Upambanuzi wa roho
Upambanuzi wa roho ni istilahi ya Kikristo inayotumiwa na madhehebu mengi kuhusu kazi ya kutofautisha roho, yaani misukumo mbalimbali inayojitokeza katika maisha ya mtu kumuelekeza kutenda mema (Mungu na malaika wake) au mabaya (shetani na ubinadamu).
Wote wanahitaji kufanya kazi hiyo kwa makini ili wasipotoke, ingawa kuna watu wenye karama maalumu kwa ajili hiyo (taz. 1Kor 12:10). Hivyo neno “upambanuzi wa roho” linaweza kumaanisha karama mojawapo kati ya zile alizoziongelea Mtume Paulo, inayotuwezesha kutambua mara k.mf. mtu akisema au kutenda kwa upendo halisi au kwa unafiki. Lakini linaweza pia kumaanisha upambanuzi unaotokana na busara ya Kikristo ikisaidiwa kutoka juu na kipaji cha shauri na neema anazojaliwa kiongozi anayewajibika.
Katika teolojia ya Kikatoliki
haririUsikivu kwa Roho Mtakatifu unadai tupambanue uvuvio wake na roho nyingine mbili ambazo kwanza zinaweza zikaonekana nzuri, kumbe zinaua.
Kwa neno “roho” tunamaanisha elekeo la kupima, kutaka na kutenda namna fulani. Hasa tunatofautisha roho tatu: ile ya Mungu; ile ya kibinadamu tu inayotegemea umbile lililoharibika, ambalo mivuto yake, utamu wake na juhudi zake za muda vinaweza kudanganya; hatimaye ile ya Ibilisi anayeona faida kufichama na kujifanya ni malaika wa mwanga. “Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetoka kwa Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1Yoh 4:1).
Kwa kawaida kila mtu anatawaliwa na roho mojawapo kati ya hizo. Waovu wanatawaliwa na shetani; watu vuguvugu wanatawaliwa na roho ya kibinadamu tu; walioanza kushika kwa bidii maisha ya Kiroho wanatawaliwa na Roho wa Mungu, lakini mara nyingi roho ya kibinadamu na ya shetani zinajiingiza, hivyo hatutakiwi kamwe kumpima mtu kwa kuzingatia matendo yake machache, bali jumla ya maisha. Hata waliokamilika Mungu anaacha wabaki na kasoro kadhaa (pengine zinaonekana tu kuwa hivyo) kusudi awatunze katika unyenyekevu na kuwapa nafasi nyingi za kutimiza maadili yanayopingana nazo. Kwa mfano, kuna watu walioendelea katika njia ya Mungu ambao kwa ugonjwa maalumu wanaelekea kukasirika; kumbe chini ya kutovumilia kwao kwa nje zinaweza kufichika subira na stahili kubwa. Basi, ni muhimu kupambanua vizuri roho ipi inatusukuma.
Kipimo kikuu kwa upambanuzi wa roho kilitolewa na Yesu: “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri” (Math 7:15-18).
Wenye nia mbaya hawawezi kuificha muda mrefu; itaonekana kwa namna mbalimbali: kwanza katika matendo ya dharura yasiyoacha nafasi ya kupanga udanganyifu; halafu katika tabu: “kuna rafiki wakati wa kufaa, ambaye yeye hatadumu wakati wa msiba wako” (YbS 6:8). Hivyo watu wanajionyesha walivyo wasipoweza kupata wanachotamani au kisha kukipata: k.mf. wanaofikia utawala wanakuja kujitokeza walivyo kweli.
Ikiwa undani wa utashi wetu ni mwema utazaa matunda mema. Wengine watatambua mapema kama tunasikiliza neno la Mungu ili kulitekeleza. Lakini hatutazaa chochote tukiridhika kumuita, “Bwana, Bwana!” tusitimize matakwa yake.
Tunaweza kutambua roho inayotusukuma kwa kuangalia matokeo yake na kuilinganisha na maadili ya Kikristo: upande mmoja unyenyekevu na kujikana, upande mwingine maadili ya Kimungu.
Dalili ya roho ya kibinadamu tu
haririKutokana na dhambi asili umbile letu ni adui wa ufishaji na wa unyenyekevu: linajifanya lengo la yote na kupuuzia kimatendo maadili ya Kimungu. Hata katika sala linajitafutia faraja na kutumbukia ulafi wa roho; matatizo (au ukavu) yakianza, linaacha maisha ya Kiroho, likijisingizia eti! Busara inataka tusizidishe ugumu wa maisha na urefu wa sala (likimaanisha kutafakari kidogo kila siku). Kwa kisingizio cha utume linajiridhisha na utendaji, likizidi kujimwaga nje na kuchanganya upendo wa Kikristo na wema wa kiutu tu; yakizuka mapingamizi na majaribu, linanung’unikia msalaba na kukasirika hata kukata tamaa. Juhudi zake ni kama moto wa nyasi: hazijali utukufu wa Mungu wala wokovu wa watu. Roho ya kibinadamu tu inajumlishwa katika neno moja: umimi.
Roho hiyo imechorwa hivi, “Mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1Kor 2:14). Anapima yote kwa mtazamo wa binafsi, si wa Mungu. Polepole anapotewa na roho ya imani, tumaini na upendo; anataka kujitegemea ingawa ni udhaifu wenyewe. Ila pengine ukubwa wa uovu wake unamkumbusha neno la Yesu: “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5).
Dalili za roho ya Ibilisi
haririShetani kwanza anatuinua kwa kututia kiburi, halafu anatubwaga katika kuhangaika, kuvunjika moyo hata kukata tamaa. Si kila mara anatusogeza mbali na malipizi; hasa katika mazingira yanayoyaheshimu anayahimiza yale ya nje, ili adumishe kiburi na kuharibu afya. Kumbe hahimizi ufishaji wa ndani (wa ubunifu, moyo, matakwa na maoni yetu) ingawa pengine kwa udanganyifu anatufanya tufadhaikie mambo madogo tusijali mazito wala ya hatari. Anatufanya tujithamini mno, tujipendelee, tujivune na kusali kama Farisayo hekaluni bila kujitambua. Mara nyingi kiburi hicho kinaendana na unyenyekevu bandia ambao tunajisema katika mambo kadhaa tusije tukasemwa juu ya mengine makubwa zaidi. Piu anatufanya tuchanganye unyenyekevu na hofu ya kushindwa na kudharauliwa.
Badala ya kulisha imani kwa kuzingatia Injili, anatuvuta pengine tufuate mambo ya pekee na ya ajabu yanayoweza kutokeza vipawa vyao; pengine tufikirie yasiyohusiana na wito wetu, kama vile mmisionari kuwaza ajifanye mkaapweke, na Mkartusi ajifanye mtangazaji wa Injili; pengine tena tufuate vitabu vya kisasa na kukanusha yapitayo maumbile.
Upande wa tumaini anatuchochea tujiamini kipumbavu, na kutaka utakatifu mara, bila kupitia hatua za lazima wala kujikana. Tukitenda dhambi anatufanya tusijivumilie bali tujikasirikie badala ya kutubu kweli.
Anastawisha umimi wetu, akiupotosha upendo kulingana na tabia na hali yetu, uwe ni upole usiopinga maovu yoyote au, kinyume chake, ari chungu ambayo inakaripia wengine badala ya kujirekebisha, inasababisha kinyongo na mafarakano badala ya amani, hata watu wakaogopa kutupinga, wakijua hatutavumilia.
Hatimaye tukija kutenda kosa tusiloweza kulificha, tunatumbukia fadhaa, hasira na kukata tamaa, ambapo shetani anatudanganya tena kwa kuzidisha ugumu wa kumrudia Mungu kama alivyotudanganya kwanza kwa kuficha hatari. Anatuunda kwa mfano wake ambaye alijiinua kwa kiburi akakata tamaa moja kwa moja. Basi, tuwe macho tukijikuta tunaguswa upande wa hisi wakati wa ibada, lakini ikimalizika tunajipendea zaidi na kukosa unyofu kwa viongozi wetu. Utovu wa unyenyekevu na wa utiifu ni dalili ya hakika ya kwamba hatuongozwi na Mungu.
Dalili za roho ya Mungu
haririTofauti na roho mbili tulizozieleza, Roho Mtakatifu anatuelekeza kujifisha upande wa mwili lakini kwa kiasi na utiifu, bila kujionyesha wala kuharibu afya. Pia anatutambulisha kuwa ufishaji huo si kitu pasipo ule wa moyo, matakwa na maoni yetu. Anatutia unyenyekevu halisi unaotuzuia tusijipendee, tusiogope kudharauliwa, tusitangaze fadhili tulizojaliwa wala kuzikanusha, tukimtukuza Mungu tu kwa hizo.
Anatuelekeza kulisha imani yetu kwa maneno sahili na ya dhati ya Injili, kwa kushika kiaminifu mapokeo na kukwepa uzushi. Anatuonyesha Bwana ndani ya viongozi, jambo ambalo linastawisha imani.
Anachochea tumaini tusijiamini kipumbavu wala kujali mno mafanikio ya kibinadamu. Anatutamanisha maji hai ya sala, akitukumbusha haja ya kuyafikia hatua kwa hatua kwenye njia ya unyenyekevu, kujikana na msalaba.
Anazidi kuwasha upendo kwa ari ya kumtukuza Mungu na kujisahau. Anaelekeza kumfikiria kabla ya yote na kumuachia atushughulikie. Anachochea upendo kwa jirani akitukumbusha kuwa ndiyo ishara kuu ya upendo kwa Mungu, na kutuzuia tusihukumu wala kukwazika bila sababu. Anatia ari pole inayojenga kwa sala na mifano mizuri, badala ya kuchukiza kwa maonyo yasiyofaa. Katika majaribu anatia uvumilivu, upendo kwa msalaba na kwa adui, amani ndani mwetu tena na wengine, na hata furaha ya rohoni. Tukija kuanguka kwa dharura anatukumbusha huruma ya Mungu. “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi” (Gal 5:22) pamoja na utiifu na unyenyekevu.
Kuhusu tendo maalumu, ni dalili ya kutembelewa na Mungu ikiwa hakuna sababu ya kimaumbile iliyoleta faraja ya dhati tunayojisikia ghafla. Ila tutofautishe dakika hiyo ya kwanza na zile zinazofuata ambapo mara nyingi tunawaza wenyewe pasipo uvuvio wa Mungu, na hivi tunaweza tukadanganyika.
Kwa nadra tu Roho Mtakatifu anajalia mafunuo (neema za pekee ambazo kuzitamani ni kujiamini kipumbavu), ila mara nyingi anawaangazia wenye juhudi neno la Injili. Hapo wafanye kama msanii anayefuata kipawa chake kuliko kufikiria kanuni za sanaa, akizitimiza kwa namna bora kutokana na kipawa chenyewe. Ndipo yanapokuja kupatana unyenyekevu na ari, upole na msimamo, unyofu wa njiwa na busara ya nyoka. Ndivyo Roho Mtakatifu anavyoongoza watu waaminifu hadi bandari ya milele.
Viungo vya nje
hariri- Catholic Encyclopedia "Discernment of Spirits"
- Rules for the Discerning of Spirits: A Brief Summary of the Church's Traditional Teaching
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Upambanuzi wa roho kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |