Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni
Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni mwa waadilifu wote wa duniani, toharani na mbinguni ndio chemchemi isiyoumbwa ya maisha ya Kiroho kadiri ya imani ya Wakatoliki, Waorthodoksi na wengineo.
Katika Biblia
haririKwanza Mungu yumo katika viumbe vyote kwa kuwa hana mipaka: “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko” (Zab 139:7-8). “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi… hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu” (Mdo 17:24-28). Kwa hakika, Mungu anaona vyote, anadumisha vyote, na kuongoza kila kiumbe kitende jinsi inavyokifaa.
Lakini Maandiko yanasema pia juu ya uwemo wa pekee wa Mungu katika waadilifu. “Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yoh 14:23). Hayatakuja tu mambo yaliyoumbwa (kama vile neema inayotia utakatifu, maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu), bali watakaokuja ni walewale wanaopenda, Baba na Mwana wasiotenganika na Roho Mtakatifu, ambaye Yesu alimuahidi na kumtuma wazi kwenye Pentekoste: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele… Ndiye Roho wa kweli… anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu…” (Yoh 14:15-17). Hao watakuja si kwa muda, bali watafanya makao yao ndani ya mwadilifu mpaka atakapodumu katika upendo.
Maneno hayo hayakuwahusu mitume tu: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:8). Huyo anaye Mungu moyoni mwake, lakini hasa Mungu anaye huyo ndani mwake akimdumishia si tu uhai wa kimaumbile, bali pia ule mpya wa neema na upendo. “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). Hatukujaliwa tu upendo ulioumbwa, bali Roho Mtakatifu aliye Upendo-Nafsi. Hao wamo ndani mwetu, lakini tutafananishwa nao kikamilifu hapo tu tutakapopokea mwanga wa utukufu. “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? ...Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe” (1Kor 3:16; 6:19). Hivyo Maandiko yanafundisha wazi kuwa Nafsi tatu za Mungu zinaishi katika waadilifu wote.
Katika Mapokeo
haririMwanzoni mwa karne II, Inyasi wa Antiokia aliwaita Wakristo halisi “waleta Mungu” kwa sababu wanaye ndani mwao. Lusia wa Sirakusa alikiri ukweli huo mbele ya mahakimu, “Ndio, wale wote wanaoishi kwa usafi na imani ni mahekalu ya Roho Mtakatifu”. Atanasi wa Aleksandria alisema kuwa Nafsi tatu za Mungu zimo ndani mwetu. Bazili Mkuu alitamka kuwa Roho Mtakatifu kwa kukaa ndani mwetu anatufanya tuwe watu wa Kiroho zaidi na kufanana na Mwana Pekee. Sirili wa Aleksandria pia alisema juu ya muungano huo wa ndani kati ya mwadilifu na Roho Mtakatifu.
Upande wa magharibi, Ambrosi alifundisha kuwa tumempata katika ubatizo na zaidi katika kipaimara. Augustino alithibitisha kwa shuhuda za mababu waliomtangulia kwamba hatupewi neema tu, bali tunajaliwa Mungu mwenyewe, yaani Roho Mtakatifu.
Ukweli huo uliofunuliwa unawekwa na Ualimu wa Kanisa machoni petu tena. Mtaguso wa Trento umesema, “Anayetufanya waadilifu ni Mungu ambaye kwa huruma yake anatutakasa bure na kutufanya watakatifu, akitupaka mafuta na kututia mhuri wa Roho Mtakatifu tuliyeahidiwa ambaye ni dhamana ya urithi wetu (taz. Ef 1:13-14)”. Papa Leo XIII alifafanua zaidi, “Inafaa sana tukumbuke maelezo yaliyotolewa na walimu wa Kanisa kadiri ya mafundisho ya Maandiko matakatifu: Mungu yumo katika vitu vyote kwa uwezo wake, kwa sababu vyote viko chini yake; halafu kwa uwepo wake, kwa sababu vyote viko wazi mbele yake; tena kwa undani wake, kwa sababu yumo ndani ya viumbe vyote kama chanzo cha uwepo wao. Lakini katika binadamu Mungu hayumo tu kwa namna ile ambayo yumo katika vitu vyote, bali zaidi kwa kujulikana na kupendwa naye, kwa sababu umbile letu wenyewe linatufanya tupende, tutamani na kufuata yaliyo mema. Kwa neema yake Mungu anakaa katika roho adilifu kama hekaluni kwa namna ya ndani na ya pekee kabisa. Ndipo kinapotokea kile kiungo cha upendo kinachofungamanisha roho na Mungu kuliko mtu na rafiki yake mkuu na kinachoifanya imfurahie kwa ukamilifu wote. Kwa ukweli wote muungano huo wa ajabu - ambao unaitwa uwemo ndani na unatofautiana na hali ya wenye heri wa mbinguni kwa namna yake tu - unasababishwa na uwemo wa Utatu mzima: ‘tutakuja kwake, na kufanya makao kwake’ (Yoh 14:23). Hata hivyo unasemwa kuwa hasa kazi ya Roho Mtakatifu, kwa kuwa tunaona alama za uwezo na za hekima ya Mungu hata katika mtu mwovu, lakini mwadilifu tu anashiriki upendo, ambao ni sifa ya Roho Mtakatifu... Wingi wa mema ya kimbingu unaosababishwa na uwemo wa Roho Mtakatifu katika roho adilifu unajitokeza kwa namna mbalimbali... Kati ya zawadi hizo zimo tahadhari za siri, na mialiko ya kifumbo ambavyo roho zinajaliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, na ambavyo visipokuwepo hatuwezi kujitahidi katika maadili, wala kuendelea, wala kufikia wokovu wa milele”.
Ufafanuzi wa teolojia
hariri“Mbali ya neema inayotia utakatifu hakuna linaloweza kuangaza jambo hilo, kwamba Nafsi ya Kimungu imo ndani mwetu kwa namna mpya... Ili tuwe nayo ni lazima tuweze kuifurahia na kuitumia. Sasa hatuwezi kufurahia Nafsi ya Kimungu isipokuwa kwa neema inayotia utakatifu na upendo” (Thoma wa Akwino). Pasipo hayo Mungu hakai ndani mwetu. Haitoshi kumjua kimaumbile (kama mwanafalsafa), wala kwa imani iliyokufa (kama Mkristo mwenye dhambi ya mauti). Ni lazima tumjue kwa imani hai na vipaji vya Roho Mtakatifu vinavyohusiana na upendo. Hiyo namna ya mwisho ya kumjua Mungu inampata si kama jambo la mbali tulilohadhitiwa tu, bali kama jambo ambalo lipo, tunalo na tunaweza kulifurahia tangu sasa.
Ili Nafsi za Kimungu zikae ndani mwetu, inatakiwa tuweze kuzifahamu kama kwa mang'amuzi ya kimapenzi, ambayo msingi wake ni upendo tuliomiminiwa unaotulinganisha na maisha ya ndani ya Mungu. Si lazima tumjue hivyo kila nukta; inatosha tuweze kufanya hivyo kwa neema ya maadili na vipaji. Basi uwemo wa Utatu Mtakatifu katika mtu mwadilifu unadumu usingizini pia, mpaka atakapodumu katika neema inayotia utakatifu. Ila mara mojamoja inatutokea kumtambua Mungu kama kiini cha roho yetu na uhai wa maisha yetu: “Mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rom 8:15-16). “Roho Mtakatifu anaithibitishia roho yetu kwa kusababisha ndani mwetu upendo kama wa mwana kwa baba” (Thoma wa Akwino). Upendo huo ni ishara inayotutia hakika fulani ya kwamba tuna neema inayotia utakatifu.
Basi, kwa namna fulani Utatu Mtakatifu unakaa katika roho adilifu vizuri kuliko Yesu anavyokaa katika maumbo ya ekaristi, kwa kuwa yeye yumo kweli katika maumbo hayo, lakini yenyewe hayamjui wala hayampendi. Kumbe Utatu Mtakatifu umo ndani ya mwadilifu kama katika hekalu hai linaloujua na kuupenda (kwa kiasi tofautitofauti). Umo katika wenye heri wa mbinguni wanaoutazama moja kwa moja, hasa ndani ya roho ya Mwokozi ambayo Neno ameungana nayo katika Nafsi moja. Kuanzia dunia hii, katika mwanga/giza la imani, Utatu Mtakatifu unakaa ndani mwetu, ingawa hatuuoni, ukizidi kutuuhisha hadi saa ya kuingia utukufu. Uwemo huo hautuondolei haja ya kukaribia ekaristi, kwa kuwa Utatu Mtakatifu unakaa ndani ya Kristo kuliko unavyokaa ndani mwetu. Ikiwa ni faida kumkaribia mtakatifu wa Mungu, jinsi gani tunafaidika tukimkaribia Mwanae!
Yatokanayo kwa maisha ya kiroho
haririIkiwa uwemo wa Utatu Mtakatifu ndani mwetu unatuwezesha kumjua Mungu kama kwa mang'amuzi, maana yake ujuzi huo si jambo la pekee (kama njozi) bali lipo katika njia ya kawaida ya utakatifu. Ujuzi huo unatokana na imani iliyoangazwa na vipaji vinavyohusiana na upendo. Kama ni hivyo, unatakiwa kustawi kadiri upendo unavyostawi. Sala ya kumiminiwa, ambayo ni kuchanua kwa aina hiyo ya ujuzi/mang'amuzi, inaanza katika hatua ya mwanga na kukamilika katika hatua ya muungano. Ujuzi huo wa Mungu na wa wema wake utakua pamoja na ule wa unyonge wetu.
Jambo lingine linalotokana na hayo tuliyosema ni kwamba upendo uliomo ndani mwetu unapostawi sana, Nafsi za Kimungu zinakuwemo mwetu kwa undani zaidi, yaani kirafiki zaidi: ndivyo inavyotokea k.mf. wakati wa uongofu wa pili ambao ni mwanzo wa hatua ya mwanga. Hatimaye hao Watatu wamo ndani mwetu si tu kusudi tuwafahamu na kuwapenda kwa namna ipitayo maumbile, bali wamo kama asili ya vitendo vinavyopita maumbile, kama Yesu alivyosema, “Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi” (Yoh 5:17), hasa katika kiini cha roho.
Lakini kiutendaji ikumbukwe kwamba kwa kawaida Mungu anajitoa kwa mtu kadiri huyo alivyo tayari kumpokea. Akiwa safi zaidi, ndani mwake Nafsi za Kimungu zinakuwemo na kufanya kazi zaidi. Hapo Mungu ni wetu nasi ni wake, na tunatamani kuliko yote tuendelee katika upendo wake. “Jambo hilo ni kati ya yale yanayotusukuma zaidi kuendelea Kiroho, kwa sababu linaifanya roho iwe daima na juhudi kwa maendeleo yake, iwe macho ili kuzaa mfululizo vitendo vyenye nguvu na motomoto zaidi na zaidi kuhusu maadili yote, ili kwa kukua katika neema, ustawi huo umlete upya Mungu ndani mwake… kwa ajili ya muungano wa dhati zaidi, wa kudumu zaidi na imara zaidi” (L. Chardon).
Mgeni huyo wa Kimungu anatuambia, “Mwanangu, nipe moyo wako” (Mith 23:26). “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” (Ufu 3:20). Mwadilifu anafanana na mbingu, kwa sababu Utatu Mtakatifu umo ndani mwake, lakini bado ana giza mpaka atakapojaliwa kuuona waziwazi ndani mwake.
Kwa kifupi wajibu wa mwadilifu kwake ni kama ifuatavyo:
- kumfikiria mara nyingi, kwa kujiambia, “Mungu anaishi ndani mwangu”.
- Kumwekea wakfu siku zetu, tena kila saa, kwa kusema, “Kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu”.
- Kukumbuka alivyo chemchemi ya mwanga, ya faraja na ya nguvu kwetu.
- Kumuomba kadiri ya neno la Bwana: “Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Math 6:6).
- Kumuabudu kwa kusema, “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu” (Lk 1:46-47).
- Kumuamini, kumtumainia, kumpenda kwa upendo unaozidi kuwa safi, mkarimu, wenye nguvu.
- Kumpenda kwa kumuiga hasa katika wema: “Basi iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6:36). “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu” (Yoh 17:21).
Hayo yote yanatuonyesha kwamba maisha ya Kiroho upande wa mafumbo (ambapo mang'amuzi ya Mungu kuwemo ndani mwetu ni ya sasa hivi) si ya pekee, bali ni ukamilifu wa kawaida. Watakatifu tu, ambao wanayo kwa kiasi kikubwa, wapo kweli wanapotakiwa. Kabla hatujafikia muungano huo wa ndani na Mungu, sisi ni kama tumesinziasinzia: fumbo tamu la uwemo wake tunalijua bado kijuujuu, kumbe ndio uzima tele tuliokaribishwa; hatujamuabudu wala kumpenda Mungu inavyotakiwa, na pengine tunahesabu kile ambacho pekee ni cha lazima kana kwamba si muhimu kuliko vyote; vilevile hatujaelewa kwa dhati ukuu wa zawadi tuliyopewa katika ekaristi, wala Mwili wa fumbo wa Kristo ni nini.
Roho Mtakatifu ndiye anayehuisha Mwili wa fumbo ambao Yesu ndiye kichwa chake. Kama vile roho nzima imo katika mwili wote na katika kila kiungo, nayo inafanya kazi bora kichwani, vivyo hivyo Roho Mtakatifu yumo mzima katika Mwili wote wa fumbo, naye anafanya kazi bora ndani ya Mwokozi na kwa njia yake kwetu pia. Kiini cha uhai kinachounganisha hivyo Mwili wa fumbo kina nguvu ya kuunganisha kuliko roho inavyounganisha mwili wake, na kuliko umoja wa familia au taifa fulani. Hivyo vinaunganishwa tu na namna fulani ya kutazama, kupima, kuhisi, kupenda, kutaka na kutenda. Roho anayeunganisha Mwili wa fumbo ana nguvu pasipo mfano, kwa sababu ni Roho aletaye utakatifu, ni chemchemi ya maji hai yanayobubujikia uzima wa milele. Mto wa neema zote unaotokana naye unapanda juu tena umrudie Mungu kama ibada, sala, stahili na sadaka. Ndiyo mambo yapitayo maumbile tunayopaswa kuyajua zaidi na zaidi. Upande wa mafumbo tu ndipo roho inapozinduka na kutambua zawadi ya Mungu ilivyo, kwa namna ile hai, ya ndani na angavu tunayohitaji ili kumrudishia kikamilifu upendo alionao kwetu.
Uwemo wa Utatu Mtakatifu katika roho iliyotakata
haririMbinguni Nafsi tatu za Mungu wanaishi katika roho iliyotakata kama katika hekalu ambamo wanajulikana na kupendwa. Utatu Mtakatifu unaonekana wazi ndani mwa roho hiyo unayoidumisha katika uhai na katika neema isiyoweza kupotezwa. Hivyo kila mwenye heri ni kama tabenakulo hai, kama hostia iliyogeuzwa, tena yenye ujuzi na upendo upitao maumbile. Utangulizi wa hali hiyo unapatikana duniani katika mtu aliyekamilika aliyefikia muungano unaotugeuza tutakaouzungumzia mbele. Kwa sasa tuseme kuwa muungano huo wa dhati ni wa nadra lakini si nje ya utaratibu wa kawaida, kwa sababu ni mwendelezo wa uwemo wa Utatu Mtakatifu ndani ya kila mwadilifu. Uhai unaoletwa na neema inayotia utakatifu ni mbegu ya utukufu; kimsingi ni uhai uleule wa milele. Ikiwa mbinguni Utatu Mtakatifu umo rohoni mwa mwenye heri ambamo unaonekana bila kizuio, ni lazima uwemo tayari ndani ya mwadilifu katika giza la imani, ukijulikana na kama kung’amuliwa naye kadiri alivyotakata. Kama vile roho inavyojing’amua kuwa asili ya matendo yake, inajaliwa pia kumtambua Mungu kama asili ya matendo yapitayo maumbile ambayo isingeweza kuyasababisha pasipo uvuvio maalumu toka juu. Kadiri mtu alivyotakata, anatofautisha ndani mwake yale yanayotokana naye kwa msaada wa kawaida wa Mungu, na yale yanayotokana na uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu.
