Kosovo (kwa Kialbania: Kosovë au Kosova, kwa Kiserbokroatia na herufi za Kisirili: Косово и Метохија, kwa alfabeti ya Kilatini: Kosovo i Metohija) ni nchi ndogo ya Balkani katika Ulaya ya kusini-mashariki. Imepakana na Serbia, Masedonia Kaskazini, Albania na Montenegro.

Bendera ya Kosovo
Ramani ya Kosovo

Mji mkuu ni Prishtina.

Historia

hariri

Kihistoria Kosovo iliwahi kuwa eneo ambako ufalme wa kwanza wa Serbia ulianzishwa wakati wa karne ya 12. Hivyo Kosovo ilikuwa kitovu cha Serbia hadi mwisho wa milki ya Serbia ya Kale iliyovamiwa na Waturuki wa Milki ya Osmani.

Chini ya utawala wa Waturuki idadi ya Waserbia ilipungua kwa sababu wengi walikimbia ukandamizi wa Waosmani dhidi ya Wakristo. Waalbania walihamia humo kutoka maeneo ya jirani yaliyokuwa pia sehemu ya Milki ya Osmani. Katika karne ya 19 idadi kubwa ya wakazi wa Kosovo walikuwa tayari Waalbania.

Kosovo ndani ya Yugoslavia

hariri

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Kosovo ilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Serbia ndani ya shirikisho la Yugoslavia. Tofauti na sehemu kubwa ya Serbia, inayokaliwa na Waserbia hasa, wakazi wengi wa Kosovo ni Waalbania waliokuwa takriban robo tatu ya watu wote wa Kosovo hadi mwaka 1990. Hali halisi ilikuwa na haki za jamhuri ndani ya shirikisho, lakini kutokana na uhusiano wa kihistoria haikupewa hadhi ya jamhuri kamili.

Wakati wa kusambaratika kwa Yugoslavia viongozi wa Serbia walifuta hali ya kujitawala ya Kosovo na kuwaachisha kazi maafisa wengi wenye utamaduni wa Kialbania. Hii ilisababisha kipindi cha upinzani na ghasia ndani ya Kosovo kwa haki za Waalbania zilizokandamizwa na polisi na jeshi la Serbia.

Amani ya Dayton ya mwaka 1995 juu ya sehemu zilizounda Yugoslavia haikuangalia masuala ya Kosovo. Hapo mwaka 1996 vikundi kadhaa vya Kialbania vilianza kuchukua silaha na kupigania uhuru kwa njia ya kijeshi. Jeshi la Serbia likajibu vikali na raia mia kadhaa waliuawa.

Vita ya Kosovo

hariri

Mwaka 1999 wakimbizi wengi kutoka Kosovo walitafuta kimbilio katika nchi jirani na Umoja wa Ulaya. Baada ya majadiliano juu ya usuluhisho kushindikana, NATO iliamua kuingilia kati kwa kusudi la kuzuia kuongezeka kwa wakimbizi na mauaji. Tarehe 24 Machi 1999 ndege za kivita zilianza kushambulia madaraja, barabara, vituo vya umeme na taasisi za kijeshi katika Serbia. Jeshi la Serbia likaongeza kampeni yake katika Kosovo na idadi ya wakimbizi ikaongezeka.

Baada ya NATO kutisha uvamizi wa Kosovo kwa jeshi la ardhi, serikali ya Serbia ilikubali tarehe 12 Juni 1999 mapatano ya kuwa Umoja wa Mataifa uchukue mamlaka juu ya Kosovo ikisaidiwa na NATO. Tarehe 10 Juni 1999 Baraza la Usalama la UM lilimwagiza Katibu Mkuu kwa azimio 1244 kuanzisha utawala juu ya Kosovo. Hatua hiYO iliunda nchi lindwa chini ya UM na jeshi la NATO ambayo kisheria iliendelea kuitwa mkoa wa Serbia.

Ndani ya Kosovo NATO haikufaulu kuzuia matendo ya fujo na ghasia dhidi ya wakazi Waserbia wa jimbo. Waserbia walipaswa kukimbia kutoka sehemu nyingi na wilaya mbili tu zilibaki kama maeneo ya Waserbia ndani ya Kosovo.

 
Newborn monument iliyotengenezwa kama ukumbusho wa tangazo la uhuru, tarehe 17 Februari 2008, mjini Pristina.

Kosovo ilikuwa sehemu ya Serbia hadi tarehe 17 Februari 2008 ilipojitangazia uhuru wake. Jumuiya ya kimataifa haina msimamo wa pamoja juu ya uhuru wa nchi. Serbia inadai Kosovo bado ni jimbo lake la kujitawala. Nchi 98, zikiwa pamoja na nchi nyingi za G8, Uturuki, Austria na Uswisi zimetambua uhuru wa Kosovo. Lakini nchi nyingine zinakataa.

Hali halisi tangazo la uhuru liliwezeshwa na maungano ya NATO ambayo imetawala Kosovo kwa niaba ya Umoja wa Mataifa. Jeshi la NATO lilizuia serikali ya Serbia lisingie kati kwa nguvu.

 
Maeneo ya Waalbania, Waserbia na wengineo ndani ya Kosovo.

Kosovo ina wakazi wasiofikia milioni mbili. Takriban asilimia 88 ni Waalbania, 7 % Waserbia na wengine mchanganyiko wa Waturuki na vikundi vidogo.

Lugha mama ya wengi ni Kialbania (95%).

Upande wa dini, Waalbania wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni na Waserbia wengi ni Wakristo Waorthodoksi lakini kuna pia Waalbania Wakatoliki na Waorthodoksi, pia Waserbia Waislamu kadhaa. Kwa jumla, Waislamu ni 95.6% na Wakristo 3.7% (Wakatoliki 2.2%, Waorthodoksi 1.5%).

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Kosovo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.