Hassan bin Omari (au Makunganya[1]; alifariki 26 Novemba 1895) alikuwa Myao Mwislamu wa Makanjila, aliyeishi mlimani, na aliyefanya biashara ya pembe za ndovu na ya watumwa, na pia kushambulia misafara iliyopita katika eneo lake la Mavuji, karibu na Kilwa Kivinje. Baada ya kupigana na Wajerumani alikamatwa, na mwishowe alinyongwa na Wajerumani, pamoja na wenzake.

Hassan bin Omari

Hassan bin Omari (aka Makunganya), kulia, Omari Muenda, katikati na Jumbe, kushoto
Amekufa 26 Novem 1895
Nchi Tanzania
Kazi yake mfanyabiashara

Kufahamu asili yake ni kuelewa sababu za uasi wake dhidi ya Wajerumani wa Afrika Mashariki wakati huu, pamoja na wengine dhidi ya Waingereza katika bara la Afrika. Hatuna maandiko mengi zaidi ya kihistoria ya wakati huu ila yale ya wazungu waliotawala nchi. Asili ya Hassan bin Omari katika watu wa kabila ya Makanjila Yao[2] ambao, kufikia karne ya 19, walikuwa wasimamizi wa njia kuu ya misafara ya biashara kutoka nchi za Nyasa na majirani ya mto wa Zambezi, mpaka pwani ya kusini ya Tanzania ya leo, hasa mji wa Kilwa Kivinje, kilomita 25 kaskazini mwa Kilwa Kisiwani, ambapo watu wengi Wayao walikuwa wamekwisha kuanza kuishi. Kilwa Kivinje ilikuwa bandari kuu ya usafirishaji wa watumwa na wa bidhaa mbali mbali katika eneo la Kilwa wakati wa utawala wa Omani na Ujerumani.

 
Deutsch Ostafrika

Makanjila Yao

hariri

Hassan bin Omari alishirikiana na watu Wayao wengine katika mapigano ya 1888. Pia, idadi kubwa ya Wayao katika karne hiyo tayari walifuata dini ya Uislamu. Biashara enyewe baina ya Uyao na Kilwa, pamoja na baina ya nchi za kusini mbele ya kisiwa cha Msumbiji, ilianza kabla karne ya 17. Misafara ya biashara hii ilifika Kilwa kila mwaka kuleta pembe za ndovu, watumwa na bidhaa zingine.[3]

"Historia ya Kilwa Kivinje" tunaambia kwamba Wayao walikuwa watu wa bara wa kwanza kukaa katika Kilwa Kivinje[4].

Makanjila III, mfalme wa Mangochi Nyasa mnamo 1870, alikaribisha Uislamu kuwa dini yake binafsi, na ya baraza yake. Pamoja na viongozi wengine Wayao, walihusika sana kukamata watu wa makabila majirani na kuwatia utumwani. James Frederic Elton mnamo Septemba, 1877 alisimulia kwamba Makanjila ni "... chifu mkuu wa biashara ya watumwa katika pwani ya mashariki ya Nyasa". Aliendelea kusema, aliona "nchi iliyolimwa vizuri ... na nyumba zilizojengwa kwa uangalifu sana... Mkuu mwenyewe anaye veranda na 'baraza' ya ukubwa kupita nyumba nyingi za Zanzibar".[5] Pia, Makanjila alionyesha heshima ya Sultani wa Zanzibar, kama aliyemwambia Johnson mnamo 1890, "Wazungu wangekuja kutwaa nchi ya Sultani wa Zanzibar, mimi, Makanjira, nitamwokoa!"[6]

