Amerika ni jina la mabara mawili makubwa upande wa magharibi wa Afrika na Ulaya.

Amerika duniani

Amerika iko kati ya Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Pasifiki kwa urefu wa kilomita 15,000 kutoka kaskazini (rasi Columbia) hadi kusini (rasi Hoorn).

Eneo lote ni km² 42,000,000 na jumla ya wakazi ni milioni 800.

Ramani ya Amerika yote

Eneo hugawiwa katika sehemu tatu au mbili, yaani ama

ama

Hesabu ya pande tatu inalingana na jiografia inayotambua hasa mabamba matatu yanayobeba sehemu hizi tatu: Amerika ya Kaskazini hulala hasa juu ya Bamba la Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kati juu ya Bamba la Karibi na Amerika ya Kusini hasa juu ya Bamba la Amerika ya Kusini.

Katika hesabu ya mabara mawili kwa kawaida Amerika ya Kati huhesabiwa kuwa sehemu ya Amerika Kaskazini. Kumbe upande wa utamaduni Amerika ya Kati na ya Kusini kwa pamoja huitwa "Amerika ya Kilatini" kutokana na lugha na utamaduni wa Kihispania na wa Kireno zilizofinyanga tabia za mataifa yake.

Jina la "Amerika"

Neno "Amerika" limetokana na jina la kwanza la Mwitalia Amerigo Vespucci (1451-1512). Vespucci alikuwa baharia na mfanyabiashara katika utumishi wa familia ya Medici kutoka Firenze (Italia). Tangu mwaka 1499 alisafiri kwenye pwani za Amerika ya Kusini na Amerika ya Kati akaandika kitabu juu ya safari zake. Humo aliandika ya kwamba hakukubaliana na Kristoforo Kolumbus ya kwamba visiwa na nchi zilizofikiwa na Kolumbus zilikuwa sehemu ya Uhindi. Amerigo alipendekeza ya kwamba zilikuwa sehemu za "dunia mpya" au bara jipya akiwa mtu wa kwanza kuandika hivyo.

Mwanajiografia Mjerumani Martin Waldseemüller alitumia jina la "Amerika" kwa heshima ya Amerigo alipochora ramani yake ya dunia ya mwaka 1507.

Historia

Wenyeji asilia kutoka Asia Kaskazini

Inaaminiwa leo ya kwamba miaka 20,000 hadi 16,000 iliyopita hakukuwa na binadamu Amerika. Wakazi asilia walianza kuingia wakati ule kutoka Siberia (Asia ya Kaskazini) kupitia nchi kavu iliyopatikana wakati ule katika eneo la mlango wa bahari wa Bering kutokana na kipindi cha baridi.

 
Waindio wa Brazil.

Hakuna uhakika jinsi gani uhamiaji huo ulitokea. Lakini wataalamu wote wanakubaliana ya kwamba karibu wakazi asilia wote walitokea kutoka vikundi vya wawindaji walioingia Amerika kutoka Siberia na kusambaa hadi kusini kabisa. Kutoka vikundi hivyo vilijitokeza mataifa na makabila mengi ya wenyeji jinsi walivyoonekana wakati wa kuja kwa Kolumbus na Wahispania ambapo habari za maandishi zinaanza kupatikana.

Kuna dalili ya kwamba labda vikundi vidogo vilivuka bahari hata baadaye kutoka Ulaya, Afrika au Asia / Pasifiki na kuingia katika tamaduni za wenyeji. Ila tu hayo yote hayana uhakika isipokuwa kufika kwa Wanorway mnamo mwaka 1000 waliounda vituo katika sehemu za Labrador (Kanada) visivyodumu muda mrefu.

Kuja kwa Wazungu

Kuja kwa Wahispania na Wazungu wengine kuanzia Kolumbus (1492) kulibadilisha historia na uso wa Amerika. Kolumbus aliamini ya kwamba aligundua njia ya kufika Uhindi akaita nchi mpya "Uhindi wa Magharibi" na wenyeji wake "Wahindi" - jina hili limebaki kwao katika lugha mbalimbali kama "Indio" (kihisp.) au "Red Indians" (kiing.). Tamaduni zote za Amerika hazikuwa zimeanza bado kutumia chuma - silaha zao za mawe na mbao hazikuweza kushindana na silaha za watu wa Ulaya.

Wenyeji walikufa kwa mamilioni, hasa kutokana na magonjwa kutoka "dunia ya kale" ambayo hawakuzoea. Vita na utumwa vilichangia katika kupungua kwa wakazi asilia. Idadi kubwa ya wenyeji walibaki tu katika nchi za milima ya Andes.

Mazao za Amerika

Ulaya na mabara mengine ya dunia yalifaidika sana na maendeleo ya utaalamu wa kilimo yaliyopatikana katika Amerika: mazao kama mahindi, viazi, nyanya, maboga, kokoa na mengine yalipelekwa kutoka Amerika katika mabara yote na kuboresha lishe ya watu.

Amerika yote ilifanywa kuwa koloni la nchi za Ulaya; Wahispania na Wareno walitawala sehemu za kusini; Waingereza na Wafaransa walishindana juu ya kaskazini ikawa Waingereza walishinda. Mataifa madogo ya Ulaya kma Uholanzi na Denmark yalipata nafasi katika visiwa vya Karibi na katika Guyana.