Bagamoyo (mji)

Mji


Bagamoyo ni mji mwambaoni mwa Bahari Hindi katika Tanzania takriban km 75 kaskazini kwa Dar es Salaam na km 45 magharibi kwa kisiwa cha Unguja.

Wilaya ya Bagamoyo
Wilaya ya Bagamoyo is located in Tanzania
Wilaya ya Bagamoyo
Wilaya ya Bagamoyo

Mahali pa Bagamoyo katika Tanzania

Majiranukta: 6°26′24″S 38°53′24″E / 6.44000°S 38.89000°E / -6.44000; 38.89000
Nchi Tanzania
Mkoa Pwani
Wilaya Bagamoyo

Vyanzo vidogo

hariri

Bagamoyo iko kati ya miji ya kale kabisa ya Waswahili katika Tanzania ya leo. Magofu ya Kaole (msikiti na makaburi ya karne ya 13 BK) yako karibu na Bagamoyo yakionyesha umuhimu wa utamaduni wa Kiislamu katika eneo hili. Lakini hakuna uhakika kuhusu historia ya Bagamoyo ya kale isipokuwa ya kwamba mnamo karne ya 18 mji haukuwa muhimu. Wakazi walio wengi wakati ule walikuwa wavuvi na wakulima, ila palikuwa na biashara kiasi cha samaki na chumvi[1].

Jina la Bagamoyo huelezwa kutokana na maneno "bwaga" na "moyo". Elezo la kawaida linarejea biashara ya watumwa kwa kudai eti watumwa waliona bahari ambako watasafarishwa hadi Unguja na mbali zaidi, hiyvo walikatishwa tamaa na "kumwaga moyo". Hayo husimuliwa mara nyingi kwa watalii wanaotembelea mji na kuangalia majengo ya kale.

Lakini asili hiyo inapingwa na wataalamu wanaoonyesha kuwa biashara ya watumwa haikuwa muhimu sana hapa na asili ya jina inapatikana zaidi kutoka kwa wapagazi waliofika hapa kwa wingi kutoka bara baada ya safari ngumu ya miezi kadhaa walipoweza kushusha mizigo yao (wengi walibeba hadi kilogramu 70[2]), kupokea mishahara na kuwa na starehe. Kwa hiyo maana si bwaga moyo kama kukataa tamaa, bali bwaga moyo kama kuachana na matatizo na wasiwasi wa safari ya hatari.[3]

Afisa Mjerumani August Leue aliandika mnamo mwaka 1900 kwamba wapagazi waliimba njiani wimbo ufuatao: "Tunakwenda Bagamoyo, roho yangu furahi, tumelia barani kuwa mbali nawe, Bagamoyo, Bagamoyo" akieleza kwamba wapagazi na pia wakazi wengine wa Mrima waliona Bagamoyo kama mji wa furaha na starehe.[4]

Mlango wa misafara ya Afrika ya Kati

hariri

Hasa kuhamia kwa makao ya Sultani wa Oman kuja Zanzibar kuliongeza umuhimu wa mwambao wa Mrima karibu na Unguja. Bandari Zote zilizotazama Unguja zilianza kukua na kupokea mizigo kutoka na kwenda Unguja na kati ya hizo Bagamoyo ilikuwa muhimu zaidi kwa sababu ilikuwa karibu zaidi na mji wa Zanzibar.

Tangu Zanzibar kuwa mji mkuu wa Omani familia za Waarabu pamoja na mawakala wa kampuni za Wahindi walihamia Bagamoyo wakipanua biashara yake. Mji ukawa kituo muhimu zaidi kwenye pwani; biashara ya misafara mikubwa ya karne ya 19 kwenda barani hadi Kongo ilianza na kurudi hapa kushinda bandari nyingine za Mrima.

Kufikia mwaka 1860 hivi Bagamoyo ilikadiriwa kuwa na wakazi wa kudumu 3,000 walioongezeka kuwa 20,000 mnamo mwisho wa karne ya 19. Pamoja na wapagazi wa misafara waliokaa miezi kadhaa mjini baada ya kufika kutoka bara na kusubiri hadi kurudi, mara nyingi wakiajiriwa kubeba tena mizigo ya safari mpya, idadi yao ilifikia watu 30,000-40,000, hivyo jumla ya wakazi iliweza kufikia 50,000 hadi 60.000 kwa muda[5].

Bagamoyo iliendelea kuwa mji mkubwa katika koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hata baada ya serikali ya kikoloni kuhamia Dar es Salaam hadi kujengwa kwa reli ya kati iliyohamisha sehemu kubwa ya biashara kule ambako reli hiyo ilianza.

Bandari ya biashara

hariri

Wafanyabiashara wa Zanzibar walikusanya bidhaa zao huko Unguja wakavuka bahari na kuajiri wapagazi waliozibeba hadi Tabora na Ujiji kwenye Ziwa Tanganyika; kutoka kule biashara iliendelea katika maeneo ya Kongo. Wapagazi wakarudi miezi au miaka kadhaa baadaye wakileta hasa pembe za ndovu zilizokuwa na soko kubwa katika Ulaya na Marekani. Wapagazi wengi walikuwa watu wa maeneo ya magharibi walioitwa kwa jumla "Wanyamwezi".

Bagamoyo imepata pia sifa ya kuwa moja ya bandari kuu za biashara ya watumwa kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki katika karne ya 19. Serikali ya Tanzania ilitumia tabia hiyo kama sababu muhimu ya kupendekeza mji huo kama sehemu ya urithi wa Dunia kwenye orodha ya UNESCO[6]. Hata hivyo, wataalamu wengi wa historia hawakubali, wakiona Bagamoyo haikuwa muhimu sana katika biashara ya watumwa ya Afrika ya Mashariki, ikilinganishwa na Kilwa na Pangani.[7] Hakika watumwa kadhaa walisafirishwa kutoka hapa kwa jahazi au dhau hadi Unguja wakiuzwa huko sokoni. Ila kundi la jeshi la maji la Uingereza lililotumwa Afrika Mashariki kwa kusudi la kuzuia biashara ya watumwa halikuwahi kulenga Bagamoyo bali hasa Kilwa na bandari za upande wa kaskazini wa Bagamoyo.[8]

Mapadre wa Roho Mtakatifu walijenga kituo chao cha kwanza cha barani katika Afrika ya Mashariki huko Bagamoyo wakiona umuhimu wa mji huo kama mlango wa bara. Kwenye eneo la misheni yao walianzisha kijiji kwa watumwa walionunuliwa nao ili kupewa uhuru, watumwa watoro waliokuta hapa mahali salama au watumwa waliopelekwa hapa na jeshi la majini la Uingereza wakikamatwa baharini wakati wa kusimamisha jahazi ambamo walibebwa,

Mji mkuu wa koloni la Kijerumani

hariri

Mnamo Aprili 1888 Sultani wa Zanzibar alikodisha eneo la pwani kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki iliyoanzisha makao makuu yake Bagamoyo. Ukali wa kampuni ulisababisha katika muda wa miezi chache ghasia ya wenyeji wa pwani iliyoleta vita vya Abushiri ambavyo vilikandamizwa na wanajeshi wa Ujerumani. Mwaka 1890 serikali ya Ujerumani ilichukua madaraka ya utawala badala ya kampuni halafu mji mkuu ukahamishiwa Dar es Salaam.

Kushuka kwa biashara

hariri

Umuhimu wa Bagamoyo ulianza kupungua kwa sababu meli kubwa zilitumia bandari ya Dar es Salaam badala ya Bagamoyo. Bandari yake haikufaa tena kwa meli kubwa zilizopaswa kutia nanga kilomita mbele ya mwambao ilhali kina cha maji huko Dar es Salaam iliruhusu meli kufika mwambaoni moja kwa moja, Hatimaye tangu ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro, Tabora hadi kufikia Kigoma biashara ya Bagamoyo ilipungua sana. Reli hiyo ilichukua nafasi ya njia ya misafara kutoka Mrima kuelekea Ziwa Tanganyika kwa sababu usafiri wake ulikuwa haraka zaidi, tena kwa bei nafuu kuliko gharama za kukodi wapagazi.

Mnamo 1913 (kabla ya Vita Kuu ya Kwanza) wakazi wa kudumu walikuwa 5.000 tu. Bado ilikuwa na ofisi za kampuni 25. Mwaka 1908 ni meli 149 zenye tani 198.305 pamoja na jahazi 689 zenye tani 15,369 zilizofika hapo. Hadi mwaka 1912 zilikuwa jahazi 402 tu zenye tani 8.465 (meli za 1912 hazikutajwa tena katika takwimu ya Ujerumani). Kinyume chake, bandari ya Dar es Salaam ilifikiwa 1912 na meli kubwa zaidi za kibiashara 164 zenye tani 644.306, meli za serikali 103 zenye tani 15.455 na jahazi 702 zenye tani 15.919[9].

Mji wa kisasa

hariri

Leo hii Bagamoyo ni mji mdogo unaofanywa na kata mbili za Magomeni na Dunda. Majengo yake ya kihistoria yako katika hali mbaya. Wakazi walio wengi wanaishi katika sehemu jipya la Magomeni na soko jipya. Majaribio ya hifadhi ya urithi wa kihistoria yaliona matatizo tangu miaka mingi. Bagamoyo ina chuo cha kitaifa kiitwacho Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo. Kinafundisha uchoraji wa jadi wa Tanzania, uchongaji, michezo, kucheza na kucheza. Mwaka 2007 kulingana na chuo, Sanaa ya Bagamoyo na Taasisi ya Kitamaduni (TaSuba) ilianzishwa. Tangu mwaka 2002 barabara ya lami imepatikana na kuleta matumaini ya kuongezeka kwa utalii. Idara ya Mambo ya Kale nchini Tanzania inafanya kazi ili kudumisha maboma ya zama za kikoloni karibu na Bagamoyo na kuimarisha mji. Mwaka wa 2006, idara hiyo iliomba UNESCO kuingiza Bagamoyo katika orodha ya Urithi wa Dunia (World Heritage), katika jamii ya kitamaduni.

Tangu kuunganishwa na Dar es Salaam kwa barabara ya lami Bagamoyo inaona ongezeko la watalii kutoka nje na pia Watanzania.

Bandari

hariri

Bandari mpya iitwayo Bagamoyo Port, inajengwa Mbegani, karibu na Bagamoyo. Serikali ya Uchina imewekeza dola la Kimarekani bilioni 10 ili kuifanya bandari hii kuwa moja ya bandari muhimu Afrika.

Wakazi maarufu

hariri

Miji dada

hariri

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. "Bagamoyo Stone Town History". Iliwekwa mnamo 2023-09-24.
  2. Rockel, S. J. (2006). Carriers of Culture: Labor on the Road in Nineteenth Century East Africa. Portsmouth, NH: Heinemann. Rougeulle, A. (1991), mlango wa 4
  3. Steven Fabian (2013): East Africa's Gorée: slave trade and slave tourism in Bagamoyo, Tanzania, Canadian Journal of African Studies/La Revue canadienne des études africaines, 47:1, ukurasa 98f
  4. Leue, August. 1900/1901. Bagamoyo. Beiträge zur Kolonialpolitik und Kolonialwirtschaft 2, uk. 11
  5. John Iliffe: A Modern History of Tanganyika, 1975, uk. 45
  6. The Central Slave and Ivory Trade Route, Orodha awali ya Urithi wa Dunia, tovuti ya UNESCO, iliangaliwa Agosti 2021
  7. Steven Fabian (2013): East Africa's Gorée: slave trade and slave tourism in Bagamoyo, Tanzania, Canadian Journal of African Studies/ La Revue canadienne des études africaines, 47:1, 95-114 http://dx.doi.org/10.1080/ 00083968.2013.771422
  8. Steven Fabian (2013): East Africa's Gorée: slave trade and slave tourism in Bagamoyo ,uk.100
  9. [1]Archived 17 Mei 2017 at the Wayback Machine. Koloniallexikon (1920), makala Bagamojo na Daressalam
  10. "Vallejo Sister City". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-04-14. Iliwekwa mnamo 2017-17-10. {{cite web}}: Check date values in: |accessdate= (help)

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Pwani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Bagamoyo (mji) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.