Kanisa la Moravian

(Elekezwa kutoka Umoja wa Ndugu)


Kanisa la Moravian (kwa Kiingereza: Moravian Church; pia: Umoja wa Ndugu kutoka jina la kihistoria la Kilatini "Unitas Fratrum", au ndugu wa Herrnhut) ni madhehebu ya Ukristo wa Kiprotestanti yaliyoanzishwa mwaka 1722 katika Ujerumani na wakimbizi kutoka Moravia.


Nembo la Kanisa la Moravian (Unitas Fratrum) linamwonyesha Mwanakondoo wa Mungu. (Dirisha lenye kioo cha rangi katika kanisa la Moravian huko Winston-Salem, NC)

Baadaye yakaenea katika nchi nyingi kwa juhudi kubwa za kimisionari; leo hii ni kanisa dogo kimataifa, lakini nchini Tanzania ni la tatu kwa ukubwa kati ya makanisa ya Kiprotestanti baada ya Walutheri na Waanglikana. Idadi kubwa ya Wakristo Wamoravian huishi Tanzania.

Katika mafundisho yake hukazia umoja wa Wakristo na ushirikiano kati ya madhehebu mbalimbali, imani ya Mkristo binafsi, uenezaji wa imani ya kikristo na muziki.

Umoja wa Ndugu ni muungano wa majimbo ya kujitegemea yanayoshirikiana chini ya katiba ya kanisa. Uongozi ni mikononi mwa sinodi ya umoja inayokutana kila baada ya miaka 7. Kamati ya umoja ina mjumbe mmoja kutoka kila jimbo.

Nembo lake ni alama ya mwanakondoo wa Mungu anayeshika bendera ya ushindi pamoja na maandishi ya Kilatini: Vicit agnus noster, eum sequamur inayotafsiriwa kama "Mwanakondoo wetu ameshinda, tumfuate" (kwa Kiingereza: "Our Lamb has conquered, let us follow Him").

Historia

hariri

Jina "Moravian" limetokana na nchi ya Moravia ambayo leo hii ni sehemu ya Ucheki. Kanisa hili lilikuwa hapa na vyanzo vyake.

Wafuasi wa Hus waliopenda amani

hariri

Lilitokea baada ya farakano ndani ya Kanisa Katoliki katika Bohemia na Moravia. Nchi hizo mbili zilikuwa sehemu ya Milki ya Kijerumani. Katika karne ya 15 kasisi na profesa Yohane Hus kutoka mji wa Praha alijaribu kutengeneza kasoro na mafundisho ya Kanisa Katoliki lililokuwa kanisa pekee halali katika sehemu kubwa ya Ulaya wakati ule, lakini aliitwa kwenye Mtaguso wa Konstanz akahukumiwa kwa amri ya huo mtaguso mkuu akachomwa moto tarehe 6 Julai 1415.

Kifo cha Hus kilisababisha uasi dhidi ya Kanisa Katoliki katika Bohemia na Moravia. Wafuasi wa Hus walichukua silaha wakijihami dhidi ya askari wa maaskofu na watawala wa milki. Kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe kilifuata kati ya Wakatoliki, wafuasi wakali na wafuasi wa wastani wa marehemu Hus. Mwishowe makaisari wa milki waliokuwa Wakatoliki walipaswa kuvumilia aina mpya ya Ukristo katika nchi hizo mbili zilizoendelea kumkubali kaisari kama bwana mkuu.

Wamoravian wenyewe huona chanzo cha kanisa lao tarehe 1 Machi 1457. Siku hiyo kikundi kidogo cha wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini waliungana katika kijiji cha Kunvald (Bohemia) kuanzisha jumuiya ya Kikristo iliyojitwa "Umoja wa Ndugu" (kwa Kicheki "Jednota Brastva"). Moravian si kanisa pekee linaloona vyanzo vyake katika ule Umoja wa Ndugu wa Bohemia, lakini ni kanisa pekee lenye uhusiano wa moja kwa moja kihistoria na kanisa hilo la zamani.

