Basil wa Caesarea

(Elekezwa kutoka Bazili Mkuu)

Basili wa Kaisarea (Kaisarea wa Kapadokia, leo Kayseri, nchini Uturuki, takriban 329 – Kaisarea wa Kapadokia, 1 Januari, 379) alikuwa mmonaki, halafu askofu wa mji huo (mkoa wa Kapadokia, leo nchini Uturuki).

Picha katika ukuta wa kanisa kuu la Ohrid inayomuonyesha Basili Mkuu akigeuza vipaji vya ekaristi.
Picha takatifu ya Kirusi ya Mt. Basili.

Ni mmojawapo kati ya Mababu wa Kanisa muhimu zaidi. Ndiyo sababu anaitwa Basili Mkuu (kwa Kigiriki Βασίλειος ο Μέγας).

Kwa jinsi alivyomkazia macho Kristo na kupenda watu, alianza kuheshimiwa kama mtakatifu punde baada ya kifo chake, na mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 2 Januari[1].

Maisha

hariri

Asili na ujana

hariri

Basili alizaliwa mwaka 329 hivi katika familia tajiri ya mhubiri maarufu Basili Mzee na ya Emelia wa Kaisarea huko Caesarea Mazaca. Wote wawili walijulikana kwa imani yao (Oratio 43.4, PG 36. 500B).

Familia yao ilikuwa na watoto 10, waliosaidiwa malezi na bibi wa Basili, Makrina Mzee. Babu yake alikuwa mfiadini. Wote wawili wanaheshimiwa kama watakatifu, kama vile Basili na watoto wengine 4: dada yake Makrina Kijana aliyekuwa mmonaki, na ndugu zake Petro wa Sebaste aliyekuwa askofu na mwanateolojia huko Armenia, Naukratio aliyekuwa mkaapweke, na hasa Gregori wa Nisa ambaye alifanywa na Basili kuwa askofu wa mji huo akaandika vitabu bora kuhusu teolojia na maisha ya Kiroho.

Basili alikuwa na vipawa vya pekee: akili kali, wema mkubwa, uwezo wa kupanga na kufanikisha mambo, nguvu katika utendaji, busara na kiasi katika yote. Ni kati ya wanakanisa kamili zaidi wa nyakati zote.

Bado mtoto alihamia mkoa wa Ponto hadi alipofiwa baba yake ambapo akarudi Kaisarea ili kupata wlimu. Huko alikutana na Gregori wa Nazianzo, akawa rafiki yake maisha yake yote.

Wote wawili walikwenda kusoma Konstantinopoli, halafu kwa miaka sita Athens, walipokutana na atakayekuwa kaisari Juliano Mwasi. Ndiko alikoanza kufikiria maisha ya Kikristo hasa. Hata hivyo hakuacha kutia maanani elimudunia, aliyokuwa nayo kwa wingi, hasa kwa ajili ya malezi ya vijana, ambao daima aliwashughulikia sana.

Kutokana na mang’amuzi yake kuhusu vitabu vya Wapagani wa zamani, alihimiza upambanuzi: “Tukiwa na hekima, tutachota katika maandishi hayo vile ambavyo vinatufaa na vinalingana na ukweli, na tutapuuzia vile vingine.”

Alipohama Athens mwaka 355 hivi, Basili alifanya kwa muda mfupi kazi ya wakili na mwalimu wa kuhubiri huko Kaisarea, lakini mwaka uliofuata alibadili maisha kisha kukutana na askofu Eustathius wa Sebaste.

Aliandika, “Siku moja, kama mtu aliyezinduka kutoka usingizi mzito, niligeuza macho yangu kwenye mwanga wa ajabu wa ukweli wa Injili… nikalia machozi mengi juu ya maisha yangu duni”. Hapo, kwa kuvutiwa na Yesu, alianza kumtazama na kumsikiliza yeye tu, akijitosa katika sala, tafakuri juu ya Biblia na maandishi ya mababu wa Kanisa, pamoja na kutekeleza upendo, kwa kufuata pia mfano wa dada yake, Makrina, aliyekwishashika maisha ya kimonaki.

Umonaki

hariri

Baada ya kupata ubatizo, Basili alisafiri tena (357) kwenda Misri, Palestina, Syria na Mesopotamia ili kufahamu zaidi maisha ya kiroho na umonaki.

Ingawa aliguswa na utakatifu wa wamonaki aliokutana nao huko, kipeo cha ukaapweke hakikumvutia zaidi. Badala yake alielekea maisha ya kijumuia. Hivyo baadaye alirekebisha umonaki usiwe mbali mno na watu wa kawaida, bali uathiri maisha yao kwa roho ya Kikristo.

Kiongozi halisi katika njia ya Mungu, hakuruhusu malipizi ya ajabuajabu, bali alidai utekelezaji wa matendo ya upendo.

Kisha kugawa mali zake kwa mafukara alikwenda kwa muda mfupi kuishi upwekeni karibu Neokaisaria mtoni Iris, lakini mwaka 358 alianza kupokea wafuasi, mmojawao ndugu yake Petro. Pamoja naye alianzisha monasteri huko Arnesi kwenye mkoa wa Ponto.

Huko walijiunga hata mama yake, dada yake Makrina na wanawake wengine, wakijitoa kusali na kutekeleza matendo ya huruma.

Ni huko kwamba Basili aliandika vitabu vyake kuhusu umonaki (Kanuni mbili) vilivyoathiri Kanisa lote hadi leo, hata akaitwa "baba wa umonaki wa mashariki". Benedikto wa Nursia mwenyewe, “baba wa umonaki wa magharibi”, alimhesabu kama mwalimu wake. Kwa jumla mfumo wa umonaki haueleweki bila kumsikiliza Basili.

Mwaka 358 alimualika Gregori wa Nazianzo ajiunge naye, halafu kwa pamoja walitunga Filocalia, mkusanyo wa maandishi bora ya Origen. Baadaye Gregori akarudi kwao.

Basili alishiriki Mtaguso wa Konstantinopoli wa mwaka 360 alipokubali neno "homoiousios" kama sahihi kuelezea Yesu ni "kama" Mungu Baba, si "sawa" wala si "tofauti" naye. Baada ya kulaumiwa na askofu wake, Dianius wa Kaisarea, aliacha mtazamo huo akashika moja kwa moja Kanuni ya imani ya Nisea.

Daraja takatifu

hariri
 
Picha takatifu ya Maaskofu watakatifu watatu: Basili Mkuu (kushoto), Yohane Krisostomo (katikati) na Gregori wa Nazianzo (kulia) kutoka Lipie, Historic Museum huko Sanok, Poland.

Mwaka 362 Basili alipewa daraja takatifu ya ushemasi kwa kuwekewa mikono na askofu Meletius wa Antiokia.

Aliitwa na Eusebius arudi kwao, akapewa upadirisho mwaka 365.

Miaka iliyofuata Basili na Gregori walishindana na uzushi wa Ario ulioenea Kapadokia. Katika midahalo wakawa washindi.

Hivyo Basili alikabidhiwa usimamizi wa mali ya dayosisi ya Kaisarea. Eusebius akamuonea kijicho akamruhusu arudi upwekeni. Lakini Gregori alimshauri arejee tena na kushika nafasi yake kama kiongozi halisi wa jimbo hilo.

Mwaka 370 Eusebius alifariki, na Basili alichaguliwa mwandamizi wake akapewa uaskofu tarehe 14 Juni 370. Kama askofu wa Kaisarea akawa pia askofu mkuu mwenye majimbo 5 chini yake.

Hapo alikataa katakata mashinikizo ya Kaisari aliyetaka aunge mkono uzushi wa Ario, kinyume chake alijitahidi kurudisha umoja ndani ya Kanisa na kutetea haki ya kushika imani ya kweli kuhusu umungu wa Yesu.

Alitetea pia umungu wa Roho Mtakatifu ambaye aliandika kitabu kizima juu yake: “lazima alinganishwe na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana”. Hivyo Basili ni kati ya mababu walioweka wazi fundisho la Utatu Mtakatifu: Mungu pekee, kwa kuwa ni upendo, ni nafsi tatu zinazounda umoja wa Kimungu, imara kuliko umoja wowote.

Pamoja na kuchunga kiroho waamini wa jimbo lake kubwa, na kujitahidi kuleta watu wote kwa Kristo, alizingatia mahitaji ya kimwili ya kila mmoja, akajitosa kwa ajili ya maskini, wezi na makahaba, akihimiza watawala kuinua hali ya wananchi hasa wakati wa maafa, na akilaumu hadharani walioshindwa kutoa hukumu kwa haki.

Alianzisha mtaa wenye majengo kwa ajili ya mafukara, wageni na wagonjwa, uliokuja kuitwa Basiliade. Ulikuwa na hospitali, shule na viwanda.

Hata katika makanisa mengine yaliyokuwa chini yake alianzisha makimbilio kwa shida yoyote ile.

Kama askofu, alianzisha maisha ya pamoja katika “jamaa” kwa lengo la kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni.

Tofauti na monasteri za Pakomi, zilizofikia kuwa na watawa elfu, jamaa hiyo haikuwa na idadi kubwa wala ngome; tena haikuwa jangwani, bali karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia.

Akiwa askofu huko alitembelea mara nyingi jamaa hizo akisisitiza, pamoja na maendeleo ya kiroho, uhusiano na Kanisa lao: alitaka watawa wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wote wafuate utakatifu wa wito wao. Tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama vile kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida.

Mtindo huo ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa.

Tofauti na unyofu wa wamonaki wa jangwani, alitia maanani masomo ya kidini, na hasa maandishi ya Origene.

Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu monasteri zote za mashariki, na kwa njia hiyo makanisa ya Kiorthodoksi kwa kuwa kwao maaskofu kwanza ni wamonaki, nao wanaelekeza Wakristo wote kufuata mifano yao.

Mhubiri mwenye nguvu, alishambulia uroho wa matajiri na ulegevu wa Wakristo wasiotimiza wajibu wao.

Pamoja na kuwajibika mfululizo kutekeleza matendo ya huruma, alirekebisha pia liturujia ya Ekaristi na kustawisha matumizi ya Zaburi kati ya waamini, kiasi kwamba walizisali hata usiku; na kuhimiza waamini wapokee kila siku Ekaristi, chakula wanachohitaji ili kupata nguvu mpya ya kuishi kikamilifu kadiri ya neema ya ubatizo. Alisema ni furaha kubwa kuweza kushiriki Ekaristi iliyowekwa “ili kudumisha bila kikomo kumbukumbu ya Yule aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu”.

Alipanga maisha ya Kanisa bila kukubali serikali iyaingilie.

Alipodaiwa na mjumbe wa Kaisari Valens alegeze msimamo wake dhidi ya Ario, Basili alimjibu, "Labda wewe hujawahi kuhusiana na askofu yeyote." Baada ya jibu hilo kwa Kaisari alikwenda kushiriki misa yake akampe eneo kwa ajili ya Basiliade. Tukio hilo lilisaidia kuonyesha mipaka kati ya mamlaka ya serikali na ile ya Kanisa.

Basili aliwasiliana pia na Papa Damaso I ili Kanisa la Roma litumie mamlaka yake kulaani uzushi wa Ario,mashariki kama magharibi.

Lakini hakuishi kirefu kutosha aone ushindi wa imani sahihi aliyotetea. Juhudi zake kubwa za kutimiza vizuri wajibu wake kama askofu zilimmaliza tarehe 1 Januari 379, akiwa na umri wa miaka 49 tu.

Katika Kanisa alitekeleza kiaminifu mpango alioufanya mapema, wa kuwa “mtume na mtumishi wa Kristo, msimamizi wa mafumbo ya Mungu, mtangazaji wa Ufalme, kielelezo na kipimo cha uadilifu, jicho la Mwili wa Kanisa, mchungaji wa kundi la Kristo, mwalimu, baba na tabibu mpendevu, mfanyakazi pamoja na Mungu, mkulima wa Mungu, mjenzi wa hekalu la Mungu”.

Mafundisho yake

hariri

Mwanga wa fumbo la Mungu unarudishwa na binadamu aliye sura yake; ni hasa kwa kumtazama Kristo kwamba tunaweza kutambua hadhi yetu. “Zingatia ukuu wako, ukikumbuka ulivyogharimiwa: tazama bei ya ukombozi wako na kuelewa hadhi yako!”

Kwa namna ya pekee Wakristo wakijilinganisha na Injili, wanapaswa kuwatambua watu wote kama ndugu, tena kujiona wasimamizi wa mali waliyojaliwa ili wawajibike kila mmoja kwa ajili ya wenzake, “wakitekeleza maagizo ya Mungu mfadhili”. “Macho ya mafukara wote yanaelekea mikono yetu kama vile ya kwetu yanavyoelekea ile ya Mungu tukiwa na shida”.

Kuhusu hilo alitumia kishujaa maneno makali katika hotuba zake, kwa sababu anayetamani kumpenda jirani kama anavyojipenda, kadiri ya amri ya Mungu “hatakiwi kuwa na mali yoyote kuliko jirani yake”. Hasa wakati wa maafa alihimiza waamini wasiwe “wakatili kuliko hayawani… kwa kujipatia vile ambavyo wote wanamiliki kwa pamoja au kwa kuteka vitu vilivyo mali ya wote”.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107

Maandishi yake

hariri
  • On the Holy Spirit
  • Refutation of the Apology of the Impious Eunomius
  • Refutation (vitabu 3 vya kwanza tu)
  • Hexaëmeron
  • Ufafanuzi wa Zaburi
  • Moralia
  • Asketika
  • Barua 300
  • MT. BASILI WA KAISARIA, Kanuni za kimaadili – tafsiri ya Familia za Maamkio – Mapanda - ed. Ndanda Mission Press – Ndanda 2005 – ISBN 9976-63-674-X

Vyanzo

hariri
 
Basilii Magni Opera, 1540

Kwa Kiswahili

hariri

•PADRE FRIDOLIN, Maisha ya Mtakatifu Makrina - ed. N.M.P. - Ndanda

Kwa lugha ntyingine

hariri
  • Bebis, George (Fall–Winter 1997). "Introduction to the Liturgical Theology of St Basil the Great". Greek Orthodox Theological Review. 42 (3–4): 273–285. ISSN 0017-3894. {{cite journal}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)CS1 maint: date auto-translated (link) CS1 maint: date format (link)
  • The New Encyclopaedia Britannica, 15th edition, v. 1. London: Encyclopaedia Britannica. {{cite book}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)
  • Keary, Charles Francis (1882). Outline of Primative Belief Among the Indo-European Races. New York: C. Scribner's Sons. {{cite book}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)
  • Murphy, Margaret Gertrude (1930). St. Basil and Monasticism: Catholic University of America Series on Patristic Studies, Vol. XXV. New York: AMS Press. ISBN 0-404-04543-x. {{cite book}}: Check |isbn= value: invalid character (help); Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)
  • Quasten, Johannes (1986). Patrology, v.3. Christian Classics. ISBN 0-87061-086-4. {{cite book}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)
  • Silvas, Anna M. (2002). "Edessa to Cassino: The Passage of Basil's Asketikon to the West". Vigliae Christianae. 56 (3). Brill Academic: 247–259. doi:10.1163/157007202760235382. ISSN 042-6032. {{cite journal}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help); Unknown parameter |month= ignored (help)
  • Corona, Gabriella, ed. (2006). Aelfric's Life of Saint Basil the Great: Background and Content. [1] Anglo-Saxon Texts 5. Cambridge: D.S. Brewer. ISBN 9781-84384-095-4. {{cite book}}: |first= has generic name (help); Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help); External link in |title= (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)

Viungo vya nje

hariri