Historia ya Kiswahili imeanza takriban miaka 1000 iliyopita kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki.

Maeneo yenye wasemaji wa Kiswahili.

Neno Swahili lina asili ya Kiarabu: Sahil ina maana ya pwani; sawahil ’’as-sawāhilī’’ (السواحلي) ni wingi wake kwa kumaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu au utamaduni wa eneo la pwani.

Lugha ya Wabantu iliyoenea kwa njia ya biashara

Utafiti umeonyesha kwamba vyanzo vya Kiswahili vilikuwa katika lugha za jamii ya wakulima Wabantu waliofika kwenye pwani za Bahari Hindi; wataalamu hutofautiana wakiona asili hiyo ama kwenye mpaka wa Kenya na Somalia au Kenya na Tanzania za leo. Wasemaji wa kwanza walikuwa karibu na wasemaji wa Kipokomo, Kimijikenda na Kikomori[1].

Mababu hao wa Waswahili wa baadaye waliunda vijiji kwenye pwani ilhali chakula chao kilikuwa hasa samaki na kome. Walijifunza kusafiri baharini wakaanza kushiriki katika biashara iliyoendelea kwenye pwani za Bahari Hindi tangu miaka kabla ya Kristo. Mfumo wa upepo wa monsuni unawezesha safari za mbali kwa kutumia vyombo sahili kwa kufuata upepo kutoka kaskazini kuelekea kusini, kusubiri huko hadi kugeuka kwa upepo na kurudi tena. Mnamo mwaka 800 BK Unguja Ukuu (kusini mwa mji wa Zanzibar) ilikuwa kitovu cha biashara ya kimataifa kwenye maeneo ya Tanzania ya leo.[2]

Utamaduni wa Kiislamu kwenye pwani

Pamoja na wafanyabiashara kutoka nchi za Kiislamu kufika kusini, watu wa pwani walisafiri wenyewe hadi Uarabuni na Bara Hindi; hapo waliweza kujiunga na Uislamu ambako kulileta faida mbalimbali: walikingwa zaidi wasikamatwe kuwa watumwa (iliyokuwa vigumu zaidi ukiwa Mwislamu), walikubaliwa kama washirikiki katika mfumo wa biashara iliyokingwa na sheria za Kiislamu. Vilevile wafanyabiashara kutoka kaskazini walikuwa salama zaidi wakikaa miezi kadhaa kwenye miji iliyotokea ikifuata desturi za Kiislamu. Misikiti ilianza kujengwa kwenye makazi ya pwani na vijiji vilibadilika kuwa miji[3].

Kiswahili kilienea kama lugha ya miji na bandari za biashara ya kimataifa kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki. Lahaja za Kiswahili ziliendelea tofauti kiasi kutokana na athira ya lugha za majirani tofauti kwenye kanda ndefu ya pwani[4]; wataalamu wanaona makundi ya lahaja za kaskazini (pwani za Kenya na Somalia) na lahaja za kusini (pwani za Tanzania na Msumbiji). Kufuatana na biashara na dini lahaja zote zilipokea maneno ya Kiarabu kwa viwango tofauti; katika Kiswahili sanifu cha kisasa chenye asili katika lahaja ya Unguja kiasi hicho hukadiriwa takriban theluthi moja ya maneno yote[5].

Kuna masimulizi kuhusu vyanzo vya miji kama vile Kilwa, Lamu ambamo miji hiyo ilianzishwa na wakimbizi kutoka Uajemi, hasa kutoka Shiraz, waliooa wenyeji. Hadi leo wenyeji wengine wa pwani na funguvisiwa la Zanzibar hujiita "Washirazi". Siku hizi wataalamu wengi hukubaliana kwamba masimulizi hayo si taarifa ya kihistoria ila visasili. Hata hivyo, utafiti wa DNA ya mifupa ya watu 80 iliyopatikana kwenye makaburi ya miji ya Waswahili kuanzia kisiwa cha Manda, Faza na Mtwapa huko Kenya hadi Kilwa, Songo Mnara na Lindi kusini mwa Tanzania, umeonyesha kwamba sampuli nyingi zilizochunguzwa zilitokana na watu waliozaliwa na mababu wa mchanganyiko kati ya wanaume Waajemi (kutoka Iran) na wanawake Waafrika.[6]

Utamaduni mpya ulijitokeza uliokuwa wa Kiafrika na wa Kiislamu ukajielewa kuwa sehemu ya dunia ya Uislamu. Hivyo Kiswahili kilizaliwa kuwa lugha ya Kibantu kilichopokea maneno mengi ya asili ya nje.

 
Kiswahili kiliandikwa pekee kwa herufi za Kiarabu hadi karne ya 19. Picha inaonyesha matini kwenye sanamu ya askari huko Dar es Salaam, Tanzania. Inasema: "Huu ni ukumbusho wa askari wenyeji Waafrika waliopigana katika Vita Kuu."

Lugha iliandikwa kwa herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 BK. Kwa bahati mbaya leo hatuna tena maandiko ya kale sana, kutokana na hali ya hewa kwenye pwani isiyosaidia kutunza karatasi na kurasa zenyewe zinaweza kuoza kutokana na unyevu hewani pamoja na wadudu wengi walioko katika mazingira ya pwani.

Lakini maandiko ya kale yanayopatikana kutoka karne ya 17 huonyesha ya kwamba tenzi na mashairi vinafuata muundo uliotangulia maandiko yenyewe kwa karne kadhaa. Sehemu kubwa ya maandiko ya kale ni tenzi yaani mashairi yenye aya maelfu. Tenzi ndefu kabisa inahusu kifo cha Mtume Muhamad ikiwa na aya 45,000.

Kiswahili kimepokewa kwa urahisi na wenyeji kwa sababu walikosa lugha ya pamoja kati yao, lugha za Kibantu ziko karibu sana na athira ya Kiarabu ilikuwa kilekile kote pwani. Haya yote yalisaidia kujenga umoja wa Kiswahili katika eneo kubwa la pwani ya Afrika ya Mashariki.

Kiajemi pia kilichangia maneno mbalimbali, kama vile "bibi" na "cherehani".

Kufika kwa Wareno huko Afrika ya Mashariki kuanzia mwaka 1500 kulileta athira mpya ikiwa maneno kadhaa ya Kireno yameingia katika Kiswahili kama vile "bendera", "gereza" na "meza".

Kuwepo kwa wafanyabiashara Wahindi katika miji mikubwa ya pwani kuliingiza pia maneno ya asili ya Kihindi katika lugha kama vile "lakhi", "gunia" n.k. Athira ya lugha za Kihindi iliongezeka kiasi baada ya Waingereza kutumia Wahindi wengi kujenga reli ya Uganda.

Lugha ya biashara

Kiswahili kilitumika kama lugha ya biashara baina ya watu wa pwani na bara katika kanda ndefu sana kutoka Somalia hadi Msumbiji wa Kaskazini. Wafanyabiashara Waswahili waliendeleza biashara ya misafara hadi Kongo.

Kiswahili kiliendelea kuenea kwenye njia za misafara hii. Kila msafara ulihitaji watu mamia hadi maelfu wa kubeba mizigo ya biashara kutoka pwani hadi pale msafara ulipolenga hata Ziwa Tanganyika. Watu hawa wote walisambaza matumizi ya Kiswahili katika sehemu za ndani.

Lakini katika maeneo fulani biashara hii ilijenga pia kizuizi. Watu kama Waganda waliona Kiswahili ni lugha ya Waislamu tena lugha ya biashara ya watumwa; hivyo hadi leo ni wagumu kukubali Kiswahili.

Wamisionari Wakristo wa awali, kama Ludwig Krapf, Edward Steere na A.C. Madan, walifanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza pamoja na kuunda mfumo wa kuandika Kiswahili kwa herufi za Kilatini.

Kiswahili wakati wa ukoloni

Karne ya 19 ilileta utawala wa kikoloni. Wakoloni walitangulia kufika katika bandari za pwani wakatumia mara nyingi makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani wakijenga vituo vyao barani. Watu hao walieneza Kiswahili pande za bara.

Wajerumani waliamua kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo walitumia kazi ya utafiti iliyofanywa na wamisionari.

Utawala wa kikoloni ulirahisisha mawasiliano kati ya wenyeji. Reli zilijengwa na wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali walishirikiana. Waafrika walilazimishwa kulipa kodi kwa wakoloni, hivyo walitafuta kazi ya ajira. Hasa katika mashamba makubwa yaliyolima mazao ya biashara pia katika migodi ya Kongo watu wa makabila mengi walichanganyikana wakitumia hasa Kiswahili kati yao. Kwa namna hiyo lugha ilienea zaidi.

Waingereza baada ya kuchukua Tanganyika kutoka kwa Wajerumani waliendela kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala. Kuanzia mwaka 1930 waliunda kamati yenye shabaha ya kuunganisha lahaja mbalimbali na kuunda Kiswahili cha pamoja kwa ajili ya Afrika ya Mashariki (Inter-territorial Language (Swahili) committee for the East African Dependencies). Mwenyekiti alikuwa Frederick Johnson, makatibu R. K. Watts, P. Mzaba na Seyyid Majid Khalid Barghash. Kamati hiyo iliamua kutumia lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa Kiswahili cha pamoja kilichoendela kufundishwa shuleni. Leo hii ni Kiswahili rasmi kinachofunzwa na wanafunzi na kuandikwa magazetini na vitabuni.

Miaka ya ukoloni ilisababisha pia kupokelewa kwa maneno mapya katika Kiswahili. Kijerumani kiliacha maneno machache kama "shule" (Kijerumani Schule) na "hela" (Heller) lakini maneno mengi sana ya asili ya Kiingereza yalipokelewa.

Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti sana, kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya Kibantu ya Kiswahili.

Lugha ya kimaandishi

Tofauti na lugha nyingi za Afrika, Kiswahili kiliandikwa tangu karne kadhaa kwa herufi za Kiarabu. Mwandiko wa Kiarabu huwa na herufi kadhaa kwa sauti ambazo haziko katika lugha za Kibantu, vilevile kuna sauti kama "p" au "g" ambazo hazina herufi kwa Kiarabu[7]. Ilhali miji ya Waswahili kwenye eneo kubwa kutoka Somalia hadi Msumbiji ilijitegemea, hapakuwa na tahajia sanifu.

Jedwali ifuatayo inaonyesha matumizi iliyokuwa kawaida mara nyingi.

Kiswahili kwa mwandiko wa Kiarabu Kiswahili kwa mwandiko wa Kilatini
mwishoni katikati mwanzoni herufi pekee
ـا ا aa
ـب ـبـ بـ ب b p mb mp bw pw mbw mpw
ـت ـتـ تـ ت t nt
ـث ـثـ ثـ ث th?
ـج ـجـ جـ ج j nj ng ng' ny
ـح ـحـ حـ ح h
ـخ ـخـ خـ خ kh h
ـد د d nd
ـذ ذ dh?
ـر ر r d nd
ـز ز z nz
ـس ـسـ سـ س s
ـش ـشـ شـ ش sh ch
ـص ـصـ صـ ص s, sw
ـض ـضـ ضـ ض dhw
ـط ـطـ طـ ط t tw chw
ـظ ـظـ ظـ ظ z th dh dhw
ـع ـعـ عـ ع ?
ـغ ـغـ غـ غ gh g ng ng'
ـف ـفـ فـ ف f fy v vy mv p
ـق ـقـ قـ ق k g ng ch sh ny
ـك ـكـ كـ ك
ـل ـلـ لـ ل l
ـم ـمـ مـ م m
ـن ـنـ نـ ن n
ـه ـهـ هـ ه h
ـو و w
ـي ـيـ يـ ي y ny

Kiswahili leo

Katika Tanzania Kiswahili kimekuwa lugha rasmi ya serikali na taifa. Shule za msingi hutumia Kiswahili lakini shule za sekondari na vyuo bado zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Tarehe 15 Februari 2015 rais Jakaya Kikwete alitangaza mpango wa kubadilisha lugha ya elimu nchini kwa kutumia Kiswahili kwenye ngazi zote hadi shule za sekondari na chuo kikuu. [8]

Kenya imetangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa lakini inaendelea kutumia Kiingereza katika shughuli za serikali. Watu wa matabaka ya juu mara nyingi hupendelea kutumia Kiingereza wakiona ni lugha bora. Lakini tangu 1986 wanafunzi wote wanatakiwa kujifunza Kiswahili katika shule za sekondari. Tatizo mojawapo ni kuwepo wa makabila makubwa kama Wakikuyu au Waluo wenye wasemaji wengi sana katika eneo moja, hali isiyosaidia kujifunza lugha tofauti. Pia kaskazini na magharibi mwa Kenya wenyeji wengi si wasemaji wa lugha za Kibantu nao hawaoni Kiswahili ni lugha rahisi.

Uganda inatumia Kiswahili kama lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo haikuongeza upendo wa Waganda kwa lugha kutokana na historia ya Uganda ya kuwa na vita na serikali za kijeshi. Lakini kinasikika pia kama lugha ya biashara masokoni. Pamoja na kwamba Waganda walikichukulia Kiswahili kama lugha ya kitumwa lakini pia lugha hii ilionekana kuwa na ustaarabu wa Kiarabu zaidi, yaani Uislamu. Lugha ya Kiswahili ilitumika katika kueneza dini hiyo.

Mashariki mwa Kongo Kiswahili kimeenea sana: ni moja kati ya lugha nne za kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwenye visiwa vya Ngazija (Comoros) kuna lahaja mbalimbali za Kiswahili zinazotumika na wananchi.

Tazama pia

Tanbihi

  1. Martin Walsh: The Swahili language and its early history, uk. 125 katika "The Swahili World", Routledge 2018, ISBN: 978-1-138-91346-2
  2. "Around the mid-eighth century, small but significant quantities of Chinese wares began to arrive, along with beads from Sri Lanka and large quantities of glazed and unglazed wares from the Persian Gulf"; ona Mark Horton na Felix Chami: Swahili origins, uk. 125 katika "The Swahili World", Routledge 2018, ISBN: 978-1-138-91346-2
  3. Mark Horton na Felix Chami: Swahili origins, uk. 144 ff
  4. Walsh u. 126
  5. Mark Horton na Felix Chami: Swahili origins, uk. 136
  6. Brielle, E.S., Fleisher, J., Wynne-Jones, S. et al. Entwined African and Asian genetic roots of medieval peoples of the Swahili coast. Nature 615, 866–873 (2023). https://doi.org/10.1038/s41586-023-05754-w, online hapa
  7. Hata hivyo, kuna wasemaji wa lahaja za Kiarabu kwa mfano Misri wanaotamka "g" wakisoma herufi ya ج ambayo ni "j" kwa Kiarabu sanifu
  8. "Sera mpya ya elimu (raiamwema)". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-04-19. Iliwekwa mnamo 2015-03-25.

Marejeo

  • Shihabdin Chiraghdin et Mathias E. Mnyampala. Historia ya Kiswahili. Oxford University Press, 1977.
  • Nurse, D. and Hinnebusch, T. J. 1993. Swahili and Sabaki: A Linguistic History. Berkeley and Los Angeles: University of California Press.
  Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Kiswahili kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.