Nikon wa Urusi

(Elekezwa kutoka Patriarch Nikon)

Nikon ( Kirusi: Ни́кон, jina la kuzaliwa Никита Минин, Nikita Minin; 7 Mei 1605 - 17 Agosti 1681) alikuwa Patriarki wa saba wa Moscow na Urusi wote wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi, akihudumu rasmi kutoka 1652 hadi 1666.

Patriarki Nikon.

Alisifika kuwa na uwezo wa kuhubiri, nguvu yake ya kufuatilia shabaha, uchaji Mungu na uhusiano wake wa karibu na Tsar Aleksei wa Urusi.

Nikon alianzisha matengenezo mengi ambayo mwishowe yalisababisha mgawanyiko wa kudumu katika Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi unaojulikana kama Raskol.

Kwa miaka mingi alikuwa mhusika muhimu wa kisiasa, mara nyingi alikuwa sawa na Tsar au hata kushinda athira yake.

Matengenezo yake katika ibada yalikataliwa na sehemu ya Wakristo waliopendelea utaratibu wa kale.

Mnamo Desemba 1666, Nikon alishtakiwa mbele ya sinodi ya kanisa akaondolewa hadhi yake ya ukasisi na kurudishwa kwenye cheo cha mtawa wa kawaida.

Maisha ya awali

hariri

Alizaliwa kwenye mwaka 1605 na mkulima mdogo katika kijiji cha Valmanovo, kilichopo takriban kilomita 96 kutoka Nizhniy Novgorod. Mama yake alifariki mara tu baada ya kuzaliwa kwake, na baba yake alioa tena. Mama wa kambo alimtendea vibaya. Alifundishwa kusoma na kuandika na kasisi wa parokia. Alipokuwa na umri wa miaka 12 alitoroka nyumbani akajiunga na monasteri ya Makaryev ambapo alikaa miaka 7 kama mtawa mwanafunzi.

 
Makao ya Nikon katika Monasteri ya Yerusalemu Mpya.

Mwaka 1624 wazazi wake walisisitiza arudi nyumbani akatii, akaoa, na kuwa kasisi wa parokia katika kijiji cha karibu.

Ufasaha wake uliwavuta wafanyabiashara kutoka Moscow ambao walikuwa wakifika katika eneo hilo kwa sababu ya maonyesho maarufu ya biashara yaliyofanyika kwenye uwanja wa Monasteri ya Makaryev. Kupitia juhudi zao alialikwa kutumikia kama kasisi wa parokia katika mji mkuu.

Alitumikia huko kama miaka kumi. Mnamo mwaka 1635, watoto wake wadogo watatu walifariki. Aliona hiyo kama ishara kutoka kwa Mungu akaamua kuwa mtawa. Akamshawishi mkewe kujiunga na jumuiya ya watawa wa kike. Mwenyewe alihamia eneo lenye ukiwa kwenye kisiwa cha Anzersky kwenye Bahari Nyeupe katika jumuiya ya watawa walioishi kila mmoja kama mkaapweke. Alipokuwa mtawa alijiita Nikon.

Mnamo 1639 alikuwa na ugomvi na abati akaondoka na kujiunga na Monasteri ya Kozheozersky, katika dayosisi ya Novgorod. Huko alichaguliwa abati wa jumuiya mnamo 1643.

Mkutano na Tsar Aleksei

hariri

Alipokuwa na safari rasmi ya kwenda Moscow mnamo 1646, alienda pia kumsalimu Tsar jinsi ilivyokuwa kawaida. Tsar Aleksei I (16291676) alikuwa kijana wa miaka 17 aliyepata kuwa mfalme tangu mwaka mmoja. Aleksei alivutiwa sana na Nikon akamteua mara moja kuwa abati wa monasteri muhimu ya Novospassky mjini Moscow. Monasteri hiyo ilifadhiliwa na familia ya Romabov waliokuwa familia ya watawala wa Urusi.

