Historia ya Utawa

(Elekezwa kutoka Historia ya utawa)
Hii ni sehemu ya mfululizo kuhusu
Kanisa Katoliki
Imani

Umoja wa Mungu
Utatu (Baba, Mwana, Roho Mtakatifu)
Umwilisho Maisha ya Yesu
Msalaba Ufufuko Kupaa
Historia ya Wokovu Ufunuo
Biblia Mapokeo Ualimu Dogma
Neema Dhambi Wokovu Sakramenti
Watakatifu Bikira Maria

Muundo

Papa: Fransisko
Urika wa maaskofu Mitaguso mikuu
Kundi la Makardinali
Kanisa la Kilatini
Makanisa Katoliki ya Mashariki

Historia

Historia Ukristo
Ukatoliki Mlolongo wa Kitume
Sifa nne za Kanisa Utetezi Ekumeni
Maisha ya kiroho Amri Kumi Utawa
Sala Falsafa Teolojia
Muziki Sanaa Sayansi

Ibada

Liturujia Mwaka wa Kanisa
Ekaristi Liturujia ya Vipindi

Mapokeo ya liturujia

Liturujia ya Kilatini (Roma Liturujia ya Trento Milano Toledo Braga Lyon Canterbury)
Liturujia ya Armenia Liturujia ya Misri
Liturujia ya Ugiriki Liturujia ya Antiokia
Liturujia ya Mesopotamia

Hatuwezi kuelewa utawa tukidhani ni kitu kimoja: jina hilo linajumlisha maisha tofautitofauti.

Katika makala hii tunataka kufuata historia ya maisha haya katika Ukristo kama kitabu bora kilichoandikwa na Mungu siku kwa siku kadiri ya mpango wake wa hekima kwa ujenzi wa Kanisa lake takatifu kwa karama za kumshuhudia Yesu katika sifa na kazi zake mbalimbali.

Kuna hatua kuu nne zilipozaliwa aina mpya za utawa (hasa magharibi) bila ya kufuta zile zilizotangulia:

Mwanzo: ubikira na juhudi nyumbani hariri

Kufuatana na mifano ya Yesu Kristo na Bikira Maria, Agano Jipya linatoa habari za wanaume na wanawake waliojinyima ndoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, kama vile mabinti wanne wa Filipo mwinjilisti waliokuwa mabikira na manabii (Mdo 21:9). Hasa mtume Paulo aliwahimiza Wakristo wowote wanaoweza wafanye hivyo kama alivyofanya mwenyewe kwa kufuata shauri la Bwana (taz. 1Kor 7:25-34).

Mababu wa Kanisa kuanzia karne I waliandika juu ya wanaume waseja wanaozungukazunguka ili kuhubiri, na juu ya mabikira ambao utakatifu wao unaonyesha Ukristo ulivyo bora kuliko ulimwengu wa anasa unaoliudhi Kanisa.

Nje ya Dola la Kirumi (Mesopotamia na Persia) useja ulitazamwa kama agano na Kristo la kuwafaa wote.

Polepole mabikira walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na askofu na kukusanywa katika jumuia. Ilitokea vilevile kwa wanaume wa toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika ufukara fulani wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku, kuimba Zaburi na kusali kwa moyo.

Umonaki na kukimbia ulimwengu hariri

 
Mt. Anthony Mkuu, anayetazamwa kuwa baba wa umonaki wa Kikristo

Tofauti na hao walioishi katika mazingira ya kawaida, mwishoni mwa karne III huko Misri ulianza mtindo wa kukimbia ulimwengu hata kimakao.

Mmonaki (kutoka neno la Kigiriki monos = mmoja) alitafuta upweke kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu, ili moyo uweze kutulia kabisa bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida. Miundo mipya ya umonaki ilitegemea matatu: mwanzilishi, kanuni, upweke.

