Bruno Gutmann (* 4. Julai 1876 huko Dresden; † 17. Desemba 1966 huko Ehingen am Hesselberg, yote Ujerumani) alikuwa mmisionari wa Kilutheri kwa niaba ya Misioni ya Leipzig katika Afrika Mashariki ya Ujerumani na Tanganyika (leo Tanzania bara) na mtafiti wa kitaalamu wa utamaduni wa Wachagga.

Asili yake hariri

Bruno Gutmann alizaliwa 1876, miaka michache baada ya maungano ya Ujerumani ya mwaka 1871. Baba yake alikuwa mtoto wa mkulima mdogo, aliyewahi kununua nyumba alipowekeza mali yake yote kwa tumaini la kupata faida lakini katika hali ngumu ya uchumi iliyofuata mradi wake uliporomoka[1]. Utoto wa Bruno ulikuwa maisha ya umaskini; mama yake alikuwa mgonjwa baada ya kumzaa mtoto wa pili. Wakati ule wazazi wa mamaye walihamia nyumba ya Gutmann ili wamsaidie mwanao: ndio hao waliomlea Bruno. Mama yake Bruno alifariki dunia mwaka 1883. Baba na dada yake waliondoka katika nyumba wakaishi kwa ndugu wengine.

Kwenye shule ya msingi alikuwa mwanafunzi bora. Alipofikia umri wa miaka 11 alipaswa kuanza kazi katika kiwanda kila alasiri baada ya shule ili achangie gharama ya maisha. Baada ya miaka miwili alifaulu kupata ajira ya ukarani kwa nusu siku kutokana na mwandiko wake mzuri. Hakuweza kuendelea kusoma sekondari baada ya darasa la nane kwa sababu ya karo. Alimaliza shule ya msingi na kupokea Kipaimara alipokuwa na miaka 15 akaendelea na kazi ya ukarani. Alijiunga pia na klabu ya YMCA na jumuiya hiyo ya vijana Wakristo ilimshawishi kutafuta maisha ya mmisionari.

Mafunzo ya umisionari hariri

Baada ya kutimiza umri wa miaka 18, Bruno alikubaliwa katika seminari ya Misioni ya Kilutheri huko Leipzig. Kunzia mwaka 1895 alifuata kozi ya kumpa elimu ya sekondari, elimu ya lugha ya Kilatini na lugha asilia za Biblia (Kigiriki na Kiebrania) na mafunzo ya theolojia ya Kiprotestanti. Kwenye seminari aliteuliwa kwenda Uhindi, hivyo alijifunza pia Kiingereza, Kisanskrit na Kitamili. Gutmann alisoma pia kozi kadhaa kwenye Chuo Kikuu cha Leipzig alipojiunga na kozi za saikolojia ya kijamii na historia. Mwaka 1901 alimaliza masomo ya theolojia akabarikiwa kuwa mchungaji akatumwa kwa mwaka mmoja kuhudumia kanisa katika kijiji kidogo ili apate uzoefu wa kazi hiyo kabla ya kuondoka Ujerumani.

Aliporudi Leipzig mwelekeo wake ulibadilishwa; Bruno alikubali kubadilishana nafasi na mwanafunzi mwenzake aliyetakiwa kwenda Kilimanjaro lakini aliogopa afya ya mke wake itakuwa hatarini kwenye mazingira magumu. Gutmann hivyo alipewa wiki chache kusoma misingi ya Kiswahili.

Hatua za kwanza katika Afrika hariri

Mwaka 1902 alipanda meli pamoja na wenzake wawili. Baada ya kufika Mombasa walitembea hadi kituo cha misheni huko Mamba, karibu na Machame kwenye mitelemko ya mlima Kilimanjaro.

Miaka 1902 hadi 1904 Bruno alikuwa msaidizi wa mmisionari mzee Gerhard Althaus pale Mamba. Kazi yake ilikuwa hasa kujifunza lugha ya Kichagga na kufundisha pia katika shule ya misioni. Wakati wa kujifunza lugha alianza tayari kukusanya hadithi na masimulizi ya Wachagga. Mwaka 1904 alihamia Machame ambako alifanya kazi chini ya wamisionari Jessen na Müller.

Alipotimia umri wa miaka 30 alipewa nafasi ya kuongoza kituo chake mwenyewe akatumwa Masama. Alihusika na ujenzi wa nyumba, kanisa na shule pamoja na kufundisha na kuendesha ibada. Mnamo 1908 alipaswa kuomba likizo kwa sababu za kiafya akarudi Ujerumani.

Wakati wa likizo alihariri maandiko yake na kutoa kitabu chake cha kwanza kuhusu "Fikra na Ushairi wa Wachagga" [2] na kuoa. Mnamo 1909 akarudi Afrika.

Moshi hariri

Baada ya kurudi Afrika, Gutmann alipewa kituo cha Old Moshi kilichokuwa kimoja kati ya vituo vya kwanza vya Misioni ya Leipzig kwenye Kilimanjaro. Hapo alikuta usharika mkubwa ulioendelea kukua. Huko Moshi Gutmann aliendelea kukusanya habari za utamaduni wa Wachagga. Katika imani yake alitambua Wachagga kama "taifa" lililoumbwa na Mungu akiona changamoto ya misioni kuunda "kanisa la kitaifa" linalolingana na tabia za pekee za taifa hilo. Hivyo aliona ni wito wake wa kidini kuhifadhi urithi wa utamaduni wa Uchagga katika kanisa la Wachagga. Aliamini kwamba binadamu aliumbwa na Mungu katika taratibu za ukoo, ujirani na kizazi au kundi la umri. Akiwa Mkristo Mlutheri aliamini kwamba utaratibu huo wa asili umevurugiwa kote duniani kutokana na dhambi, lakini aliona pia kwamba Wachagga walikuwa karibu zaidi na huo utaratibu wa uumbaji kuliko sehemu kubwa ya jamii ya Ujerumani alikotoka. Kwa msingi huo alikubali utaratibu wa rika wa Wachagga, aliona umuhimu kutovunja desturi ya unyago bali kuiendeleza katika kipaimara ya vijana. Athira za uchumi wa kikoloni aliona kama hatari kwa maisha ya jamii ya kimila aliyopenda.

Mwaka 1916 wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Moshi ilivamiwa na jeshi la Uingereza; wamisionari Wajerumani waliruhusiwa kuendelea na kazi yao hadi mwaka 1920, ambako Wajerumani wote walifukuzwa na kurudishwa kwao.

Gutmann katika Ujerumani 1920-1925 hariri

Gutmann alitumia muda alipokaa Ujerumani kupitia karatasi na kumbukumbu zake akaanza kutoa vitabu vingi kuhusu Wachagga. Kitabu chake kuhusu "Sheria za Wachagga" kilichapishwa hadi 1926; Gutmann alipewa baadaye na Chuo Kikuu cha Würzburg shahada ya uzamivu ya heshima (Dr. h.c.) katika sheria. Alieleza hitimisho ya msimamo kuhusu misioni katika kitabu "Kujenga kanisa kwenye msingi wa injili" (Gemeindeaufbau aus dem Evangelium) kilichompatia uzamivu wa heshima katika theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Erlangen.

Mwaka 1924 alitumwa Uingereza alipohudhuria kongamano la kimataifa kuhusu "elimu katika Afrika" ambako wawakilishi wa mashirika ya misioni walijadili masuala ya elimu ya shule zao.

Awamu ya tatu katika Afrika hariri

Mwaka 1926 Gutmann aliweza kurudi Moshi aliendelea kuhudumia kanisa la Kilutheri pale Old-Moshi. Katika miaka iliyofuata alitoa vitabu vitatu kuhusu "Mafundisho ya Kabila" (Stammeslehren) alivyotunga pamoja na walimu wazawa Mlasany Njau na Warikoi Masamu waliokusanya mafundisho mengi ya unyago wa kimila.

Kuanzia 1926 hadi 1930 alifanya kazi tena huko Old-Moshi. Baada ya likizo fupi huko Ujerumani mnamo 1930/1931, alikuwa tena huko Old-Moshi kutoka 1931 hadi 1938.

Alipokwenda tena Ujerumani kwa likizo kwenye mwaka 1938, Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilianza ikazuia kurudi kwake. Hadi mwaka 1950 haikuwezakana kupata tena kibali kutoka Uingereza kwa Wamisionari Wajerumani. Baadaye afya na umri havikumruhusu kusafiri tena. Aliiishi katika Bavaria alipotembelewa mara kwa mara na Wachagga waliokuwa na safari za Ulaya. Mwaka 1963 ushirika wake wa zamani wa Old Moshi uliamua kumpa cheo cha heshima "Wasahuye o Wachagga" (Babu wa Wachagga).

Bruno Gutmann aliaga dunia kwake Ehingen, Bavaria mnamo 17 Desemba 1966, akiwa na umri wa miaka 90.

Maandiko yake (kadhaa) hariri

Sehemu kubwa ya maandiko ya Gutmann hayajatafsiriwa, yanapatikana kwa Kijerumani pekee.

  • Dichten und Denken der Dschagganeger". Beiträge zur ostafrikanischen Volkskunde. Publishing house of Evangelical Lutheran Mission, Leipzig 1909.
  • Briefe aus Afrika. Publishing house of Evangelical Lutheran Mission, 3rd edition, Leipzig 1925.
  • Gemeindeaufbau aus dem Evangelium: Grundsätzliches für Mission und Heimatkirche, Publishing house of Evangelical Lutheran Mission, 1925
  • Das Recht der Dschagga. Beck publishers, München 1926.
  • Die Stammeslehren der Dschagga. 3 volumes: Beck publishers, München. Vol.1 1932, Vol 2 1935, Vol. 3 1938.
  • Afrkaner - Europäer in nächstenschaftlicher Entsprechung. (collected essays by Bruno Gutmann). On the occasion of his 90th birthday, edited by Ernst Jaeschke. Bibliography of Bruno Gutmann und literature list pp215–231. Evangelisches Verlags-Werk 1966.

Marejeo hariri

  1. Sehemu hii inafuata habari kutoka Winter, J.C.: Bruno Gutmann, 1876-1966 : a German approach to social anthropology, Clarendon Press Oxford & New York 1979, kurasa 30 ff
  2. "Dichten und Denken der Dschagganeger"
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.