Milki ya Kiptolemaio

(Elekezwa kutoka Ptolemaic Kingdom)

Milki ya Kiptolemaio (kwa Kigiriki: Πτολεμαϊκὴ βασιλεία, ptolemaaike basileia)[1] ulikuwa dola katika Misri na sehemu za Mashariki ya Kati kuanzia mwaka 305 KK hadi mwaka 30 BK. Ilitawaliwa na wafalme kutoka nasaba ya Waptolemaio waliokuwa Wagiriki na hivyo ufalme wao huhesabiwa kati ya milki za Kiheleni zilizotokea baada ya Aleksander Mkuu.

Ramani ya Milki ya Kiprolemaio.

Mandharinyuma ya Kihistoria

hariri

Aleksander Mashuhuri alivamia Misri kwenye mwaka 332 KK akipiga vita yake dhidi ya Milki ya Uajemi. Misri ilikuwa chini ya Waajemi wakati ule. Baada ya kifo cha Aleksander mnamo 323 KK, himaya yake ilisambaratika haraka ilhali majenerali wake walianza kushindana juu ya urithi wake.

 
Sanamu ya Ptolemaio I akionyeshwa kama Farao wa Kimisri.

Ptolemaio I

hariri

Mwanzilishi wa milki hiyo alikuwa Ptolemaio I Soter aliyekuwa rafiki wa Aleksander. Milki hiyo ikadumu hadi kifo cha malkia Kleopatra mnamo 30 BK. [2] Wakitawala kwa karibu karne tatu, Waptolemaio walikuwa nasaba yenye utawala mrefu kati ya nasaba zote zilizotawala Misri ya Kale.

Ptolemaio aliyekuwa Mgiriki wa Masedonia na mmoja wa marafiki wa karibu wa Alksander; alishinda udhibiti wa Misri kutoka kwa wapinzani wake akajitangaza kuwa farao (cheo cha mfalme wa Misri).[3] [4]

Ptolemaio alifaulu kushinda vita dhidi ya Waseleuko waliokuwa pia warithi wa Aleksander na hapo alifaulu kuingiza kusini mwa Syria na Lebanoni katika himaya yake; upande wa magharibi alitwaa pia Libya akaendelea kudhibiti pia Nubia kwenye kusini.

Tamaduni mbili

hariri

Aleksandria, mji uliowahi kuundwa na Aleksander na kukaliwa na Wagiriki, uliteuliwa kuwa mji mkuu. Iliendelea kuwa kitovu cha utamaduni wa Kigiriki katika Misri. Ilikuwa pia kitovu cha elimu na biashara. Ptolemaio I alianzisha Maktaba ya Aleksandria, iliyoendelea kuwa mkusanyo mkubwa wa vitabu (wakati ule vilikuwa vikinakiliwa kwa mkono) katika Afrika, Ulaya na Mashariki ya Kati.

Waptolemaio walitawala juu ya Wamisri wazawa. Hivyo walijitahidi kutumia mapokeo na desturi za Misri ili kurahisisha utawala wao. Walitumia cheo cha Farao, na walipoonekana hadharani nje ya Aleksandria walivaa pia nguo za Kimisri. Kwenye majengo ya kiserikali walifuata desturi ya Kimisri kuchora picha zao wakivaa Kimisri. Vinginevyo walitunza utamaduni wao wa Kigiriki kati yao na pia kati ya miji iliyoundwa nao na kukaliwa na Wagiriki[2]. Inasemekana malkia wa mwisho Kleopatra alikuwa Mptolemaio wa kwanza aliyejua lugha ya Kimisri vizuri kabisa, pamoja na Kigiriki.

Utawala

hariri

Walikuwa wamerithi vyombo vya dola vilivyoendelea kwa desturi za Kimisri kwenye ngazi za chini. Wagiriki wengi, hasa wanajeshi waliostaafu, walikaribishwa kukaa Misri wakapewa nafasi za kujenga makazi na kulima. Waliingiza mazao mapya. Katika oasisi ya Fayum walikausha vinamasi na kutoa ardhi kwa walowezi Wagiriki. Hata hivyo idadi kubwa kabisa ya wananchi walikuwa wazalendo walioendelea maisha yao ya vijijini, lakini matabaka ya juu ya vyombo vya dola yalijaa Wagiriki waliodhibiti shughuli za siasa, uchumi na jeshi. Wamisri asilia waliweza kupanda ngazi kama walijua Kigiriki[5].

Waptolemaio walilinda taasisi za dini asilia, hasa mahekalu ya dini ya Misri ya Kale. Waliendelea kugharamia makuhani na mahekalu wakashiriki katika sherehe na sikukuu muhimu na hivyo kutumia dini kama zana kwa utawala wao. Waptolemaio walijenga pia mahekalu mapya.

Athiri ya Kiroma na mwisho wa milki

hariri
 
Sanamu ya Kleopatra.
 
Picha ya Ptolemaio Xii akitoa sadaka mbele ya miungu ya Kimisri.

Misri ya Waptolemaio ilikuwa milki tajiri na yenye nguvu kati milki zote za Kiheleni zilizomfuata Aleksander. [6] Kuanzia katikati ya karne ya 2 KK, ugomvi ndani ya nasaba na mfululizo wa vita za kigeni viliudhoofisha ufalme, na ikazidi kutegemea Jamhuri ya Roma ya Kale. Mfalme Ptolemaio XII alipaswa kutumia msaada wa vikosi vya askari Waroma aliporudi Misri kwenye mwaka 55 KK baada ya uasi uliOwahi kumfukuza.

Malkia Kleopatra alitaka kurudisha mamlaka ya Waptolemaio lakini alijikuta kati ya pande tofauti za vita ya wenyyewe kwa wenyewe ya Kiroma. Hatimaye Roma ilivamia na kutwaa utawala juu ya Misri. Kifo cha Kleopatra kwenye mwaka 30 kilikuwa mwisho wa nasaba ya Waptolemaio na mwisho wa milki yao.

Misri ya Kiroma iliendelea kuwa jimbo tajiri la Dola la Roma na utamaduni ya Kiheleni uliendelea katika miji mikubwa; Kigiriki kilibaki lugha ya serikali hadi uvamizi wa Waarabu mwaka 641.

Orodha ya watawala Waptolemaio

hariri
  • Ptolemaio I Soter (303–282 KK) alimwoa kwanza Thaïs, halafu Artakama, halafu Eurydice, na mwishowe Berenike I
  • Ptolemaio II Philadelphus (285–246 KK)[7] alimwoa Arsinoe I, halafu Arsinoe II; alitawala pamoja na Ptolemaio Epigonos (267–259 KK)
  • Ptolemaio III Euergetes (246–221 KK) alimwoa Berenike II
  • Ptolemaio IV Philopator (221–203 KK) alimwoa Arsinoe III
  • Ptolemaio V Epiphanes (203–181 KK) alimwoa Kleopatra I Syra
  • Ptolemaio VI Philometor (181–164 KK, 163–145 KK) alimwoa Kleopatra II, alitawala kifupi pamoja na Ptolemaio Eupator in 152 KK
  • Ptolemaio VII Neos Philopator (hakutawala)
  • Ptolemaio VIII Physcon (170–163 KK, 145–116 KK) alimwoa Kleopatra II, halafu Kleopatra III; alifukuzwa kutoka Aleksandria na Kleopatra II kuanzia 131 hadi 127 KK, halafu walipatanisha 124 KK.
  • Kleopatra II Philometora Soteira (131–127 KK), kwa upinzani dhidi ya Ptolemaio VIII Physcon
  • Kleopatra III Philometor Soteira Dikaiosyne Nikephoros (Kokke) (116–101 KK) alitawala pamoja na Ptolemaio IX Lathyros (116–107 KK) na Ptolemaio X Alexander I (107–101 KK)
  • Ptolemaio IX Lathyros (116–107 KK, 88–81 KK as Soter II) alimwoa Kleopatra IV, halafu Kleopatra Selene wa Syria; alitawala pamoja na Kleopatra III katika kipindi chake cha kwanza
  • Ptolemaio X Alexander I (107–88 KK) alimwoa Kleopatra Selene, halafu Berenike III; alitawala pamoja na Kleopatra III till 101 KK
  • Berenike III Philopator (81–80 KK)
  • Ptolemaio XI Alexander II (80 KK) alimwoa na alitawala pamoja na Berenike III kabla ya kumwua; akaendelea kutawala kwa siku 19.
  • Ptolemaio XII (80–58 KK, 55–51 KK) alimwoa Kleopatra V Tryphaena
  • Kleopatra V Tryphaena (58–57 KK) alitawala pamoja na Berenike IV Epiphaneia (58–55 KK) na Kleopatra VI Tryphaena (58 KK)
  • Kleopatra ("Kleopatra VII Philopator", 51–30 KK) alitawala pamoja na Ptolemaio XIII Theos Philopator (51–47 KK), Ptolemaio XIV (47–44 KK) na Ptolemaio XV Caesarion (44–30 KK).

Marejeo

hariri

 

  1. Diodorus Siculus, Bibliotheca historica, 18.21.9
  2. 2.0 2.1 "Ancient Egypt - Macedonian and Ptolemaic Egypt (332–30 bce)". Encyclopedia Britannica (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-06-08.
  3. Robins, Gay (2008). The Art of Ancient Egypt (tol. la Revised). United States: Harvard University Press. uk. 10. ISBN 978-0-674-03065-7.
  4. Hölbl, Günther (2001). A History of the Ptolemaic Empire. UK, USA, Canada: Routledge. uk. 22. ISBN 978-0-415-23489-4.
  5. "Ancient Egypt - Macedonian and Ptolemaic Egypt (332–30 bce)". Encyclopedia Britannica (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-06-08.
  6. "Ancient Egypt - Macedonian and Ptolemaic Egypt (332–30 bce)". Encyclopedia Britannica (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-06-08."Ancient Egypt - Macedonian and Ptolemaic Egypt (332–30 bce)".
  7. Tunny, Jennifer(2001)The Health of Ptolemaio II Philadelphus. The Bulletin of the American Society of Papyrologists/ Vol.38(1/4), pp.119-134

Vyanzo

hariri

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Milki ya Kiptolemaio kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.