Laurenti wa Brindisi

Laurenti wa Brindisi ni jina la kitawa la Giulio Cesare Russo (Brindisi, leo nchini Italia, 22 Julai 1559 - Belém, Ureno, 22 Julai 1619), padri na mkuu wa shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini miaka 1602-1605.

Laurenti wa Brindisi, "mwalimu wa kitume".

Alitoa huduma ya kuhubiri katika sehemu mbalimbali za Ulaya asikubali kuchoka; alitekeleza majukumu yake yote kwa usahili na unyenyekevu, yawe ya kulihami Kanisa dhidi ya wavamizi Waislamu, ama ya kupatanisha watawala waliopigana vita ama katika kuongoza shirika lake[1].

Alitangazwa mwenye heri na Papa Pius VI mwaka 1783, mtakatifu na Papa Leo XIII mwaka 1881, hatimaye mwalimu wa Kanisa na Papa Yohane XXIII mwaka 1959.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Julai[2].

Maisha

hariri

Utoto na wito

hariri

Laurenti alizaliwa Brindisi, Italia, tarehe 22 Julai 1559.

Baada ya kufiwa baba yake utotoni, alipokuwa na miaka 7 tu, mama alimtuma aishi utawani, hivyo alisoma kwenye shule ya Wafransisko Wakonventuali hukohuko Brindisi, akavaa kanzu yao tangu mwaka 1565 hadi 1567 kama maandalizi ya kujiunga nao.

Tangu hapo alivutiwa na karama ya Fransisko wa Asizi, hata akavaa kanzu yao tangu mwaka 1565 hadi 1567 kama maandalizi ya kujiunga nao. Wakati huo ndipo alipoanza kuhubiri, kadiri ya desturi yao.

Kisha kupatwa na hali ngumu kiuchumi katika familia, alihamia kwa ndugu yake padri huko Venezia alipoendelea kusoma na kuzingatia wito wa Kifransisko hadi kujiunga na urekebisho wa Wakapuchini tarehe 18 Februari 1575 kwa kuvaa kanzu yao na kubadilishiwa jina. Wakati huo shirika hilo lilikuwa limekomaa, anavyoonyesha mwenyewe ambaye ni tunda lake kamili zaidi pande nyingi.

Huko Padova aliendelea kusoma mantiki na falsafa, halafu akarudi Venezia kusomea teolojia. Kwa wakati huohuo alikuwa anafundisha pia, kutokana na ujuzi wake mkubwa ajabu, hasa wa Biblia katika lugha zote asili, uliomsaidia hata kuhubiria kwa mafanikio Wayahudi.

Kuhusu umuhimu wa Neno la Mungu alisema, “Neno la Bwana ni mwanga wa akili na moto wa utashi, hivi kwamba binadamu aweze kumjua na kumpenda Mungu. Kwa mtu wa ndani, anayeishi kwa neema hai ya Roho wa Mungu, ni mkate na maji, lakini mkate mtamu kuliko asali na maji yanayopendeza kuliko divai au maziwa… Ni silaha dhidi ya moyo ulioshupaa katika vilema. Ni upanga dhidi ya mwili, ulimwengu na shetani ili kuangamiza kila dhambi”.

Tarehe 18 Desemba 1582 alipata upadrisho akaendelea kutumia utaalamu wake kwa ajili ya Urekebisho wa Kikatoliki baada ya Mtaguso wa Trento. Kwa kuwa alijua lugha mbalimbali, kama vile Kifaransa na Kijerumani, aliweza kufanya utume mpana sana akahubiri katika nchi nyingi za Ulaya.

Kwa ujuzi wake wa Biblia na mababu wa Kanisa aliweza kufafanua kwa utulivu na uwazi mafundisho ya Kikatoliki kwa Waprotestanti hasa wa Ujerumani, akionyesha misingi ya yale yaliyopingwa na Martin Luther, kama vile nafasi ya kwanza ya Mtume Petro na ya askofu wa Roma kati ya wenzao, asili ya uaskofu, utakaso wa dhati wa binadamu na haja ya kutenda mema ili kuokoka milele.

Hata waamini wa kawaida, wasio na elimu kubwa, walifaidika na maneno yake alipowaelekea ili kuwahimiza washike imani yao kimaisha. Ni ajabu alivyofululiza kuhubiri katika miji mingi ya Italia na ya nchi nyingine hata alipotwishwa majukumu mengine mazito, kama vile mwalimu wa teolojia na mlezi wa wanovisi.

Mwaka 1589 alianza kupata vyeo vikubwa shirikani, kama vile mkuu wa kanda na mshauri wa mkuu wa shirika. Pamoja na hayo, alitumwa Ujerumani kuongoza wanashirika wanaokwenda kuishi na kufanya utume huko.

Mnamo Oktoba 1601 aliomba kuwa mmojawapo wa mapadri wa kuhudumia kiroho wanajeshi wa Kikristo wakipambana na Waturuki wavamizi.

Tarehe 24 Mei 1602 alichaguliwa kuwa mkuu wa shirika, mwenye jukumu la kutembelea kanda zake zote.

Aliendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1605.

Kati ya majukumu mazito ndani ya shirika na ya Kanisa kwa jumla aliendelea kuwa mfuasi mnyenyekevu wa Fransisko wa Asizi, mbali ya kuandika vitabu vingi - vya ufafanuzi wa Biblia, vya maadili, vya hoja za kidini pamoja na hotuba nyingi, kama zile maarufu juu ya Bikira Maria - vilivyomstahilia jina la “Doctor Apostolicus”, yaani "Mwalimu wa Kitume".

Katika maandishi yake, alizungumzia mara nyingi liturujia.

Anakumbukwa pia kwa ibada yake kwa ekaristi na kwa neema za pekee alizokuwa anazipata wakati wa kuiadhimisha, zilizomfanya achukue masaa kila siku kuadhimisha Misa, ambayo kwake ilikuwa hai. Alikuwa kama akitekwa na huo ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana.

Pamoja na kutumia muda mwingi kusali, kwa ari yake ya pekee alikuwa akihimiza mapadri na waamini wengineo kuyapa kipaumbele maisha ya sala, kwa kuwa ndiyo njia ya kuongea na Mungu. “Lo, kama tungezingatia ukweli huu! Yaani kwamba Mungu yupo kweli na sisi tunaposema naye katika sala; kwamba yeye anasikiliza kweli sala zetu, hata tukisali kwa mioyo na akili yetu tu. Tena si tu kwamba yupo nasi na kutusikiliza, bali yuko radhi na kufurahi sana kutujalia tunachomuomba”.

Laurenti alionyesha kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini, akiwaangaza na kuwaimarisha kwa vipaji vyake waweze kuishi Injili kwa furaha. “Roho Mtakatifu anasaidia ubebaji wa nira ya sheria ya Mungu na kupunguza uzito wake, ili tuweze kushika amri za Mungu kwa urahisi mkubwa na hata kwa furaha”.

Vilevile aliangazia nafasi ya pekee ya Bikira Maria, akithibitisha kuwa alitungwa bila dhambi ya asili akashiriki kazi ya ukombozi iliyofanywa na Kristo.

Heshima iliyomfuata kila mahali ilimfanya awe anatafutwa na kusikilizwa kama mshauri.

Sifa yake nyingine ni juhudi kwa ajili ya amani. Mara nyingi Mapapa na watawala wa nchi Katoliki walimchagua kama balozi ili kutatua matatizo na kustawisha uelewano kati ya nchi za Ulaya ambazo wakati huo zilikuwa zinatishwa kuvamiwa na Dola la Waturuki Waosmani.

Mwaka 1618 alitumwa na wananchi wa Napoli walionyanyaswa na makamu wa mfalme wa Hispania akawatetee kwa mfalme mwenyewe, Filipo III. Baada ya kukwepa njama mbalimbali, alitabiri kuwa mwenyewe atakufa mapema, na mfalme atamfuata kabla ya miaka miwili kwisha, kama ilivyotokea.

Alifariki Belém, Ureno, tarehe 22 Julai 1619, labda kwa sumu, wakati wa usuluhishi huo.

Maandishi

hariri

Opera omnia, yaani maandishi yake yote katika magombo 15 yametolewa kitaalamu huko Quaracchi miaka 1926-1956. Kati yake kuna:

  • Mariale
  • Lutheranismi hypotyposis
  • Explanatio in Genesim
  • Quadragesimale primum
  • Quadragesimale secundum
  • Quadragesimale tertium
  • Quadragesimale quartum
  • Adventus
  • Dominicalia
  • Sanctorale
  • Sermones de tempore

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri