Historia ya Afrika ni historia[1] ya bara hilo lililo asili ya binadamu wote.

Mataifa ya Afrika kabla ya ukoloni kutoka nyakati tofauti
Mataifa ya Afrika kabla ya ukoloni.
Ramani ya sasa ya kisiasa ya Afrika (ikijumuisha kusini mwa Sahara na Afrika kaskazini).
Ramani ya kisiasa ya Afrika nzima leo.

Kwa ujumla, historia ni kumbukumbu ya maisha ya mwanadamu duniani, hasa ile tarehe iliyosajiliwa na kuhifadhiwa katika vitabu, maandishi mbalimbali, na simulizi au hekaya za mapokeo. Ingawa historia iliyobebwa katika simulizi na hekaya huchukuliwa na baadhi kuwa haina nguvu kwa kukosa ithbati ya maandishi, bado hivi ni vyanzo muhimu vya historia. Mara nyingi historia iliyoko katika maandishi huwa imehifadhiwa katika simulizi na hekaya kwa muda mrefu kabla ya kuandikwa.

Historia ya Afrika

Hapo kale, bara la Afrika lilishuhudia matukio mengi ya harakati za mwanadamu kuliko mabara mengine ya ulimwengu.

Wataalamu wa athari wamegundua athari za zamadamu zinazorudi nyuma kufikia hadi miaka milioni minne, na athari za ustaarabu wa Wamisri wa Kale huko Misri na Wafoinike huko Tunis na sehemu nyinginezo za Afrika ya Kaskazini katika karne ya 9 KK.

Harakati za madola makubwa ya Warumi na Waarabu ziliweza kuonekana kabla ya karne ya 4 BK, na Waarabu walianza kuingia Afrika huko Habasha (Ethiopia) tangu karne ya 7 BK na kutangaza dini ya Uislamu na kuieneza katika maeneo mbalimbali ya Afrika pamoja na kuanzisha biashara na ustaarabu na kuimarisha mamlaka zao katika Sudan ya wakati huo tangu karne ya 8 baada ya Kikristo.

Himaya za Ghana, Mali, na Songhai zilikuwa zikijulikana kwa utajiri mkubwa na biashara stawi iliyokuwa ikifanyika wakati huo ya dhahabu na bidhaa nyinginezo. Mwisho wa karne ya 15 BK, himaya ya Songhai ilikuwa na nguvu kuweza kuitia chini ya utawala wake mamlaka ya Mali. Sehemu nyingine za kusini mwa Afrika zilikuwa wakati huu hazijulikani sana, na historia yake ilikuwa bado haijasajiliwa.

Baina ya karne ya 1 KK na karne ya 16 BK watu waliokuwa wakizungumza lugha ya Kibantu watokao sehemu za Nigeria na Cameroon ya leo, ndio waliokuwa wameenea kwenye sehemu mbalimbali kusini mwa bara la Afrika, wakiwa wameanzisha vijiji, mashamba na mamlaka katika sehemu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo, za Luba na Mwememutapa, lakini makundi ya wachungaji wa wanyama walianza kuhamia kusini katika karne za 15 na 16 na kukutana na Wabantu. Ndipo walipoanzisha mamlaka zao za Bunyoro, Buganda, Rwanda na Ankole.

Ukoloni

 
Afrika mnamo mwaka 1880, kabla ya ugawaji na wakoloni; Milki za wenyeji na maeneo yaliyokuwa chini ya nchi za nje
 
Afrika jinsi ilivyogawiwa na wakoloni mnamo mwaka 1913 (kabla ya Vita Kuu I)

Wazungu walianza kugundua bara la Afrika katika karne ya 15, wakati Wareno walipokuja kwenye fukwe za bara la Afrika kutafuta njia nyepesi na ya amani ya kufikia India, na kuweza kupata nafasi ya kushikilia biashara ya dhahabu na pembe na watumwa ambayo ilikuwa ikiendelea wakati huo katika bara la Afrika. Katika mwaka 1488 Bartolomeo Dias alizunguka Rasi ya Tumaini Jema (kwa Kiingereza: Cape of Good Hope), na katika mwaka 1498 Vasco da Gama alifika ufukwe wa Afrika Mashariki na kuendelea mpaka India.

Baada ya hapo, Ureno ulianzisha vituo vya biashara Afrika, ukifuatiwa na Waholanzi, Waingereza, Wafaransa na Wazungu wengineo, na biashara ya watumwa iliyosimamiwa na Waarabu na baadhi ya Waafrika wenyewe ikashika kani na kuwa na kasi na nguvu.

Wakati huohuo Waturuki walishikilia sehemu za kaskazini ya Afrika na Waomani wakashikilia ufukwe wa Afrika Mashariki.

Kati ya miaka 1880 na 1912, Wazungu waligawana bara la Afrika, na nchi zote zikawa chini ya utawala wa Wazungu isipokuwa Liberia na Ethiopia.

Wafaransa wakachukuwa Afrika Magharibi na Kaskazini na kwa hivyo nchi za Afrika Magharibi: Dahomey (sasa Benin), Guinea, Mali, Cote d'Ivoire, Mauritania, Niger, Senegal na Volta ya Juu (sasa Burkina Faso) zilikuwa chini ya utawala wake. Hali kadhalika, Algeria, Tunisia na Morocco zilitawaliwa na wao. Aidha, Wafaransa walitawala Togoland, Somaliland, Madagascar, Comoro, na Reunion.

Waingereza nao wakatawala Afrika Mashariki na Kusini, na kuwa sehemu ya Sudan na Somalia, Uganda, Kenya, Tanzania (chini ya jina la Tanganyika), Zanzibar, Nyasaland, Rhodesia, Bechuanaland, Basutoland na Swaziland chini ya utawala wao na baada ya kushinda katika vita huko Afrika ya Kusini walitawala Transvaal, Orange Free State, Cape Colony na Natal, na huko Afrika ya Magharibi walitawala Gambia, Sierra Leone, the Gold Coast na Nigeria.

Wareno wakachukuwa sehemu ya Guinea, Angola na Msumbiji na sehemu na visiwa fulanifulani huko Afrika ya Magharibi.

Wabelgiji wakachukua Kongo na Rwanda-Urundi, na Wahispania wakachukua sehemu ya Guinea, Spanish Sahara (sasa Sahara ya Magharibi), Ifni na sehemu nyingine za Morocco.

Wajerumani nao wakachukua Togoland, Cameroon na baadhi ya nchi katika Afrika ya Magharibi na Afrika ya Mashariki, lakini baada ya vita vya kwanza vya dunia wakanyang'anywa.

Waitalia wakachukua Libya, Eritrea na sehemu kubwa ya Somalia.

Uhuru

Nchi ya kwanza kujitawala upya katika Afrika ni nchi za Afrika ya Kusini zilizojiunga na kujiendesha wao wenyewe katika mwaka 1910. Misri, katika mwaka wa 1922 walikuwa wanajiendesha wenyewe, na Tangier katika mwaka wa 1925.

Madola mengi ya Afrika yalianza kupigania uhuru katika miaka ya baina ya 1950 na 1960, na Wazungu wakasalimu amri na kuanza kutoa uhuru. Libya wakajinyakulia uhuru katika mwaka wa 1951, Eritrea katika mwaka 1952 ikiwa imejiunga na Ethiopia, Morocco katika mwaka wa 1956, na wakarudishiwa Tangier.

Katika mwaka huu wa 1956, Sudan na Tunisia vile vile walipata uhuru wao, na Ghana katika mwaka wa 1957, Guinea katika mwaka wa 1958, na vile vile Morocco wakarudishiwa Spanish Morocco.

Katika mwaka wa 1960 Ufaransa ukatoa uhuru kwa Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Congo (Brazzaville), Cote d'Ivoire, Dahomey (Benin), Gabon, Madagascar, Mali, Mauritania, Niger, Senegal na Volta ya Juu (Burkina Faso).

Vile vile, katika mwaka huohuo wa 1960 Congo (Kinshasa), Nigeria, Somalia, na Togo zikapata uhuru, na katika mwaka wa 1961 Sierra Leone na Tanganyika zikapata uhuru, na Afrika ya Kusini ikawa Jamhuri.

Katika mwaka wa 1962 Algeria, Burundi, Rwanda, na Uganda zikawa huru, na 1963 zikafuatia Zanzibar, Gambia na Kenya, na katika mwaka wa 1964 Malawi (Nyasaland), na Zambia (Rhodesia ya Kaskazini) zikapata uhuru.

Baada ya miaka miwili, katika mwaka wa 1966 Botswana (Bechuanaland) na Lesotho (Basutoland) zikajinyakulia uhuru. Mauritius na Swaziland katika mwaka wa 1968 na vile vile Guinea ya Ikweta. Hispania ikairudisha Ifni katika mwaka wa 1969 katika mamlaka ya Morocco.

Aidha, katika mwaka wa 1974 Guinea ya Kireno (Guinea-Bissau) ikapata uhuru wake, na katika mwaka wa 1975 Angola, Cape Verde, Mozambique, Sao Tome na Principe zikapata uhuru. Hispania vilevile ikaitoa Sahara ya Magharibi kwa Morocco na Mauritania katika mwaka wa 1976, lakini wananchi wakakataa kuwa chini ya nchi mbili hizi, kukazuka vita. Mauritania ukaitoa sehemu yake na kuipa Morocco katika mwaka wa 1979, tatizo ambalo mpaka sasa linaendelea baina ya Morocco na Sahara ya Magharibi, na Umoja wa Mataifa unajaribu kutatua tatizo hili. Waingereza wakawapa uhuru Shelisheli katika mwaka wa 1976, na Ufaransa ukatoa uhuru kwa visiwa vya Ngazija (Comoro).

Katika mwaka wa 1977 Jibuti (Nchi ya Afars na Issas) iliyokuwa ikitawaliwa na Wafaransa ikarudi kwa wenyewe. Rhodesia (Zimbabwe) ikapata uhuru halisi mwaka wa 1980, na South West Africa, iliyokuwa ikitawaliwa na Afrika ya Kusini ikapata uhuru katika mwaka 1990 na kuitwa Namibia.

Uingereza umebaki na visiwa vya Saint Helena na Ascension, na Ufaransa unaendelea kutawala Mayotte na Reunion. Hispania vilevile unaendelea kutawala visiwa vya Canarias pamoja na Ceuta na Melilla na visiwa viwili vingine vilivyoko karibu na Morocco.

Angalia pia

Tanbihi

  1. Wakati mwingine neno "tarehe" latumiwa badala ya historia, kutokana na maana asilia ya neno la Kiarabu "tarih"

Marejeo

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Afrika kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.