Vita za Misalaba

(Elekezwa kutoka Wanamisalaba)

Vita za Misalaba (pia: Vita vya msalaba) vilitokea kati ya mataifa ya Wakristo wa Ulaya na watawala Waislamu wa nchi za Mashariki ya Kati wakati wa karne za 11 hadi 13, hasa kuanzia 1095 hadi 1291 katika jina la dini na kwa baraka za Kanisa Katoliki. Kaisari wa Bizanti aliomba msaada wa Wakristo wa magharibi dhidi ya mashambulio ya Waturuki Waislamu. Hivyo Papa aliwaita mataifa ya Kikatoliki ya Ulaya kuikomboa nchi takatifu. Tangu mwaka 1096 hadi mwaka 1270 kampeni za kijeshi zilianzishwa Ulaya kuelekea Yerusalemu.

Mwanajeshi wa misalaba (mchoro wa karne ya 13).
Mtawa Petro mkaapweke akihubiri vita vya msalaba mbele ya makabaila wa Ufaransa.

Kwa maana nyingine na pana zaidi "vita vya msalaba" vilikuwa jitihada za watawala wa Ulaya kutetea haki za Wakristo wenzao wa nchi hizo, au kujitetea kwa silaha na vita na wakati huohuo kueneza himaya yao pamoja na Ukristo.

Jina limetokana na desturi ya wanajeshi wa vita ya kwanza ya misalaba kushona alama ya msalaba juu ya nguo zao kama dalili ya kiapo walichotoa cha kuwafukuza Waislamu katika mji wa Yerusalemu. Walifundishwa kuwa vita hivyo ni vitakatifu: atakayekufa atafika mbinguni kwa hakika. Wataalamu wanahisi kama hapo athari za mafundisho ya Kiislamu juu ya "jihadi" zimeingia katika Ukristo.

Hali ya Wakristo wa Yerusalemu na Mashariki ya Kati

hariri

Tangu mwaka 637 BK mji wa Yerusalemu pamoja na nchi nzima ya Palestina ilikuwa mikononi mwa Waarabu Waislamu waliofaulu kushinda jeshi la Bizanti. Wakazi wengi wa nchi hiyo waliendelea kufuata dini zao, hasa Ukristo na Uyahudi, lakini sehemu ya wananchi polepole waligeukia pia Uislamu.

Yerusalemu iliendelea kuwa lengo la wahiji Wakristo waliotaka kutembelea mahali ambako Yesu Kristo aliishi, hasa Kanisa la Kaburi na Ufufuo wa Yesu.

Watawala Waarabu waliwahi kuahidi kuheshimu Wakristo walioishi chini ya utawala wao na kutunza haki zao.

Hali hiyo ilibadilika vibaya mara ya kwanza wakati ya khalifa Al Hakim wa Misri aliyewatesa Wakristo kuanzia mwaka 1001; Kanisa la Kaburi na Ufufuo lilibomolewa pamoja na makanisa mengi nchini Palestina. Dhuluma ya Al Hakim ililegezwa na waandamizi wake, na kanisa hilo la Yerusalemu likajengwa upya kwa msaada wa Kaisari wa Bizanti.

Amani katika mashariki ya kati ilivurugika tena kutokana na uenezi wa Waseljuki waliokuwa kabila kubwa la Waturuki kutoka Asia ya kati waliokuwa wamehamia magharibi, kupokea Uislamu na kutawala Uajemi pamoja na maeneo ya jirani. Mwaka 1071 jeshi la Waseljuki lilishinda Wabizanti kwenye mapigano ya Manzikert na kutwaa sehemu kubwa ya Anatolia (leo Uturuki) pamoja na Siria na Palestina. Vikosi vya Seljuki walishambulia pia mara kwa mara wahiji Wakristo kutoka Ulaya walioelekea kaburi takatifu mjini Yerusalemu na hija ya Kikristo ya Yerusalemu ikaona kipindi kigumu. Wakristo waliohiji huko kutoka Ulaya walishambuliwa njiani mara kwa mara.

Mwaka 1095 Kaisari Aleksios I wa Bizanti alipanga kuwaondoa tena Waseljuki katika Anatolia kutoka sehemu walizowahi kutwaa miaka michache ya nyuma. Hapa alituma mabalozi kwa Papa Urban II wa Roma kwa kusudi la kupata msaada wa askari wa kukodiwa kutoka Ulaya. Alifanya hivyo miaka 40 baada ya kutokea kwa farakano la mwaka 1054 kati ya makanisa ya Waorthodoksi na Roma, labda kwa tumaini la kuanzisha upya maelewano.

Wito wa Papa Urban II mwaka 1095

hariri

Papa Urban II aliwapokea mabalozi wa Bizanti katika Italia akasikia ombi la Kaisari. Inaonekana aliona nafasi ya kuwaelekeza mashariki makabaila wadogo wa Ulaya ambao walizoea kuvuruga amani ya Ulaya kwa mapigano ya mfululizo na vita ndogondogo, wakiharibu mali ya watu wengi.

Kwenye sinodi ya Clermont, mbele ya maaskofu na maabati wa Ufaransa alitangaza ombi la msaada kutoka Bizanti na kuhimiza makabaila kupokea wito huu wa kuwasaidia Wakristo wenzao wa mashariki badala ya kuharibu mali ya watu wa nyumbani. Hotuba ya Papa ikapokewa na sinodi na umati mkubwa wa wasikilizaji walioitikia kwa sauti moja "Mungu anaitaka" (Deus lo vult).

Makabaila kadhaa walipiga magoti mbele ya Papa wakiomba baraka kwa mipango yao ya kuitikia wito wake. Wengine walisikia habari hizo baadaye, na makabaila wengi wa Ufaransa waliamua kujiunga na mradi wa kwenda mashariki kuwasaidia Wakristo wa huko na kuwaondoa Waislamu katika nchi zilizowahi kuwa za Kikristo.

Wahubiri walizunguka Ulaya kutangaza mpango huo. Ni wahubiri hao waliosambaza ujumbe wa kwamba shabaha ya vita ni Yerusalemu, ingawa wala Kaisari Aleksios wala Papa Urban waliwahi kutumia jina hilo. Lakini wakati ambapo watu wengi hawakujua kusoma na kuandika wala hawakuwahi kuona ramani jina la Yerusalemu lilijulikana kote hata kama wasikilizaji wengine hawakuelewa tofauti kati ya mahali pa dunia hii na Yerusalemu wa mbinguni uliohubiriwa pia kanisani.

Vita vya msalaba vilivyoanza na kuendelea

hariri

Mwaka 1096 vilikusanyika vikundi vya watu wa kawaida walioongozwa na wahubiri waliotaka kwenda mashariki kwa hiari yao, ingawa si wanajeshi. Umati huo waliomba na kutisha miji walipopita wapewe chakula na misaada kwa sababu wengi hawakuwa na kitu wenyewe. Katika miji ya Ujerumani ya magharibi na kusini walianza kushambulia Wayahudi walioishi huko na kuwaua wengi.

Mwaka 1099 jeshi la Ulaya lilifika mbele ya kuta za Yerusalemu. Baada ya mapigano mafupi jeshi la msalaba liliwashinda wateteaji Waislamu. Katika hasira ya mapigano waliua ovyo wakazi wengi sana, wazee na watoto, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi. Kabaila Mfaransa alipokea cheo cha "Mfalme wa Yerusalemu".

Lakini miaka 100 baadaye Sultani Salah-ed-Din wa Misri aliwafukuza tena wanamsalaba kutoka Yerusalemu. Miaka 40 baadaye alirudisha mji kwa hiari baada ya kupatana na Mfalme Mjerumani. Lakini muda wote huo Wazungu walitawala sehemu ya Palestina na Siria tu. Waislamu waliwaona kama maadui. Hata Wakristo wenyeji (Waorthodoksi) hawakuwakubali kuwa wakombozi kwani walijaribu kuwaunganisha Wakristo wote chini ya Kanisa Katoliki. Safari moja iliyoondoka Ulaya mwaka 1204 ili kuikomboa Yerusalemu, kumbe ilifika mpaka Bizanti tu ambako wanajeshi wa msalaba waliteka mji, kupora utajiri na kumfukuza Kaisari wa Bizanti. Miaka 100 baadaye Kaisari alirudi na kuunda upya Ufalme wa Roma ya Mashariki.

Mwaka 1291 jeshi la Kiislamu liliwafukuza kabisa wanajeshi wa msalaba katika nchi takatifu wasirudi tena. Lakini walikuwa wamevunja nguvu ya Bizanti kiasi cha kutosha. Kumbe Ulaya Magharibi iliharibu ulinzi wa dola la mashariki dhidi ya Waturuki waliofaulu baadaye kuingia Ulaya. Badala ya kufukuzwa, jeshi la Waturuki lilianza kuishambulia Ulaya Kusini-Mashariki. Mwaka 1453 ulianguka mji wa Bizanti, na mwaka 1529 Waturuki walifika mpaka Vienna, mji mkuu wa Mfalme wa Ujerumani. Hapo walirudishwa nyuma. Lakini nchi nyingi za Ulaya Kusini-Mashariki pamoja na Wakristo wao walikaa chini ya Waturuki kwa karne tatu zijazo.

Tathmini

hariri

Kwa ujumla majaribio ya vita vya msalaba ya kuikomboa nchi takatifu yalishindikana. Vita hivyo vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu. Kipindi cha vita vya kidini kilisababisha mateso mengi kwa Wakristo Waorthodoksi chini ya Waislamu. Walidaiwa kulipa madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.

Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu walivunja ahadi nyingi walizozitoa, lakini mahali pengi Wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu. Maisha haya yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliruhusiwa kuendelea na ibada zao (ila waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza). Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema.

Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Sababu kuu ni kwamba kama Mkristo alikuwa amegeuka Mwislamu hakuweza kurudi tena. Sheria ya Kiislamu inamruhusu Mkristo kugeukia Uislamu, lakini mtu aliyekuwa Mwislamu anastahili adhabu ya kifo akigeukia Ukristo au dini nyingine. Pamoja na hayo, Wakristo wengi walianza kuhamia nchi ambako watakuwa raia huru bila kasoro.

Wakati ule Wakristo wengi walikosa vilevile ustahimilivu kwa watu wenye imani tofauti. Hakuna Mwislamu aliyeweza kubaki katika nchi za Hispania na Ureno baada ya kuvunjwa wa utawala wa Kiarabu. Lakini ipo mifano mingine: Wakristo wote walifyekwa Uarabuni kwenyewe kumbe Waislamu waliweza kubaki chini ya Waaustria Wakristo waliotawala nchi za Ulaya Kusini-Mashariki. Kweli kati ya dini hizo mbili hakuna anayeweza kujisifu tu juu ya historia yake bila kukiri makosa na kasoro zake.

Viungo vya nje

hariri