Sala na kazi
Sala na kazi (kwa Kilatini ora et labora, "sali na kufanya kazi") ni kaulimbiu ya wamonaki Wabenedikto iliyoenea katika Kanisa kuanzia karne za kati hadi leo.[1]
Benedikto wa Nursia alitambua kwamba sala na kazi zinatakiwa kusaidiana katika maisha ya binadamu[2], kwa kuwa mwenyewe ni umoja wa roho na mwili.
Lengo ni kufikia maisha ya sala, yaani kuendelea kuwasiliana na Mungu hata wakati wa kufanya kazi mbalimbali.
Kufikia maisha ya sala
haririKwa kuwa sala inaitegemea neema, tunajiandaa kwa unyenyekevu kuliko kwa matendo mengine: “Amin, nawaambia: Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Math 18:3), hasa katika undani wa ufalme huo kwa maisha ya sala. Wanyenyekevu wa moyo wanafundishwa na Mungu mwenyewe. Wakipenda kutokuwa kitu, tena wakikubali dharau hata kuzifurahia, watapiga hatua kubwa na kujazwa mema mengi kuliko yale yote waliyoyatamani.
Baada ya unyenyekevu, tunajiandaa kwa ufishaji, yaani roho na matendo ya kujitenga na viumbe pamoja na umimi wetu. Tukihangaikia shughuli au kuvurugwa na mapendo ya kibinadamu mno, wivu, kumbukumbu ya makosa tuliyotendewa, na hukumu zisizo za haki dhidi ya jirani, hatutaweza kuongea na Bwana. Ikiwa mchana tunawasema wakubwa wetu na kutowasikiliza, jioni hatutamuona katika sala. Maelekeo yote yasiyofaa yafishwe ili upendo utawale rohoni mwetu na kumuinukia Mungu katika tabu na faraja vilevile.
Ili tuyafikie maisha ya sala tunatakiwa kuinua mara nyingi moyo wetu kwa Mungu, kuongea naye kuhusu lolote, kama tunavyoongea na mtu anayetuongoza kupanda mlima. Tukifanya hivyo, tutakaposimama ili kuongea naye kwa dhati zaidi, tutakuwa na neno la kumuambia na hasa tutajua kusikiliza minong’ono yake kwa sababu tumezoeana naye kitakatifu.
Hatimaye tunapaswa kuwa na kimya rohoni, kunyamazisha maono yasiyoratibiwa ili kumsikiliza mlezi wa ndani anayesema kwa sauti ya chini, kama mtu na rafiki yake. Ikiwa kwa kawaida tunajijali mno, tunajifanya lengo la kazi, la masomo na la utendaji wowote, tutawezaje kuonja utamu wa fumbo la Utatu Mtakatifu uliomo ndani mwetu, la umwilisho ulioleta ukombozi, na la ekaristi? Ni lazima fujo za hisi zikome: ndiyo sababu katika usiku wa hisi Bwana anazijaribu vikali ili zinyamaze na kuitii roho.
Kazi hizo zote zinaitwa maandalizi ya mbali ya sala. Ni muhimu kuliko maandalizi ya jirani (yaani kuchagua la kuzingatia katika sala) kwa kuwa lengo la hayo ya mwisho ni kuchochea tu huo moto wa upendo ambao hautakiwi kamwe kuzimika ndani mwetu bali kulishwa kwa bidii ya kutimiza kiaminifu wajibu wa kila nukta. Upande huo inafaa sala wakati wa kazi, yaani kujichagulia kama robo saa wakati wa kazi ya akili au ya mwili, si kwa kuisimamisha, bali kuifanya kitakatifu zaidi. Zoezi hilo litatuletea faida kubwa: tutaacha kujifanya lengo la kazi, tukifuata umbile tu na umimi, na tutaitakasa kwa kudumisha muungano na Mungu, tukiweka nguvu zetu zote katika kumtumikia badala ya kujiridhisha nayo. Hivyo kwa bidii na unyofu tutakuja kulingana na matakwa ya Mungu, na kumkumbuka karibu mfululizo. Jambo hilo litafanya maandalizi ya jirani ya sala yasihitajike sana, kwa kuwa tutajikuta tayari na kumuelekea Mungu kama jiwe linavyoelekea ardhi likiachwa hewani. Hivyo tutafikia maisha ya sala ambayo yatakuwa kama pumzi ya roho yetu.
Kudumu katika maisha ya sala
haririFaida ya udumifu ni kubwa, kumbe tusipodumu tunaweza tukapoteza yote. Kudumu si rahisi: ni lazima tupambane na nafsi yetu, uzembe na shetani anayetuelekeza kukata tamaa. Wengi wanarudi nyuma wanapoachishwa faraja walizojaliwa kwanza; hata wanaoendelea wanaweza wakarudi nyuma. Katerina wa Genoa, baada ya miaka mitano ya uchungu, aliacha maisha ya Kiroho kwa miaka mitano mpaka Mungu alipomvuta tena kwa nguvu wakati wa kitubio. Hapo kwa miaka kumi na nne ya malipizi makali alitoa fidia kamili akasema, “Ningerudi nyuma ningekubali kung’olewa macho, tena ningeona hata hilo si kitu”. Maneno kama hayo yanasisitiza kwamba ni afadhali kupofuka kuliko kupoteza neema inayotia utakatifu au hata kurudi nyuma katika njia ya milele. Hiyo ni wazi kwa mtu anayeelewa thamani ya uzima wa milele kulingana na maisha haya yanayopita.
