Papa Paulo VI

(Elekezwa kutoka Pope Paul VI)

Papa Paulo VI (26 Septemba 18976 Agosti 1978) alikuwa Papa kuanzia tarehe 21/30 Juni 1963 hadi kifo chake[1]. Alitokea Concesio, Brescia, Italia[2].

Mtakatifu Paulo VI.

Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Giovanni Battista Enrico Antonio Maria Montini.

Alimfuata Papa Yohane XXIII akafuatwa na Papa Yohane Paulo I.

Alitangazwa na Papa Fransisko kuwa mwenye heri tarehe 19 Oktoba 2014 na mtakatifu tarehe 14 Oktoba 2018.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 29 Mei[3] au 30 Mei.

Alizaliwa Concesio, kijiji cha wilaya ya Brescia, katika mkoa wa Lombardia (Italia Kaskazini), ambapo familia ya Montini ilikuwa na nyumba ya kufanyia likizo.

Wazazi wake, wakili Giorgio Montini na Giuditta Alghisi, walifunga ndoa mwaka 1895 wakazaa watoto watatu: Ludovico, aliyepata kuwa mbunge, Giovanni Battista mwenyewe, na Francesco, daktari.

Papa huyo alipozaliwa, baba yake alikuwa mkurugenzi wa gazeti la Kikatoliki "Il Cittadino di Brescia", halafu akawa mbunge.

Malezi

hariri

Mwaka 1903 alianza masomo yake kwa Wajesuiti.

Mwaka 1907 alihiji Roma kwa mara ya kwanza pamoja na familia, ili kuonana na Papa Pius X, halafu akapewa sakramenti za ekaristi na Kipaimara.

Mwaka 1916 alimaliza sekondari akajiunga na seminari ya mji wake.

Upadrisho

hariri

Tarehe 29 Mei 1920 alipewa upadrisho katika kanisa kuu la Brescia. Mwaka uleule akahamia Roma ili kusoma Sheria na Falsafa kwa wakati mmoja.

Mwaka 1923 alianza kuelekea diplomasia na kushirikiana na Ofisi za Papa, kwa agizo la Papa Pius XI. Baada ya kutumwa Warsav (Juni-Oktoba 1923), mwaka 1924 alipata digrii tatu.

Ushirikiano na Pio XI na Pio XII

hariri

Baada ya kutimiza majukumu mengine, tarehe 13 Desemba 1937 alichaguliwa kuwa makamu wa Katibu wa Kanisa, Eugenio Pacelli, ambaye mwaka 1939 alichaguliwa kuwa Papa Pius XII.

Alimuunga mkono katika jitihada zake za kuzuia vita na kurudisha amani na za kuokoa uhai wa Wayahudi (huko Roma 4.000 waliokolewa na Kanisa kutoka mikono ya Wafashisti).

Baada ya vita vikuu vya pili alijitahidi kuepusha Italia na ukomunisti.

Tarehe 1 Novemba 1954, alichaguliwa kuchunga Jimbo kuu la Milano akapewa daraja ya uaskofu tarehe 12 Desemba.

Huko alifaulu kuinua hali ya jimbo katika kipindi kigumu sana.

Ukardinali

hariri

Baada ya kifo cha Pius XII, alichaguliwa badala yake, tarehe 28 Oktoba 1958, Papa Yohane XXIII, aliyemchagua kardinali wa kwanza kati ya wale aliowateua tarehe 15 Desemba 1958.

Chini ya Papa huyo, kardinali Montini alihusika sana na maandalizi ya Mtaguso wa pili wa Vatikano, hadi ulipofunguliwa tarehe 11 Oktoba 1962.

Mtaguso ulikatika tarehe 3 Juni 1963 kwa kifo cha Papa.

Mkutano wa makardinali ulichukua muda mfupi kumchagua Montini kuwa Papa, naye alijichagulia jina la Paulo VI, tarehe 21 Juni 1963.

Mbele ya mabadiliko ya harakaharaka ya ulimwengu, Paulo VI alishika msimamo wa kujadiliana na wote na kuelekeza mtaguso mkuu uendelee kwa msimamo huo.

Haikuwa rahisi kuimarisha Kanisa Katoliki katika mvutano uliojitokeza hasa baada ya mtaguso kati ya wasiokubali mabadiliko na waliotaka kubadili hata mambo ya msingi, lakini alifaulu kwa uvumilivu mkubwa.

Mtu mpole na wa aibu, mwenye elimu kubwa pamoja na maisha ya kiroho ya hali ya juu, alifungua kurasa mpya katika ekumeni, kama alipokubaliana na Patriarki Atenagora I wa Konstantinopoli kufuta hati za mwaka 1054 zilizotenganisha Wakatoliki na Waorthodoksi (1964).

Tarehe 14 Septemba 1965, alianzisha Sinodi ya Maaskofu na tarehe 8 Desemba 1965 alifunga rasmi mtaguso.

Safari

hariri

Paulo VI alikuwa Papa wa kwanza kusafiri kwa ndege akaenda mpaka nchi ya mbali, akiwa wa kwanza kwenda Israeli na kutembelea mabara yote.

Afya yake iliharibika haraka mwaka 1978 ambapo alifariki tarehe 6 Agosti saa 3:40 usiku huko Castel Gandolfo, akiacha wasia mzuri sana.

Heshima baada ya kifo

hariri

Kwa uamuzi wa Papa Yohane Paulo II, tarehe 11 Mei 1993, Kanisa la Roma lilifungua kesi ya kumtangaza mwenye heri na hatimaye mtakatifu.

Tarehe 20 Desemba 2012 Papa Benedikto XVI alipitisha uamuzi wa kukiri ushujaa wa maadili yote ya Paulo VI, ambaye hivyo alistahili kuitwa "venerabilis".

Baada ya kuthibitisha muujiza uliopatikana kwa maombezi yake, Papa Fransisko alimtangaza mwenye heri tarehe 19 Oktoba 2014 na baada ya muujiza wa pili alimtangaza mtakatifu tarehe 14 Oktoba 2018.

Maandishi yake

hariri

Mbali ya hati za mtaguso mkuu, Paulo VI alitoa nyaraka kuu saba:

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu Papa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Papa Paulo VI kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.