Kundi hili la Kunwald walikuwa kitengo kimoja cha harakati iliyoanzishwa na Hus miaka 50 iliyopita. Waliokutana Kunwald waliona kutumia silaha hakulingani na mafundisho ya Yesu Kristo. Walitaka kuishi pamoja kwa kuiga mfano wa maisha ya Wakristo wa kwanza. Walikataa vita na matumizi ya silaka wakajaribu kuishi kama ndugu Wakristo wakikaa pamoja, kufanya kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao.

Umoja huu ulienea haraka katika mikoa ya Bohemia na Moravia ukawa mwanzo wa kanisa linaloitwa leo "Moravian". Walitafsiri Biblia katika lugha yao, wakatunga kitabu cha pamoja cha nyimbo za kiroho kwa matumizi katika ibada na pia katekisimu.

Kutoka Kanisa la kale walipokea vyeo vya shemasi, presbiteri na askofu. Askofu wao wa kwanza alibarikiwa na askofu wa Kanisa la Wavaldo mwaka 1467 akaanzisha utumishi wao wa kiroho pamoja na makasisi na mashemasi.

Baada ya kustawi vizuri kanisa hili la Umoja wa Ndugu au "Ndugu wa Bohemia na Moravia" lilipata matatizo makali wakati wa Vita ya miaka 30 na baadaye.

Kuangamizwa kwa Umoja wa Ndugu baada ya vita ya miaka 30

hariri

Umoja wa Ndugu ulienea katika Bohemia na Moravia wakati wa karne ya 16 pamoja na matengenezo ya Kiprotestanti. Lakini mwaka 1618 wakubwa wa Bohemia walipata shida na Kaisari Ferdinand II aliyekuwa mfalme mpya; hii ilisababisha vita ya miaka 30. Katika vita hii kaisari aliyekuwa Mkatoliki mkali aliweza kutwaa Bohemia na Moravia akafuta ahadi zote za uvumilivu kwa wafuasi wa Umoja wa Ndugu.

Amani iliyomaliza vita ya miaka 30 iliamua ya kwamba madhehebu matatu pekee yatakubaliwa katika Dola Takatifu la Kiroma, yaani Wakatoliki, Walutheri na Wareformed. Umoja wa Ndugu haukutajwa, hivyo kanisa hili lilipigwa marufuku. Sehemu kubwa ya maeneo walipoishi waumini wake iliwekwa chini ya watawala Wakatoliki waliofunga makanisa yao na kuwalazimisha watu wote kuhudhuria misa katoliki pekee.

Sehemu ya Wakristo wa Umoja wa Ndugu walijaribu kuendeleza maisha yao ya kiroho kwa siri lakini shirika hizi za siri zilikandamizwa vikali. Polepole wengi walikimbilia nchi jirani walipovumiliwa kwa kiwango fulani. Wakimbizi wengi walienda nchi za Waprotestanti katika Ujerumani walipojiunga na kanisa la Kilutheri au Poland walipoweza kuanzisha shirika chache. Mtaalamu Amos Comenius alikuwa kati ya wakimbizi hao na mwaka 1648 alikuwa askofu wa kwanza wa ndugu huko Poland. Katika nchi za asili idadi ya waumini iliendelea kupungua; mbali na kukimbia nchi, wengine walipaswa kujiunga na Kanisa Katoliki au kanisa la Kilutheri.

Zinzendorf na kuanzishwa upya kwa Umoja wa Ndugu

hariri
 
Nikolaus von Zinzendorf

Mwaka 1722 familia za Wakristo kutoka Moravia waliowahi kufuata imani ya Umoja wa Ndugu kwa siri waliamua kukimbia nchi yao wakaelekea sehemu za Saksonia,kaskazini mwa Ujerumani. Huko mkabaila mdogo, kwa jina Nikolaus Ludwig von Zinzendorf, alikuwa mkuu wa eneo dogo la kujitegemea, yaani lenye uhuru wa kujiamulia, kwa sababu lilikuwa moja kwa moja chini ya Kaisari wa Dola Takatifu la Kiroma jinsi milki ya Ujerumani ilivyoitwa kwa muda mrefu. Zinzendorf aliwapokea wakimbizi hao kutoka Moravia katika eneo lake na kuwapa mashamba waweze kulima na kujengea nyumba. Aliwaruhusu kuendeleza mapokeo yao ya kale akajiunga nao. Kwa njia hiyo kilianzishwa kijiji cha Herrnhut (kwa Kijerumani: "chini ya ulinzi wa Bwana") kilichoendelea kuwa makao makuu ya kanisa la Moravian.

Zinzendorf alizaliwa katika familia ya Walutheri na tangu utotoni aliguswa na imani ya uamsho wa Kilutheri unaoitwa upietisti. Lakini alijuana na kupendana na watu wa kila aina, aliwasiliana pia na maaskofu Wakatoliki kadhaa, akiheshimu namna yao ya imani katika Kristo. Huyo Mlutheri aliwakubali kama Wakristo wa kanisa la pekee, hakudai wajiunge na Ulutheri, bali aliwaruhusu kuendeleza urithi wao akashirikiana nao.

Wakimbizi wengine waliopaswa kuondoka kwao kwa sababu za dini walifika pia. Mnamo Agosti 1727 wakazi wa Herrnhut walifanya mapatano kati yao kuhusu maisha ya Kikristo. Huu ulikuwa mwanzo wa "Umoja wa Ndugu ulioanzishwa upya". Zinzendorf hakutaka kuanzisha kanisa jipya; alilenga zaidi umoja wa kiroho unaokubali Wakristo wa madhehebu mbalimbali. Hivyo Herrnhut kulikuwa na vitengo vitatu ndani ya umoja: Wamoravia, Walutheri na Wareformed.

Kati ya misingi ya umoja ulikuwa utaratibu wa kutovuta waumini kutoka makanisa mengine kujiunga nao hata kama wahubiri wa Herrnhut walizunguka kote kwa nia ya kuamsha imani hai katika Kristo kati ya wafuasi wa makanisa au madhehebu yote ya Kikristo. Kwa hiyo Kanisa la Moravian katika sehemu zake asilia (yaani Ulaya ya Kati) linajua shirika zake za Moravian pamoja na shirika za marafiki wanaoendelea kuwa Wakristo wa kanisa la Kilutheri au Kireformed. Mwaka 1927 ndugu wa Herrnhut walikuwa na uamsho kati yao, wakaanza kuhubiri furaha katika Bwana kote Ulaya, lakini hawakupenda kuwavuta Wakristo wa madhehebu mengine kujiunga nao. Kwa namna hiyo Kanisa la Ndugu (walianza kuitwa sasa Wamoravia kwani wakimbizi walioanzisha Herrnhut walitoka Moravia) limebaki kwa makusudi kanisa dogo kule Ulaya.

Kwa sababu hiyo umoja mpya ulikua polepole. Makabaila waliopenda mwelekeo huo waliwakaribisha kuanzisha vijiji katika maeneo yao na kwa njia hiyo vijiji vya ndugu vilianzishwa katika sehemu mbalimbali za Ujerumani na pia Poland. Kwa jumla walijulikana kama "watu wa Herrnhut", hata wakijiita wenyewe "ndugu" tu au "Umoja wa Ndugu".

Mwaka 1742 sinodi ya umoja ilimchagua Yesu Kristo mwenyewe kuwa "mzee mkuu" wa kanisa hili.

Katika miaka ya kwanza walikuwa na ushirikiano wa namna ya kwamba wanaume na wanawake waliishi peke yao kadiri ya jinsia; hata mume na mke hawakuishi pamoja. Watoto walilelewa kwa pamoja baada ya kufikia umri wa miaka 2.

Lakini baada ya miaka makumi kadhaa waliacha muundo huu waliendelea tu kwa muda zaidi na maisha ya pamoja kwa vijana ambao hawakuoa au kuolewa bado.

Walikaza sana kazi za mikono na kuwafundisha vijana ufundi wakasifiwa na kutafutwa kwa ubora wa kazi yao lakini mwanzoni mapato yote yalikuwa kwa ajili ya mfuko wa umoja.

Katika utawala wake Umoja wa Ndugu uliendelea kutumia muundo wa Umoja wa kale: dikoni, presbiteri na askofu kama vyeo vya watumishi. Uongozi ulikuwa mikononi mwa wazee.

Misheni na uenezaji wa kimataifa

hariri

Wakati hawakutaka kuwavuta Wakristo kutoka makanisa mengine, walikuwa kupeleka imani kwa watu wasio Wakristo. Mwaka 1732 mkabaila Mdenmark rafiki wa Zinzendorf alitembelea Herrnhut akiongozana na mtumishi wake Anton mwenye asili ya Afrika. Anton aliwahi kuwa mtumwa katika visiwa vya Karibi aliyepelekwa Denmark na kuwa mtumishi huru wa mkabaila. Anton aliwasimulia habari za hali ya kusikitisha ya watumwa walionyimwa haki za kibinadamu, uhuru na hata haki ya kusali kanisani. Hapo ndugu wawili walijitolea kwenda Karibi hata wakipaswa kuwa watumwa ili kuwahudumia watu hao. Walifika 1732 kwenye kisiwa cha St. Thomas wakaanza kuhubiri kati ya watumwa wenye asili ya Afrika. Hii ilikuwa chanzo cha kazi ya misioni ya kanisa la Moravian ambalo ni kanisa la kwanza la Kiprotestanti lililokubali wajibu wa kueneza Injili kati ya watu wasiojua imani ya Kikristo bado.

Walikata shauri kwenda mahali pasipo na Wakristo na wamisionari wengine. Tangu mwaka 1732 ndugu wa Herrnhut walituma wamisionari kwenda visiwa vya Karibi walipowahudumia watumwa kutoka Afrika, halafu Greenland walipowahubiria Waeskimo, Afrika Kusini walipowalenga Wakhoikhoi dhidi ya upinzani wa Wazungu makaburu. Katika Amerika ya Kaskazini walianzisha kazi kwenye makoloni ya Uingereza yaliyokuwa baadaye taifa jipya la Marekani na huko walilenga hasa Waindio.

Maeneo mengine walipofika katika karne ya 18 ni pamoja na Amerika ya Kusini walipoanzisha kazi kati ya watumwa wenye asili ya Kiafrika na Waindio nchini Surinam iliyokuwa koloni la Uholanzi na katika majimbo ya Milki ya Urusi kando ya Bahari Baltiki yaani Latvia na Estonia. Ndani ya Ulaya Wamoravian waliunda pia shirika chache katika Ujerumani pamoja na Uswisi, Uholanzi, Denmark na Uingereza.

Tangu kurudishwa kwa uhuru wa dini katika Ulaya walianza kazi mpya pia katika nchi ya mababu, yaani Ucheki. Leo hii idadi kubwa ya Wamoravian katika Ulaya bara wako Uholanzi ambao ni watu waliohamia kutoka Surinam wenye asili ya Kiafrika.

Kutokana na kazi kubwa ya misioni ya kanisa hili, Wakristo Wamoravian walio wengi huishi Afrika na Amerika; ni wengi zaidi kuliko katika nchi asilia za Bohemia, Moravia na Ujerumani.

Mwisho wa karne ya 19 walialikwa pia kuanza kazi katika koloni changa la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (yaani sehemu kubwa ya Tanzania ya leo pamoja na Rwanda na Burundi) walipofika mwaka 1891. Waliowaalika walikuwa viongozi wa misheni ya Kilutheri ambao waliona nafasi kubwa ya kuhubiri na uchache wa watu waliokuwa tayari kwenda Afrika, kwa hiyo walikumbuka sifa za misheni ya Herrnhut wakapiga hodi huko.

Kanisa la Moravian katika Tanzania

hariri

Mnamo 1890 Walutheri wa Ujerumani waliona nafasi ya kuanza kazi katika Afrika ya Mashariki. Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki ilikuwa imeanzisha tayari kiini cha koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lakini kwa watu wengi nchini Ujerumani hali haikueleweka bado kama koloni kamili litatokea au la. Ila tu Walutheri wa Ujerumani waliona nafasi ya kuanza kazi, wakaona pia ya kwamba walikosa maarifa na watu wa kutosha, hivyo waliwaomba Wamoravian Wajerumani kuongozana nao, wakitegemea maarifa ya kanisa hili dogo lenye historia kubwa ya kimisionari. Awali Wamoravian walisita, lakini wakati huohuo walipokea zawadi kubwa ya fedha kutoka urithi wa mfanyabiashara aliyetaka itumiwe kwa "uenezaji wa Injili kati ya wapagani na kukomboa watumwa".

Viongozi Wamoravian walichukua zawadi hiyo kama alama ya Mungu, wakakubali ombi la Walutheri. Mwaka 1891 walipatana nao juu ya kuanza kazi kwenye eneo la Konde upande wa kaskazini wa Ziwa Nyasa, yaani eneo la Wanyakyusa. Walipatana ya kwamba Walutheri waangalie upande wa mashariki wa mdomo wa mto Mbalka katika ziwa uliopo kwenye longitudo ya 34 E na Wamoravian upande wa mashariki.

Kundi la kwanza la wamisionari 4 walioongozwa na Theodor Meyer walielekea Afrika ya Mashariki wakitumia njia kupitia mto Sambezi, mto Shire na ziwa Nyasa iliyohudumiwa na meli za Waingereza. Mwezi Septemba 1891 walipatana na chifu Mwakapalila juu ya kituo chao cha kwanza wakaunda kituo cha Rungwe kilichofuatwa na Utengule (Usafwa), Isoko (Undali) na Mbozi (Unyiha).

Mwaka 1896 Waingereza wa London Missionary Society waliwakaribisha Wamoravian kuendeleza kazi yao katika Unyamwezi, kwenye magharibi ya koloni. Ni kwamba wamisionari Waingereza walialikwa na mtemi Mirambo kuanza kazi katika eneo lake, lakini tangu kuingia kwa Wajerumani kama mabwana wapya matatizo yalitokea. Waliamua kujiondoa katika koloni la Kijerumani wakiwaomba Wamoravian kuendeleza kazi yao. Mwaka 1898 Urambo ilikuwa kituo cha Moravian. Vituo vilivyofuata ni Kipambawe na Sikonge.

Kanisa la Moravian duniani

hariri
 

Mwanzo wa karne ya 21 idadi ya Wakristo Wamoravian duniani ni takriban 1,100,000. Wengi wanaishi Afrika na idadi kubwa iko Tanzania katika majimbo 7.

Herrnhut siku hizi ni ushirika katika Jimbo la Moravian Ulaya Bara linalojumlisha Ujerumani, Uholanzi, Uswisi na Skandinavia. Hata huko idadi kubwa ya Wakristo ni Wamoravian waliohamia Uholanzi kutoka Surinam (iliyokuwa koloni la Uholanzi) au watoto wao, hivyo wengi wao wana asili ya Afrika.