Kuna watu waliopambana muda mrefu halafu wakakata tamaa wakiwa wameikaribia chemchemi. Hapo, pasipo sala, hawana tena nguvu ya kubeba kwa moyo msalaba wao, wanajiachia kuishi kijuujuu na kuingia hatari ya kupotea. Kuna watu wenye akili nyingi na tabia kali wasioweza kubaki katika wastani: ama watakuwa wa Mungu katika njia ya utakatifu ama watajiabudu, kwa mfano wa malaika ambaye ama ni mtakatifu ama ni mwovu tu. Hasa kwao ni muhimu wadumu katika sala inayoweza kuwatia roho ya kitoto, la sivyo watapuuzia maisha ya Kiroho na kutumia nguvu zao zote kwa kiburi wajifanye lengo la kazi na masomo yao.
Basi, ili kudumu katika sala, yanahitajika mawili: kumtumainia Bwana anayealika wote kwenye maji hai ya sala, na kukubali kwa unyenyekevu atuongoze kwenye njia aliyotuchagulia.
Kwanza tunapaswa kumtumainia. Ni kosa kusema, baada ya muda mrefu wa ukavu, “Sala si kwa ajili yangu”, au, “Mimi sifai kusali”. Kwa msingi huo tungeweza kusema vilevile, “Kupokea ekaristi mara nyingi si kwa ajili yangu, ila kwa watakatifu wachache tu”. Kumbe Bwana anaita wote kuwa marafiki wake wa ndani.
Anajifananisha na mchungaji mwema anayewaongoza kondoo zake kwenye malisho ya milele, yaani Neno la Mungu. Katikati yake kuna chemchemi ya maji yaliyo hai ambayo Yesu alimzungumzia mwanamke Msamaria tena mkosefu. Chemchemi hiyo ndiyo Roho Mtakatifu tunayepewa pamoja na upendo unaotuunganisha naye. Tumepewa awe mlezi wa ndani na mfariji wetu ambaye atupenyeze na kutuonjesha maana ya dhati ya Injili. “Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yoh 14:26). Ahadi hiyo ilitimizwa siku ya Pentekoste, na kwa kila mmojawetu kwa kiasi chake siku ya kipaimara. Mtume Yohane aliandikia waamini wa kawaida, “Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote… Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake” (1Yoh 2:20,27). Roho Mtakatifu hakai ndani mwetu ili kupumzika bali afanye kazi kwa vipaji vyake. Basi, tusipoelewa vizuri minong’ono yake ni kwa sababu tunajisikiliza mno na kutokuwa na hamu ya kutosha ya ufalme wa Mungu kutia mizizi ndani mwetu.
Pili, tukubali kuongozwa kwenye njia aliyotuchagulia. Njia ya unyenyekevu na kuambatana na matakwa ya Mungu ni ya lazima; sisi sote tunapaswa kusali kama mtozaushuru. Lakini katika njia hiyo sehemu ina kivuli, sehemu inapigwa na jua; sehemu ni tambarare, sehemu ina mipando mirefu ya kuchosha inayofikisha juu inapofurahiwa mandhari nzuri ajabu. Mchungaji mwema anaongoza kondoo zake anapoona ni afadhali. Anaongoza wengine kwa mifano; wengine kwa mifuatano ya mawazo. Anawajalia wengine katika giza la imani wahisi kwa unyofu na undani mapana ya hekima; anaacha wengine mahali pagumu kwa muda mrefu ili kuwazoesha: kwa miaka mingi Teresa wa Yesu alilazimika kutafakari kwa msaada wa kitabu, na muda huo alikuwa akiuona mrefu mno. Bwana anawainua akina Maria kuliko akina Marta kwenye sala ya kumiminiwa, lakini hao wa kwanza wanakuta humo mateso ya ndani ambayo wa pili hawayajui, nao pia, wakiwa waaminifu, watayafikia maji yaliyo hai na kuburudika wanavyotamani.
Kama hatufurahii malimwengu bali juhudi zetu zinaelekea maendeleo ya Kiroho, hapo ukavu wa muda mrefu unafaa kwa kuwa hautokani na uvuguvugu. Kama vile moto unavyokausha ukuni kabla ya kuuwasha, ukavu huo ni wa lazima kwa kukausha hisi zetu zinazoleta vurugu, ili hatimaye zitulie chini ya roho, na upendo safi na wa nguvu ustawi juu ya maono. Hapo, tukiwa waaminifu, tutaanza polepole kumtazama Mungu katika kioo cha vitu vinavyoonekana au cha mifano ya Injili. Pengine tutamtazama katika kioo cha mafumbo ya wokovu, k.mf. tukitumia rozari. Hatimaye tutamtazama mwenyewe katika giza la imani kwa kuzingatia wema wake usio na mipaka unaotushirikisha mema yote; tutaanza kumfikiria daima akiwa ndani mwetu na kuhusisha yote naye. Hapo katika matukio yoyote, hata yale yasiyotarajiwa na ya tabu, tutakumbuka utukufu wa Mungu na kuchungulia wema mkuu ambao yote yanatakiwa kuulenga. Ndiyo maisha ya sala ambayo kwa namna fulani yanawezesha kuona yote ndani ya Mungu na ni utangulizi wa kawaida wa uzima wa milele.
Tanbihi
hariri- ↑ Anselm Grün, Linda M. Maloney (2006). Benedict of Nursia 2006 ISBN 0-8146-2910-5 page 30
- ↑ Lonni Collins Pratt, Daniel Homan (2001). Benedict's Way: An Ancient Monk's Insights for a Balanced Life ISBN 0-8294-1787-7 page 47
Marejeo
hariri- Ora et labora: prayer and action as cooperation with God by Robert Field, University of the South, 1993
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sala na kazi kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |