Lagos ni mji mkubwa wa Nigeria. Ilikuwa mji mkuu wa nchi hadi mwaka 1991.

Lagos inavyoonekana kutoka bandari yake

Ikiwa na wakazi takriban milioni 12 katika eneo la jiji na milioni 15 - 22 katika rundiko la mji ni kati ya miji mikubwa zaidi ya Afrika; inawezekana kwamba idadi ya watu imeshapita ya Kairo, hivyo kuwa jiji lenye watu wengi barani Afrika[1].

Lagos ilianzishwa kama mji wa bandari uliokua juu ya visiwa vidogo karibu na mdomo wa wangwa wa Lagos unapounganika na Bahari ya Atlantiki.

Bandari ya Lagos iko kati ya bandari muhimu zaidi Afrika[2][3].

Jiografia hariri

Lagos iko mwambaoni mwa Ghuba ya Guinea; wenyeji hutofautiana sehemu mbili kuu ambazo ni "kisiwani" (The Island) na "barani" (Mainland).

Lagos kisiwani hariri

Lagos kisiwani ni zaidi ya kisiwa kimoja, jina hili linajumlisha pande zote zilizotengwa na bara kwa mfereji ambao ni mlango wa wangwa wa Lagos kwenda baharini.

Visiwa vikubwa ni Lagos Island, Ikoyi, na Viktoria pamoja na visiwa vidogo mbalimbali, mara nyingi mifereji midogo kati yake imeshafunikwa kwa majengo na madaraja mengi au kujazwa. Sehemu hii ni kitovu cha biashara na maofisi pamoja na makazi yenye bei za juu.

Madaraja matatu makubwa huunganisha sehemu ya kisiwani na bara ambazo ni madaraja ya Carter, Eko na daraja la tatu la bara.

 
Ramani ya eneo la Lagos

Lagos bara hariri

Wakazi wengi wa Lagos huishi barani, ng'ambo ya wangwa. Huko viko viwanda vingi.

Utawala hariri

Hadi mwaka 2006 kulikuwa na manisipaa ya Lagos iliyojumlisha Lagos Visiwani pamoja na maeneo machache barani. Mwaka ule manisipaa ilivunjika na kugawiwa kwa halmashauri mbalimbali. Hali halisi jiji likaendelea kukua barani. Tangu siku zile serikali inalenga kuimarisha utawala kwenye ngazi za chini.

Ndani ya eneo la Lagos hakuna muundo wa manisipaa au jiji moja bali kuna halmashauri 16 zinazoitwa Local Government Area (LGA) na kuunganishwa katika "Metropolitan Lagos". Idadi za wakazi hapa chini zinarejea sensa ya 21 Machi 2006.[4]

Halmashauri ("LGA") Eneo
in km²
Idadi ya wakazi
(2006)
Wakazi
kwa km²
Agege 11,20 459.939 41.066
Ajeromi-Ifelodun 12,33 684.105 55.483
Alimosho 185,20 1.277.714 6.899
Amuwo Odofin 134,58 318.166 2.364
Apapa 26,66 217.362 8.153
Eti-Osa 192,35 287.785 1.496
Ifako-Ijaye 26,61 427.878 16.080
Ikeja 46,16 313.196 6.785
Kosofe 81,41 665.393 8.173
Lagos Island 8,66 209.437 24.184
Lagos Mainland 19,47 317.720 16.318
Mushin 17,48 633.009 36.213
Ojo 158,16 598.071 3.781
Oshodi-Isolo 44,76 621.509 13.885
Shomolu 11,55 402.673 34.863
Surulere 23,00 503.975 21.912
Gesamt 999,58 7.937.932 7.941

Tabianchi hariri

Lagos huwa na tabianchi ya savana tropiki (Aw) kufuatana na upambanuzi wa Koeppen. Kiwango cha mvua kinatofautiana sana baina ya majira ya mvua na ya ukame. Masika (yenye mvua) yaanza mwezi Aprili na kuishia Oktoba. Ya ukame yako kati ya Novemba hadi Machi. Mwezi wenye mvua nyingi ni Juni yenye usimbishaji wa mm 315.5, ilhali Januari ina milimita 13.2 pekee.

Lagos iko karibu na ikweta, tena kwenye uwiano wa bahari, hivyo hakuna tofauti kubwa katika halijoto kati ya miezi ya mwaka. Wakati wa Machi wastani uko kwenye sentigredi 28.5 na Agosti huwa na 25.

Historia hariri

Kiasili eneo la Lagos lilikaliwa na kabila la Waawori ambao ni sehemu ya Wayoruba. Katika karne ya 15 ikaitwa "Oko".[5][6]

Chini ya chifu wao Olofin hao Waawori wakahamia kwenye visiwa ndani ya wangwa pamoja na Kisiwa cha Lagos[7][8]

Katika karne ya 16 eneo lilitwaliwa na milki ya Benin na kisiwa cha Lagos kilikuwa kambi la kijeshi la Benin kilichoitwa "Eko".[9][10] Jina hili linatumiwa hadi leo na wenyeji wa Lagos.

Jina la Lagos lilitumiwa na mabaharia Wareno waliojenga huko kituo cha biashara na kukiita kwa heshima ya mji wa Lagos huko Ureno[11].

Mwaka 1472 baharia Mreno Ruy de Sequeira alifika Eko akaanzisha kituo cha "Lagos" - kwa Kireno neno hili lamaanisha "maziwa": ni pia jina la mji wa Ureno ya kusini.

Katika karne zilizofuata Lagos ilikuwa ufalme mdogo wa Kiyoruba. Mtawala wake alistawi na kutajiriki kutokana na biashara na wafanyabiashara kutoka Ulaya. Sehemu kubwa ilikuwa biashara ya watumwa.

Katika karne ya 19 Uingereza ilibadilisha msimamo wake kuhusu utumwa wakijaribu kukandamiza biashara hiyo katika Afrika ya Mashariki. Mwaka 1841 Oba mpya aliyeitwa Akitoye alipiga marufuku biashara ya watumwa lakini alipinduliwa kwa sababu ya upinzani wa wafanyabiashara wenyeji. Akitoye aliomba usaidizi wa Uingereza. Manowari za Kiingereza zilishambulia Lagos tarehe 26 na 27 Desemba 1852 na kumrudisha mfalme.

Matatizo ya biashara ya watumwa yaliendelea na Waingereza walichukua kisiwa cha Lagos na kuifanya kwanza eneo lindwa halafu koloni. Oba alibaki na madaraka machache.

Uchumi hariri

 
Maduka ya Galleria huko Lagos, Kisiwa cha Viktoria
 
Mtaa wa vibanda wa Makoko, Lagos

Lagos ni kitovu cha uchumi wa Nigeria. Kiasi kikubwa cha pato la taifa kinazalishwa hapa. Makao makuu ya makampuni makubwa na benki yako Lagos Kisiwani.

Lagos ni pia moyo wa tasnia ya mawasiliano (ICT) ya Afrika ya Magharibi. [12]

Sehemu za Lagos zina hali ya juu[13][14], hata hivyo theluthi mbili za wakazi huishi katika mitaa ya vibanda pasipo maji ya bomba na vyoo vya kutosha. [15]

Bandari ya Lagos ni bandari kubwa ya Nigeria iko pia kati ya mabandari makubwa ya Afrika. Ina pande tatu ambazo ni kando la kisiwa cha Lagos chenyewe halafu sehemu za Apapa (penye kituo cha kontena) na Tin Can.[16] Bandari imeunganishwa na mfumo wa reli ya Nigeria.

Sehemu muhimu ya biashara ya bandari ni petroliamu inayosafirishwa hapa kwenda kote duniani.[17] Mafuta ya petroli na bidhaa zilizotengenezwa kutoka mafuta hayo ni sawa na asilimia 14 za Jumla ya Pato la Taifa (GDP) na 90% za mapato ya fedha za kigeni.[18]

Marejeo hariri

  1. linganisha worldpopulationreview.com inayorejea taarifa ya New York Times ya 2012; ilitazamiwa 23 Novemba 2016
  2. "Africa's biggest shipping ports", Businesstech. 8 March 2015. iliangaliwa 23 Novemba 2016
  3. "Africa's top 10 ports", arabianbusiness 12 Mei 2008, iliangaliwa 23 Novemba 2016
  4. GeoHive: Lagos - Administrative Units Archived 7 Agosti 2011 at the Wayback Machine..
  5. Margaret Peil (1991). Lagos: the city is the people (World cities series). G.K. Hall. p. 5. ISBN 978-0-816-1729-93. 
  6. Anthony Appiah; Henry Louis Gates (2010). Encyclopedia of Africa, Volume 1. Oxford University Press. p. 28. ISBN 978-0-195-3377-09. 
  7. Sandra T. Barnes (1986). Patrons and Power: Creating a Political Community in Metropolitan Lagos. Indiana University Press, International African Library. p. 20. ISBN 978-0-2533-4297-3. Retrieved July 26, 2014. 
  8. Francesca Locatelli; Paul Nugent (2009). African Cities: Competing Claims on Urban Spaces. Brill. p. 114. ISBN 978-9-0041-6264-8. Retrieved July 26, 2014. [dead link]
  9. Williams, Lizzie (2008). Nigeria: The Bradt Travel Guide. Bradt Travel Guides. p. 110. ISBN 1-84162-239-7. 
  10. Smith, Robert Sydney (1988). Kingdoms of the Yoruba (3 ed.). University of Wisconsin Press. p. 73. ISBN 0-299-11604-2. 
  11. The Origin of Eko (Lagos). Edo Nation. Iliwekwa mnamo 2 June 2010.
  12. Douglas Zhihua Zeng (2008). Knowledge, Technology, and Cluster-based Growth in Africa (WBI development studies). World Bank Publications. p. 66. ISBN 9780821373071. 
  13. Tolu Ogunlesi. "Commercial hub status of Lagos sparks a chain reaction", Financial Times, May 4, 2014. Retrieved on March 17, 2016. 
  14. "Luxury living in Lagos", CNBC Africa, October 21, 2013. Retrieved on March 16, 2016. Archived from the original on 2016-03-19. 
  15. Lagos, the mega-city of slums
  16. OT Africa Line – Nigeria Page. Otal.com (1 February 2007). Iliwekwa mnamo 2 June 2010.
  17. OT Africa Line – Lagos Port Statistics. Iliwekwa mnamo 2 June 2010.
  18. Nigeria. CIA World Factbook (1 February 2007). Jalada kutoka ya awali juu ya 2020-08-31. Iliwekwa mnamo 4 April 2012.

Viungo vya nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu maeneo ya Nigeria bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Lagos kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.