Utambuzi huo wa uwemo wa Mungu unategemea hasa kipaji cha hekima kinachotufanya tupime mambo ya Kimungu kwa kulingana nayo, kwa hisi ipitayo maumbile inayotegemea upendo, na kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu anayetumia hisi hiyo aliyotutia ili tumtambue. Hivyo tunaonja mafumbo ya wokovu na uwemo wa Mungu ndani mwetu kwa mfano wa wanafunzi wa Emau walioambiana, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia Maandiko?” (Lk 24:32). Ni ujuzi ambao unafanana na mang’amuzi, unapita mifuatano ya mawazo na kulingana na ule wa roho inayojifahamu kama asili ya matendo yake. Mungu, asili ya neema na ya wokovu, yumo ndani mwetu kuliko sisi wenyewe, naye anatuvuvia tutende mambo ya dhati tusiyoyaweza peke yetu, na ndivyo anavyojitambulisha kwetu kama chanzo cha maisha ya Kiroho.
Ujuzi huo unafanana tu na mang’amuzi kwa sababu mbili: 1) haumfikii Mungu moja kwa moja, inavyotokea kwa kumuona mbinguni, bali katika tendo la upendo wa kitoto analolisababisha ndani mwetu; 2) hatuwezi kutofautisha kwa hakika matendo hayo ya upendo yapitayo maumbile na miruko ya moyo wetu inayofanana nayo: hivyo tusipojaliwa ufunuo maalumu hatuwezi kuwa na hakika ya mia kwa mia ya kwamba tuna neema inayotia utakatifu.
Uwemo wa Utatu Mtakatifu unadumu hata usingizini, mpaka tunapodumu kuwa tumeunganika na Mungu kutokana na hali ya neema. Lakini ni wazi kuwa muungano huo wa kawaida unalenga muungano tunaouzungumzia sasa, hata ule wa dhati zaidi unaotugeuza. Basi, katika roho iliyotakata inazidi kuonekana hali ipitayo maumbile ya kufanana na Mungu. Roho kwa umbile lake inayo tayari sura ya Mungu, kwa kuwa si mwili na inaweza kujua na kupenda. Kwa neema inayotia utakatifu, asili ya maadili ya Kimungu, inaweza pia kumjua na kumpenda Mungu kwa namna ipitayo maumbile. Kadiri neema hiyo na upendo vinavyokua vinatutenganisha na mambo ya chini na kutuunganisha na Mungu. Hatimaye mbinguni neema kamili itatuwezesha kumuona moja kwa moja anavyojiona na kumpenda anavyojipenda. Hapo hali ya kufanana naye itakamilika, upendo usioweza kupotezwa utatufananisha na Roho Mtakatifu aliye upendo-nafsi; heri ya kumuona Mungu itatufananisha na Neno ambaye akiwa uangavu wa Baba atatufananisha naye. Kutokana na hayo tunaelewa unavyotakiwa kuwa tangu hapa duniani muungano kamili ambao ni utayari wa moja kwa moja wa kujaliwa heri ya kumuona mara baada ya kufa bila kupitia toharani. Ndiyo siri ya maisha ya watakatifu. Pengine hali hiyo ipitayo maumbile ya kufanana na Mungu na Yesu inadhihirika mwilini pia.
Dalili za Utatu Mtakatifu kuwemo katika roho iliyotakata
haririDalili hizo zilitajwa na Thoma wa Akwino alipojiuliza kama mtu anaweza kujua ana hali ya neema. Ingawa hazimwezeshi kuwa na hakika ya imani juu ya hali hiyo, zinamwezesha kukaribia meza ya Bwana bila kuogopa kukufuru. Zile muhimu zaidi zinaorodheshwa kama ifuatavyo kuanzia zile za chini.
1) Ushuhuda wa dhamiri njema isiyojisikia kuwa na dhambi yoyote ya mauti. Ndiyo dalili ya msingi inayodaiwa na zile ambazo zinaifuata na kuithibitisha.
2) Furaha ya kusikia Neno la Mungu, si kwa kulisikiliza tu, bali kwa kulitekeleza.
3) Kuonja hekima ya Mungu hata kujisomea Injili ili kutafuta roho yake ndani ya maneno na kujilisha hata kuhusu fumbo la msalaba, ukiwa ni pamoja na ule wa kuubeba siku kwa siku.
4) Elekeo la kuongea na Mungu kwa ndani, na kuanza tena maongezi hayo yakikatika. “Urafiki unamuelekeza mtu atake kuongea na rafiki yake. Maongezi ya mtu na Mungu yanafanyika kwa kumkazia macho katika sala ya kumiminiwa, kadiri ya maneno ya mtume Paulo, ‘Sisi wenyeji wetu uko mbinguni’ (Fil 3:20). Kwa kuwa Roho Mtakatifu anatutia upendo wa Mungu anatuelekeza vilevile kumtazama. Ndiyo sababu mtume alisema pia, ‘Sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho’ (2Kor 3:18)” (Thoma wa Akwino). Kabla ya hayo, mwalimu huyo wa Kanisa aliandika kuwa maongezi ya ndani na Mungu ni kama ufunuo wa mawazo ya siri zaidi, kwa maana sisi hatuna cha kumficha, naye anatukumbusha maneno ya Injili yanayotuonyesha yale yote yanayotupasa dakika kwa dakika. Ndiyo matokeo ya urafiki ambao “kwa namna fulani unaunganisha mioyo miwili kuwa mmoja, hivi kwamba tunachomfunulia rafiki halisi tunaona hakijatutoka”.
5) Kumfurahia Mungu, kwa kukubali kwa dhati matakwa yake hata katika mapingamizi. Pengine wakati wa kuvunjika moyo tunatiwa furaha safi na ya juu inayoondoa huzuni yoyote. Hiyo ni dalili kubwa ya kutembelewa na Bwana. Yesu alipomuahidi Roho Mtakatifu alimuita Mfariji. Kwa kawaida tunamfurahia kadiri tunavyotimiza amri zake, kwa kuwa hivyo tunazidi kuwa moyo mmoja naye.
6) Uhuru wa wana wa Mungu. “Wana wa Mungu wanaongozwa na Roho Mtakatifu si kama watumwa, bali kama viumbe huru… Roho Mtakatifu anatufanya tutende akiongoza utashi wetu wenye hiari utake, kwa sababu anatufanya tumpende Mungu na anatuelekeza tutende kwa upendo wake, si kwa hofu kama watumwa” (Thoma wa Akwino). “Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rom 8:15-16). “Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru” (2Kor 3:17), yaani ukombozi kutoka utumwa wa dhambi. “Kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi” (Rom 8:13). Ndio ukombozi halisi, yaani uhuru mtakatifu wa wana wa Mungu wanaotawala pamoja naye juu ya tamaa, juu ya roho ya ulimwengu na juu ya uovu.
7) Kumzungumzia Mungu kama kwa kufurika toka moyoni. Kwa namna hiyo “mahubiri yanatakiwa kutokana na ukamilifu wa kuzama katika mafumbo ya imani” (Thoma wa Akwino). Roho Mtakatifu anazidi kujitokeza kwetu kama chemchemi ya neema mpya daima, “chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele” (Yoh 4:14), chemchemi isiyokwisha ya mwanga na upendo. Ndiyo faraja yetu kati ya huzuni za hapa uhamishoni. Katika matatizo ya kimataifa ya wakati huu, linadumu tumaini kubwa, kwa kuwa mkono wa Bwana haujafupika. Tunaona alivyo mwingi wa huruma daima katika watakatifu anaozidi kuwaleta ulimwenguni. Ndio watumishi wake wakuu wenye mifano bora ya imani, tumaini na upendo, ambayo mingi tunaweza kuifuata.
Kwa msimamo huo inafaa wanaoishi Kiroho wajiweke wakfu kwa Roho Mtakatifu ili kuongozwa naye zaidi kwa kutambua na kufuata minong’ono yake, kama vile wanavyojiaminisha kwa Maria ili awaongoze kwa Mwanae, na wanavyojiweka wakfu kwa Moyo mtakatifu wa Yesu awafikishe kwa Baba yake.
Sala ya Mt. Elizabeti wa Utatu
haririEe Mungu wangu, Utatu, ninayekuabudu, unisaidie nijisahau kabisa ili nikukazie wewe bila ya kubadilika na kwa utulivu, kama kwamba roho yangu ingekuwa tayari katika uzima wa milele.
Kisiwepo chochote cha kuvuruga amani yangu wala cha kunitoa nje yako, wewe usiyebadilika, uliye wangu; bali kila nukta nizidi kuzama katika vilindi vya fumbo lako!
Tuliza roho yangu; uifanye iwe uwingu wako, makao yako unayoyapenda zaidi na mahali pa pumziko lako. Humo nisikuache kamwe peke yako; bali niwemo mzima, mwenye kukesha na kutenda kwa imani yangu, mwenye kuzama katika kuabudu, mwenye kujiachilia kikamilifu kwa utendaji wako Muumba.
Ee Kristo mpendwa wangu, uliyesulubiwa kwa upendo, nataka kuwa bibiarusi wa moyo wako, nataka kukujaza utukufu, nataka kukupenda hadi kufa kwa upendo! Lakini nahisi unyonge wangu wote: hivyo nakuomba uwe vazi langu, ulinganishe matendo yote ya roho yangu na yale ya roho yako, unizamishe ndani mwako, uenee ndani yangu, ushike nafasi yangu, ili maisha yangu yake kioo cha maisha yako tu. Njoo ndani mwangu ili uabudu, ufidie, uokoe.
Ee Neno wa milele, Neno wa Mungu wangu, nataka kutumia maisha yangu kukusikiliza, nataka kuwa msikivu kabisa kwa mafundisho yako, nijifunze yote kwako, halafu katika usiku wa roho, katika utupu, katika unyonge nataka kukukazia macho daima na kubaki chini ya uangavu wako mkuu. Ee nyota yangu ninayoiabudu, unichanganye hata nisiweze tena kukwepa mng’ao wako.
Ee moto unaoteketeza, Roho wa upendo, ushuke ndani yangu ili katika roho yangu itokee aina ya umwilisho wa Neno! Niwe kwake mwendelezo wa ubinadamu wake ambapo aweze kutekeleza upya fumbo lake.
Nawe Baba uniinamie mimi kiumbe chako maskini, unifunike kwa kivuli chako, usione ndani yangu kitu kingine isipokuwa mpenzi wako uliyependezwa naye sana.
Enyi watatu wangu, yote yangu, heri yangu, upweke usio na mipaka, upana ambao napotea ndani yake, najiachilia kwenu kama mateka. Mzame ndani mwangu ili nami nizame ndani mwenu, wakati ninapongojea kuja kutazama katika mwanga wenu kilindi cha ukuu wenu[1].
Tanbihi
hariri- ↑ Order of Carmelites, Holy Trinity, Whom I Adore Archived 8 Novemba 2019 at the Wayback Machine., accessed 8 November 2019
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Uwemo wa Utatu Mtakatifu rohoni kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |