Kilema (maadili)
Kilema (kwa Kiingereza: vice, kutoka Kilatini vitium, yaani kasoro), katika maadili, kinafafanuliwa kama zoea la kutenda mabaya ya aina fulani. Kadiri mtu anavyorudia kulitenda, kilema husika kinaimarika ndani yake [1].
Vilema vikuu |
---|
Mapokeo ya Kikristo yameorodhesha kati ya vilema vyote vile vikuu vilivyo mizizi ya dhambi zote [2]:
Kilema tawala
haririThoma wa Akwino na wengineo wamefundisha kwamba kila mtu anaelekea zaidi kilema kimojawapo. Hicho kilema kinatawala vingine pamoja na namna yake ya kuona, kupima, kuhisi, kutaka na kutenda.
Kilema tawala kinahusiana na silika, ambayo ni kawaida yake kuelekea upande mmoja. Kuna silika ambazo zinaelekea uzembe, ulafi na uzinifu; nyingine zinaelekea hasira na kiburi. Ndiyo sababu zinahitaji kukamilishwa na maadili mbalimbali, yanayotuwezesha kutenda kadiri ya akili na imani katika nafasi na kwa watu tofauti. Hatupandi sote upande uleule kuelekea kilele cha ukamilifu; wenye silika ya upole wanatakiwa kujipatia nguvu kwa sala, neema na maadili; kumbe walio na nguvu kiumbile wanatakiwa kujifanya wapole kwa msaada wa neema.
Kabla tabia haijabadilika hivyo hatua kwa hatua, kilema tawala cha kila mmoja kinajitokeza mara nyingi. Ndicho adui wa ndani anayeweza kuangamiza kazi ya neema; ni kama ufa katika ukuta unaoonekana imara, kumbe sio: tikisiko la nguvu linaweza kuubomoa. Kilema tawala ni cha hatari zaidi kwa sababu mara nyingi kinaathiri sifa bora ya mtu, yaani elekeo jema la umbile lake linalokusudiwa kustawishwa na kuinuliwa na neema. Mmoja anaelekea kuwa mpole, lakini ikiwa kilema chake tawala (pengine ni uzembe) kinaugeuza upole kuwa udhaifu unaoruhusuruhusu maovu yatendeke tu, atafikia hatua ya kukosa nguvu yoyote. Kinyume chake mwingine anaelekea kuwa hodari, lakini akikubali kutawaliwa na hasira, nguvu yake itatumika kwa ukatili na kusababisha vurugu za kila aina, k.mf. kugombana badala ya kushirikiana na wengine.
Pamoja na kilema tawala ndani ya kila mmoja mna mvuto maalumu wa neema ambao kwa kawaida unaanza kukamilisha yaliyo bora katika umbile lake, halafu unaenea kwa yasiyo bora. Shetani analenga kustawisha zaidi na zaidi kilema tawala kiusonge mvuto maalumu wa neema ndani ya mtu. Hivyo tunaweza kuhisi hasara ambayo huenda ikatupata tusipokesha kushinda kilema hicho, ambacho ni kama mdudu anayekula tunda zuri ndani kwa ndani.
Kutambua kilema tawala
haririNi muhimu tukitambue tusijidanganye. Ujuzi huo unahitajika zaidi kwa sababu Shetani anakijua fika na kukitumia ili kuvuruga ndani mwetu na kandokando yetu. Katika ngome ya maisha ya Kiroho, inayolindwa na maadili mbalimbali, kilema tawala ni kama sehemu dhaifu isiyolindwa. Basi, tukitambuaje? Kwa wanaoanza ni rahisi wakiwa wanyofu, ila baadaye kinaelekea kufichama na kujidai ni adili: kiburi kinajidai ni moyo mkuu, na uzembe unajidai ni unyenyekevu. Hata hivyo ni lazima tukifichue ili tupambane nacho, la sivyo hatutakuwa na maisha halisi ya Kiroho.
Kwanza tunapaswa kumuomba Mungu atuangazie: “Bwana, unijulishe vizuio ambavyo, kwa kujua au kutojua, ninazuia kazi yako ndani yangu; halafu unipe nguvu ya kuviondoa, na nisipofanya hivyo kwa bidii, tafadhali uviondoe mwenyewe, hata kama itanipasa kuteseka. Sitaki lingine isipokuwa wewe, Bwana, ambaye peke yako ni wa lazima kwangu. Unijalie maisha yangu hapa duniani yawe kama mwanzo wa uzima wa milele”. Kisha kuomba hivyo kwa unyofu, tunapaswa kujitafiti kwa makini kwa kujiuliza: tunapoamka au kubaki pweke mahangaiko yetu ya kawaida, mawazo na matamanio yetu yanaelekea wapi? Katika kufanya hivyo tukumbuke kuwa kilema kinachotawala kwa urahisi maono yetu yote kinajidai ni adili na kutuzuia tusitubu, ilivyomtokea Yuda Iskarioti asiyejua wala kutaka kutawala uroho. Tunapaswa pia kujiuliza juu ya chanzo cha kawaida cha huzuni na furaha yetu, sababu kuu ya matendo yetu, asili ya kawaida ya dhambi zetu, hasa zile ambazo zinajirudiarudia au kudumu muda fulani kama kwa kupinga neema. Tunapaswa kujiuliza tena kiongozi wetu wa Kiroho anawaza nini kuhusu kilema chetu tawala. Pengine ameshakitambua na kujaribu kusema nasi juu ya hicho, lakini tukajitetea. Hiyo ni rahisi kwa sababu kilema tawala kinachochea maono yote, na kuitikia kwa dharau, hasira au utovu wa subira, kwa kuwa hakitaki kutambulikana na kupingwa. Hivyo jirani akitukosoa kuhusu hicho, pengine tunajibu, “Naweza kuwa na vilema vyote, isipokuwa hicho”. Tunaweza kutambua kilema tawala hata kwa kuzingatia vishawishi ambavyo adui anavisababisha mara nyingi zaidi ndani mwetu, kwa sababu ni kawaida yake kutushambulia hasa upande huo dhaifu. Hatimaye, tunapowaka juhudi kweli, mianga ya Roho Mtakatifu inatuomba sadaka hasa katika hicho.
Tukifuata kwa unyofu njia hizo, haitakuwa vigumu kutambua adui wa ndani anayetufanya watumwa: ni kama gereza tunalotembea nalo popote tuendapo. “Amin, amin, nawaambia: Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” (Yoh 8:34). Kwa hiyo tunatakiwa kutamani ukombozi. Ni neema kubwa kukutana na mtakatifu atuambiaye, “Tazama kilema kinachokutawala na tazama pia mvuto maalumu wa neema ambao uufuate kwa bidii ili kufikia muungano na Mungu”. Ndivyo Yesu alivyowaita “Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo” (Mk 3:17) vijana Yakobo na Yohane waliotaka kuamuru “moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize” Wasamaria waliokataa kumpokea Yesu; lakini yeye “akawageukia, akawakanya. Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo. Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa” (Lk 9:53-55). Kwa kumfuata Mwokozi hao Boanerge wakawa wapole, hata Yohane mwishoni mwa maisha yake alikuwa anajua kusema hili tu: “Wapenzi, na tupendane” (1Yoh 4:7). Akiulizwa kwa nini anakariri hilohilo, alikuwa akijibu, “Ndiyo amri ya Bwana: ukiishika, umemaliza kazi”. Katika hatua hiyo, ari yake ilikuwa imegeuka ya Kiroho na kuendana na upole.
Kupambana na kilema tawala
haririNi lazima tupambane nacho kwa kuwa ndicho adui mkuu wa ndani, ambacho kikishindwa, vishawishi vitakuwa fursa za maendeleo kuliko hatari. Ila hatuwezi kusema kilema hicho kimekoma kabla hayajapatikana maendeleo halisi ya Kiroho, kabla hatujafikia ari halisi ya kudumu, yaani kabla utashi haujawa tayari kumtumikia Mungu daima. Kwa mapambano hayo tufuate njia kuu tatu: sala, utafiti wa dhamiri na adhabu. Tusali kwa unyofu, “Bwana, unionyeshe kizuio kikuu cha utakatifu wangu, kinachonizuia nisifaidike na neema zako na matatizo yanayoweza kuchangia ustawi wa roho yangu”. “Bwana, uniondolee yale yote yanayonizuia nisifike kwako; unijalie yale yote yanayoweza kunifikisha kwako; ujichukulie nafsi yangu, na kujipatia kabisa mwenyewe” (Nikola wa Flue). “Bwana, unichome moto hapa duniani, na kunikausha hapa duniani, ili unihurumie milele” (Ludoviko Bertrand). Sala hiyo haitusamehe utafiti, bali inatuelekeza kuufanya. Tena inafaa, hasa kwa wanaoanza, tuandike kila wiki tumeshindwa na kilema tawala mara ngapi. Tukihesabu mapato na matumizi ya fedha, tujue zaidi mapato na hasara upande wa uzima wa milele. Inafaa pia tujipangie adhabu kwa kila tutakapoangukia kilema hicho ili turekebishe kosa, tutoe fidia inayostahili na tuwe macho zaidi siku za mbele.
Kabla hatujashinda kilema tawala, yale tunayodhani ni maadili yetu, mara nyingi ni maelekeo mazuri ya umbile tu; chemchemi ya neema haijafunguka vya kutosha juu yetu kwa sababu bado tunajipendea mno tusiishi kwa ajili ya Mungu kweli.
Hatimaye tushinde hali ya kukata tamaa inayotufanya tudhani kilema tawala hakiwezi kung’olewa kwa neema ya Mungu. Katika hilo mapambano ya kudumu na ya nguvu ni ya lazima kuliko ushindi, kwa sababu tukijisamehe kupambana, tunaacha maisha ya Kiroho. Hatutakiwi kamwe kupatana na kasoro zetu, la sivyo hatuwezi kulenga ukamilifu unaotupasa, wala kuwa na furaha ya ndani na amani, kwa kuwa hiyo inatokana na moyo wa kujitoa sadaka unaofisha ndani mwetu yale yote yasiyoratibiwa. Kwa njia hiyo tu upendo unafaulu kushinda kilema tawala na kushika nafasi ya kwanza rohoni mwetu. Ufishaji wa kilema tawala unatuweka huru na kuhakikisha mvuto maalumu wa neema utawale ndani mwetu. Hivyo polepole tunakuwa wenyewe kupita umbile letu, pasipo kasoro zetu. Si suala la kuiga sifa za wengine wala la kuganda wote namna moja, kwa kuwa binadamu ni mbalimbali kama maua. Lakini hatutakiwi kutawaliwa na silika, bali kuirekebisha kwa kudumisha yaliyo mema ndani yake na kuyatia chapa ya maadili, hasa yale ya Kimungu. Hapo, badala ya kujifanya kiini cha yote - kama tunapotawaliwa na kilema fulani - tunajisikia kuelekeza yote kwa Mungu, kumfikiria karibu mfululizo, kuishi kwa ajili yake tu, na kuwavuta kwake wale wote wanaotujia.
Tanbihi
haririMarejeo
hariri- Aristotle, trans. H. Rackman. Virtues and Vices, Loeb Classical Library, Harvard University Press, Cambridge, MA, 1992. vol. 285.
- Goodman, Lenn E. (2005). Islamic Humanism. Oxford University Press. ISBN 978-0-19-518914-8.
- Hess, Kären M.; Orthmann, Christine Hess (2008). Introduction to Law Enforcement and Criminal Justice. Belmont, CA: Wadsworth. ISBN 978-0-495-39090-9.
- Hirakawa, Akira; Groner, Paul (1998). A history of Indian Buddhism: from Śākyamuni to early Mahāyāna. Motilal Banarsidass. ISBN 978-81-208-0955-0.
- Newhauser, Richard, ed. In the Garden of Evil: The Vices and Culture in the Middle Ages. Pontifical Institute of Mediaeval Studies, Toronto 2005. ISBN|0-88844-818-X
Viungo vya nje
haririMakala bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |