Ukomeshaji wa Biashara ya Watumwa

Ukomeshaji wa biashara ya watumwa ni mchakato au mlolongo wa matukio yaliyopelekea ufutaji au usitishaji wa biashara ya watumwa katika karne ya 19.

"Je, mimi si mtu, tena ndugu?": mchoro wa Josiah Wedgwood kwa ajili ya kampeni ya Uingereza dhidi ya utumwa, 1787.
Boxi la kuchangia Massachusetts Anti-Slavery Society. mwaka 1850 hivi.

Biashara ya watumwa ilikuwa biashara iliyodhalilisha utu wa binadamu, hasa Waafrika ambao ndio waliotumika kwa kiasi kikubwa katika biashara hiyo. Basi, baadhi ya watu Ulaya waliweza kuona madhara mbalimbali yaliyotokana na biashara hiyo hatarishi, na kuamua kuanzisha tapo la kuikomesha. Wengi wao walikuwa watu wa dini waliosukumwa na sababu za ubinadamu.

Baadaye mataifa kama Uingereza yaliongeza bidii katika ukomeshaji wa biashara ya utumwa. Kwa kiasi fulani ukomeshaji wa biashara ya utumwa ulikuwa una manufaa ya kiuchumi kwao, hasa kufuatia matokeo ya mapinduzi ya viwanda yaliyotokea nchini mwao.

Uingereza ukiwa taifa kiongozi katika biashara hiyo, halafu katika zoezi hilo la kuikomesha, ulisaidia kwa kiasi kikubwa katika ukomeshaji wa biashara hii iliyopitia katika bahari ya Atlantiki na ile ya bahari ya Hindi. Si mataifa yote yalikubaliana na matakwa ya Uingereza ya kukomesha biashara ya utumwa, hivyo Uingereza ilipata upinzani kutoka kwa mataifa mengine yaliyokuwa bado yananufaika na biashara hii kama Ufaransa na Ureno.

Ukomeshaji

Kampeni ya ukomeshaji wa biashara ya watumwa haikutoka Afrika. Ilianzia huko Ulaya: kwa kiasi fulani kutokana na sababu za ubinadamu, na kwa kiasi fulani kutokana na kupungua kwa umaarufu wa biashara ya utumwa kupitia Atlantiki pamoja na upatikanaji wa uhuru wa Marekani; pia kubadilika kwa mwelekeo wa Ulaya kutoka Amerika kwenda Mashariki ya Mbali na Afrika.

Msukumo wa Magharibi katika ukomeshaji wa watumwa

Mfalme Luis X wa Ufaransa alifuta utumwa mwaka 1315, halafu Kaisari Karolo V, akiwa pia mfalme wa Hispania, alitunga sheria mpya za kufikia hatua hiyo mwaka 1542, lakini hazikutekelezwa.

Mwishoni mwa karne ya 17, Kanisa Katoliki lililaani rasmi biashara hiyo, jambo lililosisitizwa kwa nguvu na Papa Gregori XVI mwaka 1839. Lakini tapo la harakati ya kufuta utumwa lilianza mwishoni mwa karne ya 18 katika madhehebu ya Quakers huko Uingereza na Marekani.[1]

Hapo mawazo ya Wazungu kuhusu Waafrika yalizidi kubadilika kwa kuanza kumwona Mwafrika kwa mwelekeo wa kibinadamu zaidi. Jambo hili lilileteleza kudai ukomeshaji wa biashara ya watumwa. Biashara ya watumwa ilianza kuonekana kama biashara ovu ambayo ilisababisha vifo kwa idadi kubwa ya watu, ilizuia upanuzi wa biashara za aina nyingine katika pwani za Afrika, na kuruhusu unyama kustawi barani.

Watetezi wa ukomeshaji walijitahidi kutumia Ukristo, teknolojia ya ustaarabu wa Magharibi, na biashara ya kawaida, hasa katika bidhaa za kilimo, katika kuizima biashara ya watumwa. Hata hivyo, kwanza walipaswa kuushawishi umma huko Ulaya na Marekani kukubali ukomeshaji wa utumwa, halikadhalika fikra za serikali kuhusu biashara ya watumwa zilitakiwa nazo kubadilishwa.

Kampeni ya ukomeshaji wa biashara ya watumwa huko Magharibi iliongozwa na Uingereza. Baada ya kushindwa kwa pendekezo la ukomeshaji wa biashara ya watumwa kwa pamoja katika mwaka wa 1787 na 1807, Uingereza ilibuni mpango wa utekelezaji wenye vipengele vitatu ili kutia kani shughuli hiyo.

  • Hatua ya kwanza ilikuwa kuyafanya mataifa mengine kutunga sheria ambazo zitaharamisha raia wao kujihusisha na biashara ya watumwa.
  • Hatua ya pili ni ile ya kutayarisha mikataba ya pande mbili ambayo wanamaji waruhusiwe kupekua meli na kukamata meli za biashara za taifa jingine endapo zitapatikana zikiendesha biashara ya watumwa.
  • Ya tatu ni ushirikiano kupitia tume za pamoja zenye uwezo wa kuhukumu meli za watumwa zinazokamatwa, na kuwaachilia huru watumwa wanaopatikana ndani ya meli hizo.

Ni jambo la kushangaza kuona kuwa mpango huu haukuanzishwa Afrika, kulikotoka watumwa wengi wakati huo, ulielekezwa zaidi huko Ulaya na Marekani kulikokuwa na wanunuzi wa watumwa hao.

Serikali zilizokuwa dhaifu zilisalimu amri kwa shinikizo la Waingereza la kukomesha biashara ya watumwa, lakini katika hali nyingine, mpango huu ulikubalika tu baada ya vitisho kutoka Uingereza, Denmark, Uholanzi na Sweden zilitia sahihi ya makubaliano ya kukomesha utumwa kwa pamoja na Uingereza, Hispania na Ureno zilikubali kuizima biashara kwa fidia kutoka Uingereza mnamo mwaka 1817, ijapokuwa Ureno haikukomesha biashara hiyo moja kwa moja hadi ilipofikia mwaka 1842, baada ya tishio kutoka Uingereza. Brazil iliendelea na biashara hiyo hadi mwaka 1850, wakati Cuba haikukomesha biashara hiyo hadi ilipofikia mwaka 1866.

Nchi nyingine zilizokuwa na nguvu zaidi kisiasa kwa upande mwingine, zilitumia njia nyingine kujibu mapigo ya shinikizo la Waingereza ambalo waliliona kama uvamizi wa mamlaka yao. Ufaransa na Marekani ziliendelea na biashara hiyo kwa miaka kadhaa kabla ya kuikomesha kabisa. Ufaransa ilikubali kuikomesha biashara hiyo katika miaka ya 1830, wakati Marekani haikuikomesha hadi ilipofika nusu ya pili ya karne ya 19.

Wenye mashamba huko Marekani na katika visiwa vya Karibi walipinga ukomeshaji wa biashara ya watumwa kwa sababu mbalimbali. Hawakuona maana yoyote katika kukomesha biashara ya watumwa kwa kutumia hoja ya ubinadamu. Watu hao walikuwa wabaguzi wa rangi kiasi kwamba hawakuweza kuona ni kwa vipi ukomeshaji wa biashara ya watumwa utawasaidia watu weusi. Waling’ang’ania kwa muda mrefu faida nyingi za kiuchumi walizojikusanyia kutokana na umilikaji wa watumwa na nguvu-kazi za watumwa hao katika mashamba yao. Zaidi ya hayo, upinzani wao uliimarishwa na kuhitajika sana kwa bidhaa zilizozalishwa na watumwa huko Magharibi. Wakati huohuo, Magharibi, iliyokuwa inaongozwa na Uingereza, ilikuwa inashinikiza upigwaji marufuku wa uingizaji wa watumwa ambao wenye mashamba waliwaona ni muhimu katika kuongeza utoaji wa bidhaa hizo.

Mchakato wa ukomeshaji wa utumwa

Dhamana ya ukomeshaji wa biashara ya watumwa ilikabidhiwa kwa makamanda wa meli za kivita zilizoendesha shughuli zake, si tu katika pwani ya Afrika ya Magharibi, bali pia katika bahari ya Kati. Ufaransa iliongoza operesheni hizo katika hiyo bahari ya Mediterania kama moja ya mbinu zake za kuliwezesha jeshi lake la majini kuitawala bahari hiyo iliyozungukwa na nchi kavu.

Kwa muda, katika miaka ya 1830, Uingereza ilionekana kupoteza uongozi wake katika kukomesha biashara ya watumwa. Shughuli za meli za kivita zilikuwa na ushindi katika sehemu fulani tu. Meli za Waingereza zilikamata meli za watumwa za Wafaransa kati ya Mauritius na Bukini katika bahari ya Hindi. Lakini hakukuwepo kanuni za namna ya kuwashughulikia waliokamatwa.

Mara nyingine watumwa waliokuwa chomboni waliachiwa huru, na mara nyingine walisambazwa katika mashamba ya wenyeji. Meli za Wafaransa zilizokamatwa na Wafaransa wenyewe zilishtakiwa, na watumwa waliookolewa walipelekwa Kayenne. Hata hivyo zoezi zima la ukomeshaji wa biashara hii lilikuwa na ukosefu wa uwiano wa aina mbalimbali. Kwa mfano hukumu ilitolewa dhidi ya meli ya watumwa na si dhidi ya wafanyabiashara. Huko Marekani pia kuliwepo na tofauti kadhaa zilipingana kukamata meli za watumwa. Kwa sababu hiyo, ni meli chache sana zilizokamatwa, licha ya takribani meli sabini za kijeshi kutoka mataifa mbalimbali kushirikiana.

Wafanyabiashara ya watumwa pia waliyafanya majukumu ya kikundi cha merikebu na vita yawe magumu zaidi. Walitumia bendera bandia pamoja na njia nyingine za udanganyifu ili kuepuka kugundulika na kukamatwa. Hii ilichangia katika kuongezeka kwa vurugu. Makapteni wa vikundi vya merikebu na magavana wenyeji wa makazi ya Magharibi walianza safari za bara kuwaadhibu waliofanya biashara ya watumwa. Vituo vya biashara hatimaye navyo vilishambuliwa na kuangamizwa. Mifano ya vituo hivyo ni kama vile vilivyokuwa Cape Mount ambavyo vilishambuliwa kwa mabomu na gavana wa Liberia, mchungaji Jehudi Ashamum. Watumwa waliopatikana kutokana na safari hizo waliachiwa huru na kupelekwa Sierra Leone, Gambia na Mauritius.

Kutokana na jambo hilo, iligunduliwa kuwa muhimu kuwahusisha viongozi wa Kiafrika katika ukomeshaji wa biashara ya watumwa. Kufuatia uamuzi huo mbinu mbili mpya zilianzishwa na Uingereza na Ufaransa.

Kipindi cha miaka 1841 - 1850 kilikuwa pia maarufu kwa biashara ya watumwa ya kuvuka Sahara. Nchi za Magharibi hazikuwa na namna yoyote ya kukomesha biashara hiyo kwa sababu ilikuwa moja kwa moja mikononi mwa Waafrika na haikuenea nje ya mipaka ya Afrika. Kati ya 1841-1842, utawala wa muda wa Tunisia ulikomesha biashara ya watumwa, na Sultani wa Ottoman aliipiga marufuku biashara hiyo mnamo mwaka 1857. Hata hivyo majaribio hayakupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya watumwa waliokuwa bado wanasafirishwa nje, na jitihada za baadaye hazikuonyesha matunda yoyote.

Mwitikio wa Waafrika

Zaidi ya Waafrika milioni moja waliuzwa huko Amerika katika miongo miwili ya mwisho ya karne ya 18 kabla ya biashara ya watumwa kukomeshwa rasmi huko Magharibi. Kitendo cha kutunga sheria ya ukomeshaji wa biashara ya watumwa huko Ulaya hakikutosha kusitisha biashara hiyo mara moja. Vituo vya jadi vya biashara ya watumwa katika maeneo yaliyodhibitiwa na Wazungu kama vile Sierra Leone, Liberia na Gold Coast vilifungwa. Kutokana na udhaifu wa viongozi wa kisiasa wa jamii hizi, zoezi la kukomesha biashara ya watumwa halikuvuka mipaka yao.

Sehemu nyingine kama vile Dahomey, ambako mtawala wake alitegemea biashara ya utumwa, biashara ya kawaida ya watumwa iliendelea. Kulikuwa na uhakika wa upatikanaji wa watumwa kutoka Sudan ya Kati, na vita miongoni mwa Wayoruba vilifurisha soko la Whydah kwa watumwa. Viongozi wa jadi na wafanyabiashara ya watumwa wa pwani walitoa watumwa kwa wafanyabiashara wa Ureno na Brazil ambao walitajirika kwa biashara hii kabla ya kugeukia biashara ya bidhaa nyinginezo.

Kulikuwepo na taasisi za kienyeji pamoja na vikundi rasmi ambavyo vilihusika na sehemu kubwa ya biashara ya watumwa katika eneo la delta ya Niger na Kalabari Kongwe (Old Calabar). Miongoni mwao walikuwemo makuhani na waheshimiwa, waaguzi wa Arochukwu, na jumuiya ya Ekpe. Biashara iliratibiwa kwa kanuni zilizojulikana kwa muda mrefu, na watumwa walipatikana kutoka sehemu za mbali, kama vile Sokoto, Benue, Nupe na Kaskazini-Magharibi mwa Cameroon. Kulikuwa pia na sheria za jadi na desturi za jamii ambazo ziliruhusu watumwa kuchukuliwa kutoka karibu zaidi na nyumbani, kutoka maeneo ya ndani zaidi ya delta.

Hifadhi ya Watumwa

Sierra Leone

Mnamo mwaka 1788, Sierra Leone ilianzishwa kama makazi ya huruma na kama sehemu ya tapo la kupinga utumwa. Uhurishaji wa watumwa ulikuwa usaidiwe kwa kuwaingiza katika Ukristo na ustaarabu wa Magharibi. Walikuwa pia wapatiwe mwelekeo wa kibiashara.

Watumwa wengi zaidi walioachiwa huru waliletwa huko, na ilipofikia mwaka 1811, jumla ya watu hao ilishafikia 4,000. Ilipofikia mwaka 1838, tayari Waafrika 21,000 walikuwa wakiishi Freetown na vijiji kadhaa vilivyouzunguka mji huo. Ilipofika mwaka 1830 idadi ya watu ilishaongezeka karibu mara tatu.

Freetown ilikuwa si tu makao makuu ya utawala wa koloni la kifalme la Kiingereza na ya Makamu Mkuu wa Jeshi la Wanamaji, bali pia kituo rasmi cha ukombozi wa Tume ya Pamoja iliyokuwa ikihukumu meli za watumwa zilizokamatwa. Koloni lilifunguliwa kwa biashara ya nje mnamo mwaka 1831; kutokana na hili, ruzuku kutoka serikali ya Uingereza iliondolewa, na wakazi walitakiwa kuchukua madaraka juu ya masuala yao ya kujitegemea.

Hadi kipindi cha pili cha karne ya 19, tamaduni mbalimbali za Sierra Leone zilishaunganishwa pamoja kuunda jamii ya Krioli, kwa maendeleo yake peke yake ya ndani. Mwaka 1853, wananchi wa Sierra Leone walifanywa raia wa mfalme wa Uingereza.

Liberia

Liberia ilikuwa matokeo ya haja ya kusaidia na kustaarabisha Waafrika. Vuguvugu hizi zilianzishwa na chama cha ukoloni cha Marekani, na serikali ya shirikisho ya USA ilisaidia kwa kuiongezea idadi ya watu kwa kuwapeleka watumwa walioachiwa huru na merikebu za doria ili kuishi huko. Liberia pia ilikuwa matokeo ya nia ya kujaribu kupunguza athari za watu weusi waliopatiwa uhuru wao huko Marekani.

Tatizo la kwanza lililowakumba walowezi wa Liberia lilitokana na chuki ya viongozi wa nchi jirani za Kiafrika, ambao walichukia kuingiliwa na wageni katika nchi yao na kuwa tishio kwenye biashara ya watumwa ambayo ilikuwa shughuli yao kuu ya kibiashara ya kuvuka bahari. Pingamizi lao lilidhibitiwa na walowezi chini ya uongozi wa Jehudi Ashmum, na hivyo kutoa mwanya kwa koloni kuendelea kuwepo.

Koloni lilipewa jina la Liberia, na Monrovia ukawa ndio mji mkuu, na Ralph Randolph Gurley mnamo mwaka 1824. Liberia ilitawaliwa na Chama cha Ukoloni cha Marekani (American Colonization Society) kwa kumtumia kiongozi rasmi ambaye, kutokana na umbali, aliachiwa huru kwa kiasi fulani kutawala kulingana na ufafanuzi binafsi wa hati iliyoidhinisha makazi hayo.

Liberia iliundwa si tu na Waafrika walioachiwa huru; idadi kubwa ya walowezi wa mwanzo walikuwa watumwa waliotolewa utumwani huko kusini mwa Marekani kwa sharti la kuhama.

Biashara mbadala

Katika enzi za ukomeshaji wa utumwa, nchi za Magharibi kwa jumla zilijali zaidi kulinda biashara mpya za mazao ya kilimo kuliko kufanikisha ukomeshaji wa biashara ya watumwa. Biashara ya bidhaa nyingine haikushinda kwelikweli, na biashara ya watumwa iliendelea sambamba na biashara hiyo.

Mapinduzi ya Viwanda na Teknolojia huko Uingereza na Ufaransa yalizua soko kubwa la bidhaa za Kiafrika kama vile mafuta ya mawese, ambayo yalihitajika kulainisha mashine, na kama malighafi ya kutengeneza sabuni na mafuta ya taa. Ufaransa pia iliingiza karanga na aina fulani ya njugu kutoka Senegal na Gambia kwa ajili ya kutengeneza sabuni za nyumbani. Ukuaji wa biashara hii uliwakilisha uanzishaji wa biashara ya kuchukua nafasi ya biashara ya watumwa. Mabadiliko hayo ya kiuchumi nayo yaliongezewa kasi na ueneaji wa Ukristo, elimu ya Magharibi na athari nyingine za kitamaduni kutoka Ulaya na Marekani.

Hitimisho

Kwa namna fulani biashara ya watumwa ilibadilishwa kwa ukoloni. Chini ya utawala wa kikoloni, mabaki ya biashara ya watumwa na utumwa kama asasi ya jamii vilikomeshwa. Kwa mfano kati ya miaka 1860-1870, wakati biashara ya watumwa ilikuwa inakufa huko Magharibi na Kusini, pwani ya Afrika Mashariki ilikuwa inashuhudia kuhuishwa kwa biashara hiyo. Jitihada za Uingereza za kuzima biashara hiyo kwa kutiliana mikataba na Sultani wa Zanzibar zilikuwa na athari ndogo tu. Ni pale tu kulipoanzishwa utawala wa kikoloni katika eneo hilo, ndipo biashara ya watumwa ilipofika mwisho wake.

Hata hivyo, baadhi ya aina mbaya zaidi za ukoloni, kama vile mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Afrika ya Kusini, zilikaribiana sana na utumwa. Mapambano dhidi ya kudhalilishwa kwa utu wa binadamu yanapaswa kuendelezwa.

Utambuzi wa unyama wa biashara ya watumwa unazidi kuongezeka. Kadhalika, lipo tapo linalozidi kupamba moto la kutaka Afrika na Waafrika walioko uhamishoni kudai fidia kutokana na madhara yaliyosababishwa na biashara ya watumwa.

Tanbihi

  1. Wilson, Thomas, The Oglethorpe Plan, 201–06.

Angalia pia

Marejeo

  1. Anstey, R. (1975). Atlantic Slave Trade and British abolition, 1760-1810, Cambridge University Press, London
  2. Asiegbu, J. U. J. (1969). Slavery and the Politics of Liberation, 1787-1861: A Study of Liberated African Emigration and British Ant-Slavery Policy, Longmans Green, London
  3. Austen, R. A. (1970) The Abolition of the overseas slave trade: a distorted theme in West African history', JHSN
  4. Buxton, T. F. (1840). The African Slave Trade and its redemy, John Murray, London
  5. Duignan, P. (1963). The United States and the African slave trade, 1619-1862, Revolution and Peace Hoover Institution on War, Stanford

Viungo vya nje