Historia ya Visiwa vya Karibi

Historia ya Visiwa vya Karibi inaeleza ramani ya kisasa ya eneo hili na mchanganyiko wa lugha na tamaduni unaopatikana kwenye visiwa hivyo vilivyopo kati ya Amerika ya Kusini na Amerika ya Kaskazini.

Mageuzi ya kisiasa ya Amerika ya Kati na Karibi kutoka 1700 hadi sasa
Ramani ya kisiasa ya Karibi

Kabla ya mawasiliano na Ulaya

hariri

Miaka 10,000 - 12,000 iliyopita vikundi vya wawindaji na wavuvi walikuwa wamefika Amerika ya Kusini na kusambaa katika bara. Wengi wao walikuwa hawajaanza bado kujenga makazi ya kudumu bali walihamahama.[1]

Trinidad ilikuwa kisiwa cha kwanza cha Karibi kilichofikiwa na wanadamu takriban mnamo 9000/8000 KK ilhali wakati ule iliunganishwa bado na bara kwa nchi kavu.[2] Makazi ya kale ya miaka ya 6000 KK hadi 5100 KK yalitambuliwa pale St. Johns ambako mafungu makubwa ya kombe za kome yamegunduliwa yaliyokuwa chakula chao.

Visiwa vingine nje ya Trinidad vilianza kufikiwa na watu kuanzia miaka ya 3000 KK na akiolojia imegundua mabaki ya kipindi hicho huko Barbados, Kuba, Curaçao na St Martin, ikifuatiwa na Hispaniola na Puerto Rico. [3]

Kati ya miaka 800 na 200 KK kilitokea kikundi kipya cha wahamiaji kwenye visiwa ambao wanatambuliwa kutokana na vyungu vyao vya pekee.[4]

Kipindi cha miaka 650 hadi 800 BK kiliona mabadiliko makubwa ya kitamaduni, kijamii na kisiasa ambayo yalitokea bara na katika visiwa vingi vya Karibi.[5] Kipindi hicho kilikuwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Vipindi vya ukame viliongezeka, pamoja na kutokea kwa vimbunga. Kwa jumla idadi ya watu wa Karibi iliongezeka na jamii zilibadilika kutoka makazi katika kijiji kimoja hadi kuunda marundiko ya vijiji. Kilimo kwenye visiwa kiliongezeka.

Wakati wa kuwasili kwa Wazungu, makundi makubwa matatu ya Waindio waliishi visiwani:

  • Wataino (waliitwa pia Waarawak) katika Antili Kubwa, Bahamas na Visiwa vya Leeward;
  • Wakaribi wa visiwa na Wagalibi katika Visiwa vya Windward ;
  • Wasibonei magharibi mwa Kuba.
  • Wataino wamegawanywa katika Wataino wa Kawaida, ambao walichukua Hispaniola na Puerto Rico, Wataíno wa Magharibi, ambao walichukua Cuba, Jamaica, na visiwa vya Bahamas, na Wataino wa Mashariki, ambao walichukua Visiwa vya Leeward. Trinidad ilikaliwa na vikundi vyote vinavyozungumza Wakaarib na Arawak.

Mwanzo wa ukoloni

hariri
 
1536 ramani ya Caribbean

Mara tu baada ya safari za Christopher Columbus kwenda Amerika alipotua kwenye eneo la Karibi mara ya kwanza mwaka 1492, Hispania na Ureno zilituma jahazi zao kwa upelelezi zaidi na kuanza kudai utawala juu ya maeneo. Baada ya kugunduliwa kwa dhahabu katika visiwa kadhaa, pia mataifa mengine ya Ulaya, hasa Uingereza, Uholanzi na Ufaransa zilitarajia kuanzisha makoloni yenye faida. Mashindano ya nchi hizo yalisababisha vita kati ya milki za Ulaya kwa karne kadhaa zilizopigwa pia kwenye makoloni yao.

Mwanzo wa karne ya 19 uliona harakati ya makoloni mengi ya Hispania katika Amerika ya Kusini kupigania uhuru na himaya ya kikoloni ya Hispania iliporomoka. Lakini Kuba na Puerto Rico zilibaki chini ya taji la Hispania hadi Vita ya Marekani dhidi Hispania ya mwaka 1898.

Uvamizi wa Hispania

hariri
 
Visiwa vya Karibi vya Hispania mnamo mwaka 1600.

Wakati wa safari ya kwanza ya Christopher Kolumbus mawasiliano yalifanywa na wenyeji katika Bahamas na Wataíno huko Kuba waliokuwa na mapambo ya dhahabu. Dhahabu hiyo iliwahamasisha Wahispania kutafuta utajiri wakiwalazimisha wenyeji kuchimba metali hiyo adimu. Waindio walianza kufa, pamoja na ukali wa Wahispania hasa kutokana na maambukizo ya magonjwa kutoka Ulaya ambayo hayakujulikana awali upande huo wa bahari.

Hapo Wahispania walianza kuleta watumwa Waafrika, kwa imani kwamba hawataathiriwa na magonjwa hayo. Pia mapadre wa Kanisa Katoliku walishawishi wafalme wa Hispania kutangaza sheria zilizoweka vikwazo kwa utumwa wa Waindio. Ndio chanzo cha wakazi wengi wa Visiwa vya Karibi kuwa na asili wa Afrika. Watumwa walichukuliwa kwa kazi katika migodi na pia kwenye mashamba, hasa mashamba ya miwa ambayo ilikuwa zao lisilostawi katika sehemu kubwa ya Ulaya.

Hispania ilidai utawala juu ya visiwa vyote lakini kulikuwa na makazi kwenye visiwa vikubwa vya Hispaniola, Puerto Rico, Jamaika, Kuba na Trinidad pekee, ilhali waliacha visiwa vingi vidogo.

Wazungu wengine

hariri

Mataifa mengine ya Ulaya yaliingia baada ya kudhoofika kwa milki ya Hispania wakatwaa vituo kwenye viswa kadhaa na kubaki. Walianzisha kilimo hasa ya miwa na kwa kazi hiyo walichukua mamilioni ya watumwa kutoka Afrika.[6]

  • Francis Drake alikuwa nahodha Mwingereza aliyepewa kibali cha malkia wake kushambulia Wahispania na kupora mali yao. Alifaulu kutwaa mzigo mkubwa wa fedha iliyokuwa njiani kutoka migodi ya Peru kwenda Hispania kwenye mwaka 1573.
  • 1612 Waingereza walianza kupeleka walowezi Bermuda, ikifuatwa na Barbados mnamo 1627.
  • 1625 Ufaransa ilianza kupeleka walowezi kwenye Karibi, walianza Saint Kitts pamoja na Waingereza wakigawana kisiwa kati yao mnamo 1625. Kutoka huko waliendelea kuingia Guadeloupe (1635) na Martinique (1635).
  • Admirali Mwingereza William Penn aliteka Jamaika mnamo 1655, ikabaki chini ya utawala wa Uingereza kwa zaidi ya miaka 300. [7]
  • Kwenye miaka ya kwanza ya ukoloni maharamia wengi walikusanyika katika visiwa vya Karibi. Walivutwa na meli za Hispania zilizobeba fedha kutoka Peru na Meksiko, pamoja na nafasi za kujificha kati ya visiwa vingi vidogo.
  • Maharamia Wafaransa walianzisha makazi kwenye kisiwa cha Hispaniola. Hispania ilishindwa kuwafukuza. Makazi yao yalitambuliwa na mfalme wa Ufaransa na mwaka 1697 Hispania ilikabidhi rasmi theluthi ya magharibi ya Hispaniola kwa Ufaransa, eneo ambalo sasa ni jamhuri ya Haiti. [8] . [9]
  • Waholanzi walichukua Saba, Saint Martin, Sint Eustatius, Curaçao, Bonaire, Aruba, [10] Tobago, St. Croix, Tortola, Anegada, Virgin Gorda, Anguilla na kwa muda mfupi pia Puerto Rico.
  • Denmark ilitawala visiwa ambavyo sasa vinaitwa Visiwa vya Virgin vya Marekani tangu 1672 ikaviuza kwa Marekani mwaka 1917.

Utumwa

hariri
 
Watumwa walioletwa kwenye Karibi waliishi katika mazingira magumu. Hapo juu ni mifano ya vibanda vya watumwa huko Bonaire vilivyotolewa na wakoloni wa Uholanzi. Watumwa 2 au 3 walilala katika kila kibanda baada ya kazi katika migodi ya chumvi iliyo karibu.

Kustawi kwa kilimo kwenye visiwa vya Karibi kulihitaji wafanyakazi wengi. Wazungu walitumia nafasi ya upatikanaji wa watumwa barani Afrika. Biashara ya watumwa ya Atlantiki ilileta watumwa wa Kiafrika katika makoloni ya Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ureno na Hispania katika Amerika, pamoja na visiwa vya Karibi.

Jedwali lifuatalo linaorodhesha idadi ya watumwa walioletwa katika baadhi ya makoloni ya Karibi: [11]

Mkoloni 1492-1700 1701-1810 1811-1870 Jumla ya watumwa walioingizwa
Uingereza 263,700 1,401,300 - 1,665,000
Uholanzi 40,000 460,000 - 500,000
Ufaransa 155,800 1,348,400 96,000 1,600,200

Wapinzani wa utumwa (abolutionists) katika Amerika na huko Ulaya, hasa Uingereza walianza kupinga unyama wa utaratibu huo tangu mwisho wa karne ya 18. Uingereza ilitangaza sheria ya kukataza biashara ya watumwa kwenye mwaka 1807 ikafaulu kuingiza ukomeshaji wa biashara ya watumwa kuvukia bahari katika maazimio ya Mkutano wa Vienna wa 1815. Marekani ilikuwa pia na sheria ya kukataza kuchukuliwa kwa watumwa kutoka nje[12] tangu mwaka 1807. Usafirishaji wa watumwa kutoka milki za Afrika ulipungua, ingawa bado kulikuwa na magendo ya watumwa kutoka Afrika.

Hata hivyo, katika miongo ya kwanza utumwa uliendelea kwa hao waliokuwepo upande wa Amerika na waliozaliwa kama watoto wa mama mtumwa. Serikali zilihofia vurugu ya kiuchumi, kuporomoka kwa uchumi kwenye koloni na malalamiko ya wenye watumwa Uingereza walioweza kushtaki serikali mahakamani.

Uingereza ilipitisha Sheria ya Kukomesha Utumwa mnamo 1833. Wakati Sheria ya Kukomesha Utumwa ilipoanza kutumika mnamo 1834, karibu watumwa 700,000 katika Visiwa vya Karibi vya Kiingereza mara moja wakawa huru; watumwa wengine waliachiliwa miaka kadhaa baadaye.[13] Utumwa ulifutwa katika koloni za Uholanzi mnamo 1814. Hispania ilifuta utumwa katika himaya yake mnamo 1811, isipokuwa Kuba, Puerto Rico, na Santo Domingo; Hispania ilimaliza biashara ya watumwa kwenda makoloni haya mnamo 1817, baada ya kulipwa pauni 400,000 na Uingereza. Utumwa katika Kuba uliendelea hadi 1886. Ufaransa ilikomesha utumwa katika makoloni yake mnamo 1848.

 
Mashamba ya sukari katika koloni la Uingereza la Antigua, 1823

Kufuatia ukombozi wa watumwa mnamo 1833 nchini Uingereza, Waafrika wengi waliokombolewa waliwaacha mabwana zao wa zamani. Wengi hawakuwa tayari kurudi kwenye kazi hiyo. Hii ilileta matatizo ya kiuchumi kwa wamiliki wa mashamba ya miwa.

Waingereza walitafuta wafanyakazi waüya waisiodai mishahara makubwa. Wafanyakazi hao walipatikana China na baadaye zaidi kule Uhindi. Waingereza walitunga mfumo mpya wa kisheria wa kazi ya kulazimishwa, ambayo kwa njia nyingi ilifanana na utumwa wa muda. [14] Badala ya kuwaita watumwa, wafanyakazi hao waliitwa "wafanyakazi wa mkataba" (indentured labourers). Masharti ya kupata nafasi ya kazi ilikuwa kutia sahihi kwenye makataba ambako walikubali kuwa na deni kwa "gharama za safari" wakipaswa kukubali kufanya kazi kwa miaka mitano au zaidi bila haki ya kuondoka mapema. Katika kipindi hiki -ambako kutoroka kulitazamiwa kama kosa au hata jinai- mabwana walikuwa na mamlaka juu yao iliyofanana na utumwa.

Wakazi wengi wa leo kwenye visiwa vya Karibi ni wajukuu wa watumwa na wafanyakazi wa kimkataba mamilioni walioletwa katika Karibi [15] [16] [17] [18]

 
Wakata miwa huko Jamaica, miaka ya 1880.

Uasi wa watumwa

hariri
 
Picha mnamo 1815 inayoonyesha "Incendie du Cap" (Kuungua kwa Cape Francais) wakati wa Mapinduzi ya Haiti. Nukuu inasema: "Uasi wa jumla wa Weusi. Mauaji ya Wazungu ".

Mfumo wa kilimo na biashara ya watumwa ambayo iliwezesha ukuaji wake ilisababisha upinzani wa watumwa mara kwa mara katika visiwa vingi vya Karibi wakati wote wa ukoloni. Upinzani ulifanywa kwa kutoroka kutoka kwenye mashamba kabisa, na kutafuta kimbilio katika maeneo yasiyokuwa na makazi ya Wazungu. Jamii za watumwa waliotoroka, ambao walijulikana kama Maroons, waliungana pamoja katika maeneo yenye misitu minene na milima ya Antilles Kubwa na visiwa vingine vya Antilles Ndogo . Kuenea kwa mashamba na makazi ya Ulaya mara nyingi kulimaanisha kumalizika kwa jamii nyingi za Maroon, ingawa walinusurika Saint Vincent na Dominica, na katika maeneo ya milimani ya mbali ya Jamaica, Hispaniola, Guadeloupe na Cuba . [19]

Uasi wa watumwa wa Karibea (1522-1844)

hariri

Jedwali lifuatalo linaorodhesha maasi ya watumwa ambayo yalisababisha maasi halisi:

Kisiwa cha Karibi Mwaka wa uasi wa watumwa [20]
Antigua 1701, 1831
Bahamas 1830, 1832-34
Barbados 1816
Kuba 1713, 1729, 1805, 1809, 1825, 1826, 1830-31, 1833, 1837, 1840, 1841, 1843
Curaçao 1795-
Dominika 1785-90, 1791, 1795, 1802, 1809-14
Grenada 1765, 1795
Guadeloupe 1656, 1737, 1789,1802
Jamaika 1673, 1678, 1685, 1690, 1730-40, 1760, 1765, 1766, 1791-92, 1795-66, 1808, 1822-24, 1831-332
Marie Galante 1789
Martinique 1752, 1789–92, 1822, 1833
Montserrat 1776
Puerto Rico 1527
Saint Domingue 1791
Saint John 1733-34
Saint Lucia 1795-96
Saint Vincent 1769-73, 1795-96
Santo Domingo 1522
Tobago 1770, 1771, 1774, 1807
Tortola 1790, 1823, 1830
Trinidad 1837

Haiti, koloni la zamani la Ufaransa la Saint-Domingue huko Hispaniola, lilikuwa taifa la kwanza la Karibi kupata uhuru kutoka kwa nguvu za Ulaya mnamo 1804. Hii ilifuata miaka 13 ya vita ambayo ilianza kama uasi wa watumwa mnamo 1791 na ikageuka haraka kuwa Mapinduzi ya Haiti chini ya uongozi wa Toussaint Louverture, ambapo watumwa wa zamani walishinda jeshi la Ufaransa (mara mbili), jeshi la Hispania, na jeshi la Uingereza , kabla ya kuwa jamhuri ya kwanza na ya zamani nyeusi duniani, na pia jamhuri ya pili kwa kongwe katika Ulimwengu wa Magharibi baada ya Marikani. Hii pia inajulikana kama kuwa pekee ya mafanikio ya uasi wa watumwa katika historia. Theluthi mbili zilizobaki za Hispaniola zilishindwa na vikosi vya Haiti mnamo 1821 na kuwa chini ya Haiti. Mnamo 1844, sehemu ya Kihispania ilipata uhuru wake kama Jamhuri ya Dominika.

Kuba na Puerto Rico zilibaki kama makoloni ya Hispania hadi Vita ya Marekani dhidi Hispania mnamo 1898. Baada ya hapo Kuba ilikuwa kwa miaka kadhaa koloni la Marekani hadi kupata uhuru wake mnamo 1902, lakini Marekani ilibaki na kituo cha Guantanamo ikaingilia katika siasa ya Kuba mara kadhaa. Mapinduzi ya Kuba ya 1959 yalileta serikali ya kikomunisti iiyovunja kila uhusiano na Marekani. Puerto Rico ikawa koloni la Marekani hadi 1917 ambako watu wake walipokea uraia wa Marekani; sasa ni eneo la pekee la Marekani. Kuna raia wanaodai uhuru, kuna pia wale wanaotaka kuwa jimbo la Marekani kamili.

Kati ya 1958 na 1962 sehemu kubwa ya Karibi iliyodhibitiwa na Uingereza ilijumuishwa kama Shirikisho jipya la West Indies katika jaribio la kuunda serikali moja huru ya baadaye - lakini ilishindikana. Makoloni yalipata uhuru wao wenyewe; Jamaika (1962), Trinidad na Tobago (1962), Barbados (1966), Bahamas (1973), Grenada (1974), Dominica (1978), Saint Lucia (1979), Saint Vincent na Grenadini (1979), Antigua na Barbuda ( 1981), Saint Kitts na Nevis (1983).

Visiwa hivi sasa ambavyo si nchi za kujitegemea

hariri
 
Gari la farasi kwa watalii huko Martinique, moja ya visiwa vya Karibi ambayo haijapata uhuru. Ni mkoa wa ng'ambo wa Ufaransa, na raia zake ni raia kamili wa Ufaransa.

Kuanzia karne ya 21 sio visiwa vyote vya Karibi vilivyoendelea kuwa nchi huru. Visiwa kadhaa vinaendelea kuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Ulaya, au na Marekani.

Ufaransa ilibaki na makoloni kadhaa ambayo kwa sasa yote yana hali za kuwa sehemu za Ufaransa na hivyo hutazamiwa kama sehemu za Umoja wa Ulaya. Wakazi ni raia wa Ufaransa wenye haki zote za kisiasa na kijamii. Visiwa hivi ni Guadeloupe, Martinique St Martin na Saint-Barth.

Marekani inatwala Puerto Rico na Visiwa vya Virgin vya Marekani kama maeneo maalum. Wakazi ni raia kamili ya Marekani.

Ufalme wa maungano (Uingereza) bado una maeneo ya ng'ambo nje ya nchi kwenye visiwa vya Karibi ambayo ni pamoja na:

Aruba, Curaçao, na Sint Maarten zote ni nchi za pekee ambazo bado huhesabiwa kama sehemu za "Ufalme wa Nchi za Chini" (Kingdom of the Netherlands), pamoja na Uholanzi yenyewe. Nchi hizo si sehemu za Umoja wa Ulaya. Raia wa visiwa hivi wana uraia kamili wa Uholanzi wako pia raia wa Umoja wa Ulaya.

Marejeo

hariri
  1. Boomert, Arie (2019). Early settlers of the insular Caribbean : dearchaizing the Archaic. Hofman, Corinne L., 1959-, Antczak, Andrzej T. Leiden. uk. 123. ISBN 978-90-8890-780-7. OCLC 1096240376.{{cite book}}: CS1 maint: location missing publisher (link)
  2. Boomert, Arie, 1946- (2016). The indigenous peoples of Trinidad and Tobago : from the first settlers until today. Leiden. uk. 15. ISBN 978-90-8890-354-0. OCLC 944910446.{{cite book}}: CS1 maint: location missing publisher (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: numeric names: authors list (link)
  3. Nägele, Kathrin; Posth, Cosimo; Iraeta Orbegozo, Miren; Chinique de Armas, Yadira; Hernández Godoy, Silvia Teresita; González Herrera, Ulises M.; Nieves-Colón, Maria A.; Sandoval-Velasco, Marcela; Mylopotamitaki, Dorothea (2020). "Genomic insights into the early peopling of the Caribbean". Science (kwa Kiingereza). 369 (6502): 456–460. doi:10.1126/science.aba8697. ISSN 0036-8075. PMID 32499399.
  4. Napolitano, Matthew F.; DiNapoli, Robert J.; Stone, Jessica H.; Levin, Maureece J.; Jew, Nicholas P.; Lane, Brian G.; O’Connor, John T.; Fitzpatrick, Scott M. (2019). "Reevaluating human colonization of the Caribbean using chronometric hygiene and Bayesian modeling". Science Advances. 5 (12): 2. doi:10.1126/sciadv.aar7806. ISSN 2375-2548. PMID 31976370.
  5. Boomert, Arie, 1946- author. (2016). The indigenous peoples of Trinidad and Tobago : b from the first settlers until today. uk. 45. ISBN 978-90-8890-354-0. OCLC 1087399693. {{cite book}}: |last= has generic name (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link) CS1 maint: numeric names: authors list (link)
  6. Tony Martin, Caribbean History: From Pre-colonial Origins to the Present (2011)
  7. "History". The government of the Cayman Islands. 2009. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-04-27. Iliwekwa mnamo 2009-05-07.
  8. "Dominican Republic 2014". Iliwekwa mnamo 24 Aprili 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  9. Haggerty, Richard A. (1989). "Haiti, A Country Study: French Settlement and Sovereignty". US Library of Congress. Iliwekwa mnamo 2009-03-30.
  10. "Aruba - History and Heritage". Smithsonian.com. Novemba 6, 2007. Iliwekwa mnamo 2009-05-07.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  11. King, Russell (2010). People on the Move: An Atlas of Migration. Berkeley, Los Angeles: University of California Press. ku. 24. ISBN 978-0-520-26151-8.
  12. Act Prohibiting Importation of Slaves on 2 March 1807
  13. Charles H. Wesley, "The Negro in the West Indies, slavery and freedom." Journal of Negro History (1932): 51-66. in JSTOR
  14. Hugh Tinker (1993). New System of Slavery. London: Hansib Publishing. ISBN 978-1-870518-18-5.
  15. "Forced Labour". The National Archives, Government of the United Kingdom. 2010.
  16. K. Laurence (1994). A Question of Labour: Indentured Immigration Into Trinidad & British Guiana, 1875–1917. St Martin's Press. ISBN 978-0-312-12172-3.
  17. "St. Lucia's Indian Arrival Day". Caribbean Repeating Islands. 2009. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-04-24. Iliwekwa mnamo 2021-03-10.
  18. "Indian indentured labourers". The National Archives, Government of the United Kingdom. 2010.
  19. Rogozinski (2000). A Brief History of the Caribbean. ku. 159–160.
  20. Rogozinski (2000). A Brief History of the Caribbean. ku. 161–3.

Viungo vya nje

hariri