Alois Maria wa Montfort
Alois Maria wa Montfort (Montfort-sur-Meu, Ufaransa, 31 Januari 1673 - Saint-Laurent-sur-Sèvre, 28 Aprili 1716)
Alikuwa padri maarufu kwa mahubiri aliyoyatoa kote Ufaransa Magharibi, akitangaza fumbo la Hekima ya milele, na kurudisha wengi kwenye toba. Tena kwa maandishi yake, ambayo mpaka leo yanazidi kuathiri Kanisa Katoliki hasa upande wa heshima ya pekee kwa Bikira Maria katika maisha ya kiroho, lakini pia kuhusu Msalaba wa Yesu.
Alikuwa pia mwanzilishi wa mashirika matatu ya kitawa: Shirika la Maria, Mabinti wa Hekima na Mabruda wa Mt. Gabriel.
Alitangazwa na Papa Leo XIII kuwa mwenye heri mwaka 1888, halafu Papa Pius XII alimtangaza mtakatifu mwaka 1947.
Sikukuu yake huadhimishwa tarehe aliyofariki dunia [1].
Heshima halisi kwa Maria
haririAlois Maria wa Montfort anapoizungumzia katika kitabu chake maarufu hasemi kuhusu heshima ya nje tu, yenye kiburi, isiyodumu, ya kinafiki au ya kujitafutia faida, bali ile halisi ambayo ni “utashi kuwa tayari kutenda mara yanayohusu utumishi wa Mungu” (Thoma wa Akwino). Utayari huo, unaotakiwa kudumu hata hisi zikiwa kavu, unatuelekeza kumuabudu Bwana na kumpatia Mama yake heshima ya pekee anayostahili.
Wengine wanadanganyika wakidai kuufikia muungano na Mungu pasipo kumpitia mfululizo Yesu Kristo: hivyo wataufikia ujuzi wa kinadharia tu kumhusu Mungu, si ule mtamu unaoitwa hekima ambao ni wa juu, hai, wenye kung’amua njia za maongozi yake hata katika mambo madogo. Watulivu walidai eti! Ubinadamu wa Yesu ni njia ya kufaa mwanzoni tu mwa maisha ya Kiroho. Uzushi huo ni kutotambua upana usio na mipaka wa ushenga wa Mwokozi.
Uzushi mwingine ni ule wa wale wanaotaka kumuendea Bwana pasipo Maria. Hata baadhi ya Wakatoliki hawaoni inavyofaa kumkimbilia Bikira ili kuwa wandani wa Kristo. Wanamjua Maria “kinadharia tu, kwa namna kavu, kame, isiyojali… Wanaogopa kuzidisha heshima kwake na kumchukiza Bwana wetu kwa kumstahi mno Mama yake mtakatifu… Wakisema juu ya heshima kwa Maria, si kwa kuihimiza, bali hasa kwa kuondoa matumizi yake yasiyofaa” (Alois Maria wa Montfort). Wanaonekana kudhani Maria ni kizuio kwa kuufikia muungano na Mungu, kumbe athari yake yote inalenga kutufikisha huko. Ingekuwa sawa na kusema Yohane Maria Vianney alikuwa kizuio kwa wanaparokia wake wasimuendee Mungu. Ni kukosa unyenyekevu kupuuzia washenga ambao Mungu ameujalia udhaifu wetu.
Ngazi za heshima hiyo
haririHeshima hiyo, ambayo inatakiwa kuwemo ndani ya kila Mkristo na kustawi pamoja na upendo, ngazi yake ya kwanza ni kumuomba Bikira mara kwa mara, k.mf. kusali vizuri Malaika wa Bwana.
Ngazi ya pili ni kuwa na heshima, tumaini na upendo kamili zaidi kwake, ambavyo mtu asali kila siku walau robo ya Rozari kwa kutafakari matendo ya furaha, ya mwanga, ya uchungu na ya utukufu yaliyo njia ya kufikia uzima wa milele.
Ngazi ya tatu, ambayo ndiyo inayowafaa wanaoendelea, ni kujiaminisha kwa Bwana kwa njia ya Mama yake: “Heshima hiyo ni kujiaminisha kabisa kwa Bikira mtakatifu ili kwa njia yake tuwe mali ya Yesu kabisa. Tunapaswa kumtolea: 1) mwili wetu pamoja na hisi zake zote na viungo; 2) roho yetu na vipawa vyake vyote; 3) mali yetu ya nje... ya sasa na ya kesho; 4) mema yetu ya ndani na ya Kiroho, yaani stahili zetu, maadili yetu na matendo yetu mema ya jana, ya leo na ya kesho”.
Ili tuelewe vema tendo hilo tunapaswa kutofautisha katika matendo mema mambo yasiyoshirikishwa na yale yanayoweza kushirikishwa. Yasiyoshirikishwa ni zile stahili hasa ambazo zinatupa haki ya kustawishiwa upendo na kupata uzima wa milele. Tukizitoa kwa Bikira mtakatifu si kusudi awagawie wengine, bali atudumishie na kutuzalishia na, tukija kuzipoteza kwa dhambi ya mauti, atupatie neema ya kutubu vizuri ili turudishiwe si neema inayotia utakatifu tu bali kiwango chake tulichokuwa nacho.
Yanayoweza kushirikishwa ni stahili za kufaa tu na thamani ya matendo yetu mema kwa kufidia na kuombea. Stahili za kufaa hazitegemei haki bali upendo au urafiki unaotuunganisha na Mungu; kwa msingi huo tunaweza kumpatia jirani neema, kama vile mama mwema anavyowavutia wanae, kwa kuwa Mungu anajali nia na matendo yake maadilifu. Tunaweza kuwaombea majirani, wakosefu sugu, walio mahututi, marehemu n.k. Tunaweza kulipa kwa niaba ya wengine, kupokea kwa hiari adhabu za dhambi zao, kama Maria alivyofanya chini ya msalaba ili kuwavutia huruma ya Mungu. Tunaweza pia kuwapatia waliopo toharani rehema kwa kuwafungulia hazina ya stahili za Yesu na ya watakatifu ili kuharakisha ukombozi wao.
Tukimtolea Maria matatizo na tabu zetu zote, atatupatia misalaba inayolingana na nguvu tulizonazo kwa msaada wa neema, ili tuchangie wokovu wa watu.
Tumshauri nani ajiaminishe hivyo? Si wale watakaokubali kwa kufuata hisia za moyoni tu au kiburi kuhusu mambo ya Kiroho, wasielewe uzito wake, bali watu wenye juhudi: nao wajiaminishe kwanza kwa muda mfupi, halafu kwa mwaka mmoja, ili wapenywe na hiyo roho ya kujiaminisha, hadi waweze kujitoa kwa faida maisha yao yote.
Baadhi wanabisha wakisema tendo hilo ni kujinyima yote tusilipe madeni yetu, hivyo litarefusha tohara yetu. Bwana alimjalia Birgita wa Sweden kuelewa jinsi wazo hilo linavyotokana na umimi na linavyosahau wema wa Maria, ambaye hashindwi na yeyote katika ukarimu. Tukijinyima hivyo tutapokea mara mia. Upendo wenyewe, unaoshuhudiwa na tendo hilo, unatuondolea tayari sehemu ya tohara.
Wengine wanauliza tutafanyeje kuwaombea ndugu na marafiki kisha kumtolea Maria sala zetu zote? Jibu ni kwamba Bikira anajua wajibu wetu kwa ndugu na marafiki, na kama tungesahau kuwaombea angetukumbusha. Tena mara nyingi hatujui nani kati yao anahitaji zaidi kuombewa, kumbe Maria anajua na kutumia sala zetu kwa ajili yake. Hatimaye tunaweza kumuomba amsaidie fulani au fulani.
Matunda ya heshima hiyo
haririNjia hiyo ya kumuendea Mungu ni rahisi na inastahili zaidi, kwa hiyo ni fupi, kamili na ya hakika zaidi.
Kwanza ni rahisi zaidi. “Kwa kusema ukweli tunaweza kuufikia muungano na Mungu kwa njia nyingine; lakini itakuwa kwa misalaba mingi zaidi sana na kwa vifo vya ajabuajabu na kwa matatizo mengi zaidi sana ambayo tutayashinda kwa shida kubwa zaidi. Itatupasa kupitia giza la usiku, mapambano na mafadhaiko yasiyosemekana, milima yenye magenge, misitu ya miba inayochoma na majangwa ya kutisha. Kumbe kwa njia ya Maria tunapita kwa utamu na utulivu mkubwa zaidi. Ni kweli kuwa huko vinapatikana vita vikali ambavyo tuvipige na matatizo makubwa ambayo tuyashinde, lakini huyo Mama mwema anawakaribia watumishi wake waaminifu ili kuwaangazia giza lao, kuwashauri katika wasiwasi wao, kuwategemeza katika mapambano na matatizo yao, kiasi kwamba njia hiyo ya Kibikira ya kumpata Yesu Kristo ni ya mawaridi na asali ukiilinganisha na nyingine”. Hiyo inathibitishwa na watakatifu waliofuata njia hiyo kwa namna ya pekee.
Ingawa njia hiyo ni rahisi zaidi, kwa kuwa Bikira anatutegemeza, haiachi kustahili zaidi, kwa kuwa Maria anatupatia upendo mkubwa ulio asili ya stahili. Matatizo ni nafasi ya kustahili, lakini asili ya stahili ndiyo upendo ambao tunayashinda. Maria kwa matendo rahisi alistahili kuliko wafiadini katika mateso yao yote, kwa jinsi alivyotumia upendo mwingi katika kuyatenda.
Njia ya Maria ni fupi zaidi, kwa maana tunaifuata kwa urahisi na hivyo tunakwenda kasi zaidi. Kwa muda mfupi wa kumfuata Mama wa Mungu tunasonga mbele kuliko kwa miaka ya kufuata busara yetu. Chini yake, ambaye Neno aliyefanyika mwili alimtii, tunapiga hatua za jitu.
Njia hiyo ndiyo kamili zaidi, kwa kuwa Neno alitushukia kwa njia ya Maria asipoteze chochote cha Umungu wake; basi kwa njia yake walio wadogo wanaweza kupanda vizuri kwa Aliye Juu wasiogope chochote. Mwenyewe anatakasa matendo yetu mema na kuzidisha thamani yake akiyatoa kwa Mwanae.
Hatimaye ndiyo njia ya hakika zaidi inayotukinga dhidi ya udanganyifu wa shetani ambaye kwanza anajaribu kutupotosha kidogokidogo ili baadaye atufikishe kutenda makosa makubwa. Pia inatukinga dhidi ya udanganyifu wa ndoto na hisia za moyoni, kwa kuwa Maria kama chombo cha neema anatuliza na kuratibu hisi zetu ili roho ipokee athari ya Bwana kwa manufaa zaidi. Tena Maria ni kiumbe kitakatifu: hivyo akizingatiwa na hisi zetu anainua roho iungane na Mungu. Anatupatia uhuru mkubwa wa ndani, na pengine tukimuomba kwa udumifu atatupatia neema ya kukombolewa mara na upotovu wa hisi unaozuia sala na muungano wa dhati na Bwana. Kila athari ya Maria inalenga kutufikisha huko, kama vile Yesu anavyotufikisha kwa Baba. Inafaa kuomba msaada wake wa pekee wakati na baada ya Komunyo, ili atushirikishe ibada yake ya dhati pamoja na upendo wake, kana kwamba tungeazima moyo wake safi tumpokee Yesu inavyotakiwa.
Kiini cha kujiaminisha kwa Yesu kwa mikono ya Maria ni kama ifuatavyo: “Ee Yesu mpendwa, unayestahili kuabudiwa, Mungu kweli na mtu kweli! Nakushukuru kwa jinsi ulivyojishusha kabisa ukitwaa namna ya mtumwa ili kunikomboa kutoka utumwa wa shetani… Nakimbilia maombezi ya Mama yako mtakatifu uliyenipa awe mtetezi wangu kwako; kwa njia hiyo natumaini utanijalia majuto na msamaha wa dhambi zangu, nipate na kutunza hekima. Nakusalimu Maria usiye na doa, malkia wa mbingu na nchi, ambaye vyote vilivyo chini ya Mungu viko chini yako. Nakusalimu, kimbilio la hakika la wakosefu, wewe ambaye huruma yako haimpungui yeyote: unitimizie hamu yangu ya kupata hekima ya Kimungu, na kwa lengo hilo pokea nadhiri na matoleo ninavyokutolea kwa unyonge wangu. Mimi, mkosefu nisiye mwaminifu narudia leo na kuthibitisha mikononi mwako ahadi za ubatizo wangu. Namkataa moja kwa moja shetani, fahari zake na mambo yake yote na kujitoa kabisa kwa Yesu Kristo, Hekima aliyefanyika mwili, ili nyuma yake nibebe msalaba wangu siku zote za maisha yangu. Basi, ili niwe mwaminifu kwake kuliko nilivyokuwa mpaka sasa, nakuteua Maria uwe Mama yangu. Nakuachia na kukukabidhi mwili wangu na roho yangu, mema yangu ya ndani na vitu vya nje, hata thamani ya matendo yangu mema ya jana, ya leo na ya kesho… kwa hiyo uniweke miongoni mwa wale ambao unawapenda, unawafundisha, unawaongoza, unawalisha na kuwalinda. Ee Bikira mwaminifu, unifanye niwe katika yote mwanafunzi mkamilifu na mwigaji wa Hekima aliyefanyika mwili, Yesu Kristo Mwanao, hata nifikie kwa maombezi na mifano yako kwenye utimilifu wa ukomavu wake hapa duniani na wa utukufu wake mbinguni. Amina”.
Tazama pia
haririTanbihi
hariri- ↑ Martyrologium Romanum: ex Decreto Sacrosancti oecumenici Concilii Vaticani II instauratum auctoritate Ioannis Pauli P.P. II promulgatum, Romae 2001, ISBN 8820972107
Marejeo ya Kiswahili
hariri- Mt. Louis-Marie Grignon wa Montfort – tafsiri ya A. Nyenza, B.F. – ed. Mabratha wa Montfort wa Mt. Gabriel Tanzania -2000
Marejeo mengine
hariri- Vitabu vyake
- de Montfort, St. Louis. Preparation for Total Consecration according to the Method of St. Louis de Montfort. Bay Shore NY: Montfort Publications, 2001.
- de Montfort, St. Louis-Marie Grignion. True Devotion to Mary. translated by Mark L. Jacobson, Aventine Press, 2007 ISBN 1593304706.
- de Montfort, St. Louis. Secret of the Rosary ISBN 978-0895550569.
- de Montfort, St. Louis. God Alone: The Collected Writings of St. Louis Marie De Montfort Montfort Publications, 1995 ISBN 0910984557
- Maisha yake
- Biography of Saint Louis de Montfort [1] Ilihifadhiwa 24 Novemba 2009 kwenye Wayback Machine.
- Biography of Saint Louis de Montfort [2] Ilihifadhiwa 9 Januari 2008 kwenye Wayback Machine.
- Doherty, Eddie. Wisdom's Fool: A biography of St. Louis de Montfort. Bay Shore NY: Montfort Publications, 1993.
- Fiores, Stefano Dictionnaire de Spiritualité Montfortaine. (1360 pag.)Novalis, 1994
- Raja Rao, Joseph The Mystical Experience and Doctrine of St. Louis-Marie Grignion de Montfort Loyola Press, 2005, ISBN 9788878390300
- Hati za Papa Yohane Paulo II
- Pope John Paul II on de Montfort [3] Ilihifadhiwa 2 Desemba 2008 kwenye Wayback Machine.
- Pope John Paul II's encyclical Redemptoris Mater [4]
- Pope John Paul II's Apostolic Letter Rosarium Virginis Mariae [5]
Viungo vya nje
hariri- A Guide to Montfortian Spirituality Ilihifadhiwa 9 Mei 2008 kwenye Wayback Machine.
- Entry on the Catholic Encyclopedia about Saint Louis de Montfort
- Catholic Encyclopedia article on Missionaries of the Company of Mary - founded by de Montfort
- Catholic Books including True Devotion to Mary free online
- Montfort Center
- Founder Statue in St Peter's Basilica
- "Saint Louis Marie de Montfort" article at Catholicism.org
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |