Hatshepsut
Hatshepsut (1507 KK - 1458 KK) alikuwa farao wa tano wa nasaba ya 18 ya Misri ya Kale. [1] Alikuwa mmoja wa mafarao wa kike katika historia ya Misri. Alitawala kwa miaka 22.[2]
Binti na mke wa Farao
haririBaba yake alikuwa Thutmose I aliyefuatwa na mwanawe Thutmose II aliyekuwa kaka yake Hatshepsut aliyezaliwa na mke mwingine. Ilikuwa kawaida kati ya mafarao kwamba kaka na dada walioana. Wakati Thutmose II alipofariki baada ya miaka michache, mtoto wake mchanga Thutmose III alitangazwa kuwa farao mpya. Thutmose III hakuzaliwa na Hatshepsut bali wa mke mdogo.
Anachukua utawala
haririHatshepsut alikaimu kwa ajili ya mtoto mdogo. Baada ya miaka michache alichukua mwenyewe taji la Misri akapokea pia cheo cha farao. Sasa Misri ilikuwa rasmi na mafarao wawili waliotawala pamoja. Lakini hali halisi farao mtendaji alikuwa Hatshepsut.
Kufuatana na taarifa ya mwanahistoria Manetho wa karne ya 3 KK alitawala miaka 21 na miezi 7; mwaka wa kufariki kwake ulikuwa 1458 KK, hivyo alianza kutawala mnamo mwaka 1479 KK.
Mafanikio
haririBiashara
haririHatshepsut alirudisha mitandao ya biashara ambayo ilikuwa imevurugwa wakati wa uvamizi wa Waiksosi katika karne iliyotangulia. Kustawi kwa biashara uliongeza utajiri wa Misri.
Wataalamu wanaona kwamba sera yake ya kigeni ilikuwa ya amani. [2] Walakini, kuna ushahidi kwamba Hatshepsut aliongoza pia kampeni za kijeshi zilizofanikiwa huko Nubia na Syria mwanzoni mwa utawala wake.
Safari ya Punt
haririHatshepsut mwenyewe alisimamia maandalizi ya safari kwenda nchi tajiri ya Punt. Punt ilikuwa kwenye sehemu isiyojulikana tena lakini ilikuwa kwenye mwambao wa Bahari Nyekundu, labda pia kwenye Bahari Hindi. Katika mwaka wa tano wa malkia meli tano zilitumwa pamoja na mabaharia 210, ambao walirudi wakibeba uvumba na manemane. Malkia alitwanga uvumba akautumia kujipamba usoni[3]. Walileta pia miti 31 ya mmanemane ambayo ni taarifa ya kwanza katika historia kuhusu jaribio la kuhamisha mimea kutoka nchi moja kwenda nyingine. Miti ilipandwa katika bustani ya hekali ya mazishi pale Deir el Bahri.[4]
Miradi ya ujenzi
haririHatshepsut alikuwa mmoja wa wajenzi mahiri katika Misri ya Kale. Aliagiza mamia ya miradi ya ujenzi kote Misri, ambayo ilikuwa mikubwa na mingi zaidi kuliko ile ya mafarao waliomtangulia.
Alimwajiri mbunifu mashuhuri Ineni aliyewahi kufanya kazi kwa baba yake na pia mume wake. Wakati wa utawala wake, sanamu nyingi zilitengenezwa kiasi kwamba karibu majumba mengi ya makumbusho duniani yana sanamu za Hatshepsut kati ya makusanyo yao.
Kufuatia mila ya mafarao wengi, Hatshepsut aliongeza majengo kwenye Hekalu la Karnak. Huko Karnak alirudisha pia uwanja wa hekalu la Mut, mungu wa kike wa Misri, ulioharibiwa wakati wa utawala wa Waiksosi.
Mradi mkuu wa ujenzi wa Hatshepsut ulikuwa hekalu lake la mazishi. Ilikuwa kawaida kila farao alijenga hiyo wakati wa uhai wake. Aliteua eneo la Deir el-Bahri ambalo ni karibu kwenye bonde tunaloliita leo "Bonde la Wafalme", likitazama mji wa kifalme na hekalu mashuhuri la Luxor. Ilibuniwa na kusimamiwa na Senemut kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Nile. Hekalu lenyewe limekatwa kwenye mtelemko wa miamba inayopanda kando ya bonde la mto.
Hadhi yake
haririWanawake walikuwa na hadhi ya juu katika Misri ya zamani na walifurahia haki za kisheria za kumiliki mali, kurithi, na kuamulia urithi. Mwanamke kuwa farao ilikuwa nadra, hata hivyo. Kabla ya Hatshepsut wanajulikana watatu tu waliotawala rasmi.
Hatshepsut alikuwa ameandaliwa vizuri kwa kazi yake akiwa binti wa farao mtawala. Wakati wa utawala wa baba yake alikuwa na ofisi muhimu ya Mke wa Mungu Amun. Alipokuwa malkia wa mume wake farao Thutmose II alishiriki katika shughuli za utawala. Alipoanza kukaimu kwa farao mtoto baada ya kifo cha mumewe alikuwa na maarifa ya serikali tayari.
Farao mwenzake Thutmose III aliendelea vizuri naye, hakujaribu kumpindua ingawa aliendelea kuwa kiongozi wa jeshi alipofikia umri.
Hatshepsut alivaa mavazi yote ya kifalme pamoja na ndevu bandia zilizokuwa kawaida kwa mafarao wote. Kuna pia picha na sanamu anapoonekana ana mavazi ya kike.[5]
Utabiri kwenye hekalu la Amun ulitangaza kuwa yalikuwa mapenzi ya Amun kwamba Hatshepsut awe farao, na tangazo hilo liliimarisha hadhi yake. Alitumia msaada huo kutoka makuhani wa Amun kwa kulichonga kwenye majengo mengi aliyoagiza yajengwe:
- "Karibu binti yangu mtamu, mpendwa, Mfalme wa Misri ya Juu na Kusini, Maatkare, Hatshepsut. Wewe ndio Farao, unamiliki nchi hizi mbili ". [6]
Marejeo
hariri- ↑ "Hatshepsut". Dictionary.com. Iliwekwa mnamo 27 Julai 2007.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ 2.0 2.1 Tyldesley, Joyce 1998. Hatchepsut: The female Pharaoh. Penguin, pp. 137–144.
- ↑ Isaac, Michael (2004). A Historical Atlas of Oman. The Rosen Publishing Group. uk. 14. ISBN 978-0-8239-4500-9. Iliwekwa mnamo 5 Septemba 2014.
{{cite book}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ Njoku, Raphael Chijioke (2013). The History of Somalia. ABC-CLIO. ku. 29–31. ISBN 978-0-313-37857-7.
- ↑ Callender/Shaw p.170.
- ↑ Breasted, James Henry 1906. Ancient Records of Egypt: historical documents from the earliest times to the Persian conquest. University of Chicago Press. 116–117.
Viungo vya Nje
haririAngalia mengine kuhusu Hatshepsut kwenye miradi mingine ya Wikimedia: | |
Fafanuzi za Kiingereza kutoka Wiktionary | |
picha na media kutoka Commons | |
misaada ya kujisomea kwa Kiingereza kutoka Wikiversity | |
nukuu kutoka Wikiquote |
- Hatshepsut – Archaeowiki.org
- Mummy Of Egyptian Queen Hatshepsut Found
- Interactive, panoramic online view of Hatshepsut's mortuary temple at Deir el-Bahari, Egypt
- Video tour the Metropolitan Museum of Art's gallery of Hatshepsut sculptures
- Hatshepsut – the fifth ruler of the 18th Dynasty
- 360° Panorama images Archived 5 Februari 2010 at the Wayback Machine.
- BBC Radio 4 In Our Time : Hatshepsut
- Queen Hatshepsut