Mtindo huo wa maisha, ambao ndio mchango mkuu wa Afrika kwa Kanisa lote, ulistawi hasa baada ya Dola la Kirumi kuruhusu Ukristo (313). Maisha hayo magumu, yaliyoenea mapema hata nje ya Dola hilo, yaliamsha waamini wafuate Injili kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ulipohitajika ujasiri mbele ya hatari ya kuuawa. Hivyo umonaki ulionekana aina mpya ya kifodini kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote.

Anayeheshimiwa kama baba wa wamonaki ni Antoni abati (251-356) ambaye akizingatia maneno mbalimbali ya Injili aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa amfuate Mwokozi. Maisha yake yote akazidi kujitafutia mahali pa upweke kamili zaidi ili kumlenga Mungu tu.

Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi toka sehemu mbalimbali aliowaongoza bila ya kuacha upweke wake, isipokuwa kwa kutetea imani sahihi na umoja wa Kanisa. Mara baada ya kifo chake kitabu kilichoandikwa na Atanasi (295-373) juu yake kikaeneza mvuto wa umonaki hadi magharibi.

Maisha ya pamoja mashariki hariri

Muda mfupi baadaye, na sehemu ileile, yalianzishwa maisha ya pamoja ambamo mali na vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata kwa waamini wa ulimwenguni.

Pakomi (288-346) aliongokea imani kwa kuzingatia Wakristo walivyowatumikia wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo ya awali yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo yakaathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika umonaki akajisikia wito wa kuishi kwa upendo na wengine akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni Misri Kusini. Ndiye wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa, na ndani yake jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”.

Kanuni hiyo ikaja kuathiri maisha ya wamonaki na kanuni zao mashariki na magharibi vilevile, na ndiyo inayoongoza umati wa wamonaki wa Ethiopia tangu mwaka 500 hivi. Mbali ya mafungo na sala ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani kuwa na utiifu, huruma na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili. Karibu na monasteri za kiume kulikuwa na nyingine za kike.

Pia Bazili Mkuu (330-379), baada ya kutembelea wamonaki sehemu mbalimbali, alianzisha maisha ya pamoja katika “jamaa” ambayo lengo lake kuu lilikuwa kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni. Tofauti na monasteri ya Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya watawa, jamaa hiyo haikuwa na idadi kubwa wala ngome; tena haikuwa jangwani, bali karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia. Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa: watawa wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wafuate utakatifu wa wito wao; tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama vile kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida. Mtindo huo ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa. Pia ulitia maanani masomo ya kidini.

Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu wamonaki wote wa mashariki, na kwa njia yao makanisa ya Orthodoksi kwa kuwa kwao maaskofu kwanza ni wamonaki nao wanaelekeza Wakristo wote kufuata mifano yao.

Katika nchi ya jirani Mesrop (361-440) akaanzisha mtindo wa monasteri kuwa na shule karibu ili kuandaa watu watakaoendeleza elimu ya dini hasa kwa kutafsiri na kunakili vitabu. Mapema monasteri kubwa zikawa pia na seminari kuu au vyuo vikuu vya teolojia.

Huo umonaki wa Armenia ulidumisha utamaduni wa taifa hilo, ambalo lilikuwa la kwanza kupokea Ukristo jumla pamoja na mfalme wake (300) halafu likaushika moja kwa moja hata lilipopitia vipindi vigumu sana.

Maisha ya pamoja magharibi hariri

Tangu karne IV umonaki ulienea magharibi pia: huko Italia, Ufaransa na Hispania kulikuwa na monasteri za kike na za kiume zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni Martino wa Tours (316-397).

Hasa maandishi ya Yohane Kasiano (360-435) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea nao.

Augustino wa Hippo (354-430), babu wa Kanisa muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake, akawashirikisha utajiri wake wa akili na roho ili wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake, iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi kote.

Benedikto wa Nursia (480-547) ndiye aliyeunda umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake, Kanuni ya Mwalimu asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu wengine wa jangwani.

Kanuni yake iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na kufufua uchumi wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.

Kutokana na kila monasteri kujitegemea, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.

Kati ya aina nyingine za umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ulaya visiwani). Hao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa Kolumbani (540-615).

Hatimaye wakaja kukubali kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la Roma.

Wamonaki wengine pia walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. Augustino wa Canterbury (+605), aliyetumwa Uingereza na Papa Gregori I (540-604), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu Bonifas (672-754), mtume wa Ujerumani na mfiadini.

Marekebisho ya karne IX-XII hariri

Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii na vya ulegevu.

Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linaathiriwa na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha.

Utawa unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika karne IX hadi XII Kanisa la magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote.

Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo yanakumbukwa hasa lile la Cluny (ambalo lilikwepa kuwa mikononi mwa watawala likakazia liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi).

Wamonaki wa matawi hayo wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa, hasa Petro Damiani (1007-1072), Papa Gregori VII (1028-1085) na Bernardo wa Clairvaux (1090-1153).

Wakati huohuo Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (Wakartusi).

Ukanoni hariri

Ili kuboresha maisha ya mapadri wanajimbo, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati yao, ambamo wasali na kufanya utume kwa pamoja.

Hasa kuanzia karne XI wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makubwa kama mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji.

Inavyoweza kueleweka, hao walifuata kanuni ya Augustino na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi katika yao ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa Wapremontree.

Watawa askari, wanahospitali na wakombozi wa watumwa hariri

 
Mt. Yohane wa Matha

Katika karne XII, ambapo baadhi ya Wakristo walipiga vita vya msalaba kuikomboa nchi takatifu, na baadhi walitekwa na Waislamu kuwa watumwa, zilianzishwa aina mpya za watawa ambao washike maisha ya Kiroho pamoja na upanga ili kusindikiza, kukaribisha, kulinda na kutibu waliohiji Yerusalemu, au wajitolee kukomboa watumwa hata kwa kubadilishana nao.

Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu. Kati ya waanzilishi wakumbukwe Yohane wa Matha (1154-1213) na Petro Nolasco (1180-1249).

Mashirika ya ombaomba hariri

 
Mt. Dominiko Guzman
 
Mt. Fransisko wa Asizi

Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika.

Pia hija na vita vya msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni.

Dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na unyofu hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai.

Juu ya misingi hiyo katika karne XIII yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa Wafransisko na Wadominiko, lakini pia Waaugustino, Wakarmeli na Watumishi wa Maria) yaliyoitwa ya ombaomba kwa jinsi yalivyokaza ufukara.

Dominiko Guzman (1170-1221) akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.

Hata kuliko yeye, rafiki yake, Fransisko wa Asizi (1181-1226) alishikwa na hamu ya kulingana na Yesu kwa kufuata nyayo zake inavyofundishwa na Injili. Alifanya vilevile kazi ya kuhubiri, lakini bila ya kuzingatia elimu wala kubishana na wazushi, bali kwa kuelekeza njia ya toba kwanza kwa matendo halafu kwa maneno machache na manyofu. Kwa ajili ya Yesu alijinyima hata upweke alioupendelea, akawakaribia watu hasa wale wadogo zaidi.

Wafuasi wake hawakujifunga kuishi daima mahali fulani na watu walewale, bali walifungamana na jamaa ya kimataifa ambayo mkuu wake aweze kuwatuma popote. Hivyo iliwabidi wawe tayari kukabili mazingira yoyote na kushirikiana na ndugu mbalimbali. Tena udugu haukuishia shirikani bali ulitakiwa kuenea kwa watu na viumbe vyote. Kutokana na upya wa mtindo huo wa maisha, hata miundo yake ilipaswa kuwa mipya iweze kudumisha umoja wao.

Ufransisko ulilingana kikamilifu na madai ya urekebisho ya walei, pia uliwapendeza viongozi wa Kanisa walioona ulivyowarudishia utiifu wa waamini: hivyo ulienea kasi ajabu, hata kati ya wanawake na watu wa ndoa.

Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo. Klara wa Asizi (1193-1253), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana hadi leo kuhusu ufukara.

Tangu karne XII wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati yao Katerina wa Siena (1347-1380), wa utawa wa tatu wa Mt. Dominiko, ametangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa.

Mashirika yasiyo na nadhiri za hadhara hariri

Kuanzia karne XIII zilijitokeza pia jumuia nyingine ambazo pengine zinahusiana na mashirika ya kitawa (yaani za Utawa wa Tatu), lakini hazina nadhiri au si za hadhara. Kwa kuenea, zikaja kuwa na muundo kama wa mashirika (1401), ingawa kwa kawaida ya kwao yalikuwa na jumuia za kiume na za kike ndani yake.

Baada ya upinzani mwingi, wanawake wakaja kukubaliwa wafanye utume na kuanzisha mashirika yasiyobanwa na ugo. Kwa namna ya pekee Anjela Merici (1474-1540) alitaka wafuasi wake waishi na kutumikia kati ya watu; baada ya karne nne shirika lake likakubaliwa kutambulika kuwa la kilimwengu.

Upande wa wanaume Filipo Neri (1515-1595) ni maarufu kati ya walioanzisha jumuia ambapo watu wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya kuwekwa wakfu.

Mashirika ya kikleri hariri

 
Livio Mehus, Mtakatifu Petro wa Alkantara akimkomunisha mtakatifu Teresa wa Avila; picha ya mwaka (1683) inayotunzwa Prato (Italia)

Karne XVI ilidai sana urekebisho wa Kanisa lote. Katika jitihada hizo Waprotestanti walifikia hatua ya kujitenga, lakini wengine walirekebisha mashirika ya zamani: matokeo muhimu zaidi ni Ndugu Wadogo Wakapuchini (1525), halafu Wakarmeli Peku wa Teresa wa Yesu (1515-1582) na Yohane wa Msalaba (1542-1591).

Wengine walianzisha matapo mapya ya Kiroho na mashirika yanayolenga hasa utume, kwa kupunguza ukubwa wa nyumba na urefu wa sala za pamoja: pengine hayahitaji ratiba wala ushirikiano isipokuwa kati ya kiongozi na mtawa mmojammoja. Mashirika hayo hayana kanuni bali katiba tu.

Kati ya yote lile la Yesu (Wajesuiti) ndio muhimu zaidi. Mwanzilishi wake, Ignas wa Loyola (1491-1556), ambaye kabla hajaongoka alikuwa askari, alileta utawani mtindo wa kijeshi, akisisitiza utiifu kwa viongozi wa shirika na kwa Papa (baadhi wanajifunga kwake kwa nadhiri ya nne, nguzo kuu ya shirika). Hivyo Mjesuiti jumuia yake halisi ni shirika tu ambalo linaweza kumtuma kokote duniani, naye atafanya kazi yoyote kwa niaba ya shirika, tayari kukabili mazingira na hali yoyote.

Mashirika ya kutolea huduma maalumu hariri

Baada ya mashirika ya namna hiyo yaliyolenga wakleri, Yohane Batista de La Salle (1651-1719) alianzisha la kwanza kwa ajili ya mabradha tu, kwa lengo la kuendesha shule kwa maskini.

Halafu mashirika ya kike na ya kiume zaidi ya 2000 yalilenga huduma maalumu inayohitajika lakini haina wa kuitoa, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha mafukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji habari. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa jimbo na hasa katika karne XIX.

Kati ya waanzilishi muhimu zaidi wakumbukwe Vinsenti wa Paulo (1576-1660), Alois Maria wa Montfort (1673-1716), Paulo wa Msalaba (1694-1775), Alfonso Maria wa Liguori (1696-1785), Karolo Yosefu Mazenod (1782-1861), Vinsenti Pallotti (1795-1850), Antoni Maria Claret (1807-1870), Yohane Bosco (1815-1888), Daniele Comboni (1831-1881), Arnold Janssen (1837-1909). Kati ya wanawake, Yoana Antida Thouret (1765-1826), Magdalena wa Canossa (1774-1835), Visensya Gerosa (1784-1847) pamoja na Bartolomea Capitanio (1807-1833), Fransiska Saveri Cabrini (1850-1917), na hatimaye mama Teresa wa Kolkata (1910-1997).

Mashirika ya kilimwengu na jumuia mpya hariri

Karne XX, ngumu kwa Kanisa na kwa dunia yote, ilileta mang’amuzi mapya hasa katika maisha ya ulimwenguni. Kwa mara nyingine walei walichangia sana hali mpya ndani ya Kanisa, ya kuthamini na kushughulikia mambo ya kidunia.

Katika juhudi za kuratibu nyanja zote za maisha ya binadamu, baadhi walijisikia haja ya kuwekwa wakfu bila ya kujitenga na maisha ya kawaida. Polepole Kanisa likafikia uamuzi wa kuwakubalia (1950) mashirika ya kilimwengu ambayo waamini wanawekwa wakfu wawe chumvi, mwanga na chachu kati ya watu. Hivyo wanajitahidi kuwa na moyo wa kujikana na bidii ya kitume kama watawa, lakini pia utaalamu wa kisasa na urahisi wa kupenya mazingira yoyote kama walei.

Halafu Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965) uliagiza uanzishwe tena utawa wa mabikira ambao waishi ulimwenguni na kuwekwa wakfu kwa ajili ya jimbo, si kwa shirika lolote.

Nusu ya pili ya karne hiyo ilililetea Kanisa Katoliki neema za matapo mengi yaliyoanzishwa kwa kawaida na walei na kuenea kati ya watu milioni na milioni. Mbali ya watawa wengi kuyafuata na miito mingi kupatikana ndani yake, baadhi ya wafuasi wa matapo hayo hawaingii shirika fulani bali wanakusanyika kuishi kijumuia au kuwekwa wakfu katika matapo yenyewe ili wayaongoze Kiroho kwa kuchimba karama yake.

Wengine pia waliona haja ya kujumuika hata nje ya miundo ya kitawa, wakifuata mitindo ya kimonaki au kutoa huduma kwa wasiojiweza ndani ya jumuia, ingawa baadhi yao wana ndoa.

Muundo wa pekee ulikubaliwa kwa Opus Dei ambayo ina mapadri, seminari mbalimbali na walei popote duniani: ni kama jimbo lisilo na eneo maalumu. Mwanzilishi wake ni Yosefu Maria Escrivà (1902-1975).

Mbele ya upya huo wote sheria za Kanisa siku hizi zinamhimiza askofu yeyote afanye utambuzi wa aina mpya za maisha yaliyowekwa wakfu zikijitokeza jimboni.

Utawa kati ya Wakristo wa madhehebu mengine hariri

Pamoja na kudumisha moja kwa moja umonaki kati ya Waorthodoksi, Roho Mtakatifu ameongoza Waprotestanti kadhaa kuanzisha upya maisha ya kitawa baada ya babu zao kuyafuta kama kitu kinyume cha Injili.

Kuanzia mwaka 1836 katika nchi mbalimbali watu wa madhehebu hayo walianza tena kuishi kijumuia kwa kufuata pengine mapokeo ya Kibenedikto na ya Kifransisko.

Maarufu zaidi ni Jumuia ya Taizé, ambayo ilianzishwa na ndugu Roger Schutz (1915-2005) na kupokea Wakatoliki pia; lengo lake hasa ni umoja wa Wakristo na kuinjilisha vijana.

  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Utawa kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.