Shaaban Robert (1 Januari 1909 - 22 Juni 1962) alikuwa mshairi na mwandishi wa riwaya. Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa kwani kazi zake zinaheshimika katika fasihi ya Kiswahili na pia zinatumika shuleni.

Maisha

Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 Januari 1909 katika kijiji cha Vibambani, jirani na Machui, kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga.

Wazazi wake wote wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Wayao, lakini hakujiita Myao kabisa, bali alikuwa mmojawapo wa wachache ambao daima walijiita Waswahili.

Kabla ya baba yake kuitwa Roberto [1], mwanzo alifahamika kwa jina la Ufukwe na jina hili lilitokana na Mzee Robert kuzaliwa karibu na ufukwe [2]. Jina la Roberto lilitokana na tajiri mmoja aliyekuwa amemuajiri baba yake (babu yake Shaabani Robert). Baada tu ya Shaaban Robert kuingia katika shule za Wazungu alibadili jina kutoka Roberto na kuwa Robert.

Alipata elimu yake katika shule ya Msimbazi, jijini Dar-es-Salaam kati ya miaka 1922 na 1926, akawa mtu wa pili katika wanafunzi kumi na mmoja waliofaulu mitihani yao na kupewa shahada ya kutoka chuoni, yaani School Leaving Certificate.

Akaajiriwa na serikali ya kikoloni akawa karani katika idara ya forodha huko Pangani miaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi hivi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Waswahili tena mahali patulivu kulisaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.

Tangu mwaka 1944 hata 1946 alihamia ofisi nyingine ya Hifadhi ya Wanyama, baadaye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga (tokea mwaka 1952 hata 1960).

Alipandishwa cheo kuwa Grade III Higher Division mwaka 1929, na katika mwaka wa 1944 akapandishwa tena kuwa Grade II Local Service.

Kwa ujumla Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na mbili. Baadhi ya vitabu hivi ni: Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini, Utubora Mkulima.

Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi.

Mbali na maandiko yake alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee, East Africa Literature Bureau na Tanganyika Languages Board. Alikuwa pia mwanachama wa Tanga Township Authority.

Alifariki dunia huko Tanga tarehe 22 Juni 1962 akazikwa Machui. Aliacha wake watatu na watoto watano, ingawa aliwazaa kumi. Mke wa kwanza alikuwa Mdigo. Pia aliacha dada yake (wa baba mmoja) Mwana Saumu, na mama yake.

Alituzwa kwa zawadi ya waandishi inayoitwa ‘Margaret Wrong Memorial Prize’; pia alikuwa ametuzwa nishani ya M.B.E.

Vitabu vyake

  • Mwafrika Aimba (1969), Nelson. Nairobi
  • Almasi za Afrika (1971), Nelson, Nairobi
  • Koja la Lugha (1969), Oxford, Nairobi
  • Insha na Mashairi (1967), Nelson, Nairobi
  • Ashiki Kitabu Hiki (1968), Nelson, Nairobi
  • Pambo la Lugha (1968), Oxford, Nairobi
  • Kielezo cha Fasili (1962), Nelson, Nairobi
  • Masomo Yenye Adili (1959), Art & Literature, Nairobi
  • Mapenzi Bora (1969), Nelson, Nairobi
  • Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam (1973), TPH, Dar-es-Salaam
  • Utenzi wa Vita vya Uhuru (1961), Oxford, Nairobi
  • Almasi za Afrika Na Tafsiri Ya Kiingereza (1960), Art & Literature, Nairobi
  • Mashairi ya Shaaban Robert (1971), Nelson, Nairobi
  • Sanaa ya Ushairi (1971), Nelson, Nairobi

Nathari

Tanbihi

  1. Robert, Shaaban, 1909-1962. (2004). Kielezo cha fasili. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers. ISBN 9976-973-15-2. OCLC 31497478.{{cite book}}: CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: numeric names: authors list (link)
  2. Robert, Shaaban, 1909-1962. (2004). Kielezo cha fasili. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers. ISBN 9976-973-15-2. OCLC 31497478.{{cite book}}: CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: numeric names: authors list (link)

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shaaban Robert kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.