Lakini, katika karne ya 19, vikosi vya Ujerumani na Uingereza vilipigana na wenyeji wengi kwa sababu ya kuondoa biashara hii ya utumwa mpaka mwisho, biashara ambaye ilikuwa ya faida kubwa kwa watu kama Wayao. Wakati ule ule wa kutua Wajerumani kwa pwani ya Afrika Mashariki mnamo 1888 kutweka bendera zao, na manowari za Ujerumani na zingine za Ulaya zilizolinda miji ya pwani, Wayao waliteswa na kampuni na vikosi vya Uingereza dhidi eneo lao katika mkoa wa Nyasa. Harry Johnston, pamoja na kikosi chake cha wanajeshi wa Sikhi na wa Zanzibar, kwa maneno yake akajulisha kwamba "ongezeko kubwa la nguvu nilizonazo ziliniwezesha, katika msimu wa vuli wa 1893, kutekeleza ushindi kabisa wa Makanjira. Tulimfukuza kwanza kutoka pwani ya magharibi ya ziwa...na kisha kumshambulia katika nchi yake na kuteka kila moja ya miji yake kwa mfululizo".[7]

Tunaweza kutambua pia kwamba Makanjila, wakati huu, alikuwa Mwenchande Salimu ambaye, baada ya kushindwa mikononi mwa Johnston, alikimbilia "Mwembe kwa rafiki yake Che Mataka, mwenzake; baadaye alijiunga na Che Makunganya mrimani(ambapo alikaa) hadi mnamo 1914 aliporudi."[8] Angalifika pwani mnamo 1894 au 1895, angekuwa pamoja na Makunganya, yaani Hassan bin Omari, wakati huo.

Uasi wa Kilwa Kivinje wa 1888

hariri

Kufuatana na Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki (Kijerumani: Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft (DOAG)) kupata haki mwezi wa Aprili, 1888, ya kumiliki forodha na biashara ya pwani mkabala na Zanzibar, na usimamizi wa eneo lile badala ya Sultani wa Zanzibar, kampuni hii ilifanya harakati kuanza kumiliki bandari zote muhimu, pamoja na Kilwa Kivinje, mwezi wa Agosti 1888. Watu wa kampuni hii walishuka katika miji muhimu yote ya pwani kutweka bendera ya kampuni badala, au pamoja na ya ile ya Sultan wa Zanzibar. Lakini, baada ya siku chache, kero ya watu iliyokuwepo hapo awali ilibadilika kuwa michafuko mikubwa katika miji ya pwani, kama Pangani, Saadani na Bagamoyo.[9] Ingawa huitwa "Uasi wa Kiarabu" (Kijerumani: Araberaufstandes), ni wazi kwamba uasi huo ulijumuisha idadi kubwa ya watu wa asili, haswa Wayao katika eneo la Kilwa. Septemba mwaka ule, katika Kilwa Kivinje, baada ya liwali wa Sultani aliondoshwa, watu walishika silaha mikononi na waliwaambia maafisa wa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki kushusha bendera yao na kuacha Kilwa. Walipokataa, maafisa ya kampuni, Heinrich Hessell na Gustav Krieger, walizingirwa katika boma siku kadhaa. Mjerumani mmoja, Krieger, aliuawa kwa kupigwa na risasi alipojaribu kutoka nje ya ngome ili kumpa habari kwa meli ya kijeshi ya Ujerumani iliyosimama baharini; yule mwingine, Hessell, aljifungia ndani ya chumba cha juu, na alijiua mwenyewe na risasi.[10] Kifo cha maafisa wao, na ukubwa wa uasi, ulikuwa kwa Wajerumani "das Signal ... fur eine Reihenoch nicht beendeter Kampfe" ('ishara ya mfululizo wa vita bila mwisho')[11]

Baadaye, ukumbusho uliimarishwa huko Kilwa Kivinje kukumbukia kifo cha maafisa hawa wawili Wajerumani. Kwa sababu ya mambo haya yamekwisha elezwa hapo juu, tunaweza kuamini habari iliotuma Gustav Michahelles, Balozi wa Ujerumani huko Zanzibar, kwa Otto von Bismarck, kwamba "Waarabu, wafanyabiashara wa watumwa karibu na Ziwa Nyasa, walichochea Wayao kushambulia Wajerumani", na haikuwa ghasia iliosababishwa na nia mbaya ya eneo hilo dhidi ya utawala wa Ujerumani, lakini "ilikuwa na chimbuko lake kusini mwa Rovuma ndani ya majimbo ya Ureno na majirani ya Ziwa Nyassa"(Kijerumani:"Ausgangpunkt sudlich von Rovuma hinter den portugiesichen Provinzien und aus den Gegenden Nyassa-Sees genommen").[11]

Baada ya ghasia za pwani za 1888

hariri

Muda mfupi baadaye, mnamo tarehe 2 Februari 1889, Bunge(Reichstag) la Ujerumani walikubali kuokoa kampuni ya DOAG kwenye hali mbaya, na Hermann von Wissmann alichaguliwa kuwa kamishna wa kifalme, kuongoza kikosi kwenda Afrika Mashariki kukabiliana na ghasia za pwani. Hermann von Wissmann aliwasili na wanajeshi wake mamluki mnamo Machi 1889. Pamoja na kusaidiwa na meli za Ujerumani zilizolinda miji ya bahari, alifaulu kutuliza sehemu kaskazini ya pwani. Halafu akaelekeza Kilwa na nchi ya kusini, alitua na wanaume 1200 kusini mwa Kilwa, na alifika mji wa Kilwa Kivinje kwa miguu. Alichukua mji kwa kutumia nguvu za meli baharini pamoja na za watu barani. Mabomu yalipiga Kilwa Kivinje kuanza Mei 3, na kuendelea usiku kucha na siku iliyofuata. Karibu robo ya mji uliangamizwa. Kufikia Juni 1890, waasi wote walikuwa wamekimbia milimani, eneo la Mavuji, ambalo Hassan bin Omari alikuwapo na ngome yake. Wissmann aliacha Von Zelewski pamoja na kampuni mbili za Waafrika, Wazungu 15, na bunduki 5 mjini, kusimamia kituo cha kudumu huko Kilwa. Muda wa amani ulifuata baadaye bila sumbuo, hata baada ya wakati von Zelewski alipowakamata watu waliotuhumiwa na vifo vya maafisa wa Kampuni ya Kijerumani ya Afrika Mashariki, Hessell na Krieger, na alipowaua.[12]

 
Boma la Ujerumani katika Kilwa Kivinje

Mnamo Juni 1894, Luteni Fromm, kwa maagizo kutoka kwa Gavana, alikwenda kuingia milima ya Mavuji, na kuvamia ngome ya Hassan bin Omari, lakini hakupata kushika Omari kwani aliweza kutoroka baada ya kusikia habari hii. Shajara ya Josef Weinberger, askari Mjerumani, ambaye alishirikiana katika msafara dhidi ya 'mafiti'(neno la jumla lililotumiwa katika Afrika Mashariki ya Ujerumani kwa kabila lolote linalopenda kufanya vita kama 'Wazulu'), inatupa habari ya jaribio hilo. Jioni ya tarehe 5 Juni, aliandika kwamba kutofaulu kukamata Hassan bin Omari kulitokana na usaliti wa akida wa Kilwa, Abdalla bin Omari, kama ilivyofumbuliwa na mfungwa mpelelezi, ambaye alikiri hivyo baada ya kupigwa vibaya.(Kijerumani: "Gefangener Spion gesteht es, nachdem er unzählige aufgezählt bekommen"[13]).

Shambulio dhidi ya Boma la Ujerumani, Kilwa Kivinje, mwaka wa 1894

hariri

Mapema Septemba, ilisikiwa kuwa watu wa Mavuji wameharibu laini ya simu kati ya Mohoro na Kilwa. Siku chache baadaye, alfajiri ya tarehe 7 Septemba 1894, kufuatia uvumi mwingi, watu wa Hassan bin Omar, pamoja na Wayao kwa maelfu, walipiga risasi kwenye kituo cha Kilwa, na wakapepea bendera mbili nyekundu za Sultan wa Zanzibar.[14] Msikiti wa karibu uliingiwa na mashaka katika matata haya kwa sababu ya sauti kubwa au kelele zilizotokea wakati wa sala ya 'fajr'. Milio mikali ya risasi iliendelea pande zote mbili, na mizinga ilipigwa na wao ndani ya kituo. Karibu saa sita za mchana, majirani ya kituo yalikuwa yametulia, na watu wa Hassan bin Omari walikuwa wamerudi nyuma. Kwa upande wa Wajerumani, mzungu mmoja na askari wanne wa rangi walijeruhiwa, na upande wa Wamavuji walifiwa 37, na hawa wakaachwa karibu na kituo hicho. Baada ya mambo haya, wafungwa kadhaa walinyongwa wakati Luteni Kanali von Trotha alipokuja Kilwa. Zilisikiwa pia habari wakati huu kwamba mikebe 600 ya baruti, makasha 6 ya mirao, na masanduku 10 ya fedha vilipelekwa kwa chombo kutoka Zanzibar kwenda Mtapatapa, kufikishwa mikononi Hassan bin Omari.[15]

Katika "Shairi la Makunganya", ingawa ni utenzi wakusifia Wissmann mno, na bali kushahidi matata haya mwenyewe, mshairi amelitunga kutokana na kisa zilizosikia yeye muda fupi baadaye, inadaiwa kwamba Hassan bin Omari alikuwa na mpango wa kumkamata Wissmann mwenyewe, bila Omari kujua kwamba yeye amekwisha ondoka mjini kwa muda, na dhana ile ile hupatikana pia katika magazeti ya habari za wakati huu.[1]

Shambulio hilo lilitisha Wajerumani sana na lilikuwa sababu kubwa ya msako mkali wa Hassan bin Omari na wenzake.

Baada ya shambulio la boma la Kilwa Kivinje, 1894

hariri

Katika miezi iliyofuata, Hassan bin Omari, mkuu wa Mavuji, alionekana kuingia tena katika uvamizi wa misafara na biashara, pamoja na uporaji wa mikoa, mauaji, na kuteketeza miji na mashamba kwa moto. Alishtakiwa pia kuwa alilazimisha wengine kupandisha bendera yake, badala ya bendera ya Ujerumani, na kunyakua silaha na dhahabu. Mashambulio hayo yalifikia maeneo mengi, kutoka Kilwa hadi Kiswere, kijiji na bandari kidogo cha zamani kusini mwa Kilwa ambapo, mwezi wa Novemba 1894, alikuwa ameiba bidhaa kutoka ofisi ya forodha yenye thamani ya rupia 17,000, na kusababisha wafanyabiashara wahindi wote kuacha eneo hilo. Matata kama haya yaliendelea mara kwa mara katika mwaka uliofuata.[16] Mnamo Oktoba 1895, Wissmann alikazia macho juu ya mambo haya ya Kilwa. Alitangaza kwamba hawezekani kuvumilia Hassan bin Omari kuwalazimisha wenyeji kutweka bendera yake badala ya bendera ya Ujerumani. Tena, mbali ya kufanya jeuri na kushambulia boma la Ujerumani, alidhulumu majirani ya Kilwa mpaka mtu yeyote asingeweza kutoka mji zaidi ya muda wa nusu saa bila hatari. Aliendelea kusema Hassan bin Omari amekamata wajumbe, na mara nyingi amewauwa, na pia amempa mkono Machemba, ambaye ni mtekaji mkubwa ya watumwa.[17]

Wissmann sasa aliona imekuwa kazi muhimu kuangamiza Hassan bin Omari na kuisha hali hii ya mambo mabaya. Kutia adhabu kali kwake haitakuwa kama mithali kwa watu wengine tu, bali itaweza kusaidia kushikiza matatizo ya wakuu wengine. Alitangaza zawadi ya rupia 1000 kuleta habari yake, na adhabu ya faini kwa wao wanaopandisha bendera yake. Alisimamisha kampuni nne chini ya kamanda wa Schutztruppe, kikosi cha ulinzi, washughulike na Hassan bin Omari. Aliamuru kampuni mbili kumaliza ujenzi wa boma karibu na kijiji chake ili kuwawekana macho na kuanza mazingazinga ya eneo hilo. Kampuni zingine mbili zilitumwa kuondoa mvuto wake na kuvirudisha vijiji tena kutii utawala wa Wajerumani. Alitaka vita dhidi yake kuendelea kabla ya msimu wa mvua, yaani mwezi moja na nusu kutoka mtangazo.

Kukamatwa Hassan bin Omari

hariri

Baada ya kupata idhini iliyotakiwa kufanyiza kazi hizo, kampuni nne za wanajeshi walitumwa mwezi wa Novemba 1895. Wanajeshi wa namba 8 walikaa Kiswere, wa 9 walipenya barani, wa 3 walipanda milimani, juu ya mto Mavuji, na wa 6 walipiga kambi huko Mavuji, kuweka msingi wa boma milimani kule. Siku ya tarehe 13, kutoka Kiswere baada ya kupokea habari kwamba Hassan bin Omari alikuwa amekaa na Myao aliyeitwa Saidi Mitole, huko Mpingiro, wanajeshi hawakuweza kumkamata yeye, kwa sababu alikuwa amekwisha toroka. Luteni Fromm alianza kumfuata chapu chapu kwa miguu, na mwishowe akagundua kuwa alikuwa amerudi Mavuji. Akifika mto Luawa, alisikia kwamba Hassan bin Omari alikuwa na mahali pale, ambapo alikaa pamoja na wanawake wake wengi. Tarehe ya 15, wanajeshi wote waliingia ndani ya eneo hilo na nguvu kamili, bila taabu kubwa, na katika mruko wa pili, Luteni Glauning alipata kushika watu wawili, mmojawao mwenye kigongo [Kijerumani: "eines kleinen buckligen Mannes"], ambaye alijaribu kujitetea na kisu. Huyo alikuwa Hassan bin Omari. Muda mfupi baadaye, waziri wake Omari Muenda, na Jumbe pia, walikamatwa. Mtu maarufu miongoni mwao, Sham bin Shaude, alipata kutoroka. Vifaa na vyakula vyingi vilipatikana kule, na vilichomwa na moto, ingawa katika mlipuko afisa wa chini, Lachemeier, aliungua vibaya. Siku iliyofuata, tarehe 16, walivunja kambi na walirudi kituoni kwao.[18]

Kifo cha Hassan bin Omari

hariri

Pamoja na kumkamata Hassan bin Omari, wanajeshi walivumbua sanduku kubwa ya maandiko, na ya barua zake. Hans Sache, aliyeandama Gavana Wissmann, alichaguliwa kuwa hakimu kuyachunguza mambo haya, na mahakama ilikutana. Omari alikuwa ameziwekea barua zote, za "uhaini sana", kutoka miaka mingi. Carl Velten, msomi mashuhuri wa Mashariki, alipewa kazi la kutafsiri maandishi haya ambayo kwa sehemu kubwa yalikuwa yameandikwa katika Kiarabu. Hatimaye, uchunguzi ulihusikiana na watu zaidi ya mia moja, na haukumalizika hata mwisho wa wiki saba. Hukumu za kifo kumi na sita zilifanyikwa kwa jumla, pamoja na Hassan bin Omari na Jumbe, na wote walinyongwa.[1] Makran bin Shaude, wali wa Kilwa, na Abdalla bin Omari, akida, wote wawili ambao waliokuwa wameaminiwa sana katika hudumu ya serikali tangu ghasia za 1888, walihusishwa katika matata haya na walifungwa. Yule wa kwanza alikufa usiku ule ule gerezani. Mji wote ulitiliwa hatiani, na kutoa faini. Wahindi wanne, walioheshimiwa sana, wafanyabiashara wakuu, ambao katika vitabu vyao vya kumbukumbu za hali ya fedha vilivyonyang'anywa walikuwa wametumia neno la 'mshenzi' kummaanisha Hassan bin Omari na neno lile, walihukumiwa wauawe, mmojawao ambaye alitajwa katika 'Shairi la Makunganya' na jina la Kassam Peera. Lakini, halafu, hukumu hii ilibadilishwa kuwa kufungiwa minyororoni na kifungoni, hata mwishowe ilibadilishwa tena, kuwa faini na kufukuzwa nchini, ingawa waliingia merikebuni baado minyororoni, kwenda Dar es Salaam, na baadaye Mombasa na Aden.

Hitimisho

hariri

Hawa wote walitungikwa tanzi la roho chini ya mwembe huku Kilwa Kivinje, na mti huu uliitwa 'mwembe kinyonga'. Mti ulikufa baadaye, lakini kuna ukumbusho pale wa "Mashujaa walionyongwa na Mjerumani Vita vya Maji Maji", bali ni kosa kutaja jina la 'Hasani O Makunganya' la kwanza pale, kwa sababu yeye hakuwa hai wakati wa Maji Maji. Mwalimu Julius Nyerere, alifanya ziara ya ukumbusho huo wakati wa uhuru wa Tanzania, kwa heshima ya mababa wa Kilwa Kivinje waliouawa wakati ule.[19]

Jambo lote la Hassan bin Omari lilionekana na walowezi wengi Wajerumani kama dalili ya kufanya nguvu dhidi ya maasi wote, na vitendo hivi vya Kilwa Kivinje vilikuwa kama mifano ya kufunzisha wenyeji wote, mpaka ukatili ule ule au zaidi ulitumiwa katika uasi wa Maji Maji uliozuka miaka michache tu baadaye.

Ilitia moto zaidi pia katika wale walowezi waliochukizwa na Wahindi, wengine wao ambao walifananisha Wahindi na Wayahudi, kama hula riba, na huwa wananchi hafifu ya moyo, na hukataa kutumia utaratibu na hesabu za Ulaya katika daftari zao, na hushirikiana pamoja na waasi, ingawa hulinda uhusiano wao wa Uingereza.[20]

Wengine walisema Hassan bin Omari katika maisha yake alikuwa na viungo vya kike na kiume, lakini uchunguzi wa daktari baada ya kifo chake haukuthibitisha hivi.[1]

"Shairi la Makunganya", lililotungwa na Mzee bin 'Ali bin Kidogo bin al-Qadiri wa Zanzibar kwa amri ya Hans Sache, lilitungwa na habari mshairi alizosikia tu, na mbali ya kuwasifia Wajerumani, hasa Wissmann na Sache, lina makosa kadhaa. Walakini, kuachilia yale, kiitiko cha shairi cha kuwauliza watu wa Kilwa ni kufikiria:

                                                  "Leo mnajuta nini,
                                                   Baa la kujitakia?"[1]

Machemba, yule mporaji wa watumwa wa kusini, aliyepeana mikono na Hassan bin Omari, ingawa awali aliishi kwa amani na Wajerumani baada ya kufanya mapatano nao, aliharibu kazi tena kwa kuvunja ahadi. Shikwa na hofu ya shambulio, alifanya kutoroka kwenda Msumbiji mnamo 1899, na baadaye alipigana kule na Wareno hadi kifo chake. [17]

Marejeo

hariri
  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 1.4 'Das Makunganya-Liedin Mittheilungen des Seminars für Orientalische Sprachen an der Königlichen Friedrich Wilhelms-Universität zu Berlin 1898; http://archive.org/details/bub_gb_aibWAAAAMAAJ
  2. https://smb.museum-digital.de/index.php?t=people&id=67762
  3. Alpers, Edward A. “Trade, State, and Society among the Yao in the Nineteenth Century.” The Journal of African History 10, no. 3 (1969): 405–20. http://www.jstor.org/stable/179674.
  4. Chittick, H. Neville. (1969). The early history of Kilwa Kivinje. 1–9. https://jstor.org/stable/10.2307/al.ch.document.sip200044
  5. Frederic Elton, Travels and Researches Among the Lakes and Mountains of Eastern and Central Africa (London, 1879), p286
  6. Msiska, Augustine W.C. “The Spread of Islam in Malawi and Its Impact on Yao Rites of Passage, 1870-1960.” The Society of Malawi Journal 48, no. 1 (1995): 49–86. http://www.jstor.org/stable/29778728.
  7. Johnston, H. H. (1895). The British Central Africa Protectorate. The Geographical Journal, 5(3), 193–214. https://doi.org/10.2307/1773928
  8. The Yaos = Chiikala cha Wayao by Abdallah, Yohanna B.1973.https://archive.org/search.php?query=external-identifier%3A%22urn%3Aoclc%3Arecord%3A1151859060%22
  9. Akinola, G. A. (1975). THE EAST AFRICAN COASTAL RISING, 1888-1890. Journal of the Historical Society of Nigeria, 7(4), 609–630. http://www.jstor.org/stable/41971217
  10. 'Bericht des deutschen Generalconsuls über der Aufstand an der ostafrikanischen Küste' in Deutsche Kolonisation in Ostafrika, Heinrich Hessell, Karl Hessell. Bonn: Weber, 1889. https://www.deutsche-digitale-bibliothek.de/item/W75YSOGVGMXDDL5XQYYN7APSNS3TBTZF
  11. 11.0 11.1 Deutsche Kolonisation in Ostafrika : aus Briefen und Tagebüchern des am 24. September 1888 zu Kilwa umgekommenen Beamten der Deutsch-Ostafrikanischen Gesellschaft, Heinrich Hessel. https://katalogplus.sub.uni-hamburg.de/vufind/Record/1043293787?rank=2
  12. Aus Deutsch-Ostafrikas Sturm- und Drangperiode. Becker, Alexander; Halle a.S., [1911]
  13. JWeinberger, Josef. Josef Weinberger aus Tölz: ein bayerischer Unteroffizier als Sergeant bei der Kaiserlichen Schutztruppe in Deutsch-Ostafrika ; 1891 - 1895. N.p., Hubach.
  14. Meinecke, Gustav Hermann. Aus dem Lande der Suaheli: Reisebriefe und Zuckeruntersuchungen am Pangani. Germany: Deutscher Kolonial-Verlag, 1895.
  15. Aus Deutsch-Ostafrikas Sturm- und Drangperiode; Becker, Alexander Halle, [1911]
  16. Deutsches Kolonialblatt Band 6 1895 passim http://books.google.com/books?id=GmDiAAAAMAAJ
  17. 17.0 17.1 Iliffe, J. (1979). A Modern History of Tanganyika (African Studies). Cambridge: Cambridge University Press. doi:10.1017/CBO9780511584114
  18. Bericht des Kompagnieführers Fromm über die Ergreifung Hassan bin Omaris und seines Bezirs Omari Muenda. Deutsches Kolonialblatt: Amtsbl. für d. Schutzgebiete in Afrika u.d.Südsee; 7.1896
  19. And Home Was Kariakoo: A Memoir of East Africa; M.G. Vassanji. 2016
  20. Angalia, kwa mfano, 'Die zukunft Deutsch-Ostafrikas, "Soll Deutsch-Ostafrika eine deutsche Kolonie werden oder eine hamburgisch-indische Domäne bleiben?" Bernhard Perrot 1908