Mbeya (mji)
Jiji la Mbeya ni mji mkubwa kusini-magharibi mwa Tanzania yenye hadhi ya jiji yenye Postikodi namba 53100.
Jiji la Mbeya | |
Mahali pa mji wa Mbeya katika Tanzania |
|
Majiranukta: 8°53′24″S 33°25′48″E / 8.89000°S 33.43000°E | |
Nchi | Tanzania |
---|---|
Mkoa | Mbeya |
Wilaya | Mbeya Mjini |
Idadi ya wakazi | |
- Wakazi kwa ujumla | 300,000 |

Mbeya ni kitovu cha Nyanda za Juu za Kusini ambazo ni eneo la uzalishaji wa mazao mengi.
Ni makao makuu ya mkoa.
Jiografia Edit
Mji umeenea katika bonde kati ya safu za milima ya Mbeya na milima ya Uporoto. Mlima mkubwa unaoonekana kutoka mjini ni Mlima wa Mbeya (Mbeya Peak) wenye urefu wa m 2818.
Eneo la mji ni kati ya m 1600 kitovuni na m 1900 au zaidi juu ya UB kwenye mitelemko ya mlima Loleza.
Hali ya hewa haina joto kali kutokana na kimo. Wakati wa Juni-Julai halijoto wakati wa usiku inaweza kushuka chini hadi 0 °C, mlimani hata chini zaidi.
Mvua zinaanza mwezi Novemba hivyo ni wakati wa kupanda. Kwa kawaida mvua zinasimama tena Januari-Februari na kunyesha kwa wingi Machi-Aprili.
Uti wa mgongo wa mji ni barabara kuu ya TANZAM inayounganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.
Kitovu kipya cha mji kinahamishwa kwenda kata ya Foresti iliyoko kando ya barabara kuu.
Historia Edit
Jina la Mbeya limetokana na neno la Kisafwa "Ibheya" ambayo maana yake ni chumvi, kwani miaka mingi wafanyabiashara walikuwa wanafika mahali hapo kubadilishana mazao yao kwa chumvi.
Mlima mkubwa ulio karibu ulijulikana kwa jina la "Mbeya"[1] wakati wa ukoloni wa Kijerumani, na mji ulipokea baadaye jina kutokana na mlima huu.
Mji wa kisasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati ule dhahabu ilianza kupatikana mlimani karibu na Mbeya hadi Chunya.
Edit
Mji ulianzishwa katika sehemu zinazoitwa bado Uhindini, Uzunguni na Majengo. Mji ulipangwa kufuatana na kawaida ya miji wa kikoloni ya Afrika ya Mashariki kuwa na sehemu tatu:
- Uzunguni ni sehemu ya nyumba za Wazungu na karibu na ofisi za serikali (District Officer, polisi, mahakama)
- Uhindini ni mtaa wa biashara uliokuwa hasa mikononi mwa wafanyabiashara wenye asili ya Uhindi na
- Majengo kama sehemu kwa wafanyakazi Waafrika na familia zao.
Makanisa ya kale kama ishara ya historia Edit
Mahali pa makanisa ya kale panaonyesha ugawaji huu wa kihistoria:
- Kanisa la Anglikana lililokuwa dhehebu rasmi la Uingereza lipo chini ya Uzunguni na karibu na ofisi za kiserikali (zinazoelekea siku hizi kuhamishwa kwenda Foresti) kama Mkuu wa Mkoa na mahakama. Kanisa hili ni jengo dogo kwa sababu lilipangwa kwa kundi dogo la maafisa na wafanyabiashara pamoja na wakulima Waingereza wa Mbeya.
- Kanisa la mjini la Moravian, ambalo ni dhehebu la Kikristo asilia la Mbeya liko Majengo iliyokuwa sehemu kwa Waafrika. Kati ya Waingereza hawakuwepo Wamoravian.
- Kanisa Kuu Katoliki lilihudumia Wazungu wachache, hasa Waeire, kati ya wakoloni pamoja na Wahindi kutoka Goa na pia Waafrika: kwa hiyo iko kati ya Uzunguni na Uhindini karibu na Majengo.
Mji uliendelea kupanuka pande zote. Barabara kuu ya TANZAM inaunganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.
Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi ni Wakristo, hasa wafuasi wa Kanisa Katoliki, Kanisa la Moravian na Kanisa la Kilutheri. Makundi makubwa mjini ni Wasafwa (wenyeji) na Wanyakyusa waliohamia kutoka Rungwe. Wanyakyusa ndio waliotangulia kuleta Ulutheri mjini.
Mawasiliano Edit
Mbeya ni njiapanda ya njia mbalimbali muhimu: Barabara kuu ya lami kutoka Dar es Salaam (km 850) hugawanya hapa kwenda Malawi – Msumbiji kupitia Tukuyu/Rungwe, na kwenda Zambia – Afrika Kusini kupitia Tunduma/Mbozi.
Vilevile njia ya reli ya TAZARA hupita Mbeya kuelekea Zambia. Kuna ghala kubwa kwa ajili ya mizigo ya Malawi inayofikishwa kwa reli kutoka Dar es Salaam bandarini ikihamishwa kwa malori kwenda Malawi.
Mbeya imekuwa na uwanja wa ndege mdogo usiokuwa na huduma ya kawaida kwa muda mrefu. Lakini kuna mipango ya kujenga uwanja mpya huko Songwe zipatazo km 40 kufuata njia ya kwenda Zambia.
Tangu miaka ya 1990 kitovu cha mji kinahamishwa kutoka eneo la zamani kwenda karibu na barabara kuu ya Dar es Salaam – Zambia.
Wakazi Edit
Mbeya ni mji wa nne kwa ukubwa nchini Tanzania. Idadi ya wakazi imehesabiwa kuwa 385,279 katika sensa ya mwaka 2012. Wengine 300,000 hivi wanaishi katika mazingira karibu na Mbeya mjini.
Kiasili Mbeya ilikuwa eneo la Wasafwa. Siku hizi sehemu kubwa ya wakazi wanaweza kuwa mchanganyiko wa Wasafwa pamoja na makabila ya Wanyakyusa kutoka wilaya za Rungwe na Kyela, Wanyiha kutoka Mbozi, Wandali kutoka Ileje na Wakinga kutoka Makete.
Uchumi Edit
Uchumi wa Mbeya mjini umetegemea kilimo cha mazingira yake na biashara.
Viwanda mbalimbali vilianzishwa, lakini havikufaulu sana. Kuna viwanda kwa mfano Zana za kilimo, Highland Soap, Mbeya Textiles. Mbeya Ceramics iliporomoka kitambo.
Elimu Edit
Pamoja na shule za sekondari kuna taasisi kadhaa za elimu ya juu kama vile:
- Chuo Kikuu Teofilo Kisanji ambacho ni chuo kikuu cha Kanisa la Moravian Tanzania kinachotoa kozi za ualimu na teolojia tangu mwaka 2005. Kilitanguliwa na chuo cha Motheco.
- Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) ambacho zamani kilijulikana kama Mbeya Technical College (MTC) kilichopo eneo la Iyunga, Mbeya
- Chuo cha Kilimo Uyole (Agricultural Research Institute -ARI- Uyole) ambacho ni taasisi ya uchunguzi wa kisayansi pamoja na chuo.
- Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Kampasi ya Mbeya ambacho ni tawi la Chuo Kikuu Mzumbe kilichopo Morogoro
Waandishi toka jiji la Mbeya Edit
Marejeo Edit
- ↑ Wajerumani waliandika "Mbeja" wakitamka "j" kama "y", linganisha Kamusi ya Koloni za Kijerumani, makala "Usafua"
Viungo vya nje Edit
- Maelezo ya Manispaa ya Mbeya toka Redet Archived 27 Machi 2009 at the Wayback Machine.
Kata za Jiji la Mbeya - Tanzania | ||
---|---|---|
Foresti • Ghana • Iduda • Iganjo • Iganzo • Igawilo • Ilemi • Ilomba • Isanga • Isyesye • Itagano • Itende • Itezi • Itiji • Iwambi • Iyela • Iyunga • Iziwa • Kalobe • Maanga • Mabatini • Maendeleo • Majengo • Mbalizi Road • Mwakibete • Mwansekwa • Mwansanga • Nonde • Nsalaga • Nsoho • Nzovwe • Ruanda (Mbeya) • Sinde • Sisimba • Tembela • Uyole |