Pio wa Pietrelcina

Pio wa Pietrelcina (25 Mei 1887 - 23 Septemba 1968) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mtawa wa Ndugu Wadogo Wakapuchini.

Mt. Pio wa Pietrelcina.

Kwa miaka 50 katika konventi ya San Giovanni Rotondo alijitosa kuongoza kiroho waumini na kupatanisha watubu pamoja na kushughulikia kwa upendo maskini wa kila aina.

Alivumilia kishujaa kupingwa na kudhulumiwa, lakini pia aliheshimiwa na umati wa watu, kutokana na karama zake za pekee na wingi wa miujiza iliyoshuhudiwa nao.

Alimaliza maisha yake akiwa amelinganishwa vizuri ajabu na Yesu msulubiwa [1].

Mwaka 2002 alitangazwa na Papa Yohane Paulo II kuwa mtakatifu: sikukuu yake inaadhimishwa kila tarehe 23 Septemba, siku ya kifo chake[2].

Miaka ya kwanza (1887-1918)

hariri

Alizaliwa na wakulima Grazio Maria Forgione na Maria Giuseppa De Nunzio tarehe 25 Mei 1887 huko Pietrelcina, karibu na Benevento, akabatizwa kesho yake katika kanisa la Mtakatifu Anna na kupewa jina la Francesco kwa heshima ya Fransisko wa Asizi.

Tarehe 27 Septemba 1899 alipokea sakramenti za Kipaimara na Ekaristi.

Francesco hakufuata shule kwa utaratibu uliotarajiwa kwa sababu alitakiwa kusaidia familia yake shambani.

Alipofikia umri wa miaka 12 padri Domenico Tizzani, alimsomesha kwa miaka 2 elimu yote ya msingi.

Hamu ya kuwa mtawa na padri ilijitokeza mapema, hasa kwa kumuona bradha Camillo wa Sant'Elia a Pianisi akipitia kijijini kuombaomba. Mwaka 1902 alianza utaratibu wa kujiunga na shirika, ambalo baada ya kumkataa mara ya kwanza, lilimkubali.

Alisimulia kuwa tarehe 1 Januari 1903 alianza kujaliwa njozi: moja ilimfunulia wito wake wa kupambana na shetani, nyingine ilimhakikishia upendeleo wa Mungu na Bikira Maria.

Tarehe 22 Januari alianza mwaka wa unovisi kwa jina la ndugu Pio. Kisha kuumaliza na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu, alikwenda masomoni na tarehe 27 Januari 1907 aliweka nadhiri za daima.

Mnamo Novemba 1908 alihamia Montefusco, kwa masomo ya teolojia. Tarehe 18 Julai 1909 alipewa daraja takatifu ya ushemasi, na tarehe 10 Agosti 1910 ile ya upadri.

Miaka hiyo alianza kuugua sana na kupatwa na mateso yaliyomshirikisha yale ya Yesu, kama vile madonda mikononi, mapigo ya mijeledi na taji la miba kichwani.

Madonda kutokea kwa namna ya kudumu (1918-1920)

hariri
 
Picha ya Padre Pio kijana ikionyesha madonda yake ya mikononi.

Akiwa San Giovanni Rotondo, katika wilaya ya Foggia, mkoa wa Puglia, mnamo Agosti 1918 Pio alisema ameanza kutokewa na mtu anayemchoma kwa mkuki ubavuni, na hatimaye akaonekana na madonda matano ya Yesu.

Ukaguzi (1919-1931)

hariri

Viongozi wa Kanisa walianza kutuma mfululizo wataalamu kufanya uchunguzi uliomsumbua sana padri Pio.

Hatimaye tarehe 31 Mei 1923 walitoa hati ya kuangalisha watu wasiamini ni mambo ya Kimungu.

Miaka 8 baadaye ilitolewa hati nyingine iliyomkataza asiadhimishe Misa hadharani wala sakramenti ya kitubio. Padri Pio alitii kwa unyenyekevu wote.

Ukaguzi mpya (1933-1968)

hariri

Mwaka 1933 Papa Pius XI alifuta makatazo hayo na Pius XII alihimiza watu kumtembelea.

Tarehe 9 Januari 1940 kwa misaada iliyotoka duniani kote alianza ujenzi wa hospitali kubwa Casa Sollievo della Sofferenza ili kutibu na kuliwaza wagonjwa.

Mwaka 1950 idadi ya watu waliotaka kuungama kwake iliongezeka na kuhitaji ufanyike mpango wa kujiandikisha.

Papa Yohane XXIII aliagiza ukaguzi mwingine kutokana na mashtaka mapya, lakini Papa Paulo VI alikuwa anamheshimu sana.

Madonda yake yalitoweka wakati wa Misa siku tatu kabla ya kifo, kilichotokea tarehe 23 Septemba 1968 padri Pio akiwa na miaka 81.

Kutangazwa mtakatifu

hariri

Kuna ushahidi wa watu mbalimbali kuhusu Padri Pio kuwa na karama ya kusoma moyo wa mtu, kupatikana mahali pawili kwa wakati mmoja (kwa Kiingereza: bilocation) n.k.[3]

Kesi ya kumtangaza mwenye heri ilianza mapema, lakini ilichukua muda mrefu, kutokana na upinzani wa watu mbalimbali.

Papa Yohane Paulo II, aliyewahi kumtembelea padri Pio miaka 40 ya nyuma, tarehe 21 Januari 1990 alitangaza ushujaa wake katika maadili yote, tarehe 2 Mei 1999 alimtangaza mwenye heri na tarehe 16 Juni 2002 alimtangaza mtakatifu.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. https://www.santiebeati.it/dettaglio/71750
  2. Martyrologium Romanum
  3. Carroll-Cruz, Joan (Machi 1997). Mysteries Marvels and Miracles In the Lives of the Saints. Illinois: TAN Books. ku. 581. ISBN 978-0-89555-541-0.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya nje

hariri
 
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.