Ufalme wa Merina ni mlolongo wa watu ambao waliwahi kuwa watawala wa Bukini (sasa inafahamika zaidi kama Madagaska) katika kipindi cha miaka themanini kuanzia mwaka 1787 hadi mwaka 1897.

Bendera ya Ufalme wa Merina
Nembo ya Ufalme wa Merina

Watawala hao walikuwa watu kutoka familia ya Andrianampoinimerina, mwanzilishi wa taifa hilo ambaye alikuwa ametokea katika kabila la Wamerina ambalo ndilo lilikuwa kabila lilioenea sehemu kubwa ya Bukini.

Watawala hao wa kifalme waliweza kutekeleza mambo mbalimbali kuendeleza Bukini katika vipindi vyao kabla ya kuja kwa utawala wa kigeni wa Uingereza na Ufaransa ambao kwa kiasi fulani ulidhoofisha mamlaka ya kifalme.

Utangulizi

hariri

Bukini ya karne ya 19 ilikuwa na jumla ya makabila 18. Kabila la Wamerina ndilo lililokuwa kubwa na muhimu kuliko yote. Kabila hilo lilikuwa na makazi yake katika uwanda wa juu wa kati.

Idadi ya watu katika kundi hilo ilikuwa ni moja ya sita tu ya watu wote wa Bukini, lakini ndio lililotawala kisiwa cha Bukini kabla ya kuchukuliwa na Wafaransa.

Makabila yote ya Kimalagasi (wenyeji wa Bukini) yalizungumza lugha moja na yalikuwa na mila na desturi zinazofanana, hivyo yaliweza kujenga umoja wa kiutamaduni uliowafanya wawe jamii moja kimsingi.

Wamerina waliweka makao makuu ya utawala wao mjini Antananarivo; kutoka hapo waliweza kueneza mamlaka yao katika sehemu nyingine za kisiwa hicho.

Mfalme Andrianampoinimerina (1787-1810)

hariri
 
Mfalme Andrianampoinimerina (1787-1810)

Andrianampoinimerina alikuwa muasisi wa ufalme wa Merina ambaye alipata madaraka yake na kuimarisha nafasi yake katika uwanda wa juu wa kati katika karne ya 19.

Mwaka 1875, Andrianampoinimerina alijipa madaraka ya kuwa mfalme wa mojawapo ya falme zilizokuwa zikipigana vita katika Imerina ya kati baada ya kumpindua mtawala aliyepita. Kwa kutumia mbinu za kidiplomasia na za kijeshi aliendelea kuzichukua tawala za jirani katika himaya yake.

Mnamo mwaka 1792 aliuhamishia mji mkuu wake huko Antananarivo, ambapo alianza kujenga mifumo ya kisiasa na ya kijamaa ya ufalme mpya.

Baada ya mwaka 1800 alianzisha sera ya kuyapiga vita majimbo mengine visiwani humo kwa nia ya kuyaunganisha makabila yote 18. Katika kutimiza jukumu hilo, alikabiliana na upinzani wa hali ya juu kutoka kwa makabila mengine kisiwani humo kama vile Wasakalava, Wabezanozano na Waambongo.

Hata hivyo, wakati wa kifo chake hapo 1810, Andrianampoinimerina alikuwa ameifanya tayari Imerina kuwa pengine ufalme wenye nguvu zaidi kuliko falme zote katika kisiwa cha Bukini.

Mfalme Radama I (1810-1828)

hariri
 
Mfalme Radama I (1810-1828)

Mfalme Radama alirithi kiti cha ufalme mwaka 1810 akiwa na umri wa miaka 18. Jukumu lake la kwanza kabisa baada ya kushika ufalme lilikuwa kuyapiga makundi ya ndani ya ufalme huo yaliyoasi.

Hata hivyo, mafanikio yake makubwa zaidi yalihusiana na upanuaji wa mipaka. Alitafuta njia moja kwa moja hadi baharini ili kufanikisha biashara baina yake na Wazungu na kuupanua utawala wa Merina.

Jeshi lake si tu kuwa lilitumika kuyapiga majimbo mengine, bali pia kudumisha sheria na utulivu katika maeneo yaliyotekwa.

Hadi mwaka 1825, Radama alikwisha kuliteka eneo lote la pwani ya mashariki ya Bukini, kuanzia Vohema hadi ngome ya Dauphin. Aidha aliishinda sehemu kubwa ya magharibi, ila ilikuwa vigumu kuiteka Sakalava.

Pamoja na hayo yote, hadi mwaka 1823 Radama aliweza kuupanua utawala wa Merina katika sehemu kubwa sana ya kisiwa hicho. Ingawa utawala wake katika kisiwa hicho chote haukukamilika, hakukuwa na kipingamizi chochote kikubwa dhidi ya kujitangaza kwake kuwa mfalme wa Bukini.

Alifariki mwaka 1828 akiwa na umri wa miaka 36.

Malkia Ranavalona I (1828-1861)

hariri
 
Malkia Ranavalona I (1828-1861)

Malkia Ranavalona I alikuwa binamu na mke wa kwanza wa Radama I. Kwa kuwa alisaidiwa kupata umalkia na makabila na wakuu wa majeshi ambao Radama aliwaondoa madarakani katika harakati zake za kukijenga kisiwa hicho upya, washauri wake walikuwa watu waliozipinga sera muhimu za mfalme aliyefariki.

Mkazo wa sera za Ranavolona ulikuwa kuulinda uhuru wa Bukini dhidi ya athari za kigeni, hasa zile zilizoathiri asasi za kitaifa, mila na desturi. Kuhusu sera ya mambo ya nje, aliegemea zaidi katika kuitoa nchi yake kutoka kwenye athari za Waingereza, hasa katika nyanja za siasa na dini.

Malkia Ranavalona aliendelea na upanuzi ambao Radama I aliuanzisha na kuuimarisha utawala wake katika majimbo aliyoyateka. Kabila la Wasakalava liliendelea kuupinga utawala wake.

Hatimaye majeshi ya serikali yalipowashinda machifu wa Sakalava, walikimbia na watu wao na kwenda kwenye visiwa vya jirani ambapo walijiweka kwenye hifadhi ya Wafaransa. Hali hiyo baadaye ilikuwa ndiyo msingi wa madai ya Wafaransa kwa majimbo yaliyoko magharibi mwa Bukini.

Utawala wake unaweza kuelezwa katika namna mbili. Kwa upande mmoja, ulikuwa ni utawala wenye vitisho kwa wamisionari na watu wengine waliotekwa na kuwa chini ya utawala wa Kimerina. Kwa upande mwingine, ulikuwa kipindi cha maendeleo makubwa ya viwanda, na ambacho kiliimarisha elimu ya Kizungu na kuiweka nchi katika mwelekeo wa usasa.

Kwa jumla, kwa raia zake wengi, Ranavalona alikuwa ishara ya utaifa wa Kimalagasi.

Ranavalona alifariki mwaka 1861 baada ya kumtangaza Rakoto Radama kuwa ndiye atakayetawala baada yake.

Mfalme Radama II (1861-1863)

hariri
 
Mfalme Radama II (1861-1863)

Shughuli za mfalme Radama II zilielekezwa katika kuzibadilisha sera zote zilizokuwa zinapinga mambo yaliyoletwa na Wazungu ambazo mfalme aliyetangulia alikuwa akizitumia. Mwelekeo huo ulisababisha upinzani mkubwa dhidi ya utawala wake kutoka kwa watu mashuhuri nchini humo, hali iliyosababisha kuanguka kwake.

Sera ya mfalme ya kusaini mikataba ya siri bila ya maofisa wake kufahamu iliongeza mashaka zaidi kwa viongozi hao. Zaidi ya hayo, kuongezeka kwa athari za wamisionari na Wazungu wengine kitalani kwa mfalme hakukusaidia kitu.

Jambo lililommaliza kabisa ni jaribio lake la kuwaondoa baadhi ya maafisa waandamizi wa nchi ambao ndio walikuwa uti wa mgongo wa serikali yake na badala yao kuwaweka marafiki wake wa ujanani. Hili lilifufua mlolongo mrefu wa malalamiko dhidi ya mfalme, na tarehe 12 Mei 1863 akauawa.

Utawala wa Kibaraka (1863-1880)

hariri
 
Malkia Rasoherina (1863-1868)
 
Malkia Ranavalona II (1868-1883)
 
Malkia Ranavalona III (1883-1897)

Baada ya kifo cha Radama II, madaraka halisi ya serikali ya Bukini yaliingia mikononi mwa maofisa wakuu wa utawala, ambao walimtawaza Malkia Rasoherina kama mtawala kibaraka.

Malkia Rasoherina alitawala kuanzia mwaka 1863 mpaka 1868 na kufuatiwa na Malkia Ranavalona II (1868-1883). Watu hao hawakupinga uendelezaji wa nchi wala hawakuwachukia Wazungu. Sera yao ya nje ililenga uhuru wa nchi yao kwa imani kwamba uendelezaji wa nchi kulingana na wakati usifanywe kwa namna itakayoua mila za Kimalagasi. Hivyo, serikali mpya iliazimia kufanya marekebisho muhimu katika sera za Rahama.

Uingereza na Ufaransa zilipokea taarifa za kupinduliwa kwa Radama na mapendekezo ya mabadiliko ya sera ya mambo ya nje ya Bukini kwa hisia tofauti.

Hitimisho

hariri

Pamoja na yote hayo, kisiwa hicho hatimaye kiligeuzwa kuwa koloni. Hii ni kwa kuwa, ingawa sera ya kuisasisha ya Bukini kwa namna fulani iliimarisha uwezo wa nchi hiyo wa kutetea uhuru wake, lakini kwa ujumla sera hiyo ilidhoofisha ufalme huo kwa kuongeza utegemezi wake kwa mataifa ya kigeni.

Marejeo

hariri
  • Rebecca L. Green: Merina. The Rosen Publishing Group, New York, 1997, ISBN 0-823-91991-9 (The heritage library of African peoples). Google Books
  • Matthew E. Hules, et al (2005). The Dual Origin of the Malagasy in Island Southeast Asia and East Africa: Evidence from Maternal and Paternal Lineages. American Journal of Human Genetics, 76:894-901, 2005.
  • Mervyn Brown (2000). A History of Madagascar. Princeton: Markus Wiener Publishers. ISBN 1-55876-292-2.
  • Stephen Ellis and Solofo Randrianja, Madagascar – A short history, London, 2009
  • Brown, M. (1978) Madagascar Rediscovered: A History from Early Times to Independence (London: Damien Tunnacliff)
  • Campbell, G. (1981) Madagascar and slave trade, 1850-1895, JAH

Viungo vya nje

hariri