuri za mkoa wake kuliko wenye maeneo yale ambao mawazo yao yote yalilenga tu kuyazalisha iwezekanavyo.
Basi, msamiati huo unatuamsha kutoka lepe la usingizi na kutuonyesha lililo muhimu peke yake.
Kulinganisha lugha ya walimu wa kiroho na ile ya wanateolojia
haririKila mojawapo ina stahili zake. Kwa teolojia inafaa zaidi lugha ya kinadharia, sahihi, inayotumia misamiati kwa maana halisi tu. Lakini kwa kuongoza watu wajikane kwa bidii ili kuungana na Mungu, misamiati ya walimu wa Kiroho inafaa zaidi kwa sababu ni hai, ya kuvutia, mifupi na inaeleweka kimaisha. Haitokezi tu mawazo, bali mang’amuzi na upendo motomoto wa Mungu. Inaepa mizunguko ya maneno na mibainisho inayoweza ikazuia mruko wa upendo huo. Kinyume chake inatuongoza tumtafute Mungu mwenyewe ikitukumbusha kuwa hata kama ukweli wa mawazo umo akilini mwetu, wema unaolengwa na utashi uko nje ya roho yetu, umo ndani ya Mungu; tena inatufanya tufikirie kwamba yale ambayo ndani ya Mungu hayaeleweki wala hayasemeki, ndiyo mema makuu yanayoweza kupendwa motomoto hata yasipojulikana wazi.
Tofauti ya lugha hizo mbili inaonekana katika kulinganisha maneno yafuatayo ya Yesu na ufafanuzi wake wa kiteolojia: “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele” (Yoh 12:25). Ufafanuzi wa maneno hayo mafupi, hai na ya kimaisha ni kama ifuatavyo: anayejipenda kinyume cha upendo wa Mungu atajipoteza; lakini hatajipoteza akijipenda kimaumbile, yaani kwa pendo lililo tofauti na upendo wa Mungu lisiwe kinyume chake; zaidi tena hatajipoteza akijipenda kwa pendo lililomo ndani ya upendo wa Mungu. Kubainisha aina hizo tatu za kujipenda ni jambo la lazima kwa teolojia, lakini ni kazi ya akili inayochunguza mambo, kumbe maneno ya Yesu yanatufanya mara tupende kwa bidii.
Ipi lugha bora kati ya hizo mbili?
haririLugha bora ni ile inayotokeza wazo la juu zaidi. Sasa, sala ya kumiminiwa, ingawa si wazi, ni ya juu kuliko nadharia. Basi, lugha ya wanaotushirikisha yale waliyomiminiwa katika sala ni bora kuliko ile ya wanateolojia. Inafaa kwamba baadhi ya wanaozama katika mafumbo ni pia wanashairi hodari waweze kutujulisha vizuri mang’amuzi yao ya ndani, jambo ambalo si la lazima kwa wanateolojia. “Ingawa tunajua kidogo sana mambo ya juu kabisa, kile kidogo tunachokijua kinatosha kutufanya tukipende na kukitamani kuliko ujuzi sahihi kabisa wa mambo ya chini ambao tunaweza tukawa nao” (Thoma wa Akwino). Hivyo, wazo la kufaa kuhusu Utatu, hata lisipokuwa la wazi, lina thamani kuliko hakika zote za hisabati, kutokana na ubora wa jambo husika. Vilevile sala ya kumiminiwa inang’amua uwepo wa Mungu, jambo bora kuliko tunalolizingatia kwa teolojia; tena namna yake ya kujua ni bora zaidi.
Tuliyoyasema yanathibitishwa na kwamba lugha ya Yesu ndiyo bora; sasa ile ya walimu wa Kiroho inalingana nayo kuliko ile ya wanateolojia. Lugha hiyo inadumisha imani na upendo kwa Mungu, yaani roho yenyewe ya teolojia. Upande mwingine, lugha ya falsafa na teolojia ni ya lazima kwa kufafanua ukweli uliofunuliwa dhidi ya udanganyifu unaoweza ukaupotosha. Ndiyo sababu walimu wa Kiroho waliwaheshimu wanateolojia bora, kumbe waliojidai tu kuzama katika sala waliwapuuzia. Basi, anayeongoza watu Kiroho anatakiwa kujua lugha hizo mbili na kuweza kuzifafanua moja kwa njia ya nyingine. Hatuwezi kusema mtu anaelewa lugha ya walimu wa Kiroho asipoweza kuifafanua kiteolojia, wala kusema anaelewa ukuu wa teolojia asipojua inavyohusiana na maisha ya Kiroho.
Marejeo
hariri- F. VAN VLIJMEN, W.F., Safari ya Kiroho, Mafundisho kwa Watawa (vitabu 2) – ed. T.M.P. Book Department – Tabora 1978
- R. GARRIGOU-LAGRANGE, O.P., Hatua Tatu za Maisha ya Kiroho, Utangulizi wa Uzima wa Mbinguni – tafsiri fupi ya Rikardo Maria, U.N.W.A. – ed. Ndugu Wadogo wa Afrika – Morogoro 2006
Viungo vya nje
hariri- [1] Ilihifadhiwa 24 Januari 2012 kwenye Wayback Machine. Tafsiri fupi ya kozi ya maisha ya kiroho "Hatua Tatu ya Maisha ya Kiroho" iliyoandikwa kwa Kifaransa na padri Reginald Garrigou-Lagrange wa shirika la Wadominiko
- Ascetic theology Ilihifadhiwa 6 Juni 2004 kwenye Wayback Machine. from 1902 Catholic dictionary