Kutafuta mabadiliko

Wakati akihudumia katika Monasteri ya Novospassky, Nikon alishirikiana na kundi la makuhani waliojadiliana kuhusu mabadiliko katika nchi na katika kanisa. Urusi ulikuwa umepita kipindi cha njaa na vita ya wenyewe kwa wenyewe, na wanakundi waliamini matatizo hayo yalikuwa ishara ya hasira ya Mungu iliyosababishwa na utovu wa dini kati ya Warusi.

Wanakundi waliona haja ya kutafuta mategenezo katika kanisa na ibada zake pamoja na uamsho wa kiroho kati ya Wakristo. Waliona tatizo la vitabu vya liturgia kuwa na kasoro na pia kuingiliwa na athari ya Kanisa Katoliki. Kati ya wanakundi walikuwemo makuhani na maabati muhimu, waliosaidia Nikon achaguliwe askofu wa Velikiy Novgorod.

Wakati wa uongozi wake, ghasia zilianza jijini, na Nikon alipigwa sana na umati. Walakini, aliweza kutatua mambo hayo kwa amani, kwa kuongoza maandamano ya kidini dhidi ya wanaghasia. [1]

Kuchaguliwa kama Patriaki (1652)

hariri

Mnamo 1 Agosti 1652 alichaguliwa patriarki wa Moscow. Nikon alijua kuwa makabaila hawakumpenda akakataa wito huo mara kadhaa. 

Ilikuwa tu kwa shida kabisa kwamba Nikon aliweza kushawishiwa kuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Urusi. Hatimaye alikubali baada ya Tsar mwenyewe na wakubwa wake kupiga magoti mbele yake wakimwomba akubali. Alikubali tu baada ya kupata kiapo cha mkutano wote kilichokuwa kiapo cha utii kwake katika kila jambo kuhusu mafundisho, kanuni na ibada za Kanisa la Kiorthodoksi.

Matengenezo ya Nikon

hariri

Wakati Nikon alipochaguliwa mabadiliko yalikuwa yameshaanza tayari. Marehemu patriarki Joasaph aliwahi kuagiza kundi la makuhani viongozi wapitilie vitabu vya ibada za kanisa, pamoja na marekebisho kadhaa madogo ya maadhimisho kadhaa ya zamani. Lakini walikuwa waoga mno ili kujaribu kitu chochote chenye ufanisi.

 
Aleksey Kivshenko . Patriaki Nikon na Epifany Slavinetsky wakikagua vitabu vya liturgia.

Nikon alianzisha matengenezo makali. Alitafuta ushauri wa wataalamu wakuu kati ya Wagiriki Waorthodoksi akawaalika wataalamu kutoka Konstantinopoli na Kiev kwa warsha mjini Moscow.

Wataalamu hao walimweleza kuwa vitabu vya ibada vya Moscow vilijaa makosa yaliyovitenga na imani ya Kiorthodoksi; pia waliona kuwa ikona au picha takatifu zilizokuwa zikitumika zilikuwa zimeondoka mbali na mifano asili ya Konstantinopoli, kwa sababu athira kutoka picha za Wakatoliki iliwahi kuingia katika sanaa hiyo.

Nikon alikosoa vikali utumiaji wa ikona hizo mpya; aliamuru utafutwaji wa nyumba kwa nyumba kwa picha hizo. Wanajeshi wake na watumishi walipewa amri kwanza kutoboa macho kwenye picha halafu kuzibeba kupitia mji kwa dhihaka. Alitoa pia amri iliyotishia adhabu kali zaidi wale wote ambao wangeendelea kutengeneza au kutumia ikona kama hizo.

Mnamo mwaka wa 1654, Nikon aliitisha sinodi ili kuchunguza tena vitabu vya huduma vilivyorekebishwa na Patriarki Joasaf. Wanasinodi wengi walikubali kwamba "Wagiriki wanapaswa kufuatwa badala ya desturi za wazee wetu."

Pamoja na kupokea matini za liturgia kutoka kwa Wagiriki, Nikon aliongeza mabadiliko mengine; alibadilisha namna ya kuinama kanisani, aliagiza alama ya msalaba itiwe kwa vidole vitatu badala ya viwili, akaongeza halleluya moja pale ambako desturi ya Moscow ilikuwa kuiimba mara mbili.[2]

Baada ya maazimio hao kulitokea kundi la wapinzani, pamoja na idadi ya makuhani viongozi na askofu mmoja.

Nikon alisisitiza pia kuwa majengo ya makanisa yafuate mfano wa Bizanti. Alipinga hasa makanisa yaliyopewa paa la juu kwa umbo la hema, jinsi yalivyojengwa kama staili ya Kirusi katika karne iliyopita. Aliamuru kubomolewa kwa idadi ya makanisa yenye paa la hema.

Sinodi ya pili ilifanyika Moscow mnamo 1656 na kuidhinisha marekebisho ya vitabu vya liturgia kama ilivyopendekezwa na mkutano wa kwanza. Wapinzani walilaaniwa.

Matengenzo ya Nikon yalitokea pamoja na epidemiki ya tauni katika Urusi na wapinzani waliamini ugonjwa huo ulikuwa adhabu wa mabadiliko hayo.

Baada ya sinodi mbili za 1654 na 1656 mamlaka ya Nikon ilikuwa bila vikwazo vyovyote. Lakini watu wengi walianza kumpinga moyoni kutokana na ukali wake, jinsi alivyolazimisha watu kufuata maazimio yake, na kutumia nguvu na adhabu kali dhidi ya hao wasiokubaliana naye.

Upinzani wa kidini dhidi yake ulitokana na waumini wa kawaida na pia kutoka sehemu kubwa ya makasisi wa kawaida. Makasisi wengi wa ngazi wa chini hawakuwa na elimu kubwa wakitekeleza ibada kwa kutumia maneno waliyowahi kukariri. Hawakupenda kujifunza yote upya. Waumini wengi walishtushwa kama patriarki aliwaagiza kupuuza matendo waliyojifunza kama matakatifu, kama matumizi ya vidole vitatu ya kujitia msalaba. Hivyo matengenezo ya Nikon, labda zaidi ukali wake, yalisababisha farakano la Raskol katika kanisa la Urusi na kutokea kwa Waumini wa Kale (kwa Kirusi: Raskolniki).

Miradi ya ujenzi

hariri

Nikol alijenga na kupamba monasteri nyingi tena nzuri kwa kuweka maktaba muhimu. Wajumbe wake walitafuta Urusi na nchi chini ya utawala wa Uislamu kwa muswada za thamani za Kigiriki na Kislavoni, zote za kidini na za kidunia.

Miongoni mwa monasteri kubwa alizoanzisha kulikuwa na Monasteri ya Valday Iversky, Monasteri ya Yerusalemu Mpya, na Monasteri ya Kisiwa cha Kiy.

Nguvu za kisiasa

hariri
 
Nikon alimtangaza Askofu Philip ametangazwa kuwa mtakatifu na masalia yake yalihamishiwa Kremlin ya Moscow kama ukumbusho kwa tsars juu ya uhalifu ambao walikuwa wamefanya dhidi ya kanisa (uchoraji na Alexander Litovchenko ).

Kuanzia 1652 hadi 1658, Nikon alikuwa na mamlaka kubwa ya kisiasa iliyolingana na tsar mwenyewe. Mwaka 1654 wakati Tsar Aleksei aliondoka Moscow kwa vita dhidi ya Poland, alimkabidhi Nikon mamlaka yote nchini akamwomba hasa kutunza familia yake. Hatua hiyo alirudia mwaka 1657 alipoelekea tena magharibi kuongoza jeshi la Urusi. Katika vipindi hivyo Nikon alikuwa na mamlaka yote ya Tsar. [3]Lakini mamlaka hiyo ilizaa pia maadui, hasa kati ya familia ya makabaila wakubwa.

Tsar Aleksei aliporudi mwaka 1658 aliambiwa kwamba uwezo wa patriarki ulionekana mkubwa kuliko wake mwenyewe. Tangu kuamini hayo, tsar alisita kumwona Nikon tena.

Nikon anaondoka Moscow (1658)

hariri

Nikon alisikia mabadiliko haya akajaribu kumlazimisha tsar kuwa karibu naye tena na kuelewa umuhimu wake. Hivyo tarehe 20 Julai 1658 alitangaza kujiuzulu mbele ya ushirika wa ibada akahamia monasteri ya Voskresensky.

Ni dhahiri Nikon alitegemea kwamba tsar Aleksei angemfuata na kumwomba arudi tena lakini hii haikutokea. Baada ya miezi kadhaa alijaribu mwenyewe upatanisho na tsar aliyekaa kimya. Nikon alibaki katika monasteri kwa miaka 8 hadi 1666. Aleksei alisita kuchukua hatua zaidi kwa sababu Nikon alijiuzulu kama askofu wa Moscow lakini si kama mkuu wa kanisa lote. Hatimaye mwaka 1666, wakati pia vita dhidi ya Poland ilielekwa kwisha, tsar Aleksei aliitisha sinodi alipoalika pia patriarki wa Antiokia na yule wa Aleksandria.

Kulingana na Robert Massie, wakati wa kesi hiyo, Nikon alitetea kwa bidii imani yake kwamba mamlaka na nguvu ya kanisa ilikuwa na inapaswa kuwa ya juu. [4] Bado Nikon alikuwa akisisitiza kwamba mamlaka na mamlaka ya kanisa inapaswa kuwa ya juu tu katika maswala ya kanisa.

Mnamo Desemba 12 sinodi ilimtangaza Nikon na hatia ya kumtukana tsar na Kanisa lote la Urusi, la kumtoa Paul, askofu wa Kolomna, kinyume na kanuni, na ya kupiga na kutesa wadogo wake. Hukumu yake ilikuwa kuondolewa haki zake zote za kikuhani. Tangu sasa alikuwa anajulikana tu kama mtawa Nikon. Siku hiyo hiyo aliwekwa kwenye sleji na kupelekwa kama mfungwa katika monasteri ya mbali ya kaskazini mwa Ferapontov. Walakini sinodi yenyewe iliyokuwa imemwondoa madarakani ilithibitisha mabadiliko yake yote na kulaani watu wote ambao wanayakataa.

Nikon aliishi uhamishoni hadi kifo cha Tsar Aleksei mnamo 1671 akaendelea kubaki pale. Mnamo 1681 tsar mpya Fedor (mtoto wa Aleksei), aliposikia kwamba Nikon alikuwa mgonjwa, alimruhusu kurudi Moscow na kukaa katika nyumba yake ya zamani ya Moscow, Monasteri ya Yerusalemu Mpya. [5] Lakini Nikon alikufa njiani alipoelekea Moscow mnamo 17 Agosti 1681.

Marejeo

hariri
  1. Никон (Минов) // Nikon (Minov) www.hrono.ru (in Russian)
  2. https://www.britannica.com/biography/Nikon
  3. Никон (Минов) // Nikon (Minov) www.hrono.ru (in Russian)
  4. Robert K. Massie, Peter the Great, His Life and World (1980), p 60.
  5. Massie, p.60.

Kusoma zaidi

hariri
  • Lobachev, Sergei V. "Kuinuka kwa Nguvu ya Dume Nikon." Mapitio ya Slavonic na Ulaya Mashariki (2001): 290-307. huko JSTOR
  • Meyendorff, Paul. Urusi, ibada, na mageuzi: mageuzi ya liturujia ya Nikon katika karne ya 17 (RSM Press, 1991)
  • Shusherin, Ioann. Kutoka kwa Mkulima hadi Patriaki: Akaunti ya Kuzaliwa, Uasi, na Maisha ya Utakatifu wake Nikon, Patriarch wa Moscow na Urusi Yote (2008)
  • Spinka, Mathayo. " Patriaki Nikon na Utiifu wa Kanisa la Urusi kwa Jimbo. " Historia ya Kanisa 10 # 4 (1941): 347-366. huko JSTOR
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.