Usultani wa Zanzibar

(Elekezwa kutoka Masultani wa Zanzibar)

Usultani wa Zanzibar ulikuwa nchi kwenye pwani ya Afrika mashariki kati ya 1856 na 1964.

Eneo la Usultani wa Zanzibar mnamo 1885.
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Tangu 1890 ilikuwa nchi lindwa chini ya Uingereza.

Ilianzishwa wakati wa kugawa Usultani wa Omani mwaka 1856 ikaishia mwaka 1964 baada ya mapinduzi ya Zanzibar na muungano na Tanganyika uliozaa Tanzania.

Sayyid Said kuhamia Unguja

hariri
Makala kuu: Said bin Sultani

Usultani ulianzishwa wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja.

Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.

Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini.

Biashara ya karafuu na watumwa

hariri

Sayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara.

Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.

Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.

Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844.

Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat

 
Bendera ya Usultani wa Zanzibar

Kugawiwa kwa Omani kulikuwa mwanzo wa Zanzibar

hariri
Makala kuu: Sayyid Majid

Baada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/18351870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki.

Usultani mpya ulikuwa nchi yenye nguvu kati ya Rasi Delgado (mpakani na koloni la Kireno ya Msumbiji) hadi Mogadishu (Somalia). Athira yake ilienea kupitia njia za misafara ya pembe za ndovu na watumwa hadi mto Kongo.

Wafanyabiashara kama Tippu Tip waliokuwa raia wa Usultani wakapita Tabora na Ujiji kwenda ziwa Tanganyika na kuingia ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo. Wapagazi wao walibeba bidhaa kutoka Zanzibar zilizobadilishwa kwa pembe za ndovu hasa. Watumwa walikamatwa au kununuliwa wakabeba pembe hadi pwani.

 
Jumba la Sultani Zanzibar

Pamoja na hayo, sultani alipokea kwa moyo wamisionari Wakristo.

Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu.

Waanglikana wa chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) ambacho kiliundwa ili kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika, waliingia Zanzibar mwaka 1864.

Baadaye wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.

Sayyid Barghash

hariri
Makala kuu: Sayyid Barghash

Sultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Barghash (1870-1888), alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Barghash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa.

Barghash alikuwa na wanajeshi wa kudumu. Mwanzoni alitumia mamluki walioajiriwa kutoka Uarabuni na Uajemi, hasa Baluchistan, pamoja na watumwa[1]. Kuanzia mwaka 1877 alianzisha kikosi kipya cha askari mia kadhaa chini ya afisa Mwingereza Lloyd Mathews waliofundishwa kufuatana na utaratibu wa Kizungu; askari hao waliteuliwa chini ya Waafrika wa Unguja.[2]

Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin wa 1885.

Mwaka 1885 Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani.

Kuenea kwa ukoloni

hariri

Mwaka 1886 mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Barghash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.

  • 1887/1888 pwani ya Kenya ilikodishwa kwa Waingereza. Wakati wa uhuru wa Kenya sehemu hii ikaingizwa katika Jamhuri ya Kenya.
  • Pwani ya Tanganyika ikakodishwa kwa Wajerumani mwaka 1888 na hatimaye kuuzwa mwaka 1890.
  • Miji kwenye pwani ya Somalia ikakodishwa kwa Italia mwaka 1892 ikauzwa mwaka 1906, ila Mogadishu mwaka 1924.

Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu.

Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa.

Mkataba wa Zanzibar-Heligoland na mwisho wa uhuru

hariri

Mkataba wa Zanzibar-Helgoland kati ya Ujerumani na Uingereza ulileta patano la kuwa Zanzibar itakuwa chini ya Uingereza.

Tangu mwaka 1890 waziri mkuu wa Sultani alikuwa Mwingereza aliyepokea amri kutoka London.

Tangu mwaka 1913 nafasi ilichukuliwa na afisa mkazi mkuu.

Kwa muda wa miaka 26 usultani ulikuwa na fedha yake ya pekee iliyoitwa Riali ya Zanzibar.

Uhuru 1963 na mapinduzi

hariri

Zanzibar ilipata uhuru wake tarehe 10 Desemba 1963. Uhuru wa usultani ukadumu muda mdogo tu. Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 yakamuondoa Sultani. Mauaji ya familia nyingi zenye asili ya Kiarabu yakafuata.

Tarehe 26 Aprili 1964 Zanzibar ikaunganika na Tanganyika kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Masultani wa Zanzibar

hariri
  1. Sayyid Said (1856–1870)
  2. Barghash bin Said (1870–1888)
  3. Khalifah bin Said (1888–1890)
  4. Ali bin Said (1890–1893)
  5. Hamad bin Thuwaini (1893–1896)
  6. Khalid bin Barghash (1896)
  7. Hamud bin Muhammed (1896–1902)
  8. Ali bin Hamud (1902–1911) (abdicated)
  9. Khalifa bin Harub (1911–1960)
  10. Abdullah bin Khalifa (1960–1963)
  11. Jamshid bin Abdullah (1963–1964)

Mawaziri

hariri
  1. Sir Lloyd William Matthews, (1890 hadi 1901)
  2. A.S. Rogers, (1901 hadi 1906)
  3. Arthue Raikes, (1906 hadi 1908)
  4. Francis Barton, (1906 hadi 1913)

Maafisa wakazi wakuu

hariri
  1. Francis Pearce, (1913 hadi 1922)
  2. John Sinclair, (1922 hadi 1923)
  3. Alfred Hollis, (1923 hadi 1929)
  4. Richard Rankine, (1929 hadi 1937)
  5. John Hall, (1937 hadi 1940)
  6. Henry Pilling, (1940 hadi 1946)
  7. Vincent Glenday, 1946 hadi 1951)
  8. John Sinclair, (1952 hadi 1954)
  9. Henry Potter, (1954 hadi 1959)
  10. Arthur Mooring, (1959 hadi 1963)

Tanbihi

hariri
  1. Richard F. Burton: Zanzibar; City, Island, and Coast, vol I, London 1872, uk. 266., online hapa
  2. Robert Nunez Lyne, Zanzibar in Contemporary Times, 1905 Hurst And Blackett, London, uk. 100, online hapa