Waamuzi (Biblia)
Kitabu cha Waamuzi ni cha saba katika orodha ya vitabu vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.
Kinaleta mapokeo mbalimbali kuhusu historia ya Israeli kwenye miaka 1200-1025 hivi K.K.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Baada ya makabila 12 ya Waisraeli kugawana nchi takatifu, kila moja likaanza kujitegemea: lakini bila ya umoja hakuna nguvu upande wa dini wala wa siasa.
Upande wa dini, Waisraeli wakaanza kuchanganyikana na wenyeji Wapagani na kufuata utamaduni wao uliostaarabika zaidi, hata wakaabudu miungu yao kwa ukahaba wa kidini na kwa kuitolea sadaka watoto wao.
Kutokana na makosa hayo, Mungu akawaacha wanyanyaswe na makabila mbalimbali.
Mara kwa mara Waisraeli wakamlilia, naye akawainulia mwanamume au mwanamke fulani awashinde maadui na kuwarudishia amani (Amu 2:6-19).
Watu wa namna hiyo wanaitwa “waamuzi” kwa maana ya “watawala”. Majina yao ni: Othniel, Ehud, Shamgar, Debora, Gideoni, Tola, Yair, Yefta, Ibsan, Elon, Abdon, Samsoni.
Habari za waamuzi hao 12 haziwezi kupangwa kitarehe, kwa kuwa hazina dalili zinazotusaidia kujua ipi ilitangulia na ipi ilifuata. Waandishi wenyewe hawakujua mwaka wa matukio hayo, hivyo walikusanya kumbukumbu walizokuwanazo kama kwamba waamuzi walifuatana mmoja baada ya mwingine kuongoza Israeli. Ukweli ni kwamba waliweza kuongoza kwa wakati mmoja huyu huku na huyu huku, kwa kuwa kila mmoja alihusika na eneo fulani tu. Kwa kuwapanga mmoja baada ya mwingine, waandishi waliweza kusisitiza mara 12 kwamba Waisraeli walirudiarudia dhambi, na kwa sababu hiyo walirudiarudia kupewa na Mungu adhabu aliyoitabiri Musa. Lakini fundisho muhimu zaidi ni kwamba Bwana, bila ya kujali ugeugeu wao, daima alikuwa tayari kuwaokoa walipomlilia msaada.
Mazingira
haririKitabu cha Waamuzi kinasimulia matukio ya Israeli katika miaka 200 hivi baada ya Yoshua kuiteka nchi ya Kanaani, lakini kinaleta picha tofauti na kile cha Yoshua kuhusu hali ya nchi ya Kanaani baada ya uvamizi. Kinaonyesha kuwa Waisraeli hawakufukuza wenyeji wote, bali waliteka baadhi tu ya maeneo yao wakaishi jirani nao. Chini ya Yoshua Waisraeli walishinda vita vile vikubwa, lakini hawakutii amri ya Mungu ya kuangamiza au kufukuza Wakanaani wote. Matokeo yake, Wakanaani waliobaki nchini kila wakati walisababisha matatizo kwa Waisraeli, upande wa dini na upande wa siasa pia.
Wakati ule katika historia ya Israeli hali fulani iliingia ambayo habari zake tunaweza kuzisoma katika kitabu cha Waamuzi mara kwa mara. Baada ya muda, Waisraeli walimwacha Mungu wao wakaiga desturi za dini za jadi za Wakanaani, wakawa dhaifu upande wa siasa, na mwisho wakashindwa na Wakanaani au na mataifa ya jirani. Lakini Mungu, aliyewatumia maadui wale ili kuwaadhibu watu wake waliomwasi, alikuwa mvumilivu sana kwao katika neema yake. Kila mara, kwa wakati wake mwenyewe, aliwapa kiongozi na mwokozi ambaye aliwashinda maadui na kuwaongoza Waisraeli ili wamtambue Mungu wao tena.
Watu hao walioleta wokovu waliitwa Waamuzi kama ilivyokuwa kawaida kwa watawala wengine wa eneo lile. Wengi wao walitimiza uamuzi wa Mungu, wakiwashinda maadui na kuwaokoa watu wake. Wengine wasiokuwa watu wa vita, walitimiza uamuzi wa Mungu kwa kuongoza mambo ya kila siku ya watu wa Mungu kadiri ya sheria yake. Kutokana na viongozi wale, wakiwa wa kiraia au wa kijeshi, kitabu hiki kilipata jina lake.
Waisraeli na maadui wao
haririInaonekana kwamba vita mbalimbali dhidi ya mataifa ya jirani na ushindi wake, na mapinduzi ya baadaye yaliyoletwa na Waamuzi wa Israeli, mara nyingi vilikuwa katika sehemu fulani ya nchi tu, bila ya kuhusu nchi yote ya Kanaani. Kwa kawaida makabila yaliyohusika yalikuwa yale ya maeneo yao tu. Pia iliwezekana kwamba ushindi na mashambulio yake yalikuwa sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja. Kwa mfano, habari za Yefta na Waamoni ziliweza kuwa zimetokea wakati ule ule ambao Samsoni alishughulika na Wafilisti (taz. 10:7-8; 11:5; 13:1). Haukuwepo umoja sana katika Israeli, na kila kabila, au hata makundi ya makabila fulani, yaliangalia mambo yaliyotokea katika maeneo yao, bila ya kujali mambo ya makabila mengine.
Sababu kuu ya ukosefu huo wa umoja ilikuwa kwamba, watu walikuwa wamemwacha Mungu, kwa sababu kama wangalimfanya Yeye kuwa mkuu na kiini cha maisha yao ya kitaifa, uaminifu wao kwa Mungu ungaliwaunganisha. Pia ngome za Wakanaani (pamoja na askari zao waliobaki sehemu mbalimbali za maana) zilizuia umoja wa makabila ya Israeli. Katika nchi yenyewe ya Kanaani (yaani eneo la kati ya Mto Yordani na Bahari ya Kati), makabila ya Israeli yalikuwa katika makundi makubwa matatu, yaani ya kaskazini, ya katikati na ya kusini, ambapo Mto Yordani ulitenga makabila ya mashariki na mengine.
Matengano hayo ya makabila ya Israeli hayakuwa ya kisiasa au ya kieneo tu, bali pia yalileta shida kwa umoja wa kidini, kwa sababu watu wengi walitengwa na mahali maalumu pa kuabudia, yaani hema la kukutania lililokuwepo Shilo (Yos 18:1; 22:9).
Kwa kifupi, matatizo yote ya Waisraeli, yakiwa ya maendeleo, ya kisiasa au ya kidini, yalitokana na ukosefu wa watu wa kutii amri za Mungu (taz.1:21, 27-36; Kumb 7:2-4; 9:5; Yos 24:14-24).
Dini za Wakanaani
haririMiungu ya Wakanaani ilijulikana kwa jina la Baalim au Mabaali (wingi wa Baali; taz. 2:11; 10:10; 1 Fal 16:31), na miungu ya kike iliitwa Maashtorethi (wingi wa Ashtorethi; taz. 2:13; 1 Sam 7:3-4), na Asherimu au Ashera (wingi wa Ashera; taz. 6:25-26; 2 Fal 23:4; kumbuka neno la Kiswahili 'Uasherati').
Miungu hiyo ilikuwa ya kustawisha uzazi wo wote, pia iliaminiwa kuwa ingeweza kuongeza ustawi wa mimea. Waisraeli walijua kwamba Mungu alikuwa Mwumbaji wa hali yote ya uzazi na ustawi, na hivyo ilikuwa hatua ndogo tu kwa Waisraeli kuunganisha na kuchanganya mawazo ya Kikanaani na ujuzi wao wenyewe, na hivyo kumwabudu Yahweh kama Baali mwingine. Maana ya neno 'baali' ilikuwa bwana, mume, au mwenyewe. Waisraeli walimjua Yahweh (YHWH) kuwa Mume na Bwana wao, kwa hiyo walikuwa katika hatari zaidi ya kuunganisha Mabaali wa Kikanaani na Mungu wao aliye Yahweh (Hos 2:5-10).
Mahali ambapo Wakanaani walipenda kuendesha ibada zao kwa Mabaali na Asherimu palikuwa katika vilele vitakatifu vya milima mbalimbali palipoitwa 'mahali pa juu' (Hes 33:51-52; 2 Fal 23:13). Baadhi ya vitu vilivyotumiwa mahali pale vilikuwa miti mitakatifu na nguzo za mawe matakatifu vilivyoitwa Maashera (au Ashera, mungu wa kike ambaye vitu vile vilichukua jina lake; taz. 6:25-26; 1 Fal 14:23). Tangu mwanzo Waisraeli walikuwa wamemwabudu Mungu mahali mbalimbali katika milima (taz. Mwa 22:2; Kut 17:8-15; 19:3), na hapo pia ilikuwa rahisi kuteleza na kuchukua sehemu za juu za Mabaali na kuzitumia kwa ibada zao kwa Yahweh. Mambo hayo yote yalifanyika, ingawa Mungu alikuwa ameamuru kwamba sehemu zote za ibada ya Mabaali zibomolewe kabisa (Hes 33:52; Kum 12:2-3).
Makahaba wa kike na wa kiume walipatikana katika 'mahali pa juu' kwa ajili ya sherehe mbalimbali za uzazi na ustawi wa nchi. Sherehe hizo zilikuwa za kidini nao waliamini kwamba sherehe hizo za kuingiliana kimwili zingestawisha nafaka, mifugo yo yote na hata maisha ya familia (1 Fal 14:23-24; Yer 13:27). Katika kuyafuata mambo ya Mabaali, watu wa Israeli walikuwa na hatia ya zinaa ya kidini pia. Agano baina ya Waisraeli na Mungu lilifananishwa na ndoa, na hivyo Waisraeli walipojiunga na Mabaali na miungu mingine, walifanya dhambi ya zinaa dhidi yake (taz. 2:12-13, 17; Yer 2:20; 3:6-8; Hos 2:13; 4:12).
Nyongeza ya kitabu inaonyesha kuwa kumwasi Mungu kulisababisha hatimaye Waisraeli kupigana wenyewe kwa wenyewe. Ni kwamba, ukivunja amri ya kwanza unaweza kuja kuzivunja zote, na ukimkataa bab, hutakubali tena ndugu zako. Mstari wa mwisho unaeleza sababu nyingine ya fujo hizo: kutokuwepo mfalme mmoja juu ya makabila yote 12. Kwa kusema hivyo, kitabu kinatuandaa kusikia katika vitabu vinavyofuata jinsi ufalme wa Israeli ulivyoanzishwa kwa usimamizi wa Samweli, nabii na mwamuzi wa mwisho lakini mkuu kuliko hao 12.
Yaliyomo
hariri1:1-2:5 Utangulizi kuhusu ushindi wa Yoshua
2:6-16:31 Utawala wa Waamuzi
17:1-21:25 Machafuko katika Israeli
Tanbihi
haririMarejeo
haririUfafanuzi
hariri- Amit, Yairah. "Judges" Introduction and Annotations. The Jewish Study Bible. Ed. Adele Berlin and Marc Zvi Brettler. New York: Oxford University Press, 2004. 508-557.
- Alter, Robert, trans. and commentary. Ancient Israel: The Former Prophets: Joshua, Judges, Samuel, and Kings. New York: W. W. Norton & Company, 2013. Print.
- "Book of Judges in the Revised Version, The." Google Books. 4 April 2014. p. xvii.
- Davis, John J. and Herbert Wolf. Judges Introduction and Annotations. Zondervan NIV Study Bible (Fully Revised). Ed. Kenneth L. Barker. Grand Rapids, MI: Zondervan, 2002. 326–363.
- Guest, P. Deryn (2003). "Judges". Katika James D. G. Dunn and John William Rogerson (mhr.). Eerdmans Commentary on the Bible. Eerdmans. ISBN 978-0-8028-3711-0.
- Matthews, Victor Harold (2004). Judges and Ruth. Cambridge University Press. ISBN 978-0-521-00066-6.
- Niditch, Susan (2008). Judges: a commentary. Westminster John Knox Press. ISBN 978-0-664-22096-9.
- Soggin, Alberto (1981). Judges. Westminster John Knox Press. ISBN 978-0-664-22321-2.
- Telushkin, Joseph. Biblical Literacy: The Most Important People, Events, and Ideas of the Hebrew Bible. New York: William Morrow and Company, 1997.
Marejeo mengine
hariri- Bacon, Gershon and S. David Sperling. "Judges (Heb.שופתטים), Book of." Encyclopaedia Judaica. Second Edition, Volume 11. pp. 561–566.
- Eynikel, Erik (1996). The reform of King Josiah and the composition of the Deuteronomistic history. Brill. ISBN 978-90-04-10266-8.
- Knight, Douglas A (1995). "Deuteronomy and the Deuteronomists". Katika James Luther Mays, David L. Petersen and Kent Harold Richards (mhr.). Old Testament Interpretation. T&T Clark. ISBN 978-0-567-29289-6.
- Knoppers, Gary (2000a). "Introduction". Katika Gary N. Knoppers, J. Gordon McConville (mhr.). Reconsidering Israel and Judah: recent studies on the Deuteronomistic history. Eisenbrauns. ISBN 978-1-57506-037-8.
- Knoppers, Gary (2000b). "Is There a Future for the Deuteronomistic History?". Katika Thomas Romer (mhr.). The Future of the Deuteronomistic History. Leuven University Press. ISBN 978-90-429-0858-1.
- Malamat A. "Chapter VII: The Period of the Judges." Judges. The World History of the Jewish People. 3. Givatayim, Israel: Rutgers UP, 1971. pp. 129–163.
- Miller, J Maxwell (1995). "The Ancient Near East and Archaeology". Katika James Luther Mays, David L. Petersen and Kent Harold Richards (mhr.). Old Testament Interpretation. T&T Clark. ISBN 978-0-567-29289-6.
- Perdue, Leo G (2001). "Preface: The Hebrew Bible in Current Research". Katika Leo G. Perdue (mhr.). The Blackwell companion to the Hebrew Bible. Blackwell. ISBN 978-0-631-21071-9.
- de Pury, Albert; Romer, Thomas (2000). "Deuteronomistic Historiography: History of Research and Related Issues". Katika Albert de Pury, Thomas Romer, Jean-Daniel Macchi (mhr.). Israël constructs its history: Deuteronomistic historiography in recent research. Sheffield Academic Press. ISBN 978-1-84127-099-9.
{{cite book}}
: CS1 maint: multiple names: editors list (link)
- Spieckerman, Hermann (2001). "The Deuteronomistic History". Katika Leo G. Perdue (mhr.). The Blackwell companion to the Hebrew Bible. Blackwell. ISBN 978-0-631-21071-9.
- Van Seters, John (1997). In search of history: historiography in the ancient world and the origins of biblical history. Eisenbrauns. ISBN 9781575060132.
- Walton, John H (2009). "The Deuteronomistic History". Katika Andrew E. Hill, John H. Walton (mhr.). A Survey of the Old Testament. Zondervan. ISBN 978-0-310-22903-2.
Viungo vya nje
hariri- Kitabu chenyewe kwa Kiebrania
- שֹּׁפְטִים – Shoftim – Judges Ilihifadhiwa 16 Mei 2017 kwenye Wayback Machine. (Hebrew – English at Mechon-Mamre.org)
- Tafsiri za Kiyahudi kwa Kiingereza
- Judges at Mechon-Mamre Ilihifadhiwa 23 Januari 2009 kwenye Wayback Machine. (Jewish Publication Society translation)
- Shoftim – Judges (Judaica Press) translation [with Rashi's commentary] at Chabad.org
- Book of Judges Ilihifadhiwa 8 Mei 2014 kwenye Wayback Machine. (G-dcast interpretations)
- Tafsiri za Kikristo kwa Kiingereza
- Online Bible at GospelHall.org
- Judges at Bible Gateway (various versions)
- Judges at Wikisource (Authorised King James Version)
- Katika Kamusi Elezo ya Kiyahudi
- Book of Judges article (Jewish Encyclopedia)
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Waamuzi (Biblia) kama historia yake au athari wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |