Majina ya nyota yanapatikana kwa nyota mia kadhaa zinazoonekana vema kwa macho matupu. Majina hayo yanaweza kuwa tofauti katika tamaduni mbalimbali duniani. Katika matumizi ya kisasa ni hasa majina kutoka urithi wa Ugiriki ya Kale, Roma ya Kale na Uarabuni ndio hasa yanayoendelea kutumiwa hadi leo. Pamoja na desturi ya kutunga majina kwa nyota angavu kuna pia desturi ya kupanga nyota za anga katika kundinyota zenye majina. Kundinyota ni idadi ya nyota zinazoonekana karibu kwenye anga ya usiku.

Ramani ya Ulimwengu kufuatana na Ptolemaio - Dunia iko katikati ikizungukwa na njia za sayari, Jua na Mwezi. Sayari zinachorwa hapa miungu ya Kiroma iliyotoa majina yao kwa sayari katika lugha za Ulaya

Leo hii Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA) unatumia mpangilio wa kundiyota 88 zenye majina maalumu na ndani ya kundinyota hizi ilitambua majina rasmi kwa nyota angavu zaidi. UKIA ulianza kuorodhesha majina yenye asili ya Kigiriki na Kiarabu ikaendelea kukubali pia majina kutoka urithi wa tamaduni mbalimbali. Hadi mwaka 2017 majina 313 yalitambuliwa hivyo na UKIA.[1]

Kusudi la kubuni majina ya nyota

Mataifa mengi walitumia elimu ya nyota kwa kupanga kalenda yao. Kila baada ya mwaka mmoja nyota za anga zinaonekana tena jinsi zilivyokaa siku 365.25 zilizopita. Nyota nyingi hazionekani mwaka wote, hivyo kuonekana kwa nyota fulani iliweza kuwa ilani ya kuandaa mashamba, na hapo asili ya jina la „Kilimia“ katika lugha za Kibantu kwa fungunyota mashuhuri. Mabaharia kama Wagiriki na Waswahili wa Kale walitegemea nyota kwa kutafuta njia zao baharini wakati wa usiku katika karne pasipo na GPS wala dira. Wasafiri katika nchi za joto kama Uarabuni walipaswa kusafiri hasa gizani ili kuepukana na joto hatari la mchana walipotegemea nyota sawa na mabaharia ili wasipotee jangwani. Matumizi hayo ya elimu ya nyota yalirahisishwa kwa kutumia majina yaliyoeleweka.

Mataifa mengi yalipamba elimu yao kwa kuunganisha nyota na hadithi za wazee kuhusu mashujaa wa kale na miungu ya imani yao. Hadi leo tunatumia kumbukumbu ya mitholojia ya Wagiriki na Waroma tukitaja kundinyota kama Andromeda (sw. Mara (kundinyota)) au Hercules (sw. Rakisi (kundinyota)); majina ya UKIA kwa sayari yanatunza majina ya miungu ya Kiroma kama vile Mercurius, Venus, Mars, Jupiter na kadhalika.

Historia ya majina ya kimagharibi ya nyota

 
Picha ya kundinyota Farisi (Perseus) katika kitabu cha Kiajemi; nyota zilitajwa kulingana na picha kama "ya bega, ya kando, ya mguuni, ya mkononi, ya kichwani" na majina haya ya Kiarabu mara nyingi yamekuwa chanzo cha majina ya kisasa.

Kumbukumbu ya kale zaidi kuhusu majina ya nyota imehifadhiwa kutoka tamaduni za Mesopotamia kama Babeli na Sumeri. Walitazama nyota kwa umakinifu mkubwa wakipanga kalenda na hivyo waliweka misingi ya astronomia. Walitambua tofauti kati ya nyota za kawaida zisizobadilika, nyota zinazotembea angani, yaani sayari, na nyota zinazoonekana kwa muda mfupi tu kama vile vimondo au nyotamkia. Ilhali waliamini ya kwamba nyota ni wawakilishi wa miungu yao, waliunda pia imani ya kwamba miendo ya nyota inaruhusu kutabiri nia ya miungu na hivyo waliweka misingi kwa elimu ya unajimu iliyoendelea sambamba na astronomia bila kutofautishwa kwa karne nyingi. Elimu ya Babeli ilikuwa msingi kwa maendeleo ya elimu hii katika Ugiriki ya Kale na Uhindi.

Wagiriki waliendeleza elimu walioirithi na kuiunganisha na falsafa na hisabati wakilenga kueleza miendo ya nyota iliyotazamwa angani. Elimu yao ilipokelewa kutoka Waroma wa Kale walioendelea kutafsiri majina mengi kwa lugha yao ya Kilatini.

Hitimisho ya elimu ya kale kuhusu nyota ni kitabu cha Almagesti kilichoandikwa mnamo mwaka 200 BK na Klaudio Ptolemaio huko Aleksandria, Misri na kuwa kitabu kikuu cha astronomia kwa zaidi ya miaka 1000 baadaye. Humo nyota zinatajwa kufuatana na nafasi zao katika picha zilizochorwa za kundinyota, mfano "kwenye goti, kwenye mguu wa kushoto, ya kichwani, ya mkononi, ya bega“ na kadhalika.

Baada ya kuporomoka kwa ustaarabu wa Wagiriki na Waroma, ni Waarabu Waislamu waliovamia sehemu kubwa za maeneo yao na kuyatawala. Walianza kutafsiri vitabu vya Wagiriki na kuendeleza elimu yao, pia kuhusu nyota. Kuhusu majina ya Wagiriki walitafsiri sehemu ya majina hayo, kwa nyota nyingi walitumia majina ya kale ya Kiarabu, na hasa walitafsiri maelezo ya Ptolemaio katika Almagesti. Matoleo ya Almagesti yalitafsiriwa baadaye kutoka Kiarabu kwa Kilatini kilichokuwa lugha ya elimu ya Ulaya ya Magharibi ambako elimu ya kale ilisahauliwa tayari.

Kuanzia karne ya 15 na 16 elimu ilianza kusogea mbele katika Ulaya na kupita sayansi ya nchi za Kiislamu. Tangu ugunduzi wa darubini na tafiti za Galileo Galilei nchini Italia nyota nyingi mpya zilijulikana. Teknolojia ya ubaharia ya Ulaya iliwezesha kuzunguka Dunia yote ikaleta umuhimu mpya wa elimu ya nyota kwa kusudi ya kukadiria njia baharini na kuchora ramani.

Wataalamu wa Ulaya walirejea vitabu vya Kiarabu na mara nyingi kutumia majina waliyoyakuta mle. Mfano ni jina la nyota Rigel = mguu kutoka ar. رجل rijil. Wakati mwingine walitambua asili ya majina ya Kiarabu katika hadithi za Wagiriki na Waroma zilizojulikana huko Ulaya na hapo walitumia majina ya Kigiriki na Kilatini, hasa kwa ajili ya kundinyota kama vile Aries, Taurus, Leo, Virgo. Halafu walijitahidi kubuni majina mapya kwa ajili ya kundinyota na nyota muhimu kwenye angakusi zilizotazamiwa na mabaharia Wareno, Wahispania, Waingereza, Waholanzi na Wafaransa waliozunguka sasa kote duniani na kuchora ramani za nyota ambazo hazikujulikana kwa wazee wa Kiarabu na Kigiriki.

Majina ya kimataifa ya nyota kulingana na UKIA

Urithi huu wa mchanganyiko uliingia katika kawaida ya astronomia ya kisayansi iliyopanuka mbio tangu karne ya 19. Urithi huo ulikuwa pia msingi wa orodha za kwanza za kimataifa zilizotungwa katika karne ya 20 tangu kuundwa kwa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA). Kwa hiyo majina yaliyokubaliwa kwa matumizi ya kimataifa ni mchanganyiko wa majina yenye asili ya Kigiriki, Kilatini na Kiarabu. Orodha hii inaendelezwa na kamati ya UKIA kwa jina la IAU Catalog of Star Names (IAU-CSN)[2]

Majina ya nyota kwa Kiswahili na katika tamaduni nyingine

tazama makala ya pekee Majina ya nyota kwa Kiswahili

Tamaduni mbalimbali zina historia ya kuangalia na kutumia nyota pamoja na majina yao. Mapokeo ya kimaandishi hupatikana hasa katika China na Uhindi.

Waswahili wa Kale walitegemea pia nyota wakiwa mabaharia stadi waliovuka Bahari Hindi yote. Hapa kuna urithi mkubwa wa majina ya nyota kwa Kiswahili. Majina hayo yalipokewa kiasili hasa kutoka Kiarabu, lakini pia kutoka Kiajemi na lugha za Kihindi.

Majina ya kimtaifa na namba za orodha

Pamoja na kugunduliwa kwa nyota nyingi mpya kadiri ya kuboreshwa kwa vifaa vya darubini, orodha za nyota zilitungwa ambako nyota zilitajwa zaidi kwa namba fulani kuliko majina. Hata hivyo majina ya nyota zilizojulikana tangu kale yanaendelea kutumiwa. Orodha ya kwanza ya aina hii imekuwa majina ya Bayer, ambako nyota inatajwa kwa jina la kundinyota halafu herufi ya Kigiriki kwa utaratibu wa mwangaza wake. Baada ya muda ilionekana idadi ya herufi za Kigiriki haikutosha kwa idadi kubwa ya nyota na hapo majaribio mengine yalifuata kama namba za Flamsteed.

Wakati violwa vipya vilipogunduliwa katika mfumo wa Jua wanaastronomia waliendelea kutumia majina kutoka mitholojia ya Kiroma au ya Kigiriki, kwa mfano majina ya Uranus na Neptun kwa sayari za mbali, na pia majina ya miezi ya sayari hizo. Tangu mwanzo wa karne ya 21 UKIA ilichagua pia majina kutoka mitholojia ya mataifa mbalimbali ya Dunia hata nje ya mapokeo ya Kigiriki - Kiarabu.

Leo hii wanaastronomia wanatumia mifumo mbalimbali kandokando na zaidi orodha zinazoweza kutunzwa kwa kompyuta tu ambazo zinaorodhesha mamilioni ya nyota. Hizi zinatajwa pamoja na majina ya kale kwa nyota angavu 200-300 na majina ya Bayer kwa takriban nyota 1500.

Marejeo

  1. Naming stars
  2. IAU Catalog of Star Names (IAU-CSN), tovuti ya Ukia ya 19 November 2017, iliangaliwa Juni 2018
 
Mradi wa Astronomia Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano