Ukristo barani Afrika
Ukristo barani Afrika una historia ndefu inayokaribia miaka elfu mbili.
Ukristo uko Afrika katika wingi wa madhehebu yaliyopatikana katika historia ya Kanisa, baadhi katika bara hilo, baadhi katika mabara mengine.
Kwa sasa ndiyo dini kubwa zaidi barani, hasa Kusini kwa Sahara, pamoja na Uislamu ambao unaongoza Kaskazini kwa jangwa hilo.
Ustawi wa Ukristo leo
haririLeo karibu nusu ya Waafrika wote ni Wakristo. Lakini asilimia ya Wakristo inaweza kuwa ndogo katika nchi kadhaa na kubwa katika nchi nyingine. Katika Afrika Kaskazini Wakristo ni wachache. Kumbe ni wengi kwa theluthi mbili za bara kusini kwa Sahara.
Kwa jumla Wakristo wanaishi kati ya wafuasi wa dini nyingine, hasa Uislamu na dini za jadi.
Idadi yao inaongezeka haraka sana. Kila baada ya nukta nne Mwafrika mmoja anaingia Ukristo. Wengine huzaliwa katika familia ikiwa mzazi mmoja au wote wawili ni Wakristo tayari. Katika madhehebu mengi iko desturi ya kuwabatiza watoto wadogo. Ubatizo huo unawafanya kuwa wanakanisa. Wakikua watafundishwa na pengine kukaribishwa kwenye Kipaimara. Katika ibada hiyo kijana atarudia ahadi ya ubatizo wake na kuwekewa mikono na askofu au mchungaji mwingine na kuombewa ili Roho Mtakatifu amsaidie katika maisha yake ya Kikristo. Madhehebu mengine hayabatizi watoto wadogo. Yanaweza kuwapokea katika Kanisa kwa ibada maalumu lakini yanasubiri mpaka mtoto atakapokuwa mtu mzima, halafu apokee ubatizo na kuwa Mkristo rasmi.
Njia nyingine ya kukua kwa Kanisa ni kuongoka. Maana yake mtu asiye Mkristo anasikia habari za imani na kuvutiwa moyoni. Halafu anafika kwa kiongozi wa Kanisa na kupata mafundisho juu ya imani na maisha ya Kikristo. Halafu anaweza kubatizwa. Atakuwa mwanakanisa katika dhehebu fulani lakini ni vilevile Mkristo katika Kanisa moja takatifu la Bwana Yesu lililopo popote duniani. Wakristo Waafrika wengi kidogo ni watu walioongoka: waliwahi kuwa wafuasi wa dini nyingine (hasa dini za jadi, lakini wengine Uislamu), wakasikia Habari Njema wakaamua kumfuata Yesu.
Historia
haririWakati mwingine tunaweza kusikia kuwa Ukristo uliingizwa Afrika juzijuzi tu, na asili yake ni Ulaya. Hili si kweli. Ukristo ni imani ya kale sana katika Afrika. Tangu mwanzo wa Kanisa walikuwepo Wakristo Waafrika.
Ila Afrika Mashariki historia ya Ukristo si ndefu. Mwaka 1900 katika eneo la Tanzania ya leo Wakristo walikuwa elfu kadhaa tu. Ongezeko lilikuja haraka sana. Leo hii wako zaidi ya milioni 20. Wakati ule kati ya Watanganyika 100, Wakristo walikuwa 2 tu. Leo zaidi ya 50 kati ya Watanzania 100 ni Wakristo.
Afrika na sehemu nyingine za dunia wakati wa Yesu
haririMiaka 2000 iliyopita mawasiliano kati ya nchi na nchi hayakuwa rahisi. Hapakuwa na redio wala simu wala ndege wala magari. Usafiri ulikuwa kwa miguu au kwa kupanda wanyama (k.v. farasi, ngamia, punda), halafu kwa meli za tanga. Meli hizo ziliweza kufuata pwani tu, hazikuwa imara kutosha kuvuka bahari kubwa.
Lakini hata kwa vyombo hivyo iliwezekana kufanya biashara kati ya Mediteranea na nchi za mbali kama Bara Hindi au Afrika Mashariki. Tunafahamu kitabu ambacho kiliandikwa mwaka 100 BK na kueleza usafiri wa baharini kutoka Misri hadi pwani ya Afrika Mashariki (iliyoitwa na Wagiriki "Azania"). Lakini watu waliojua habari hizo walikuwa wachache.
Jangwa la Sahara lilikuwa kizuizi kikuu cha mawasiliano na usafiri kati ya sehemu kubwa ya Afrika na sehemu nyingine. Mabara ya Amerika na Australia hayakujulikana na wataalamu wa Asia, Afrika na Ulaya.
Watu wengi waliamini dunia kuwa tambarare yenye umbo la duara (kama sahani), ingawa wataalamu wengine katika Misri walikwishagundua kwa njia ya kupima dunia kuwa ina umbo la chungwa. Lakini si watu wengi walioamini au kujali elimu hizo. Ilikuwa nje ya upeo wao. Hali hii ilibadilika tu karne nyingi baadaye, wakati meli za kuvuka hata bahari kubwa zilipopatikana.
Tukiona ya kwamba asili ya Ukristo ni eneo la Yerusalemu tunaweza kuelewa jinsi gani mitume wa Yesu waliweza kutumia usafiri uliopatikana wakati ule na kufika nchi zilizojulikana katika mazingira yao lakini hawakufika mbali zaidi.
Wakati wa Yesu Afrika Kaskazini pia ilikuwa chini ya utawala wa Roma. Wakati ule wakazi wake hawakuwa Waarabu. Kiutamaduni palikuwa na sehemu mbili: Misri upande wa Mashariki na nchi za Waberberi upande wa Magharibi. Nchi hizo za Waberberi (Moroko, Algeria, Tunisia na Libia za leo) zilikuwa pia na miji mingi walipokaa wahamiaji kutoka Italia waliotumia lugha ya Kilatini. Mji mkuu wa sehemu ile ni Karthago (karibu na Tunisi ya leo). Mji mwingine unaoonekana katika Biblia ni Kurene (kule Libia).
Misri ilikuwa kitovu cha elimu ya juu tangu karne nyingi. Mji mkuu wa Misri ulikuwa Aleksandria. Eneo la utawala wa Roma lilifika mpakani mwa Sudani ya leo (eneo lililoitwa "Nubia").
Nchi hizo hazikuwa na mawasiliano mengi na nchi za kusini mwa jangwa la Sahara lililozuia usafiri. Hivyo imani ya Kikristo ilifika haraka katika sehemu ya Kaskazini kwa Sahara ila haikuvuka jangwa hilo kubwa. Lakini mawasiliano yalikuwepo na sehemu za Ulaya Kusini na Asia, hasa kupitia Bahari ya Kati. Ilikuwa rahisi kwa mitume wa Kristo kutumia mawasiliano hayo yaliyokuwepo tayari.
Watu wa Mediteraneo walifanya tayari biashara kwa meli na pwani ya Afrika Mashariki. Tunaweza kuwaza ya kwamba wafanyabiashara Wakristo walitembelea mapema sehemu hizo pia lakini hakuna kumbukumbu yoyote kama walihubiri n.k.
Nchi hizo za Afrika Kaskazini zilikuwa tajiri. Hali ya hewa wakati ule ilikuwa afadhali kwa kilimo kuliko leo. Milima ya Atlas ilijaa misitu. Katika Algeria na Tunisia ya leo ililimwa ngano kwa wingi na kuilisha Italia. Hata jina la "Afrika" lina asili yake katika kipindi cha Kiroma. "Afrika" ilikuwa jina la mkoa mmoja uitwao leo Tunisia. Kutoka kule jina hilo lilitumika baadaye kwa sehemu nyingine za bara hilo.
Kwa jumla watu walifuata dini zao za asili za kuabudu miungu mingi. Palikuwa na mchanganyiko wa imani mbalimbali. Wanajeshi Waroma waliokaa katika nchi nyingi walileta miungu yao na kuwajengea mahekalu pale walipokaa. Kule Misri na sehemu za Kurene waliishi pia Wayahudi wengi waliotumia hasa lugha ya Kigiriki. Kwa njia ya Wayahudi hao habari za Mungu mmoja zilikuwa zinasikika sehemu nyingi.
Watu wa Afrika Kaskazini walisafiri na kukaa pia katika miji ya Ulaya na Asia. Kutokana na mawasiliano mazuri tunaona Waafrika mbalimbali katika taarifa za Agano Jipya. Tuone mifano: - Yesu alipobeba msalaba wake kule Yerusalemu akaanguka chini. Maaskari wakamkamata mtu aliyepita mtaani jina lake ni Simoni wa Kurene. Jina linaonyesha ya kwamba alikuwa mgeni kutoka Kurene (Libia). (Lk 23:26) - wakati wa ushirika wa kwanza kule Yerusalemu, Filipo mwinjilisti alikutana na msafiri kutoka Kushi akambatiza. Kushi ni jina la kale la sehemu ya Sudan Kusini ya leo (matoleo mengine ya Biblia hutafsiri: Mhabeshi au Mwethopia). (Mdo 8:26 n.k.). - katika ushirika wa mji mkubwa wa Antiokia (Asia Magharibi) tunasikia juu ya watu wa asili ya Afrika waliokuwa viongozi wa ushirika huo. Mmoja ni Lukio Mkurene. Mwingine ni "Simeoni aitwaye Nigeri". Neno "Nigeri" linatafsiriwa "Mweusi". Kumbe hata huyu anaonekana ametokea Afrika kutokana na rangi yake. (Mdo 13)
Haya yote si ajabu. Nchi za Misri mpaka Sudan na Afrika Kaskazini-Magharibi zilikuwa sehemu ya Dola la Roma wakati Ukristo ulipoanza kuenea.
Yesu mwenyewe alikaa miaka kadhaa Afrika. Alitoka nje ya Israeli-Palestina mara moja tu katika utoto wake wakati wazazi wake walipokimbilia pamoja naye Misri kwa sababu Mfalme Herode Mkuu alitaka kumwua mtoto Yesu. Mpaka leo Wakristo wenyeji wa Misri wanatunza kumbukumbu ya Familia Takatifu katika nchi yao. Makanisa mbalimbali yapo mahali panapokumbukwa ya kwamba Yosefu, Bikira Maria na mtoto Yesu walipumzika.
Asili ya Ukristo nchini Misri
haririHatuna habari ndani ya Biblia juu ya shirika za kwanza zilizoundwa kule. Lakini Wakristo wa Misri wanamkumbuka Marko Mwinjili aliyefika Aleksandria na kuhubiri Habari Njema Afrika hata kuanzisha Kanisa pale Misri. Ndiye hasa mwinjilisti wa Afrika. Marko alikuwa amesafiri na Mtume Petro kama mwanafunzi wake.
Hakuwahi kuwa mwanafunzi wa Yesu, lakini aliandika Injili, yaani taarifa juu ya maisha na mafundisho yake. Alikuwa mwandishi wa kwanza wa habari hizo. Mtume Mathayo na Luka mwinjili walitumia taarifa ya Marko walipoandika Injili zao.
Anasemekana alikufa akiwa shahidi wa imani wakati wa mateso ya kwanza chini ya serikali ya Roma. Anakumbukwa kama Askofu wa kwanza wa Aleksandria. Ndiyo sababu mpaka leo Askofu Mkuu wa Aleksandria huitwa "Mwandamizi wa Marko".
Ushujaa wakati wa dhuluma (64-309)
haririTuna habari nyingi juu ya Wakristo kule Misri na Karthago (magofu yake yako nchini Tunisia) wakati wa karne ya 2. Habari hizo zinaeleza maisha na mateso yao.
Hao na Wakristo wa kwanza walio wengi waliishi chini ya serikali ya Roma. Kwa jumla hiyo iliwaruhusu watu wote kuendelea na desturi na dini zao. Serikali iliona ni muhimu kuabudu miungu yote kwani ingekuwa hatari mungu fulani angesahauliwa hata kusababisha akasirike.
Matendo ya Mitume 17:16-23 inasimulia kwamba Mtume Paulo alishangaa kuona sanamu nyingi za miungu kule Athene. Kati ya sanamu hizo aliona madhahabu (altare) yaliyotengwa kwa ajili ya "Mungu asiyejulikana". Kumbe serikali ya Athene iliogopa kumsahau mungu yeyote ikatoa sadaka za tahadhari.
Kaisari naye, yaani Mfalme Mkuu wa Roma, alipewa heshima ya kimungu. Raia walitakiwa kushiriki ibada za kumtolea sadaka mbele ya sanamu zake. Kwa watu wengi waliozoea kuabudu miungu mingi haikuwa vigumu sana kumwingiza Kaisari kama mungu wa nyongeza katika mawazo yao. Lakini kwa Wakristo haikuwezekana kushiriki ibada hizo. Kwa hiyo walionekana kama maadui wa serikali. Walikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani.
Ukali wa mateso ulitegemea siasa ya wakuu wa mikoa ya Kiroma. Wakati mwingine waliweza kujipatia sifa wakitoa taarifa ya kwamba wamekamata Wakristo wengi na kuwahukumu. Wakati mwingine waliona afadhali kuwaacha Wakristo na kutosababisha vurugu katika mkoa. Nje ya suala la kidini Wakristo walikuwa raia wema.
Wafiadini nchini Misri
haririKatika karne ya 3 mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hiyo ilikuwa uasi. Wakaona ni lazima kuzima uasi huo.
Kati ya miaka 302 na 308 B.K. maelfu wakauawa kule Aleksandria. Wakakatwa vichwa na maaskari, wakapelekwa katika kiwanja cha michezo mbele ya wanyama mwitu, wakachomwa moto. Lakini idadi ya Wakristo waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaua.
Kumbe mwaka 312 ilikuwa kama ukombozi kwa mji wa Aleksandria. Kaisari mpya, kwa jina Konstantino Mkuu akatangaza mwisho wa mateso. Akatoa sheria ya kuwa Ukristo ni dini halali katika Dola la Roma.
Urithi wa Misri kwa Kanisa zima: elimu na umonaki
haririMisri ilikuwa kitovu muhimu cha Ukristo wa kale. Uhodari wa Wakristo wake ulishinda dhuluma za serikali ya Kiroma. Katika mapambano hayo Wakristo Wamisri wakaunda silaha mbili ambazo zimekuwa muhimu katika Kanisa zima mpaka leo: 1. Elimu ya Kikristo 2. Utaratibu wa umonaki.
Elimu ya kikristo: Chuo cha Aleksandria
haririJiji la Aleksandria lilikuwa na maktaba kubwa kuliko zote duniani. Wakati ule haikujulikana jinsi ya kupiga chapa vitabu. Kila kitabu kiliandikwa kwa mkono kikawa na bei kubwa sana. Kununua kitabu kulikuwa na gharama zinazofanana na ile ya kununua gari leo. Kwa hiyo elimu ilikuwa na thamani kubwa, na maktaba kubwa ilikuwa na thamani kupita kiasi. Wataalamu toka pande zote za dunia walifika Aleksandria, mji wa elimu, ili kusoma na kunakili vitabu. Si ajabu kwamba Agano la Kale lote lilitafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kigiriki huko Aleksandria mwaka 150 hivi K.K.
Hivyo Wakristo wa Aleksandria walijisikia hawana budi kuwa tayari kujadiliana na watu wenye elimu. Wawe tayari kujibu maswali yao juu ya Injili hata kutetea imani kwenye ngazi inayolingana na elimu ya hali ya juu. Wakristo wenye elimu walijitolea kuelimisha Wakristo wenzao. Katika mafundisho hayo kilitokea chuo cha Kikristo cha kwanza. Masomo yake yalihusu imani na Biblia lakini pia elimu kwa jumla. Falsafa ilikuwa muhimu katika mawazo ya wataalamu hata katika mafundisho ya kidini ya Wapagani na Wayahudi. Basi, ilionekana afadhali mwalimu Mkristo ajue falsafa na awe na msimamo wake juu ya uhusiano kati ya falsafa na imani ya Kikristo.
Chuo cha Aleksandria kilipata sifa chini ya Panteno. Mnamo mwaka 200 BK huyo aliacha uongozi wa chuo akawa mmisionari huko Bara Hindi. Aliyemfuata alikuwa Klementi wa Aleksandria aliyefaulu sana kuvuta Wapagani wenye elimu kumpokea Kristo.
Mwanafunzi wake mashuhuri alikuwa Origene, ambaye baadaye akapewa uongozi wa chuo hicho. Alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 25. Origene alikuwa mtaalamu wa pekee: ndiye wa kwanza kutumia njia ya kisayansi katika kuchunguza fasiri za Biblia. Pamoja na makarani wake akaandika maneno yote ya Kiebrania ya Biblia pamoja na fasiri zake katika nguzo sita kwenye ngozi kubwa. Njia hiyo ilisaidia kuona mara moja makosa au udhaifu katika fasiri hizo. Aliwafundisha vijana wengi kutumia akili yao katika kutafakari imani kwani akili ni kipawa cha Mungu.
Kwa njia hiyo Chuo cha Aleksandria kimekuwa mwanzo wa elimu ya juu katika Ukristo. Mpaka leo ni kawaida kwamba mtumishi wa Kanisa awe na elimu. Wachungaji, mapadri na watawa wanasomeshwa katika vyuo mbalimbali hadi ngazi ya chuo kikuu. Ukristo umekuwa imani ya wasomi. Asili ya jambo hilo ni katika juhudi za Wakristo wa Misri.
Baadaye, hukohuko Aleksandria ulitokea uzushi mkuu wa historia yote ya Kanisa: padri Ario alikanusha umungu wa Yesu. Mafundisho yake yalienea kote mashariki na kuungwa mkono na watawala kwa nguvu za dola. Lakini ni Kanisa la Misri lililompinga kwa uimara wa pekee, bila kujali dhuluma.
Kati ya wote, alijitokeza Atanasi wa Aleksandria anayeitwa Mkuu (Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373), Patriarki wa Kanisa Katoliki la madhehebu ya Misri kati ya mitaguso mikuu miwili ya kwanza: Nisea I (325) na Konstantinopoli I (383).
Maisha yote ya Atanasi yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema “nguzo ya Kanisa” (Gregori wa Nazianzo).
Pamoja na kupatwa na vurugu nyingi maishani (hasa kufukuzwa mara tano kutoka mji wake), Atanasi aliandika sana: hotuba na barua, lakini pia vitabu juu ya imani, historia, ufafanuzi wa Biblia, pamoja na maisha ya Kiroho. Kitabu chake maarufu kimojawapo kinahusu umwilisho wa Neno; humo aliandika kuwa Neno wa Mungu “alifanyika mtu ili sisi tuweze kufanywa Mungu”.
Lakini kitabu ambacho kilienea na kuathiri zaidi maisha ya Kanisa labda ni "Maisha ya Antoni" ambacho kilieneza umonaki haraka mashariki na vilevile magharibi.
Utawa na umonaki - maisha ya pekee
haririWatawa ni Wakristo walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Mara nyingi tumezoea kuwaona katika Kanisa Katoliki. Lakini wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa si wengi. Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptisti.
Mtawa amepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo (ambaye hakuoa): «Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo» 1Kor 7:8. Yesu mwenyewe aliwahi kueleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila familia na uzazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (Mt 19:12: "Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni»).
Kwa jumla watawa ni kundi muhimu linalosaidia sana kazi ya kiroho katika Ukristo. Wako huru kuliko wengine kujitolea katika huduma za Kanisa, kwani hawalazimiki kufikiria maendeleo ya watoto wao. Watawa wanaweza kuishi peke yao lakini mara nyingi wanajiunga na shirika au jumuiya na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu.
Asili ya jumuiya hizo iko Misri. Katika karne ya 3 mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma Wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani wakiogopa kulazimishwa kutoa sadaka kwa sanamu. Wengine waliona jinsi familia yao ilivyouawa katika dhuluma za kidini. Wengine karibu walikata tamaa wakiona Wakristo wengine walivyokana imani kwa kuogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya kawaida, wakajitenga na dunia wakaenda porini kuishi kule maisha ya kufunga na kusali.
Watawa hao waliitwa kwa jina la Kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake). Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala wa Kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Walitumia muda mwingi wakisali na kusoma Biblia. Watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao katika mambo ya kiroho au maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k. Wengine walizoea kupokea zawadi za wanavijiji wakaelekea maisha ya kuombaomba.
Wamonaki wa kwanza walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana. Antoni wa Misri alikuwa mmojawao, naye akaona umuhimu wa kuweka utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake.
Mwanafunzi wake Pakomi aliendeleza mkazo wake akawaunganisha wamonaki mahali pamoja akawapa utaratibu wa kazi na sala. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1. Useja mtakatifu: atachagua maisha bila ndoa; badala yake kujiunga na shirika la wenzake kama familia ya kiroho. 2. Ufukara: ataacha mali yake ya binafsi na hatatafuta tena utajiri wa kidunia. 3. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo aliyechaguliwa kati yao (huitwa "Abba/Abati") na kutii taratibu za ushirika wake.
Utaratibu huo wa umonaki ulienea haraka: watawa wakaanza kukaa na kufanya kazi pamoja ili kujipatia mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu ambapo sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k.
Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile maisha ya kimya katika sala au huduma za upendo: hospitali, nyumba za mayatima, ufundishaji, uinjilishaji, misheni, au n.k. Hivyo mtawa anaweza kuwa na maisha ya kutotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya Wakristo na wasio Wakristo akiwatolea huduma zake.
Wamisionari Wamisri katika mabara matatu
haririPanteno wa Chuo cha Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri walianzisha Kanisa katika Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia za leo.
Hata sehemu mbalimbali za Ulaya zinakumbuka wamisionari kutoka Afrika waliohubiri huko Injili wakati wa Dola la Roma. Askari Wamisri katika jeshi la Roma walikaa miaka mingi Uswisi na kwingineko. Kati yao kulikuwa na Wakristo waliohubiri huko Injili kwa mara ya kwanza. Mji wa Zurich mpaka leo hii unaonyesha katika nembo yake majina ya Wamisri watatu waliokuwa wainjilisti wa kwanza wa eneo lake.
Kule Ireland Wamisri waliunda monasteri mnamo mwaka 500 na kufundisha Injili. Waireland wanafunzi wa Waafrika hao ndio wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi baadaye.
Perpetua na Felista
haririMnamo mwaka 203 B.K. aliishi mama kijana mwenye miaka 22 kwa jina Perpetua katika mji mkubwa wa Karthago. Perpetua alitokea familia tajiri na kuwa na mtoto wa kiume. Wazazi wake walikuwa wanaheshimiwa sana.
Kumbe Perpetua akashtakiwa kuwa Mkristo akakamatwa. Baba akamwendea mkuu wa mkoa wakapatana Perpetua atoe sadaka mbele ya sanamu ya Kaisari ili shtaka lifutwe. Kutoa sadaka maana yake ilikuwa kushika nafaka kidogo na kuitupa kwenye karai ya mkaa uliowaka mbele ya sanamu. Baba akamweleza mtoto wake gerezani alivyopatana na mkuu wa mkoa. Perpetua akakataa. Baba akamsihi akamwomba asilete aibu juu ya wazazi wake na amhurumie mtoto wake mdogo. Perpetua akamjibu baba ya kuwa tendo hilo halipatani na imani yake.
Felista alikuwa msichana Mkristo na wanawake hao wawili walikuwa marafiki ingawa Felista alikuwa mtumwa. Akafungwa pamoja na Perpetua na vijana watatu. Walipokataa kutoa sadaka wakapewa wote adhabu ya kifo.
Hao vijana Wakristo watano wakapelekwa katika uwanja wa michezo wa Karthago. Watu wengi wakatazama. Kuua wakosaji kulikuwa kama mchezo au burudani kwa wakazi wa miji. Walizoea kutazama maonyesho ya kuua wakosaji wenye hukumu ya mauti. Vijana Wakristo waliposimama uwanjani milango ya chini ikafunguliwa. Wanyamapori wakali waliokuwa wanahifadhiwa katika vyumba vya chini katika uwanja huo, wakiwekwa tayari ili kuwararua Wakristo wakatokea. Kuwatupa Wakristo mbele ya wanyama wakali ilifanywa kama onyesho la kuburudisha halaiki. Hao vijana wakashambuliwa na wanyama; wengine wakawaua na wengine wakajeruhiwa vibaya. Mwishoni wote waliojeruhiwa waliuawa kwa upanga.
Maonyesho hayo yalikusudiwa kutisha watu waogope kuwa Wakristo. Lakini yakageuka kampeni kwa ajili ya Ukristo, kwa sababu watazamaji walianza kujiuliza: Je, watu hao wana kosa gani? Ni imani gani inayowapa nguvu ya kusimama mbele ya wanyama mwitu na kuuawa badala ya kutoa sadaka mbele ya sanamu? Kwa nini wale wanaokufa hivyo wanajulikana kuwa watu wasioiba wala kusema uongo, lakini wengine wenye tabia mbaya hawana matatizo wakitoa sadaka tu mbele ya sanamu? Kumbe damu ya mashahidi ilikuwa mbegu ya kukua kwa Kanisa.
Wakati Roma ilipotawala Wakristo wengi Waafrika walionyesha uhodari kwa kutokana imani yao na kufa kama mashahidi wa Yesu. Mfano huo ulisababisha Wapagani wengi kuwa Wakristo. Lakini si wote walisimama imara mbele ya vitisho. Wengi wakatoa sadaka mbele ya sanamu wakatubu baadaye na kuomba wasamehewe udhaifu huo. Wengine waliwahonga maafisa wa serikali wakanunua vyeti vilivyothibitisha ya kwamba walitoa sadaka zile ingawa haikuwa kweli. Katika eneo la Karthago jambo hili lilisababisha farakano ndani ya Kanisa lililoitwa kwa jina la askofu Donato Mkuu.
Augustino
haririAugustino (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354 – Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.
Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5.
Katika historia yote Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.
Kati ya mababu wa Kanisa, ndiye aliyetuachia maandishi mengi zaidi, kuanzia yale maarufu sana yanayoitwa "Maungamo", kwa kuwa humo miaka 397-400 aliungama sifa za Mungu na ukosefu wake mwenyewe kwa kusimulia alivyoishi hadi miaka ya kwanza baada ya kuongoka.
Kila wakati ulifurahia zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika kujichunguza na kutoa siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.
Uzingatifu wake wa fumbo la nafsi yake ambamo fumbo la Mungu limefichama, ni mzuri ajabu kiasi cha kubaki hata leo kilele cha kujitafiti kiroho. Aliandika: “Usiende nje, rudi ndani mwako; ukweli unakaa katika utu wa ndani; na ukiona umbile lako ni geugeu, panda juu yako. Lakini kumbuka, unapopanda juu yako, unapanda juu ya roho inayofikiri. Basi, ufikie pale mwanga wa akili unapowaka”. Tena: “Naona ni lazima wanadamu warudishiwe tumaini la kupata ukweli”.
Posidi, mtu wa kwanza kuandika habari za maisha ya Augustino (kwa Kilatini, “Vita Augustini”), alisema “waamini wanamkuta daima hai” katika vitabu vyake. Kweli havionyeshi imepita miaka 1600 tangu viandikwe: humo anaonekana kama rafiki yetu wa wakati huu anayesema nasi kwa imani isiyozeeka.
Augustino mwenyewe aliviorodhesha 1,030, ambavyo si vyote.
Kazi yake kubwa haikuwa kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali na kutoa majibu yaliyo muhimu mpaka leo.
Akilinganisha imani na akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu (Ukweli mkuu na Upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wa Mungu). Huyo katika roho yake isiyokufa, bado ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu, ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.
Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya mapokeo na kuathiri Kanisa lote la Magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi). Kitabu muhimu zaidi kuhusu Utatu (kwa Kilatini kinaitwa “De Trinitate”) alikiandika miaka 399-420. Kilichukua muda mrefu kwa kuwa alisimamisha uandishi wake miaka minane “kwa sababu ni kigumu mno na nadhani wachache tu wanaweza kukielewa; basi kuna haraka zaidi ya kuwa na vitabu vingine tunavyotumaini vitafaidisha wengi”.
Hivyo alielekeza nguvu zake kutunga vitabu vya katekesi kwa wasio na elimu (hasa “De Catechizandis Rudibus”). Akijibu hoja za Wadonati, ambao walitaka Kanisa la Kiafrika na kuchukia mambo ya Kilatini, alikubali kurahisisha lugha hata kufanya makosa ya kisarufi kusudi wamuelewe zaidi akifafanua umoja wa Kanisa ulivyo muhimu kwa mahusiano na Mungu na kwa amani duniani.
Hasa hotuba zake, zilizoandikwa na wengine wakati alipokuwa anazitoa kwa watu akiongea nao kirahisi, zimechangia kueneza ujumbe wake. Tunazo bado karibu 600, lakini zilikuwa zaidi ya 3,000.
Pia alifafanua upya imani kuhusu umwilisho wa Mwana wa Mungu, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451): uwepo wa hali mbili (ya Kimungu na ya kibinadamu) katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”.
Ukristo kuenea Sudan hadi Ethiopia
haririJangwa kubwa la Sahara lilifanya mawasiliano yote kati ya Afrika Kaskazini na sehemu nyingine za bara kuwa magumu. Lakini tangu zamani mto Nile ulisaidia biashara na athari za kiutamaduni na za kisiasa kuvuka kanda la jangwa. Hivyo upo uhusiano wa pekee kati ya Misri na eneo linaloitwa leo "Sudan" (pamoja na Ethiopia na Eritrea).
Zamani nchi hiyo kusini kwa Misri iliitwa kwa jumla "Nubia"; sehemu moja ilijulikana kwa miaka mingi kwa jina la "Kushi". Mdo 8 inaonyesha kwamba safari kati ya Kushi (Sudan) na Misri mpaka Yerusalemu zilikuwa kawaida. Njiani Filipo alimbatiza "towashi wa Kushi" yaani afisa wa serikali ya malkia Kandake wa Kushi katika mji mkuu wa Meroe (Agano Jipya tafsiri ya Kiswahili cha Kisasa linatumia hapa kwa kosa jina la "Ethiopia"). Lakini hatuna habari zaidi kama huyo afisa alihubiri Injili kwao.
Kuanzia karne ya 3 athari za Ukristo katika Nubia zinajulikana. Wamonaki Wamisri walihubiri Injili huko. Kuanzia mwaka 600 wakazi wengi wa Kushi walikuwa Wakristo. Makanisa mengi tena makubwa yalijengwa na kupambwa katika miji mikubwa kama Dongola na Soba. Kwa miaka elfu moja utamaduni wa Kikristo uliendelea. Kutoka Dongola wamisionari walifika kusini mwa Sahara mpaka eneo la Tibesti (yaani Chad ya leo) ambapo maghofu yanaonyesha alama za Ukristo kule.
Kusini-Mashariki kwa Kushi tunakuta eneo kubwa lenye milima mirefu inayosimama kama mnara katika tambarare ya nchi jirani. Ni nyanda za juu za Ethiopia au Uhabeshi. Mnamo mwaka 300 B.K. kulikuwa na ufalme katika eneo la Aksum (Ethiopia ya leo) na Ukristo ulikuwa umeshafika kupitia wafanyabiashara wa Bahari ya Shamu.
Wakati alipotawala Kaisari Konstantino kule Roma, meli moja ilikuwa safarini kutoka Shamu kwenda Bara Hindi ikaharibika kwenye pwani ya Ethiopia. Vijana wawili waliokolewa wakapelekwa mbele ya mfalme kule Aksum. Mmojawao kwa jina Frumensyo alipata haraka sifa za kuwa mwenye elimu na hekima. Akapanda ngazi kuwa mshauri wa mfalme na mwalimu wa mwana wa mfalme aliyeitwa Ezana. Frumensyo aliweza kupanda mbegu za imani moyoni mwa kijana huyo. Baada ya kuwa mfalme, Ezana akaendelea kumtumia Frumensyo kama mshauri wake.
Siku moja Frumensyo aliomba ruhusa ya mfalme aende nyumbani kuangalia kama wazazi wake bado wanaishi. Mfalme akamruhusu akamwomba atafute kule walimu wanaoweza kufundisha elimu aliyokuwa nayo Frumensyo pamoja na imani ya Kikristo. Frumensyo akamwendea Askofu Mkuu wa Misri aliyemweka wakfu kuwa askofu kwa ajili ya Waethiopia. Hivyo Kanisa lilipata sakramenti ya daraja takatifu katika nyanda za juu za Ethiopia. Baadaye mfalme Ezana akabatizwa akifuatwa na watu wengi wa makao makuu.
Baadaye tena kule Ethiopia walifika wamonaki kutoka Misri na Shamu. Ndio walioanza kufundisha na kuwabatiza Wahabeshi wengi. Ndio mwanzo wa taifa la Kikristo la Ethiopia. Wahabeshi wametunza urithi wao wa Kikristo mpaka leo. Ukristo wao unafuata mapokeo ya Waorthodoksi wa Mashariki yalivyo hata Misri. Mpaka karne ya 20 walipokea Maaskofu wao wote kutoka Kanisa la Kikopti la Misri.
Mabadiliko katika karne ya 7: kuja kwa Uislamu
haririLabda tumeshangaa kusikia ya kwamba leo hii wako Wakristo milioni kadhaa kule Misri, kwa sababu tumesikia mara kwa mara ya kwamba wenyeji wa Misri ni Waarabu na Waislamu. Kumbe katika karne saba za kwanza baada ya Kristo hali ilikuwa tofauti. Afrika Kaskazini ilikuwa nchi ya Wakristo, lakini baadaye yalitokea mageuzi makubwa yaliyokuwa muhimu sana katika historia ya Afrika: uenezi wa Uislamu.
Mnamo mwaka 610 B.K. sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini iliunganika tena chini ya Dola la Roma lililotawaliwa kutoka mji wa Bizanti (Roma ya mashariki). Lakini utawala huo ulikuwa hafifu kulingana na zamani za Roma ya Kale.
Wenyeji wa Misri na mkoa wa "Afrika" (= Tunisia ya leo) walipinga utawala wa Bizanti. Wakristo wengi katika nchi hizo walikataa usimamizi wa Askofu Mkuu wa Bizanti wakiwafuata viongozi wao wa kitaifa. Viongozi wa Kanisa la Kikopti (Misri) waliteswa na serikali ya Bizanti. Dola la Roma ya Mashariki ilichosha nguvu zake vitani dhidi ya majirani yao wa Uajemi na makabila yasiyostaarabika kutoka kaskazini.
Hali hii ilibadilika ghafla mwaka 640 B.K. Habari za imani mpya kati ya Waarabu zilisikika tangu mwaka 622 kutoka eneo la Maka na Madina. Kiongozi mpya aliyeitwa Muhamad aliunganisha makabila yote ya Waarabu katika jina la Mungu mmoja, "Allah".
Baada ya kifo cha Muhamad wafuasi wake walitoka nje ya jangwa la Uarabuni na kushambulia maeneo jirani ya Bizanti na Uajemi. Walipigana na majeshi ya nchi hizo na kuyashinda. Mwaka 640 waliingia Misri. Baadhi ya wenyeji Wakopti waliwapokea kwa matumaini ya kuwa watamaliza utawala wa Bizanti. Jeshi la Bizanti lilishindwa kwa kukosa msaada wa wazalendo. Kiongozi Mwislamu aliahidi madhehebu yote yataheshimiwa. Alifanya mkataba na Wakristo waendelee na ibada zao na desturi zao.
Lakini baada ya muda Wamisri waliona ya kwamba wamekuwa watu wa ngazi ya chini nchi mwao. Mabwana wapya walianza kubadilisha utamaduni wa nchi. Aliyejiunga na Uislamu na kujifunza Kiarabu alikubalika lakini Wakristo wenyeji waliotunza urithi wao walibaguliwa. Majaribio yote ya kupigania uhuru yaligandamizwa vikali.
Miaka mia iliyofuata Waislamu waliteka sehemu iliyobaki ya Afrika Kaskazini. Miaka 670/696 waliteka mkoa wa "Afrika" ya Kiroma pamoja na Karthago (Tunisia ya leo). Mwaka 711 wakavuka mlangobahari na kuingia Hispania (Ulaya Kusini). Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na wenyeji mwaka 732 lakini walitawala sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata.
Kule Tunisia na Algeria Ukristo ulikuwa dhaifu kutokana na mafarakano mengi ya miaka ya nyuma na dhuluma za Wavandali. Baada ya karne za kulaumiana kati ya Wakristo, wengine walikuwa na wasiwasi juu ya ukweli wa mafundisho ya Kanisa. Katika nchi za jirani (Italia na Hispania) vita vikali vilipigwa kati ya Waarabu walioshambulia na Wakristo waliojitetea. Labda hali hiyo iliongeza moyo wa Waislamu kutovumilia kuwepo kwa Wakristo. Kanisa katika Afrika Kaskazini lilipotea baada ya karne chache.
Sababu za Wakristo wengi kugeuka Waislamu
haririWafuasi wa Muhammad walishambulia maeneo jirani ya Waroma wa Bizanti hasa Afrika Kaskazini. Uislamu ulienea haraka sana kwa nguvu ya kijeshi katika nchi zilizokuwa na Wakristo wengi.
Sababu kubwa ya udhaifu wa Wakristo Waorthodoksi ilikuwa mafarakano kati yao, na hasa majaribio ya serikali ya Bizanti kuwalazimisha Wakristo wote kufuata uongozi wake, wakiitumia na kuitawala dini kama nguzo ya siasa yake. Lakini mambo ya imani hayafai kulazimishwa.
Hivyo katika nchi kama Misri Wakristo waliotafuta uhuru wa kisiasa walilazimishwa kuwa chini ya Askofu wa Bizanti, wakajisikia wanagandamizwa kidini pia, si kisiasa tu. Waarabu Waislamu walipofika walikaribishwa mahali pengine kama wakombozi wanaomaliza utawala wa kidikteta. Waliwaahidi vikundi vyote vya Wakristo uhuru wa dini. Ahadi hiyo ilitimizwa kwa namna tofauti.
Utawala wa Kiislamu ulifikia nchi hizo kwa njia ya vita. Mwanzoni walikuwa Waarabu kadhaa tu: walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Walifundishwa kwamba ikiwa watakufa vitani watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.
Chini ya utawala wa Waarabu Waislamu, wenyeji waliruhusiwa kuendelea na desturi zao lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walijiona wanabaguliwa mbele ya Waislamu. Walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani.
Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.
Masharti ya kujiunga na Uislamu yalikuwa rahisi sana. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haikuwezekana kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu iliruhusu Mkristo kugeuka Mwislamu lakini ilikataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.
Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea.
Lakini mara kwa mara upande wa watawala na wakubwa yalijitokeza matendo mabaya, kama makanisa kubomolewa au kugeuzwa misikiti, n.k. Kwa mfano msikiti mkuu wa Dameski (Siria) ulikuwa zamani Kanisa la Mt. Yohane Mbatizaji. Mwanzoni Waarabu waliahidi kuliheshimu, lakini mtawala aliyefuata alitaka jengo kubwa lililopatikana mjini kwa ajili ya ibada yake. Ndivyo ilivyotokea Waturuki walipoteka Konstantinopoli. Kanisa Kuu la Hagia Sofia (Hekima Mtakatifu) liligeuka msikiti.
Vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi, Wafuasi wa dini ya Uajemi n.k.). Lakini Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali.
Hasa vipindi vya vita kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu kwa Wakristo chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa, n.k.
Kwa ujumla majaribio ya vita vya msalaba ya kuikomboa nchi takatifu yalishindikana. Pamoja na hayo vita hivyo vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu. Ilibidi walipe madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.
Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengine Wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso.
Maisha yao yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea na ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza). Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao.
Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Tena Wakristo walianza kuhamia nchi ambako watakuwa raia huru bila kasoro.
Mazingira ya uenezi mpya
haririTangu kuja kwa Uislamu uenezaji wa Injili katika Afrika ulikwama na kurudi nyuma. Kusini mwa Sahara ilifika kupitia Nubia lakini baada ya Nubia kuwa ndani ya eneo la Kiislamu athari hii haikuendelea.
Karne za 15 na 16 zilikuwa muhimu katika historia ya Ukristo. Anguko la Bizanti mwaka 1453 lilisababisha wataalamu wengi wa mashariki kukimbilia Ulaya Magharibi wakileta vitabu vyao. Elimu ilisonga mbele. Hasa mijini shule ziliundwa. Mawazo mapya yalienea duniani.
Mjerumani kwa jina Gutenberg alitengeneza mashine ya kwanza ya kupiga chapa vitabu. Hivyo vitabu vilianza kupatikana kwa urahisi. Habari zikazunguka haraka kati ya nchi na nchi, hali isiyojulikana karne nyingi tangu anguko la Dola la Roma.
Wataalamu walianza kusoma tena vitabu vya Wagiriki na Waroma wa kale. Wakaanza kusambaza tena mafundisho ya kale kuwa dunia si tambarare lakini mviringo kama chungwa.
Hapo alijitokeza nahodha Mwitalia kwa jina Kristoforo Kolombo aliyetaka kujaribisha mafundisho haya mapya. Ikiwa dunia kweli ina umbo la chungwa inawezekana kuelekea magharibi kutoka Hispania na kufika mashariki katika Bara Hindi. Kwa njia hiyo inawezekana kufanya biashara moja kwa moja na nchi tajiri za mashariki bila kuwapa faida wafanyabiashara Waarabu. Mfalme wa Hispania akampa Kolombo fedha za kuandaa meli tatu.
Mwaka 1492 Kolombo akaondoka Hispania akakuta bara jipya magharibi lililoitwa baadaye Amerika. (Mwenyewe alifikiri amefika Bara Hindi, hivyo akawaita wenyeji "Wahindi" na visiwa alipofika mwanzoni mpaka leo huitwa "West Indies" = India ya Magharibi). Wahispania walipora utajiri wa mataifa ya Amerika yaliyokosa silaha za kushindana nao. Utajiri huu mpya ulisaidia maendeleo ya Ulaya kupita yale ya mataifa ya Waislamu na ya Asia.
Miaka michache baadaye, huku Urekebisho wa Kikatoliki ukiendelea, yalitokea Matengenezo ya Kiprotestanti yaliyogawa moja kwa moja Kanisa la Magharibi katika madhehebu mengi ajabu.
Wakati huohuo ulikuwa pia kipindi kilicholeta habari za nchi mpya kwa watu wa Ulaya. Mataifa ya Wahispania na Wareno yalijenga aina mpya za meli zilizoweza kusafiri kote duniani hata kuvuka bahari kubwa. Wafanyabiashara na wanajeshi wao walizunguka pande zote za dunia wakiambatana na mapadri wao. Hao walikutana na wenyeji wengi wa nchi mbalimbali wasio Wakristo, au walikuwa Wakristo lakini si washiriki wa Kanisa Katoliki (kama Waethiopia au Wahindi wa Kusini). Wakaanza kuwaeleza imani, wakahubiri mbele ya Mfalme wa China, mbele ya Negus Negesti wa Ethiopia na mbele ya watawala wa Amerika Kusini. Tatizo la misheni hizo lilikuwa kwamba liliambatana na uenezaji wa kijeshi wa Hispania na Ureno.
Ukristo ulivyoendelea
haririMnamo mwaka 1500 Ukristo ulikuwa umeshapotea Afrika Kaskazini-Magharibi. Huko Wakristo pekee walikuwa watumwa kutoka Ulaya. Waarabu wa kule walikuwa wameshindwa vitani Hispania, hivyo wakimbizi wao kutoka huko hawakuwa na moyo wa kustahimili Wakristo kati yao.
Kumbe Misri Ukristo uliendelea. Wakristo Wakopti walikwisha kuathiriwa na utamaduni wa Kiarabu, lakini waliendelea kuimba kwa lugha ya Kikopti (Kimisri cha kale) katika ibada zao. Katika miji mikubwa ya Kairo na Aleksandria, vilevile katika vijiji vya Misri Kusini, Wakristo walikuwa wengi kidogo. Hasa Aleksandria tangu karne nyingi waliishi pia Wagiriki Wakristo.
Nubia ni jina la kale la Sudan. Tangu karne ya 6 wafalme wa Nubia walikuwa Wakristo. Mmisionari mkuu alikuwa Juliano wa Aleksandria aliyefika Nubia mwaka 546. Baada ya Uislamu kuingia Misri, Wakristo wa Nubia walijitetea kwa silaha. Lakini polepole Waarabu wahamiaji wakaelekea kusini.
Baada ya mwaka 1200 vita vikatokea tena na tena kati ya Waarabu Waislamu na Wanubia Wakristo. Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa sababu ya majaribio ya jeshi la msalaba toka Ulaya ya kuteka Palestina. Mtawala Mwislamu wa Misri, kwa jina Salah ed Din, akalipa kisasi akishambulia madola ya Wakristo kusini kwa Misri. Mji mkuu wa Nubia ulikuwa Alodia (karibu na Khartoum ya leo).
Mwaka 1504 jeshi la Waarabu iliuteka. Kutokana na historia hii ya vita vikali watawala wapya hawakuonyesha ustahimilivu kwa Wakristo wa Nubia ulivyokuwa kule Misri. Ukristo ulianza kugandamizwa katika eneo hilo hadi kukoma. Leo tunaweza kuona magofu tu ya makanisa ya kale chini ya mchanga wa jangwa la Sudan.
Kuenea kwa Uislamu katika Nubia na Pembe la Afrika kulifanya mawasiliano ya Ethiopia na nchi za nje kuwa magumu. Taifa hilo la Kikristo lilijikuta kama kisiwa katika bahari ya Kiislamu.
Mawasiliano na Misri yaliendelea kwa shida. Kanisa la Ethiopia lilikuwa limekubali usimamizi wa kiroho wa Askofu mkuu wa Aleksandria. Lakini, kama kawaida katika mapokeo ya Kiorthodoksi, lilikuwa chini ya usimamizi wa kisiasa wa Negus Negesti (Mfalme wa Ethiopia).
Tangu mwaka 1400 Manegus wakatambua kwamba msaada wa mataifa mengine ya Wakristo haupatikani mpaka Ulaya. Wakatuma wasafiri waliopeleka barua kwa watawala mbalimbali wa Ulaya, hasa mfalme wa Hispania na Papa wa Roma (mwaka 1424 na 1441). Negus (Mfalme) Zara Yakubu akatuma ujumbe Italia kwa Papa akajaribu kujenga umoja wa Kanisa ila haukutekelezwa kwa sababu tu ya ukosefu wa mawasiliano. Safari kati ya Ulaya na Ethiopia kupitia maeneo ya nchi za Waislamu ilikuwa jambo la kubahatisha.
Mwaka 1493 mjumbe wa mfalme wa Ureno alifika katika mji mkuu wa Lalibela (karibu na ziwa Tana). Ziara hiyo ilianzisha kipindi cha mawasiliano kati ya Ureno na Ethiopia.
Mwanzoni Wareno walisaidia Ethiopia kujitetea dhidi ya mashambulio ya Waarabu wa pwani. Waarabu walisaidiana na askari Waturuki walioleta bunduki kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo. Walipoanza kushinda, msaada wa Wareno ulifika na Wahabeshi walipata pia bunduki. Mwaka 1543 Wahabeshi na wasaidizi wao Wareno wakawashinda Waarabu na Waturuki katika mapingano ya ziwa Tana.
Kipindi kilichofuata kilileta uhusiano mgumu. Wajumbe Wareno wakaendelea kufika. Mapadri wa Shirika la Yesu wakaanza kuhubiri na kufundisha vijana. Wafalme wawili wakajiunga na Kanisa Katoliki.
Lakini majaribio ya kuunganisha Ukristo wa Ethiopia na Kanisa la Roma yalisababisha ghasia za wananchi. Mapadri kutoka Ulaya waliona wasiwasi: hawakuelewa desturi nyingi za Kanisa la Uhabeshi. Ukristo wake ulionyesha uso uliolingana na utamaduni wa Kiafrika: katika Misa ngoma hupigwa, makasisi huchezacheza kiibada, wavulana hutahiriwa kama desturi ya kanisa.
Kumbe Wajesuiti waliyaona mambo haya kama ni ya Kipagani. Wakamshawishi Negus Sussenyos aliyekubali Ukatoliki "kutakasa" Kanisa, yaani kukataza desturi mbalimbali na kusoma Misa kwa kufuata Liturujia ya Roma. Ghasia zilifuata. Mwaka 1632 Negus Susneyos akajiuzulu. Wajesuiti wakafukuzwa. Wahabeshi Wakatoliki wakalazimishwa kurudi katika Ukopti.
Hivyo kuingia kwa wageni kulisaidia kutetea taifa lakini kulileta vurugu ya ndani. Nafasi ya kuelewana tena haikupatikana kwa sababu Wareno walifukuzwa miaka ileile kwenye pwani za Uswahilini na Uarabuni. Ethiopia ikawa tena kama kisiwa cha Kikristo katika bahari ya Uislamu.
Uinjilishaji chini ya Wareno
haririUreno ni nchi ndogo jirani na Hispania. Kwa karne nyingi Wakatoliki wa nchi hizo mbili walishindana na Waarabu waliotawala sehemu ya rasi hiyo. Mwaka 1492 Waarabu wa mwisho wakatoka katika Hispania.
Mabaharia Wareno wakaanza kufuata pwani za Afrika Magharibi kuelekea kusini. Elimu mpya iliwasaidia. Mnamo mwaka 1450 vitabu vya kwanza vilikuja kupatikana vikieleza uhusiano kati ya nyota, majira ya mwaka na jiografia. Pamoja na chombo kipya cha "compass" vikawawezesha mabaharia kupiga hesabu juu ya safari zao baharini wakipima nyota hata bila kuona pwani.
Mwaka 1497 nahodha Vasco da Gama akazunguka Afrika Kusini akatembelea bandari za Uswahilini na kufika Bara Hindi. Katika bandari za Kilwa, Zanzibar na Mombasa Wareno wakashangaa kukutana tena na Waarabu Waislamu waliozoea kuwa maadui wao tangu karne nyingi nyumbani kwao.
Shabaha ya safari za Wareno ilikuwa biashara na Bara Hindi. Kwa kutumia elimu mpya ya jiografia wakaona kwamba inawezekana kuchukua bidhaa za mashariki kwa njia ya bahari badala ya kutegemea biashara mikononi mwa Waarabu kupitia Mashariki ya Kati. Lengo lingine lilikuwa kufikia Ethiopia ili kuungana na mfalme wake Mkristo dhidi ya Waislamu.
Katika njia hiyo walihitaji vituo kwa ajili ya meli zao katika pwani za Afrika. Huko walikutana na jamii za wenyeji. Hivyo walitumia nafasi ya kufanya biashara na Waafrika wa pwani.
Katika Afrika Mashariki na eneo la mto Kongo (Kongo/Angola) walijaribu kuunda vituo vya biashara. Wamisionari walitumia nafasi hizo kuhubiri Injili.
Afrika Magharibi walikutana na watu walioishi chini ya watawala wenye nguvu. Kwa jumla wamisionari walijaribu kuwasiliana na viongozi hao ili kuwaongoa kwa kutumaini watu wa kawaida watafuata.
Benin ilikuwa kitovu cha maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kisanii tangu mwaka 900 B.K. Mwaka 1486 Mreno d`Aveira alimtembelea Mfalme wa Benin mara ya kwanza. Wakati wa Mfalme Esigie wamisionari wakaruhusiwa kuingia na kuanza kazi. Mfalme Orhogbua alikuwa Mkristo mnamo mwaka 1550. Lakini chini ya waandamizi wake maendeleo ya Ukristo yalikwama na kuisha.
Mifano ya aina hiyo inapatikana vilevile Gambia, Sierra Leone na Ghana.
Mambo yalikwenda vizuri zaidi Kongo, kusini mwa mdomo wa mto huo. Tangu karne ya 14 Mfalme kwa cheo cha Manikongo alitawala nchi. Wakati wa Mfalme Nzinga Nkuwu Wareno wa kwanza walifika na kujenga ubalozi.
Baada ya kusikia mahubiri ya wamisionari Mfalme akabatizwa akipokea jina la Yohane; mji mkuu ukapewa jina la "San Salvador" (=Mtakatifu Mwokozi). Wakati wa mwanae, Mfalme Afonso I (1508-1545) Kanisa lilikua sana.
Mtoto wake akasoma teolojia kule Lisbon. Akasafiri Roma alipowekwa wakfu na Papa Leo X akiwa na umri wa miaka 26 akarudi kama askofu wa kwanza Mwafrika kusini kwa Sahara, akiongoza na mapadri wapya 4, ila alifariki miaka tisa baadaye. Baba yake aliendelea kufanya bidii za kuimarisha Kanisa, ila alikosa wamisionari au alileta mapadri wasiofaa.
Tena, pamoja na wamisionari Wareno waliingia pia wafanyabiashara ya watumwa. Wakati uleule wamisionari walipofundisha Injili na heshima ya binadamu kuwa kiumbe wa Mungu, wafanyabiashara wale walivunja amani nchini. Walichukua watumwa kutoka maeneo ya jirani lakini pia ndani ya Ufalme. Hivyo uhusiano kati ya serikali ya mfalme Mkristo wa Kongo na wageni Wakristo Wareno ulikuwa mbaya mpaka kupigana kwa silaha. Kwa jumla biashara ya utumwa ndiyo iliyoangusha ufalme huo wa Kikristo ambapo hata hivyo kwa kiasi fulani imani imeendelea moja kwa moja hadi leo.
Kutofanikiwa kwa majaribio hayo kulitokana naː
- a) matatizo ya wamisionari Wazungu katika hali ya hewa (iliyokuwa ngumu na hatari kwaoː kabla ya kupatikana kwa dawa ya "Kwinini" dhidi ya malaria Wazungu wengi katika nchi za joto walikufa shauri ya homa).
- b) Wamisionari Wakatoliki wa karne zile walifanya mara nyingi kosa la kutofundisha kiasi cha kutosha kabla ya kubatiza. Hivyo sehemu ya Wakristo wenyeji hawakuelewa imani mpya.
- c) Kisiasa pwani ya Afrika Magharibi ilikuwa katika hali ya fujo. Kutokana na biashara ya dhahabu na watumwa mataifa ya Ulaya yalishindana kati yao. Wareno, Wahispania, Wafaransa, Waingereza, Waholanzi, Waswidi, Wadeni na pia Wajerumani walipigana au walishirikiana pamoja dhidi ya watawala wazalendo juu ya biashara hiyo. Ili kuzuia ushindani huo, Wareno waliruhusu kwa nadra tu wamisionari kutoka nchi nyingine, na wa kwao walikuwa hawatoshi.
- d) Wakristo wachanga wa Afrika Magharibi ya Kati waliona kila siku mifano ya Wakristo wabaya. Wanajeshi na wafanyabiashara Wazungu mara nyingi hawakufurahia kupelekwa katika nchi zenye hatari kiafya na tofauti sana na mazingira ya nyumbani, wakaanguka katika ulevi na uasherati, hali iliyokuwa mbaya zaidi kutokana na uharibifu wa kiroho uliosababishwa na biashara ya watumwa mioyoni mwa mawakala wake.
Pamoja na hayo, katika karne ya 16 biashara ya watumwa ilianza kuongezeka. Wareno na Wahispania waliunda utawala wao kule Amerika. Walitafuta madini ya nchi hizo wakaanzisha mashamba makubwa.
Lakini wakaona ugumu wa kutumia Wahindi wekundu kama wafanyakazi. Watu hao waliishi miaka elfu kadhaa bila mawasiliano na watu wengine. Magonjwa yaliyokuwa ya kawaida Ulaya, Afrika na Asia (kwa sababu watu wa kule waliwahi kuambukizana tangu karne nyingi) yaliua wenyeji wengi wakiishi pamoja na Wazungu. Tena walowezi Wazungu walikuwa wakatili mno. Wahindi wekundu waliofanywa watumwa wakafa kwa mamilioni.
Hapo wazo jipya lilijitokeza: kuchukua watumwa kutoka Afrika ili wafanye kazi Amerika! Waliopendekeza wazo hili walisema Waafrika wana nguvu na afya kuliko wenyeji wa Amerika. Ndivyo ilivyotokea. Msingi wa maendeleo ya Ulaya uliwekwa kwa malighafi za Amerika zilizochimbwa na kulimwa na watumwa Waafrika.
Kwa karne tatu biashara ya watumwa ilikua na kuongezeka kwenye pwani za Afrika. Katika karne ya 16 Wareno walikuwa mstari wa mbele katika biashara hii ya aibu, halafu Waingereza wakashika nafasi ya kwanza kabisa wakawauza watumwa popote.
Ki-Zerbo, mtaalamu wa historia ya Afrika alisema: "Biashara ya watumwa ilifanya vita kuwa hali ya kudumu kati ya makabila. Vita vilikuwa vikali zaidi. Watawala wa madola ya pwani wakauza watumwa. Watumwa waliouzwa wakawawezesha kununua bunduki nyingi. Bunduki nyingi ziliwawezesha kukamata watumwa wengi zaidi. Watawala wa pwani waliingia katika mzunguko wa kishetani wakipigana vita kwa shabaha ya kupata wafungwa watakaouzwa kuwa watumwa. Watawala wakaanza kuwaangalia raia wao kuwa bidhaa tu zinazosaidia kujipatia yote wanayotamani".
Kumbe watu wakorofi hawakuwa tayari kuwatazama Wakristo wa Kongo tofauti na Waafrika wengine waliofaa machoni pao kuwa watumwa. Wafanyabiashara wale waliona mahubiri ya Injili kuwa kizuizi tu cha biashara yao.
Nia nzuri za Mfalme wa Ureno na vilevile wamisionari wenyewe hazikuwa na nguvu mbele ya uovu wa watu hao na pesa zao.
Mfalme Afonso alijitahidi sana kuwafukuza, lakini kufuatana na mkataba wake na Ureno alipaswa kuwarudisha Wareno ili waadhibiwe kwao. Kumbe walipokabidhiwa kwa maafisa Wareno kwenye vituo vya pwani ya Afrika walitumia hela zao kuwalipa mahakimu wawekwe huru tena. Mara nyingi walitumia mapato ya biashara yao kuwahonga hata maafisa wa mfalme wa Kongo waanze kumpinga.
Hivyo Ufalme wa Kongo ulidhoofishwa ukaingia katika kipindi kirefu cha vita vya ndani, dhidi ya majirani wake na hata dhidi ya Wareno. Mwishoni uchumi na utaratibu pamoja na Ukristo viliharibika, ingawa katika miaka 1640-1835 Wakapuchini 440 kutoka Dola la Papa walifanya kazi kubwa na kubatiza watu milioni mbili, bila kujihusisha na biashara yoyote: walifika na breviari tu, wakaondoka na breviari tu, wakiacha kumbukumbu ya watu waadilifu.
Ureno ulishindwa wakati uleule kujenga taifa la marafiki Wakristo kwa mkono mmoja na kuruhusu wafanyabiashara wake kuwafanya marafiki hao kuwa watumwa kwa mkono mwingine.
Kati ya miaka 1500 na 1800 wamisionari Wakatoliki walihubiri kwenye pwani ya Afrika Mashariki. Walifuata uenezi wa Wareno waliojaribu kutawala pwani hiyo kama vituo vya biashara kati ya Ulaya na Bara Hindi.
Kutoka kwa makao yao ya Sofala na Msumbiji walijaribu pia kutawala biashara ya dhahabu iliyochimbwa katika eneo la Mwene Mtapa (Zimbabwe).
Katika pwani za Uswahilini Wareno wakafika kuanzia mwaka 1505 wakitafuta njia ya Bara Hindi. Waislamu wa pwani hawakufurahia kupokea Wakristo. Vilevile hawakuvutwa na picha ya kwanza waliyoipata juu ya Wareno kwa ujumla. Viongozi Wareno waliwaangalia Waislamu wa Afrika moja kwa moja kuwa maadui kama Waislamu nyumbani kwao walipowahi kupigana nao karne nyingi.
Chini ya ulinzi wa kijeshi wa Ureno wamisionari wakaanza kazi yao. Mapadri wa Shirika la Yesu wakaingia ndani ya bara kuwahubiria wafuasi wa dini asilia za Kiafrika. Mashirika mengine yalijaribu kujenga vituo kama hospitali na kuwasaidia maskini. Kazi kati ya Waislamu iliendelea polepole. Lakini kisiwani Pemba na vilevile Mombasa mamia wakabatizwa na kuwa Wakristo.
Mwaka 1630 kijana kwa jina Jerome Chungulia akapokea cheo cha Mfalme wa Mombasa kwa msaada wa Wareno. Alikuwa mtoto wa Sultani Mwislamu. Wareno walimwua baba vitani na kumlea mwanaye. Baada ya masomo kule Goa (Bara Hindi) alirudi kama Mkristo.
Lakini mwaka 1631 alikumbuka jinsi Wareno walivyomuua baba yake akalipiza kisasi. Akajitangaza kuwa Mwislamu tena akawaongoza Waislamu wa Mombasa kuwaua Wareno mjini. Waswahili wote waliopokea Ukristo waliuawa pia. Hukumbukwa kama "Mashahidi wa Mombasa".
Mnamo mwaka 1560 mmisionari Mjesuiti kwa jina Gonsalo Da Silveira akafika Msumbiji akaendelea kuhubiri sehemu za ndani akafika Manica (mji mkuu wa Mwene Mtapa).
Baada ya kuhubiri kwa muda wa majuma matatu Mwene Mutapa (mfalme) alikuwa tayari kupokea ubatizo pamoja na wakubwa 300. Lakini washauri Waislamu wa Mwene wakamshtaki Da Silveira kuwa mpelelezi na mchawi. Mwene akageuka akamwua Da Silveira alipolala usingizi. Maiti yake ikatupwa mtoni.
Wamisionari wengine walifaulu tena kufika Zimbabwe mwaka 1570. Walijifunza lugha ya nchi, walihubiri na kujenga makanisa. Katika karne ya 17 wafalme wa Mwene Mtapa walikuwa mara nyingi Wakristo Wakatoliki. Watoto wa wakubwa walisomeshwa katika shule za misheni kule Tete (Msumbiji) au Goa.
Mwana wa Mwene Kapararidze kwa jina Miguel (Mikaeli) alichukua digrii ya Daktari wa Teolojia kule India mwaka 1670. Baadaye alihudumia kanisa la Mt. Barbara huko Goa na kufundisha kama Profesa wa seminari. Ndiye mtaalamu wa kwanza wa kisasa kutoka Zimbabwe.
Lakini maendeleo hayo yote yaliingiliana na siasa ya Ureno. Biashara ya dhahabu ilisababisha maafisa Wareno kuhujumu utawala wa Mwene Mtapa kwani walipendelea watawala wasio na nguvu waliowapa nafasi za kujitajirisha, wakapindua watawala waliojaribu kujenga hali ya kujitegemea.
Kumbe kati ya mashambulio ya makabila ya ndani (Rozwi, Zimba) na kuingiliwa na Wareno Ufalme wa Mwene Mtapa ulianguka kabisa. Ukristo ulitegemea mno nguvu ya kifalme ukaanguka pamoja na utawala wake.
Hivyo mizizi ya Kanisa Afrika ilikauka tena kwa sababu ya kuingiliana kwa hotuba ya Injili na siasa ya ukoloni. Udhaifu wa kibinadamu uliongezea ugumu wa mazingira na hali ya hewa kwa ajili ya wamisionari kutoka Ulaya.
Mwanzo wa umisionari wa Kiprotestanti
haririUenezaji wa tatu wa Ukristo katika Afrika ulianzishwa na Wakristo kutoka nchi za Ulaya zilizoendelea kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mapinduzi ya viwandani yaliongeza sana uwezo wa kiuchumi wa mataifa hayo.
Biashara ya kimataifa ilianza kuunganisha nchi za mbali sana. Vyombo vya usafiri kama vile meli, reli na baadaye hata ndege vilifikisha watu na bidhaa kila sehemu za dunia. Watu walianza kupata habari za nchi zisizojulikana kwao mpaka wakati ule.
Wakristo wa nchi za Ulaya walitumia mawasiliano hayo. Labda tunaweza kulinganisha hali hiyo na sera za mitume ambao walitumia njia zilizofunguliwa na biashara ya Kiroma katika karne za kwanza. Wengine waliona uwezo wao kama wito wa Mungu kwa Wakristo wa Ulaya katika karne ile hasa.
Mahali pengi Ulaya Wakristo hawakuridhika tena na hali ya Kanisa. Ukristo ulikwisha kuwa sehemu ya utamaduni na jambo la kawaida. Bila kutafakari sana, mtoto alibatizwa, akafundishwa na kupewa Kipaimara, akafunga ndoa kanisani, akawabatiza watoto wake halafu akazikwa kwa ibada.
Hasa katika nchi za Kiprotestanti Kanisa lilikuwa kama idara ya serikali iliyosaidia taifa kuweka utaratibu wa kidini kwa manufaa ya maadili ya umma. Serikali zilihimiza watu washiriki na kuhudhuria ibada. Wasipofika kanisani waliweza kutozwa faini.
Lakini mazingira na hali ya maisha vilibadilika. Watu walianza kuhamia mijini, jumuiya za vijiji zilianza kulegea na kuvunjika. Mahali pengi watumishi wa makanisa hawakujua kujibu maswali mapya ila tu kukumbusha mazoea ya kale na mila nzuri za zamani.
Ndiyo asili ya matapo ya uamsho iliyotokea kwa nguvu sana. Wasioridhika na hali hiyo walikutana nje ya makanisa. Katika maeneo ya Kiprotestanti hali ilitegemea. Penye uongozi wenye busara walipewa nafasi zao shirikani. Watu waliguswa upya na neno la Mungu na Roho wake, walitafuta njia mpya za kuishi na kuonyesha imani yao. Hivyo vilijitokeza vyama vya kusaidia wagonjwa, wajane, mayatima na maskini.
Kumbe penye uongozi mkali uliokataa njia na mbinu mpya Wakristo walikutana na kusali katika nyumba za watu. Wengine walianzisha jumuiya na madhehebu ya pekee. Lakini sehemu kubwa ya Wakristo wa uamsho walielewa kazi yao ya kutengenezwa upya makanisa yao badala ya kuunda vikanisa vipya.
Katika maeneo ya Wakatoliki matapo yaliyofanana na uamsho yalisababisha mara nyingi kutokea kwa shirika jipya la watawa au la walei. Muundo wa Kanisa Katoliki unasaidia kuwapa watu wenye wito au vipawa vya pekee nafasi zao katika mashirika hayo.
Sababu mojawapo ya kuangalia upya Afrika ilikuwa habari za biashara ya watumwa zilizopatikana sasa kwa watu wengi. Katika karne ya 18 na 19 mamilioni ya Waafrika walichukuliwa kama watumwa na kupelekwa hasa Amerika.
Makanisa makubwa yalinyamaza au kufumba macho mbele ya maovu hayo. Wakristo wa madhehebu madogo ya Kiprotestanti katika Uingereza (kama "Makweka" au "Marafiki" na Wamethodisti, baadaye pia sehemu ya wafuasi wa makanisa makubwa) ndio walioanza kupinga utumwa. Walifaulu kupata hukumu ya mahakama iliyosema si halali kuwa na watumwa nchini Uingereza. Lakini bado utumwa uliendelea katika makoloni.
Wakristo walimtumia Mbunge Wilberforce pamoja na wahubiri kanisani kukaza kampeni kote nchini. Mwaka 1807 walifaulu kupata sheria bungeni iliyopiga marufuku biashara ya watumwa kwa Waingereza na katika makoloni ya Uingereza (lakini watumwa waliokuwepo walibaki hivihivi).
Waliendelea kudai matumizi ya meli za kijeshi za Uingereza dhidi ya biashara ya mataifa mengine kama vile Wafaransa, Wareno na Waarabu. Baada ya mapambano marefu walipata sheria iliyoweka huru watumwa wote katika makoloni yote ya Uingereza. Lakini bado nchi nyingine ziliendelea na utumwa wa ndani.
Afrika Mashariki biashara ya watumwa iliendelea hata baada ya Waingereza kumlazimisha Sultani wa Zanzibar kufunga soko la watumwa mjini mwaka 1874.
Mskoti David Livingstone (1813-1873) ndiye aliyetumia nguvu zake zote kupeleleza habari za biashara ya utumwa na kuzipeleka Uingereza. Alikuwa mmisionari na daktari aliyezunguka nchi zote za Kusini mwa Afrika hadi Ujiji (leo katika Mkoa wa Kigoma) kwenye ziwa Tanganyika. Akafa mwaka 1873, moyo wake ukazikwa Chitambo (Zambia). Alifaulu kuamsha watu wengi dhidi ya biashara ya watumwa.
Biashara ilikomeshwa tu baada ya kuundwa kwa utawala wa kikoloni. Lakini watu walishikwa kama watumwa mpaka mwanzo wa karne ya 20, serikali za kikoloni zilipofanya taratibu za kuwaweka huru.
Katika kampeni hizo Wakristo ndio waliosukuma serikali zao na kuonyesha aibu kubwa juu ya mataifa ya Kikristo ya Ulaya kushiriki biashara ya watumwa katika karne zilizopita, karibu sawa na walivyofanya Waarabu Waislamu.
Tumeshaona kwamba tangu mwisho wa karne ya 15 wamisionari Wakatoliki walienda sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 17 na 18 Waprotestanti walianza kuiga mifano yao.
Kanisa la Anglikana liliunda kamati ya kupeleka Injili katika nchi za ng'ambo lakini ilishughulikia hasa Waingereza waliohamia makoloni. Polepole wazalendo wachache walianza kuwaendea pia, jambo lililokuwa gumu kutokana na hali ya ukoloni wenyewe.
Kanisa la kwanza la Kiprotestanti lililotuma wamisionari hasa kwa watu wasiomjua Kristo lilikuwa ni la Ndugu wa Herrnhut (Wamoravia). Katika kijiji hicho cha Ujerumani waliishi wakimbizi Wamoravia waliopewa ustahimilivu kuanzisha upya ushirika wa Umoja wa Ndugu kufuatana na urithi wao kutoka Ucheki. Walikuwa watu wa kawaida kama wakulima na mafundi.
Siku moja katika mwaka 1732 walikutana na mgeni, kwa jina Antoni, mtumishi wa Mdenmark aliyemtembelea Mkuu wa Herrnhut, Ludwig von Zinzendorf. Antoni alikuwa mtumwa mwenye asili ya Afrika aliyenunuliwa na bwana wake katika Visiwa vya Karibi. Baadaye akapewa uhuru wake akasafiri pamoja na bwana wake hadi Denmark.
Kwa Antoni Ndugu wa Herrnhut wakasikia kwa mara ya kwanza habari za hali mbaya ya watumwa Waafrika kule Karibi, na jinsi walivyozuiwa kusikia neno la Mungu pamoja na mateso yao mengine.
Usiku ule ndugu wawili wakasali pamoja na asubuhi yake wakamwendea Mkuu wa Herrnhut wakamwomba ruhusa ya kusafiri hadi Karibi ili wawahubirie wale watumwa. Katika sala hiyo ya maseremala wawili ilianza kazi ya misheni za Kiprotestanti.
Baadaye Ndugu Wamoravia waliendelea kuhubiri kule Greenland, Urusi, Nikaragua, Afrika Kusini na kati ya Waindio wa Amerika. Mawasiliano mapya yakaleta katika kila pembe ya dunia habari hizo zisizosikika zamani kwa watu wengi.
Wamoravia walihubiri mahali pengi Ulaya kati ya Wakristo wa madhehebu yote bila kuwashawishi wajiunge nao lakini walieneza sana habari za misheni.
Wakiitikia mfano wa Ndugu wa Herrnhut Wakristo kutoka vikundi mbalimbali vya uamsho walianza kuelewa wajibu wao wa kueneza Injili kote duniani.
Kuelekea mwaka 1800 Wakristo Waingereza waliunda vyama mbalimbali vya misheni, kama Wabatisti (1792), Chama cha Misioni cha London (1795) na Chama cha Misioni cha Kanisa (la Kianglikana = Church Missionary Society/CMS) (1799). Waprotestanti wa nchi nyingine za Ulaya walifuata.
Wamisionari wa kwanza tangu zamani za Wareno waliofika Afrika Mashariki walikuwa Wajerumani waliotumwa na CMS. Majina yao ni Ludwig Krapf na Johannes Rebmann. Wanakumbukwa pia kwa kutunga kamusi ya kwanza ya lugha ya Kiswahili.
Mara nyingi wakati ule si viongozi wa madhehebu ya Kiprotestanti (isipokuwa kwa kiasi Waanglikana) walioendesha kazi ya misheni, kwa kuwa walijali maeneo yao tu wakikosa mtazamo wa dunia nzima kama wenzao Wakatoliki.
Kumbe walikuwa walei na wachungaji wa kawaida waliounda vyama vya misheni, kuiombea kazi hiyo, kutafuta habari za nchi nyingine na kuchanga pesa wakiandaa vijana watakaokuwa tayari kuacha ndugu zao wakielekea nchi za mbali zisizojulikana nao.
Katika Kanisa Katoliki vyama vipya viliundwa hasa kwa ajili ya Afrika. Cha kwanza kilichoingia Afrika mashariki kilikuwa cha mapadri wa Roho Mtakatifu.
Anayekumbukwa sana ndiye askofu Mfaransa Charles Lavigerie. Mwaka 1868 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Afrika (linalojulikana kama "White Fathers") na mwaka 1869 Shirika la Masista Wamisionari wa Afrika. Baadaye Lavigerie alipewa cheo cha Askofu Mkuu wa Algeria. Alijitahidi sana kukomesha biashara ya watumwa na kueneza Injili. Tofauti na mashirika mengine ya Wakatoliki hao Mapadri Weupe walishambulia moja kwa moja wafanyabiashara ya watumwa na kuwapokea watumwa waliotoroka.
Wamisionari wa madhehebu mbalimbali waliunda vituo katika sehemu za pwani ya Afrika. Vituo hivyo vilipokea watumwa waliochukuliwa na jeshi la Uingereza kwenye meli za wafanyabiashara. Walinunua pia watumwa na kuwapa uhuru.
Wengine kati yao walipokea ubatizo na kuwa Wakristo wa kwanza katika nchi zao. Vituo vya kwanza vya watumwa waliowekwa huru vilikuwa Freetown (= Mji wa watu huru) huko Sierra Leone, halafu Bagamoyo na Masasi katika Tanzania ya leo, na Freretown karibu na Mombasa, Kenya.
Kwa namna hiyo uinjilisti ulianza kwanza Afrika Magharibi. Kazi ya kuhubiri Injili ilianzishwa na watu kutoka Ulaya lakini ikaendeshwa baadaye na wainjilisti au wachungaji Waafrika.
Samuel Crowther aliwahi kuwa mtumwa utotoni. Alinunuliwa na wamisionari Waanglikana, akapewa uhuru, akasomeshwa teolojia na kuwa kasisi wa Kianglikana. Mwaka 1864 alibarikiwa kule Nigeria kuwa Askofu wa kwanza wa Kianglikana katika Afrika. Hivyo msingi wa Kanisa la Kiafrika kusini kwa Sahara uliwekwa.
Chama cha Misheni cha Kianglikana kiliona madhumuni yake kuwa kusaidia kutokea kwa "kanisa la Kiafrika linalojitawala, linalojitegemea kiuchumi na linalojiendeleza".
Hatuna budi kukumbuka kilichotokea mwanzoni mwa historia ya Kanisa katika Afrika Mashariki huko Uganda.
Buganda ilikuwa ufalme mkubwa. Mtawala wake kwa cheo cha Kabaka aliyeitwa Mutesa aliwakaribisha wageni.
Katika miaka 1877 hadi 1879 walifika Buganda wamisionari Wazungu, wakitangulia Waanglikana wa C.M.S. wakifuatwa na Wakatoliki wa shirika la Mapadri Weupe.
Mara moja Waingereza wa C.M.S. na Wafaransa wa Mapadri Weupe walianza kushindana mbele ya mfalme na wakubwa wake. Mashindano hayo yalidhoofisha sifa za wamisionari mbele ya Kabaka.
Zaidi ya hayo washauri Waislamu walimweleza Kabaka kwamba wageni wale walitaka tu kuangusha ufalme wake. Mfalme na wakubwa walisita kukaribia zaidi mahubiri mapya.
Lakini makao makuu yalijaa vijana kutoka familia za machifu waliofanya kazi ya kumhudumia mfalme. Wamisionari walitafsiri Biblia katika Kiganda wakafundisha kusoma. Ilikuwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kiganda kuandikwa.
Vijana wengi walivutwa na mahubiri ya Kikristo pamoja na elimu mpya. Kwa namna hiyo Kanisa la Uganda lilianza na vijana. Mwaka 1882 Waanglikana walianza kubatiza.
Baada ya kifo cha Mutesa alifuata Kabaka Mwanga aliyekuwa na wasiwasi juu ya wamisionari. Mwaka 1885 watumishi watatu wa mmisionari Mackay waliuawa kwa amri ya mfalme huyo walipomsindikiza kinyume cha katazo lake.
Waziri wa Mfalme, ambaye alifuata dini za jadi na kuwa na mpango wa kumwangusha mfalme na kufukuza wageni wote, aliendelea kumshawishi.
Tarehe 25 Mei 1886 hasira ya Kabaka iliwaka. Aliamua kuwaondoa Wakristo wote katika mazingira yake. Vijana wote waliitwa mbele yake wakaulizwa kama wako tayari kuacha Ukristo. Walio wengi walikataa.
Tarehe 3 Juni 1886 kwa amri ya Mfalme zaidi ya vijana Wakristo 30 walichomwa moto wakiwa hai. Mahali pa vifo paliitwa Namugongo. Inajulikana kwamba wamisionari Waanglikana na Wakatoliki waliendelea kuvutana juu ya matatizo hayo mpaka dakika ya mwisho. Lakini pale Namugongo Wakristo walikufa pamoja; kati yao, Wakatoliki 12 na Waprotestanti 9 wanajulikana; juu ya wengine hakuna uhakika. Baadhi walikuwa hawajabatizwa, walikuwa bado wanafunzi wa ubatizo.
Chini ya ukoloni
haririHali ilibadilika baada ya mageuzi ya kisiasa. Kipindi kipya cha ukoloni kilianza. Mwaka 1885 serikali za Ulaya ziligawanya Afrika kati yao. Sehemu zote za Afrika ziliwekwa chini ya utawala wa kikoloni, isipokuwa Ufalme wa Kikristo wa Ethiopia, uliojitetea dhidi ya Waitalia, na Liberia iliyokuwa chini ya ulinzi wa Marekani. Ukoloni ulileta mabadiliko gani kwa kazi ya misheni katika Afrika?
Serikali za kikoloni zilijiingiza katika kazi ya wamisionari. Mara nyingi ziliwategemea kutoa huduma za elimu na afya nao walifaidika na ulinzi wa serikali za kikoloni. Walipata msaada wa kumiliki ardhi na kukabidhiwa madaraka katika ustawi wa jamii.
Mara nyingi wamisionari walipokea kwa shukrani ulinzi huo wa pekee kutoka kwa serikali yenye uraia wao. Hii ilileta matatizo mara kadhaa ikiwa serikali ya kikoloni iligandamiza wenyeji lakini wamisionari walisita kuwatetea kwa sababu walikuwa karibu mno na serikali yao.
Lakini si kweli kwamba serikali za kikoloni ziliendesha misheni za Kikristo. Shabaha ya ukoloni ilikuwa kutawala bila matatizo.
Katika sehemu nyingine, hasa zenye Waislamu wengi, wamisionari walizuiwa wasifanye kazi kwa sababu wakoloni walishirikiana na watawala (machifu) Waislamu na kuogopa vurugu. Nchini Tanzania makanisa yaliweza kuanza kazi sehemu nyingi za pwani baada ya uhuru tu. Ndivyo ilivyokuwa katika nchi mbalimbali za Afrika Magharibi.
Ukoloni uliambatana na mawazo ya kibaguzi. Tangu watawala na walowezi kutoka Ulaya walipoingia itikadi ya kuwa Mwafrika si mwanadamu kamili ilienea. Itikadi hiyo iliwasaidia wakoloni kujitetea mbele ya wananchi wenzao nyumbani kwao jinsi walivyoendesha ukoloni.
Itikadi hiyo ikasababisha mageuzi ya mawazo. Wakristo wengi Ulaya walipata shaka kama kweli inawezekana kuwakabidhi Waafrika mara moja madaraka ndani ya kanisa. Pale ambapo Kanisa la Kiafrika lilishaanza kujitawala kama Afrika Magharibi maendeleo yake yalikwama kwa muda mrefu. Askofu Crowther alishambuliwa sana na aliyemfuata alikuwa Mwingereza tena.
Hata hivyo viongozi wengine wamisionari walilenga mapema kuwaandaa wenyeji kuwa viongozi baadaye, kama vile wamisionari Waanglikana na Wakatoliki kule Uganda.
Mara nyingi serikali za kikoloni zilisisitiza kuwa na wamisionari kutoka mataifa yao. Mfano ni Tanganyika ambako vituo vingine vya Waanglikana (Waingereza) vilifungwa baada ya kuingia kwa Wajerumani. Badala yake serikali ya Ujerumani iliomba Walutheri pamoja na Wamoravia (toka Ujerumani) kuanza kazi katika Tanganyika.
Baadaye kuingiliana kwa namna hiyo kati ya kanisa na serikali kulisababisha kufukuzwa kwa wamisionari Wajerumani wakati wa vita vikuu vya kwanza (1914-1918) nchi ilipotekwa na Waingereza.
Katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki kazi ya kuhubiri ilianzishwa na wamisionari Wazungu. Lakini baada ya muda mfupi mzigo mkubwa wa kuhubiri Injili ulibebwa tayari na wazalendo.
Wamisionari walijitahidi zaidi kuendesha vituo kama shule, seminari na hospitali. Pia walishika muda mrefu shughuli kama ubatizo, Chakula cha Bwana na sakramenti kwa jumla kwani hizo zimewekwa kwa wachungaji au mapadri, vyeo ambavyo havikupatikana mwanzoni kwa wenyeji (tofauti na Afrika Magharibi jinsi tulivyoona juu).
Lakini baada ya muda mfupi wa mwanzo kazi kubwa ya kuhubiri vijijini, ushuhuda wa moja kwa moja na hata kufundisha katika shule za msingi iliendeshwa na Wakristo Waafrika. Wamisionari walikazia zaidi kuwaandaa hawa wainjilisti, makatekista na walimu.
Hivyo tunaweza kusema kazi ya misheni tangu mwanzo ilikuwa kazi ya Waafrika wenyewe, ingawa chini ya uongozi wa wamisionari Wazungu.
Kuanzia karne ya 20
haririMwanzoni mwa karne ya 20 Kanisa la Afrika lilikuwa bado chini ya uongozi wa wamisionari Wazungu. Leo hii ni Waafrika wenyewe, bila viongozi wengi wa nje, ambao wanahubiri neno la Mungu kwa wenzao.
Karne hiyo imeshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanya Ukristo Afrika uwe unavyoonekana leo. Sababu zifuatazo zilichangia mabadiliko:
Vita vikuu vya dunia vilisaidia kukomaa kwa Kanisa la Afrika. Kwa mfano, mahali pengi Tanzania makanisa yalianzishwa na wamisionari Wajerumani (Wakatoliki, Walutheri, Wamoravia, Wasabato n.k.). Katika vita vikuu vya kwanza (miaka 1914-18) jeshi la Kiingereza liliingia na kuteka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (baadaye Tanganyika, Rwanda na Burundi). Raia wa Ujerumani walifukuzwa pamoja na wamisionari.
Kwa muda wa miaka saba Wakristo Waafrika walibaki karibu peke yao mpaka wamisionari Wajerumani waliporuhusiwa kurudi. Bila maandalizi makubwa wainjilisti, makatekista na walimu Waafrika walipaswa kuongoza Kanisa changa. Wengi walihofu kwamba litarudi nyuma, kumbe mahali pengi idadi ya Wakristo iliongezeka mpaka wamisionari waliporudi.
Kwa kiasi fulani hali hiyohiyo ilitokea wakati wa vita vikuu vya pili (1939-1945). Safari hiyo wamisionari Wajerumani waliwabariki wainjilisti Waafrika kuwa wachungaji kabla ya kufukuzwa na serikali ya Kiingereza kutoka Tanganyika. Katika vipindi hivyo ieleweke kwamba wamisionari wachache wa mataifa mengine au madhehebu mengine walisaidia, kama vile Walutheri kutoka Marekani na Skandinavia, au Wapresbiteri kutoka Malawi katika eneo la Wamoravia.
Ingawa ukoloni ulikuwa na ubaguzi mkali, viongozi wengine walitunza msimamo wa kueleleka Kanisa la Kiafrika litakalojitawala na kujitegemea. Kazi kubwa ilikuwa kuunda taasisi zilizoweza kutosheleza madai ya elimu ya juu kwa vijana waliotokea mazingira bila vitabu wala shule.
Afrika Mashariki walikuwa hasa wamisionari katika Uganda waliofanya mapema maandalizi ya kuwa na mapadri na wachungaji Waafrika. Huko Askofu Mwanglikana Tucker aliwahi kubariki makasisi wa kwanza mwaka 1893, akifuatwa na Wakatoliki mwaka 1913. Wakatoliki walisonga mbele walipomweka wakfu askofu Kiwanuka mwaka 1939.
Baada ya vita vikuu vya pili duniani kote makanisa mengi yaliyoongozwa na wamisionari yalianza kuandaa viongozi wenyeji kushika madaraka. Mapambano ya kupata uhuru wa kisiasa yaliharakisha mwendo huu hata ndani ya makanisa yaliyochelewa kufanya maandalizi hayo.
Mtanzania wa kwanza aliyepata cheo cha kimataifa alikuwa Laurean Rugambwa, askofu aliyewekwa wakfu mwaka 1952. Miaka minane baadaye alipewa cheo cha "kardinali": ndiye kardinali Mwafrika wa kwanza. Kardinali ni askofu Mkatoliki anayekabidhiwa usimamizi wa kanisa moja jimboni Roma pamoja na haki ya kumchagua Papa. Halmashauri ya makardinali inakaa na Papa na kumshauri juu ya uongozi wa Kanisa. Papa akifa ndio makardinali tu wanaokutana kumchagua Papa mpya.
Katika nchi mbalimbali ukali wa ukoloni ulisababisha mafarakano katika makanisa yaliyoongozwa na wamisionari, hadi kutokea kwa makanisa huru ya Kiafrika ("African Independent Churches"). Mifano hii ipo Kenya, Kongo, Afrika Kusini na kwingineko.
Huko Kenya wenyeji walishtushwa sana na tendo la ardhi yao kutolewa kwa walowezi Wazungu. Uchungu huo mkubwa ulionekana pia katika shaka juu ya wamisionari. Wakikuyu walipoanza kupinga siasa hiyo wamisionari waliwashauri Wakristo watulie huku wakijaribu wenyewe kutetea haki za wenyeji mbele ya serikali ya kikoloni.
Kumbe wainjilisti na walimu pamoja na Wakristo wengi walianza kujitenga na makanisa yaliyoongozwa na wamisionari wakaanzisha makanisa yao. Mara nyingi makanisa hayo yalikuwa ya kikabila na kuendelea kufarakana, lakini yalifaulu kuunganisha utamaduni asili na imani ya Kikristo kwa namna yao.
Huko Kongo mwinjilisti Simon Kimbangu alionekana kuwa na kipawa cha uponyaji. Watu wengi walimwendea kutafuta nafuu wakasikia mahubiri yake, lakini serikali ya kikoloni ya Ubelgiji iliogopa mikutano mikubwa ya Waafrika bila usimamizi wa Wazungu au machifu. Hivyo Kimbangu akaagizwa na wamisionari kwa amri ya serikali aache mahubiri na uponyaji lakini hakuweza kutii. Wabelgiji wakamkamata wakamfunga gerezani miaka mingi mpaka kifo.
Wafuasi wake wakamwamini kuwa nabii wa Mungu, wengine walisema ndiye Yesu aliyerudi, wakatoka katika uongozi wa wamisionari walionyamaza mbele ya tendo la serikali kumfunga Kimbangu bila kosa. Kati ya wafuasi wake limetokea "Kanisa la Kristo kwa Mtume wake Simon Kimbangu" ambalo leo lina waumini milioni kadhaa.
Kule Afrika Kusini milioni za Wakristo ni wafuasi wa makanisa yanayoitwa ya "Kisayuni" au ya "Kiethiopia".
Kwa jumla makanisa hayo yalitokea kwenye ukoloni mkali, ugandamizaji kupita kiasi au kuingia kwa walowezi Wazungu waliochukua ardhi ya wenyeji ikiwa wamisionari waliomba Wakristo wao kutulia na kutii serikali. Siasa kali ya kikoloni ilisababisha uchungu mkubwa ulioleta mafarakano. Kumbe Tanganyika makanisa hayo hayakuwa na Wakristo wengi, isipokuwa katika maeneo ya mipakani, kwa mfano Mara (Maria Legio Church kutoka Kenya) au Mbeya.
Siku hizi jina la "African Independent Churches" lina utata kwa sababu hata madhehebu ya kimataifa yamekuwa makanisa ya Kiafrika yanayojitawala, tena tangu miaka mingi. Lakini kwa mazoea jina hilo limebaki kwa makanisa hayo yaliyoanzishwa wakati wa ukoloni kama alama ya Waafrika kuchukua Injili mikononi mwao hata bila kibali cha wamisionari au serikali ya kikoloni.
Kanisa linakua Afrika haraka kuliko katika mabara mengine yote. Kadiri ya wataalamu wa takwimu Wakristo na Waislamu wanashindana: ni nani mwenye waumini wengi zaidi barani? Hata hivyo zipo alama za kwamba tangu mwaka 2000 idadi kubwa ya Waafrika ni Wakristo wa madhehebu mbalimbali.
Tangu uhuru wa kisiasa Wakristo wameongezeka sana katika nchi kusini kwa Sahara. Hakuna bara lingine ambako idadi yao iliwahi kuongezeka haraka hivyo. Sababu ziko nyingi, kwa mfano:
- a) imani asilia zimefifia kwani si rahisi kuzifuata nje ya mazingira ya jadi yanayoendelea kubadilika.
- b) Ukristo umeambatana na elimu tangu mwanzo. Elimu inaonekana kuwa mlango wa maendeleo, hivyo kwa watu wengi Ukristo na maendeleo vinakwenda sambamba. Karibu shule zote zilianzishwa na wamisionari au makanisa. Viongozi walio wengi wa Afrika huru (Wakristo na Waislamu vilevile) walipitia shule za misheni (hata wale waliotaifisha baadaye shule za makanisa).
- c) Kanisa lilijitahidi kuunganisha Injili na utamaduni wa Kiafrika. Ni kweli kwamba wamisionari wengi hawakuelewa kwa urahisi pande zote za utamaduni huo. Sababu mojawapo ya farakano kati yao na Wakristo Wakikuyu kule Kenya ilikuwa kutoelewana juu ya kukeketwa kwa wasichana. Lakini lugha nyingi za Kiafrika ziliandikwa kwa mara ya kwanza wakati wamisionari walipojitahidi kujifunza lugha hizo na kutafsiri Biblia. Hiyo imekuwa chombo kikuu. Leo hii Biblia nzima au angalau Agano Jipya vimepatikana katika lugha mia kadhaa za Kiafrika. Vilevile nyimbo za Kikristo zinazidi kutumia tuni za Kiafrika, ingawa ziko tofauti kubwa kati ya madhehebu juu ya desturi ya kutumia zaidi tuni za kale za Ulaya au zile za kienyeji.
- d) Sababu muhimu ya kukua kwa Kanisa Afrika ni ushuhuda na mfano wa Wakristo wenyewe unaotolewa kwa majirani wao. Ujumbe huo hueleweka vizuri kadiri maisha ya watu wanaoitwa "Wakristo" kwa jina la Kristo yanavyolingana na upendo na amani vinavyotoka katika Injili.
Kanisa la Afrika hupatikana katika madhehebu mamia. Hali hiyo kwa kiasi fulani ni urithi wa wamisionari walioleta mafarakano yao ya kale kutoka Ulaya au Marekani mpaka Afrika. Waafrika wa leo wangeuliza swali kama sababu za mafarakano kule Ulaya miaka 500 iliyopita bado zina nguvu kwao. Lakini sasa idadi kubwa ya madhehebu imetokana na mafarakano ndani ya makanisa yaliyokuwepo tayari Afrika.
Pia hali ya uchumi ina uzito wakeː siku hizi vikundi vingi vya Kikristo kutoka nchi tajiri vinaendelea kufika Afrika na kuvuta wafuasi kwa uwezo wao wa kutoa misaada mbalimbali. Wakati mwingine vinajitahidi zaidi kuvuta Wakristo wahame madhehebu kuliko kuinjilisha wasio Wakristo.
Kwa neema ya Mungu ushirikiano upo pia, si mafarakano tu. Wamisionari wenyewe, hasa upande wa Uprotestanti, waliona tayari umuhimu wa ushirikiano. Kwa mfano Walutheri waliomba Wamoravia kuanza kazi pamoja katika Tanganyika Kusini-Magharibi. Wamisionari wao walifika mwaka uleule wa 1891 wakitumia njia ya Ziwa Nyasa wakagawana maeneo yao kama walivyogawana wachungaji wa Ibrahimu na Lutu. Baadaye walichapisha hata kitabu cha pamoja cha nyimbo za Kikristo.
Hasa karne ya 20 imekuwa ya kurudisha umoja. Wakristo wa madhehebu mbalimbali yanashirikiana kirahisi katika shughuli mbalimbali. Mwaka 1936 viongozi wa madhehebu kama Walutheri, Waanglikana, Wabatisti na Wamoravia waliunda "Baraza la Misheni Tanzania". Baraza hilo lilikuwa mtangulizi wa CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania / Christian Council of Tanzania). Katika miaka ya 1960 viongozi wa makanisa ya Kiprotestanti waliongea juu ya kuunda Kanisa la Muungano katika Afrika Mashariki.
Kwa bahati mbaya wafadhili wengine kutoka ng'ambo waliona hawawezi kusaidia kanisa la muungano kama si tena la madhehebu yao. Ilionekana hiyo ni hatari kwa kazi kama hospitali na shule zilizotegemea msaada kutoka ng'ambo, hivyo muungano ulisimamishwa. Lakini madhehebu yaliyoongea hivyo wakati ule yanaendelea kushirikiana katika vyombo vya pamoja kama vile CCT. Wanachama wa CCT ni kama wafuatao: Walutheri, Waanglikana, Wamoravia, African Inland Church, Wabatisti, Wapresbiteri, Jeshi la Wokovu, Kanisa la Uinjilisti (Mbalizi), pia vyama kama TCRS/Huduma ya Kikristo ya wakimbizi Tanzania.
Ushirikiano umejengwa pia kati ya Waprotestanti na Kanisa Katoliki. Zamani za wamisionari uhusiano huo ulikuwa mgumu mara nyingi. Lakini mabadiliko mengi yamejenga msingi wa uelewano na hali ya kuheshimiana.
Hatua muhimu sana ilikuwa mkutano mkuu wa Kanisa Katoliki duniani ulioitwa Mtaguso wa pili wa Vatikano miaka 1962-1965. Hapo maaskofu wote chini ya uongozi wa Papa (kwanza Yohane XXIII, halafu Paulo VI) walitamka kwamba Wakristo wote ni ndugu na kwamba kujenga umoja wa Kanisa ni wajibu wa kila mmojawao. Leo hii makanisa ya CCT na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hushirikiana katika shughuli mbalimbali kama vile Baraza la Kikristo la Afya Tanzania (Tanzania Christian Medical Board) au katika kuandaa mafundisho ya pamoja katika elimu ya Kikristo mashuleni.
Chama cha Biblia ni chombo kingine cha ushirikiano kati ya madhehebu. Chama hicho kina kazi ya kutoa Biblia kwa bei nafuu kwa watu wengi. Kinasimamia tafsiri ya Biblia katika Kiswahili cha kisasa na lugha nyingine. Kinaandaa matoleo mapya ya Biblia na misaada ya kuielewa kama "Itifaki ya Biblia".
Siku hizi Wakristo kote duniani huishi pamoja na watu wa dini nyingine. Barani Afrika ni hasa watu kutoka makundi mawili: Waislamu na wafuasi wa dini asilia.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu una umuhimu wa pekee kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Katika sehemu mbalimbali za Afrika Wakristo na Waislamu waliwahi kushirikiana vema katika mambo mengi ya kijamii lakini uhusiano huo umeanza kuwa mgumu. Sababu moja ni mzigo wa historia tunaoubeba mara nyingi bila kujua. Mzigo huo ni urithi wa mahusiano magumu kati ya Waislamu na Wakristo kule Ulaya na Asia. Itakuwa muhimu sana kwa vijana wa leo kukataa mzigo wa historia na kuvumiliana.
Kwa mfano, Waislamu wanaweza kutumia neno "jihadi" wakiongea juu ya jitihada za kuimarisha jumuiya yao au kueneza imani yao, lakini Wakristo walio wengi wanasikia neno hilo vibaya kwa sababu "vita vitakatifu" vya Waislamu vilivyoitwa "jihadi" vilileta mateso mengi kwa Wakristo katika nchi mbalimbali. Kumbe neno halimaanishi vita hasa ila liliwahi kutumika hivyo tangu muda mrefu.
Vilevile Wakristo wengi hawaoni tatizo kutumia neno "Crusade" kwa ajili ya mikutano ya kiroho. Lakini Waislamu wanaweza kuchukua neno hili vibaya pia kwani kiasili "Crusade" (maana yake "Vita vya Msalaba") linamaanisha hasa kipindi cha miaka 800 hivi iliyopita. Wakati ule Wakristo wa Ulaya Magharibi walijaribu kufuta utawala wa Kiislamu katika nchi za Mashariki ya Kati kwa vita vilivyoendelea muda wa miaka 200.
Ukristo na Uislamu viko karibu katika mambo mengi lakini hutumia mafundisho yanayogongana katika sehemu nyingine, hivyo mpaka leo hii kwa Waislamu ni vigumu sana kupokea Injili. Wakati wa vita vya msalaba Fransisko wa Asizi aliona hakuna njia ya kuwavuta Waislamu kwa mabavu. Mashindano pekee yanayoruhusiwa kwa Mkristo ni yale ya upendo ya kumfuata Yesu.
Kwa jumla mawazo ya Mt. Fransisko yamethibitishwa na historia. Kwa hiyo si vibaya kujiandaa kushirikiana na Waislamu Kikristo kwa kufahamu kidogo imani yao na kutambua sifa nzuri zilizopo katika maisha na mafundisho yao pia.
Wakristo kwa jumla wasijivunie sifa zao kuwa bora kuliko za Waislamu. Anayesoma "Historia ya Kanisa" ataona mifano mingi ya jinsi Wakristo walivyosahau mafundisho ya Yesu na kutendeana kwa unyama. Kwa hiyo mtu asijivune kwamba Ukristo ni dini ya upendo au imani yenye maendeleo kama mwenyewe si mfano wa upendo huo na maendeleo hayo.
Kwa Wakristo wengi ni fumbo kwa nini Mungu alikubali kutokea kwa dini hiyo mpya. Lakini mwanzoni mwa Uislamu Mfalme Mkristo wa Ethiopia alipokea na kuhifadhi wakimbizi Waislamu kutoka Maka. Mapokeo ya Kiislamu yanasema mfalme huyu aliyekuwa na jina "Negasi" aligeukia Uislamu baadaye. Lakini "Negasi" si jina la mtu fulani, ni cheo cha wafalme wote wa Ethiopia hadi mwaka 1974 (kwa kawaida huandikwa "Negus"). Halafu hakuna kumbukumbu ya kwamba mfalme yeyote wa karne zile aliacha Ukristo wake.
Kuhusu wanaofuata bado imani asilia pia ni kwamba wanatunza katika mila na desturi zao urithi wa utamaduni. Hata maadili mengine yanayofundishwa kwao yanalingana na sehemu za Biblia. Hakika si vema Wakristo wakiwacheka na kuwaita kwa majina ya dharau kama "Wapagani". Hata juu ya imani hizo za jadi ni kweli kwamba zilimjua Mungu kwa namna fulani kutokana na uumbaji wake jinsi alivyoandika Mtume Paulo katika Rom. 1.
Katika nchi nyingi Kanisa limekuwa nguvu ya kutetea haki za binadamu. Tumesikia habari za Desmond Tutu kule Afrika Kusini au za Janani Luwum katika Uganda jinsi walivyojaribu kutetea haki za wananchi dhidi ya utawala mbaya. Ikiwa Wakristo wanajisikia wito wa kusimama na kusema mbele ya wakubwa hukumbuka manabii wa Agano la Kale hadi Yohane Mbatizaji. Wanakumbuka pia Wakristo wengi katika historia walioweza kusimama mbele ya wafalme na kutetea haki za watu. Labda tunamkumbuka Askofu Ambrosio wa Milano (aliyemvuta kijana Agostino kuwa Mkristo) alivyomtenga Kaisari na Kanisa kwa sababu ya uuaji wa wananchi wengi wasio na kosa uliofanywa na wanajeshi wa serikali. Msingi wake ni katika mafundisho juu ya kazi ya uumbaji. Mbele ya Mungu tuko sawa: kuna msingi gani kuona wengine ni sawa zaidi?
Lakini si Wakristo wote wanakubali na kufurahia msimamo wa aina hiyo. Wengine huona imani ya Kikristo haihusiki na taratibu za dunia hii au huona ni wajibu wa Mkristo kutii serikali yoyote wakikumbuka maneno ya Mtume Paulo katika Rum 13. Pamoja na hayo katika Ukristo yapo mapokeo ya kutoshindana na wenye mamlaka bali kuwavumilia katika yote. Labda huona hofu ya kuwa dini inaingizwa mno katika siasa.
Tazama pia
haririViungo vya nje
hariri- BBC - The Story of Africa and Christianity
- African Christian
- African Christianity Faq
- Modern Evangelical African Theologians: A Primer Ilihifadhiwa 14 Julai 2011 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Ukristo barani Afrika kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |