Jiografia ya Afrika

Jiografia ya Afrika inahusu bara hilo ambalo ni la pili duniani kwa ukubwa, likiwa na eneo la kilometa za mraba zipatazo 30,368,609 (6% za eneo lote la dunia, sawa na 20% za nchi kavu) na vilevile kwa idadi ya wakazi, hao wakiwa 1,275,920,972 (mwaka 2018). Asia ndiyo bara pekee la kushinda Afrika.

Afrika duniani.
Afrika kutoka satelaiti.
Mlima Kilimanjaro.
Beseni la mto Naili[1].
Uwiano kati ya Afrika, Asia na Amerika.

Kuna umbali wa kilomita 8,000 kutoka Ras ben Sakka nchini Tunisia (37°21' N, sehemu ya kaskazini kabisa) hadi rasi ya Cape Agulhas nchini Afrika Kusini (34°51'15" S, sehemu ya kusini kabisa)[2] .

Umbali ni km 7,400 kutoka upande wa magharibi (rasi ya Cape Verde, 17°33'22" W) hadi mashariki (Ras Hafun nchini Somalia, 51°27'52" E)[3].

Mlima mrefu zaidi barani unapatikana nchini Tanzania: ni volkeno Kilimanjaro (mita 5,895 juu ya usawa wa bahari) ambao ni pia mlima mrefu kuliko yote duniani usiojitokeza katika safu ya milima.

Mto mrefu zaidi barani na duniani ni Naili ukiwa na mwendo wa kilometa 6,758 kuanzia nchini Rwanda na Burundi, kupitia Tanzania, Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Ethiopia, Sudan na hatimaye Misri.

Katika mwendo wake wa awali maji ya Naili yanakusanyika katika ziwa Nyanza/Viktoria ambalo ni pana kuliko yote barani na la pili duniani likiwa na kilometa mraba 59,947.

Afrika imezungukwa na bahari karibu pande zote. Kuna kiungo chembamba cha nchi kavu upande wa kaskazini mashariki na bara la Asia kwenye rasi ya Sinai [4].

Upande wa kaskazini iko Bahari ya Mediteranea, upande wa mashariki kuna Bahari Hindi pamoja na Bahari ya Shamu na upande wa magharibi iko Bahari Atlantiki.

Pwani yote ya Afrika ina urefu wa kilomita 26,000.

Kuna kisiwa kikubwa cha Madagaska na funguvisiwa mbalimbali.

Jiolojia hariri

 
Uoto barani Afrika

Kijiolojia Afrika iko kwenye bamba la Afrika. Lile bamba la gandunia la Afrika linaenea mbali zaidi kuliko maeneo tunayotazama kuwa Afrika kijiografia, ni pamoja na maeneo chini ya bahari linapopakana na mabamba ya Ulaya-Asia, Uarabuni, Uhindi na Australia, Antaktika, Amerika ya Kusini na Kaskazini. Upande wa mashariki wa bamba la Afrika kuna ufa unaozidi kupanuka ikielekea kujitenga kutoka Afrika kama bamba la Somalia.

Tabianchi hariri

Tabianchi ya Afrika ni pana, kuanzia kanda za tropiki hadi kufikia maeneo ya nusu-aktiki (baridi) kwenye ncha za milima mirefu.

Nusu ya kaskazini ya bara ni jangwa au angalau yabisi. Sehemu za kati na za kusini zina maeneo ya savanna na kanda za msitu wa mvua.

Afrika ni bara lenye joto kuliko mabara yote na asilimia 60 za uso wake ni maeneo yabisi au jangwa. [5]

Nchi za Afrika hariri


Barani kuna nchi huru 54 zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa, maeneo 9 yenye hali ya pekee na madola mawili ambayo yanajitawala bila kutambuliwa kimataifa.

Nchi kubwa ya Afrika ni Algeria na nchi ndogo ni Shelisheli, funguvisiwa la Bahari Hindi.[6] Nchi ndogo Afrika bara ni Gambia.

Wakazi hariri

Wataalamu wengi wanakubaliana kutambua Afrika kama asili ya binadamu wote walioko duniani. [7]

Mwaka 2010 idadi ya wakazi wa nchi zote za Afrika ilipita bilioni 1. Ni kwamba idadi yao imeongezeka sana katika miaka 40 iliyopita, ikipiku zile za Ulaya na Amerika.

Ilhali mwaka 1950 walikuwepo Waafrika milioni 229 pekee, idadi iliongezeka kuwa milioni 630 mwaka 1990 na milioni 1200 mnamo 2014. [8] [9]

Hivyo asilimia ya watoto na vijana ni kubwa. Kuna nchi kadhaa ambako zaidi ya nusu ya wananchi wako chini ya umri wa miaka 25.[10] Wakazi wa Afrika ni vijana kuliko wale wa mabara mengine yote;[11][12] mwaka 2012 umri wa wastani ulikuwa miaka 19.7, wakati kidunia ulikuwa 30.4.[13]

 
Mwanamke wa Benin.

Zaidi ya lugha elfu za Kiafrika zinazungumzwa barani leo, ingawa nyingi zinazidi kufifia.

 
Ramani ya dini barani Afrika.

Waafrika wana imani za dini nyingi tofauti, lakini takwimu zinazotolewa hazina hakika, pia kwa sababu suala hilo ni nyeti kisiasa kwa serikali zenye mchanganyiko mkubwa wa watu, kama vile Nigeria, Ethiopia na Tanzania.[14][15]

Kadiri ya World Book Encyclopedia, Islam ndiyo inayoongoza, ikifuatwa na Ukristo. Kumbe kadiri ya Encyclopedia Britannica, 45% za wakazi ni Wakristo, 40% ni Waislamu na 10% wanafuata dini asilia za Kiafrika. Wachache tu ni Wahindu, Wabuddha, Wabaha'i au hawana dini yoyote.

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

  1. The Nile River. Nile Basin Initiative (2011). Jalada kutoka ya awali juu ya 2 September 2010. Iliwekwa mnamo 1 February 2011.
  2. Lewin, Evans. (1924) Africa, Clarendon press
  3. (1998) Merriam-Webster's Geographical Dictionary (Index), Merriam-Webster, pp. 10–11. ISBN 0-87779-546-0.
  4. Drysdale, Alasdair and Gerald H. Blake. (1985) The Middle East and North Africa, Oxford University Press US. ISBN 0-19-503538-0.
  5. "Africa: Environmental Atlas, 06/17/08." Archived 5 Januari 2012 at the Wayback Machine. African Studies Center, University of Pennsylvania. Accessed June 2011.
  6. Hoare, Ben. (2002) The Kingfisher A-Z Encyclopedia, Kingfisher Publications. p. 11. ISBN 0-7534-5569-2.
  7. Homo sapiens: University of Utah News Release: Feb. 16, 2005 Archived 24 Oktoba 2007 at the Wayback Machine.
  8. "Past and future population of Africa Archived 24 Septemba 2015 at the Wayback Machine.". Source: United Nations, Department of Economic and Social Affairs, Population Division (2013).
  9. UNICEF Report: Africa's Population Could Hit 4 Billion By 2100. National Public Radio (NPR). 13 August 2014.
  10. Africa Population Dynamics. Jalada kutoka ya awali juu ya 2015-02-17. Iliwekwa mnamo 2020-04-19.
  11. http://www.washingtonpost.com/news/wonkblog/wp/2015/08/17/5-ways-the-world-will-look-dramatically-different-in-2100/
  12. Harry, Njideka U.. "African Youth, Innovation and the Changing Society", Huffington Post, 11 September 2013. 
  13. ABDOULIE JANNEH (April 2012). item,4 of the provisional agenda - General debate on national experience in population matters: adolescents and youth. UNITED NATIONS ECONOMIC COMMISSION FOR AFRICA. Iliwekwa mnamo 15 December 2015.
  14. "African Religion on the Internet" Archived 9 Mei 2008 at the Wayback Machine., Stanford University
  15. Onishi, Normitsu. "Rising Muslim Power in Africa Causing Unrest in Nigeria and Elsewhere", The New York Times, November 1, 2001. Retrieved on 2009-03-01. 

Viungo vya nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: