Bahari ya Hindi ni bahari ya tatu kwa ukubwa duniani ikiwa imechukua asilimia 20 ya uso wa dunia na kuzungukwa na mabara manne.

Bahari Hindi na bahari za pembeni upande wa kaskazini-magharibi

Upande wa kaskazini imepakana na Asia ya Kusini; magharibi imepakana na Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Shamu na Afrika; mashariki imepakana na Ghuba ya Malay, visiwa vya Sunda (Indonesia), na Australia; na upande wa kusini imepakana na Bahari ya Kusini.

Bahari hii ni njia muhimu ya usafiri na usafirishaji kwa meli kati ya Asia na Afrika.

Jiografia

Mipaka

Mipaka ya Bahari Hindi imeelezwa na Shirika la Kimataifa la Hidrografia kama ifuatayo:

  • upande wa magharibi (Atlantiki) ni mstari unaoelekea kusini kutoka Rasi Agulhas (Afrika Kusini) kwenye longitudo ya 20° mashariki
  • upande wa mashariki ni mstari unaoelekea kusini kutoka sehemu ya kusini zaidi cha Tasmania (Australia) kwenye longitudo ya 146°55'E
  • kati ya Australia na Asia ni mstari wa visiwa vya Indonesia
  • upande wa kaskazini ni pwani za Asia na Afrika
  • upande wa kusini imeamuliwa kutumia latitudo ya 60°S kama mpaka wa Bahari Hindi na Bahari ya Kusini inayozunguka bara la Antaktiki.

Kwa hiyo eneo lote la uso wa bahari hii ni kilomita za mraba 70,560,000 km²; kina cha wastani ni mita 3,741 ilhali kina kikubwa kinafikia mita 7,906. Mjao wake ni kilomita za ujazo 264,000,000 km³ inayolingana na asilimia 19.8% ya mjao wa bahari zote duniani.

Jiolojia

Chini ya Bahari Hindi kuna mabamba ya gandunia mbalimbali yanayopakana hapa:

Bamba la Antaktiki, Bamba la Afrika, Bamba la Uarabuni, Bamba la Uhindi na Bamba la Australia.

Kama kawaida, pale ambako mabamba yanaachana kuna nafasi inayoruhusu kupanda juu kwa joto na magma kutoka kiini cha dunia na kutokea kwa volkeno pamoja na safu za milima chini ya maji.

Tetemeko la ardhi na tsunami ya 2004, iliyosababisha uharibifu na vifo katika sehemu za kaskazini za Bahari Hindi, ilisababishwa na mwendo wa ghafla la bamba la Australia juu ya bamba la Uhindi.

Bahari za pembeni

Bahari za pembeni, ghuba na hori za Bahari Hindi ni pamoja na:

Tabianchi

Kwa jumla Bahari Hindi ina halijoto ya juu kulingana na bahari kubwa nyingine za dunia. Tofauti na Atlantiki na Pasifiki haina maeneo makubwa kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia hivyo haipokei baridi kutoka Aktiki.

Upande wa kazkazini wa ikweta kuna monsuni; upepo kutoka kazkazini-mashariki uko kuanzia Oktoba hadi Aprili, kinyume chake upepo kutoka kusini[1] unaendelea kuanzia Mei hadi Oktoba. Badiliko hili linafuata utaratibu wa kila mwaka na lilikuwa msingi kwa usafiri na biashara katika bahari hii maana iliwezekana kutumia upepo kwa jahazi tangu kale.

Wakati wa badiliko la monsuni dhoruba kali zinaweza kutokeas hasa katika Bahari ya Uarabuni na Hori ya Bengali.

Nchi zinazopakana na Bahari Hindi

Asia

Israel na Jordani (kupitia Ghuba ya Akaba na Bahari ya Shamu), Ufalme wa Uarabuni wa Saudia, Yemen, Omani, Falme za Kiarabu, Qatar, Kuwait, Iraq, Iran, Pakistan, India, Bangladesh, Myanmar, Uthai, Malaysia, Indonesia na Timor ya Mashariki.

Australia

Australia

Afrika

Afrika Kusini, Msumbiji, Tanzania, Kenya, Somalia, Jibuti, Eritrea, Sudani na Misri (kupitia Bahari ya Shamu).

Nchi za visiwani

Ndani ya Bahari Hindi kuna mataifa huru ambayo ni nchi za visiwani pamoja na Bahrain (Ghuba ya Uajemi), Komori, Madagaska, Maldivi, Morisi, Shelisheli na Sri Lanka.

Indonesia na Timor ya Mashariki ni nchi za visiwani zinazopakana na Bahari Hindi.

Visiwa katika Bahari Hindi

Agalega, Anjouan, Bahrain, Cargados Carajos, Visiwa vya Cocos (Keeling), Diego Garcia, Kilwa Kisiwani, Kirimba (visiwa), Kisiwa cha Mafia, Komori, Kisiwa cha Krismasi, Lamu (kisiwa), Morisi, Madagaska, Mahore, Mahé, Maskarena, Mayotte, Moheli, Msumbiji (kisiwa), Mwali, Ngazija, Pamanzi, Pate, Pemba (kisiwa), Rodrigues (kisiwa), Réunion, Shelisheli, Sokotra, Unguja, Îles Éparses,

Tanbihi

  1. "upepo wa kusi" katika lugha ya Waswahili wa pwani

Kujisomea

  Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.