Uanachama

hariri
Jimbo (mwaka wa kuanzishwa) au eneo la misioni Shirika Wanachama
Afrika 907.830
Burundi (jimbo la misioni) 40.000
Tanzania, Kaskazini (2007) 25 3.910
Tanzania, Mashariki (2007) 56 28.510
Tanzania, Rukwa (1986) 60 66.410
Tanzania, Kusini (1891) 170 203.000
Tanzania, Kusini Magharibi (1978) 211 300.000
Tanzania, Ziwa Tanganyika (2005) 30 32.100
Tanzania, Magharibi (1897) 61 104.000
Zambia (1989) 17 5.210
Afrika Kusini (1792/1737) 87 98.000
JD Kongo (2005) 80 21.500
Malawi (2007) 10 5.190
Karibi na Amerika ya Kilatini 204.980
Kosta Rika (1980/1941) 3 1.900
Guyana (1878/1835) 960
Honduras (1930) 85 34.450
Jamaika (1754) 65 8.100
Nikaragua (1849) 226 97.000
Surinam (1735) 67 30.000
Eastern West Indies (1732)
Trinidad, Tobago, Barbados, Antigua, St. Kitts, na Visiwa vya Virgin pmoja na St. Croix, St. John, St. Thomas, Tortola na Grenada
52 15.100
Honduras (jimbo la misioni) 16.870
Kuba (1997) (jimbo la misioni) 600
Amerika ya Kaskazini 39.150
Alaska -1885 22 1.690
Marekani Kaskazini (1741/1735)
Greenland, Kanada na madola ya kaskazini ya Marekani
89 20.530
Marekani Kusini (1753)
madola ya kusini ya Marekani
55 15.030
Labrador (1771/1752) (jimbo la misioni) 1.900
Ulaya 20.180
Jimbo la Ulaya Bara(1727)
Ujerumani, Uholanzi, Denmark, Uswidi, Uswisi, Albania, Estonia, Latvia
24 14.530
Jimbo la Britania (1742)
Ufalme wa maungano (Uingereza) na Ireland
30 1.200
Ucheki (1862/1457) 29 3.800
Ucheki II (jimbo la misioni) 650
Maeneo ya misioni
Belize, Guyana ya Kifaransa, Garifuna, Haiti, Kenya, Uhindi ya Kaskazini & Nepal, Rwanda, Zanzibar, Sierra Leone, Tansania Kiwele, Kivu na Katanga kwenye JD Kongo, Tanzania Iringa; Tansania Ruvuma/Njombe, Uganda, Peru
25.000
Total 1.112.120

Muundo

hariri

Leo hii Kanisa hilo linajitawala kwa utaratibu wa kisinodi kwenye ngazi ya kila jimbo (linalolingana na dayosisi katika makanisa mengine).

Majimbo ya Moravian hushirikiana kwenye ngazi ya taifa kama kuna majimbo zaidi ya moja katika nchi; kwa mfano majimbo ya Tanzania hushirikiana katika "Kanisa la Moravian Tanzania".

Majimbo yote ya dunia hukutana kila baada ya miaka 7 kwenye "Sinodi ya Umoja" na kuchagua "Kamati ya Umoja" (Unity Board).

Moravian wana ngazi 3 za utumishi wa kiroho ambao ni dikoni, presbiteri na askofu.

Askofu ana mamlaka ya kiroho tu, hana mamlaka ya kiutawala isipokuwa kama anachaguliwa kwa muda kuwa mjumbe wa kamati ya uongozi katika jimbo lake. Vinginevyo utawala hufuata utaratibu wa kisinodi maana watumishi viongozi wanachaguliwa na sinodi kwa muda wakitekeleza taratibu zilizoamuliwa na sinodi au kamati zake.

Majimbo

hariri

Kiutawala kanisa hili linajua ngazi za Jimbo la Umoja (Unity Province), Jimbo la Misioni (Mission Province) na Maeneo ya Misioni (Mission Area). Tofauti zinatokana na kiwango cha kujitegemea kwa kila sehemu. Kila Jimbo la Umoja linajitegemea kabisa; Jimbo la Misioni bado linasimamiwa na jimbo lingine katika shughuli kadhaa na Eneo la Misioni liko kabisa chini ya jimbo fulani.

Majimbo ya Umoja

hariri

Kila jimbo lina eneo maalumu:

Majimbo ya Misioni

hariri

Maeneo ya Misioni

hariri

Mradi wa Umoja

hariri