Muhammad Ali Pasha

(Elekezwa kutoka Muhammad Ali of Egypt)

Kwa watu wengine wenye jina hili tazama Muhammad Ali (maana)

Muhammad Ali Pasha

Muhammad Ali Pasha (kwa Kiarabu محمد علي باشا, Februari 1769 - 2 Agosti 1849) alikuwa mwanajeshi wa Milki ya Osmani aliyeendelea na kuwa mtawala wa Misri na Sudan.

Hata kama alipaswa kukubali rasmi ukuu wa Sultani wa Osmani na kutawala kama gavana wake, alifanya Misri kuwa nchi ya kujitegemea akaunda nasaba ya watawala wa Misri walioendelea hadi mwaka 1952.

Anatazamwa kama mwanzilishi wa Misri ya sasa kutokana na mabadiliko makubwa aliyoleta katika jeshi, uchumi na utamaduni wa Misri.

Utoto na kuja Misri

hariri

Alizaliwa mjini Kavala (leo hii nchini Ugiriki, wakati ule Milki ya Osmani) na lugha yake ya kwanza ilikuwa Kialbania. Hakusoma shule, akajifunza kusoma na kuandika tu alipokuwa na miaka 40.

Baba yake alikuwa mwanajeshi akifanya pia biashara ya tumbaku na Muhammad Ali alimfuata baba katika shughuli zote mbili. Mwaka 1787 alimwoa Amina (17701823).

Mwaka 1801 Milki ya Osmani ilikusanya jeshi la kwenda Misri iliyowahi kuvamiwa na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kikosi cha askari 300 kutoka Kavala kilikuwa sehemu ya jeshi hilo na Muhammad Ali alishiriki akiwa makamu wa mkuu wa kikosi. Baada ya kifo cha mkuu miaka kadhaa baadaye aliongoza kikosi hiki cha Waalbania.

Kupanda ngazi

hariri

Baada ya kuwafukuza Wafaransa kulitokea ugomvi katika Misri kati ya wawakilishi wa Sultani na mamluki wa Misri. Mamluki wa Misri walikuwa askari watumwa waliowahi kutawala Misri kwa karne kadhaa kwa niaba ya Sultani. Wamamluki walidhoofishwa kutokana na uvamizi wa Kifaransa na idadi yao ilipungukua lakini hawakutaka kuachana na nafasi yao ya utawala.

Katika ugomvi uliofuata gavana mpya wa Kiosmani alifukuzwa na wanajeshi, kwa kushindwa kulipa mishahara yao. Mkuu mpya alikuwa mwanajeshi aliyeuawa na wapinzani wake, hapo mkuu wa Mamluki alitawala tena juu ya Kairo.

Baada ya yeye kudai kodi kubwa kutoka kwa wananchi viongozi wa Kairo waliwasiliana na Muhammad Ali aliyetumia kikosi chake cha Waalbania kuwafukuza Wamamluki kutoka Kairo mwaka 1804.

Gavana mpya wa Sultani aliwakasirisha tena wananchi wa Kairo kwa madai ya kodi kubwa na mwaka 1805 ulema na viongozi wazalendo walimpiga kura Muhammad Ali kuwa gavana mpya akathibitishwa na serikali ya Sultani.

Mwaka 1807 Waingereza walivamia Aleksandria na hapo Muhammad Ali akajiunga na Wamamluki akafaulu kuwafukuza. Lakini aliona Wamamluki kama hatari na mwaka 1811 alikaribisha viongozi kwa karamu kubwa kwake Kairo akawaua wote.

Mkuu wa Misri

hariri

Kazi yake ya kwanza ilikuwa kubadilisha jeshi lake kuwa la kisasa baada ya kuona uwezo wa majeshi ya Ulaya kutokana na nidhamu na usimamizi tofauti. Baada ya Waalbania wake kukataa mabadiliko, aliwatuma kupiga vita Uarabuni walipokufa.

Shabaha yake ilikuwa kujenga dola lenye nguvu kwa kuiga mifano ya Ulaya. Alilenga kutenga Misri na Milki ya Osmani na kuanzisha nasaba ya watawala kutoka watoto wake. Kwa kufikia shabaha hiyo alipaswa kubadilisha jamii ya Misri, kuimarisha uchumi, kupata wasomi kwa kazi za utawala na kupata jeshi la kisasa.

Alianzisha mfumo mpya wa kodi ambako serikali yenyewe ilipokea kodi badala ya kukodisha haki ya kusanya kodi kieneo kwa mawakala. Alidai kodi pia kutoka mashamba ya wakfu za taasisi za Kiislamu.

Wakulima na wazalishaji wa bidhaa walipaswa kuuza mavuno na bidhaa kwa serikali pekee iliyoendelea kuuza vitu hivyo ndani na nje ya Misri. Hapo ilikuwa hasa kilimo cha pamba kilicholeta faida kubwa kwa Misri. Pia serikali yake ilipanua eneo la mashamba kwa kutengeneza mifereji ya umwagiliaji.

Pamoja na kupanua sekta ya kilimo, Muhammad Ali alijenga pia tasnia mbalimbali. Alianza viwanda vya silaha kama gobori na mizinga. Huko Aleksandria alianzisha kiwanda cha meli kwa kujenga manowari. Alianzisha pia viwanda vya nguo.

Kwa sehemu kubwa ya shughuli za ujenzi pamoja na jeshi alitegemea kulazimisha wakulima. Wakulima wengi walijaribu kuepuka, wengine walikimbia nchi. Kwa kuepukana na huduma ya kijeshi katika vita vyake wengine walijikata kidole cha mkono wa kulia au kujiharibu jicho moja.

Alituma vijana Ulaya wapate kuona na kujifunza jinsi gani mambo ya utawala, elimu na teknolojia yanashughulikiwa huko akiwapa baadaye kazi katika ofisi za serikali. Alitumia vijana hao pamoja na Wazungu kuanzisha shule na hospitali.

Akiwa gavana wa Sultani katika Misri alipewa kazi ya kufanya vita kwa niaba ya serikali ya Waosmani. Alifaulu kuwashinda Waarabu wa Al-Saud na kuteka Makka na Madina. Baadaye alivamia Sudan akaunda mji wa Khartoum. Shabaha yake ilikuwa kukamata watumwa wengi akitaka kuwatumia baadaye kama wanajeshi wake lakini wengi walikufa kabla ya kufika Misri.

Mwaka 1824 Sultani alidai usaidizi wa Muhammad Ali kukandamiza uasi wa Wagiriki. Jeshi kubwa lilienda Ugiriki likawashinda, lakini baadaye nchi za Ulaya waliingilia kati, wakazamisha manowari ya Muhammad Ali hata alipaswa kurudisha jeshi lake Misri.

Mwaka 1831 alidai apewe mamlaka pia juu ya Shamu (Syria) iliyokuwa jimbo la Milki ya Osmani. Alipokataliwa alivamia nchi hii akashinda mara kadhaa jeshi la Waosmani, akaendelea hadi Konya katika Anatolia (leo Uturuki wenyewe) na Sultani Mahmud II alikubali utawala wa Muhammad Ali juu ya Shamu.

Mwaka 1839 mapigano kati ya jeshi la Muhamad Ali na Waosmani yalianza upya. Nchi za Ulaya yaani Uingereza, Austria, Prussia na Urusi ziliogopa kuporomoka kwa Milki ya Osmani wakamlazimisha Muhammad Ali kurudisha Shamu na Uarabuni kwa Sultani, wakimkubali mwenyewe na nasaba yake kama mtawala wa Misri.

Miaka yake ya mwisho Muhammad Ali alikuwa mgonjwa; mwishoni alishindwa kuelewa habari ya milki yake akaaga dunia mjini Aleksandria tarehe 2 Agosti 1849 akazikwa Kairo katika msikiti aliowahi kuujenga.

  Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Muhammad Ali Pasha kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.