Malindi (Kenya)

(Elekezwa kutoka Malindi, Kenya)


Malindi (iliwahi kujulikana kama Melinde) ni mji wa Kenya kwenye pwani ya Bahari Hindi. Iko takriban km 100  kaskazini kwa Mombasa, katika Malindi Bay kwenye mdomo wa mto Athi-Galana-Sabaki.

Malindi
Malindi is located in Kenya
Malindi
Malindi

Mahali pa mji wa Malindi katika Kenya

Majiranukta: 3°13′0″S 40°07′0″E / 3.21667°S 40.11667°E / -3.21667; 40.11667
Nchi Kenya
Kaunti Kilifi
Tovuti:  www.malindimunicipal.org
Nguzo ya Vasco da Gama.
Mtazamo wa zamani wa mji wa Malindi

Idadi ya wakazi ni takriban 207,253 (sensa ya mwaka 2009[1]): ndio mji mkubwa zaidi wa kaunti ya Kilifi na ni kitovu muhimu cha utalii kwenye pwani ya Kenya.

Malindi huhudumiwa na uwanja wa ndege na barabara kuu kati ya Mombasa na Lamu.

Historia

hariri

Malindi ni kati ya miji ya kale ya Waswahili. Mji umejulikana kuwepo tangu karne ya 13 BK kwenye mwambao uliojulikana kama "Azania" tangu zamani za Waroma na Wagiriki wa Kale. Kwa karne nyingi Malindi ilikuwa dola-mji muhimu wa Uswahilini ulioshindana na Mombasa juu ya kipaumbele kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki.

Wachina na Wareno kufika Malindi

hariri

Malindi ya karne ya 15 iliona ziara za wageni wawili kutoka mbali:

Mnamo 1414 jahazi za mpelelezi Mchina Zheng He zilifika Malindi. Sultani wa Malindi aliamua kumtuma balozi wa pekee pamoja na zawadi ya twiga kwenye meli hizi kwenda Nanking, mji mkuu wa China wakati huo. Mwaka 1419 Wachina walirudi na kuwarudisha mabalozi. Lakini ziara hizi hazikuleta mawasiliano ya kudumu kwa sababu China iliamua baadaye kidogo kuacha safari za upelelezi.

Mwaka 1498 Mreno Vasco da Gama alifika Malindi kutoka kusini katika safari yake ya kwanza ya kuelekea Bara Hindi. Wareno walikuwa watangulizi wa mataifa mengine ya Ulaya katika kutafuta njia ya Uhindi kwa sababu walitafuta faida ya biashara ya moja kwa moja iliyokuwa imebaki mikononi mwa wafanyabiashara Waislamu waliowahi kutawala biashara kati ya Ulaya na Asia.

Vasco da Gama alipatana kushirikiana na sultani wa Malindi kwa kusaini mkataba wa biashara ulioendelea mpaka mwisho wa kuwepo kwa Wareno Uswahilini. Alipewa nahodha ya kumwongoza hadi Bara Hindi, akajenga nguzo ya kumbukumbu unaosimama hadi leo karibu na bandari ya wavuvi Malindi. Nguzo hiyo inasimama hadi leo hii, ingawa kumekuwa na wito kutoka kwa wahafidhina kutunza nguzo hii, kwani mmomonyoko wa udongo unaweza kuangusha nguzo hii ndani ya bahari.

Katika mwaka wa 1499 Wareno walianzisha kituo cha biashara mjini Malindi ambacho kilikuwa kituo cha kupumzika njiani kwenda na kutoka India. Kanisa lilianza wakati huo.

Mwaka 1593 Wareno walihamisha kituo chao kutoka Malindi kwenda Mombasa walipojenga boma la Yesu.

Katika Uswahili mpya baada ya kufukuzwa kwa Wareno tangu mwaka 1693 umuhimu wa Malindi uliendelea kushuka na mnamo mwaka 1800 ilikuwa mahali pa pori na maghofu tu.

Utawala wa Zanzibar

hariri

Utawala wa Usultani wa Zanzibar ulifufua mji. Familia za makabaila kutoka kisiwa hicho na kutoka Omani walipewa ardhi karibu na Malindi wakaanza kujenga nyumba upya na kulima mashamba ya mazao ya biashara kama pamba kwa kazi ya watumwa.

Utawala wa Waingereza

hariri

Tangu mwaka 1888 Malindi pamoja na pwani ya Kenya ilikodishwa na Zanzibar kwa Uingereza na kuondoka katika utawala wa Sultani.

Kupigwa marufuku kwa utumwa wakati wa Waingereza ulisababisha kukwama kwa mashamba makubwa na kurudi nyuma tena kwa mji, ingawa Waingereza waliweka hapa kituo cha Mkuu wa Wilaya.

Utalii

hariri
 
Uvuvi wa Octopus.

Polepole mwambao mzuri wa Malindi umepata sifa kama mahali pa kupumzika kati ya Waingereza tangu miaka ya 1920. Hasa nafasi nzuri ya kuvua samaki kubwa ilivuta watalii wenye pesa kama Ernest Hemingway. Ndio mwanzo wa utalii wa Malindi.

Mji huu ni maarufu hasa miongoni mwa watalii kutoka Italia ambao wamependa Malindi na kununua nyumba na kujenga hoteli kadhaa.

Eneo hili laonyesha mifano maarufu ya usanifu wa Waswahili. Majengo mengi ya jadi huwa hadi leo, ikiwa ni pamoja na Msikiti wa Juma na ikulu katika pwani, eneo maarufu kwa watalii. Magofu ya Gedi (pia inajulikana kama Gede) ziko kusini mwa Malindi.

Utawala wa Mitaa

hariri

Malindi imeunda baraza la manispaa ikiwa na kata kumi na tatu zifuatazo: Barani, Ganda / Mkaumoto, Gede, Gede Kaskazini, Gede Kusini, Kijiwetanga, Madunguni, Malimo, Malindi kati, Malindi Kaskazini, Maweni, Shella, mji wa Watamu. Zote ziko ndani ya jimbo la Malindi. [2]

Malindi ina maeneo nane zifuatazo: Chakama, Ganda, Gede, Goshi, Jilore, Langobaya, Malindi na Watamu.[3]

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. Sensa ya Kenya 2009 Archived 9 Januari 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya KNBS, ilitazamwa Januari 2009.
  2. Vituo vya kupigia kura nchini Kenya. Archived 25 Juni 2008 at the Wayback Machine. Tume ya Uchaguzi ya Kenya (The defunct ECK) (www.eck.or.ke)
  3. Kenya Tawala Levels 1-4. Archived 21 Mei 2011 at the Wayback Machine. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu.

Viungo vya nje

hariri