Makanisa Katoliki ya Mashariki
Makanisa Katoliki ya Mashariki ni madhehebu 23 ya Ukristo ambayo yanafuata mapokeo mbalimbali ya Mashariki katika ushirika kamili na Askofu wa Roma (Papa), hivyo pia na Kanisa Katoliki lote duniani.
Mapokeo hayo ni hasa yale ya Aleksandria (Misri), Antiokia (kihistoria jiji la Siria, leo nchini Uturuki), Konstantinopoli (kihistoria jiji la Ugiriki, leo nchini Uturuki), Armenia na Wakaldayo (kihistoria Mesopotamia, leo Iraq).
Baadhi ya mapokeo hayo yamezaa matawi, kama ya Misri yale ya Ethiopia na Eritrea.
Pamoja na hayo, kama Makanisa ya Waorthodoksi, hayo pia yanaambatana na utamaduni wa taifa, na kuyafanya yagawanyike kiutawala hata kama teolojia, liturujia n.k. zinaendelea kuwa zilezile kadiri ya mapokeo.
Kwa jumla yanakubali kuwa mapadre watu waliooa lakini hawana maaskofu waliooa.
Historia
haririChanzo cha Wakatoliki wa Mashariki ni tofauti: baadhi (hasa wale wa Kanisa la Wamaroni) wanadai kuwa wamedumu tangu mwanzo katika ushirika kamili na Papa, au walijikuta hawana tena mawasiliano na Patriarki wao kutokana na hali ya siasa, hivyo wakaanza kushirikiana na Kanisa la Kilatini (hasa Kanisa la Waalbania wa Italia). Wengine wametokana na makubaliano kati ya Papa na baadhi ya Waorthodoksi walioona umuhimu wa kuwa na umoja naye, hata wakakubali kutengana na Makanisa yao ya asili (kwa mfano Kanisa Katoliki la Kisiria la Malankara).
Kwa mengine mengi ni kwamba siku za nyuma kulikuwa na majaribio mbalimbali ya Mapapa ya kuunganisha Makanisa ya Kiorthodoksi na Kanisa la Roma baada ya mafarakano yaliyotokea hasa katika karne ya 5. Majaribio hayo kwa jumla yalishindikana, lakini pengine yalisababisha mafarakano mapya katika makanisa ya Kiorthodoksi ambamo askofu fulani alikubali mamlaka ya Papa na kuungana na Kanisa la Roma pamoja na wafuasi wake. Mara kadhaa hao walikuwa wanagombea vyeo vikuu katika Makanisa ya Kiorthodoksi, halafu wakaamua kuungana na Papa baada ya kutochaguliwa katika makanisa yao ya asili. Kwa sababu hiyo, wanatazamwa vibaya na Waorthodoksi.
Siku hizi Kanisa Katoliki limetamka wazi kwamba halina tenga mipango kama hiyo katika kulenga umoja na madhehebu mengine, bali linafuata njia za ekumeni.
Mtaguso wa pili wa Vatikano uliyazungumzia Makanisa Katoliki ya Mashariki na kuyatolea hati "Orientalium Ecclesiarum" ili yastawi upya na kuwa daraja kati ya Wakatoliki na Waothodoksi.
Takwimu
haririKuna Makanisa 23 yaliyounganika hivyo na Roma. Kati ya hayo makubwa zaidi ni:
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraina
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar
- Kanisa la Wamaroni
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Wamelkiti
Katika Afrika yako hasa Makanisa ya:
- Kanisa Katoliki la Kikopti (nchini Misri)
- Kanisa Katoliki la Kiethiopia (nchini Ethiopia )
- Kanisa Katoliki la Kieritrea (nchini Eritrea)
Leo Wakatoliki wa Mashariki ni asilimia 1.5 ya Wakatoliki wote, yaani kwa jumla kuna walau Wakristo milioni 18 katika makanisa hayo.
Kati yao wengi wanafuata mapokeo ya Kigiriki, Kimesopotamia na ya Kisiria.
Uongozi
haririKwa kawaida Makanisa hayo yangetakiwa kuongozwa na Patriarki, lakini upinzani wa Waorthodoksi umefanya Papa asiyapatie cheo hicho yale yasiyokuwa nacho tayari. Badala yake kilibuniwa kile cha Askofu mkuu kabisa, ambacho kina mamlaka karibu sawa katika madhehebu makubwa 4: Waukraina, Wasiro-Malabari, Wasiro-Malankara na Waromania.
Mengi ya makanisa haya yanakubali kuwapa upadri waamini waliooa, lakini maaskofu na sehemu ya mapadri hawaoi. Kwa kawaida wanachagua maaskofu wao wenyewe watakaothibitishwa na Papa, tofauti na Wakatoliki wengi katika Kanisa la Kilatini ambako ni Papa anayemteua askofu mpya moja kwa moja.
Katika nchi kadhaa Makanisa mbalimbali ya Kikatoliki yanaishi kandokando, kwa mfano Misri kuna Kanisa la Kikopti-Katoliki, la Kigiriki-Katoliki, la Kiarmenia-Katoliki, la Kikaldayo-Katoliki na la Kilatini.
Mapadri (lakini si maaskofu) Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, ya Kigiriki, ya Kiarmenia na ya Kikaldayo wanaweza kuwa na ndoa na huendesha Misa katika taratibu zao za kale; kumbe mapadri Walatini hawawezi kuwa na ndoa na hufuata liturujia ya Roma.
Wote hao hukubali uongozi wa Papa bila kushindana, yaani wengine wanahudumia Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, wengine wale wa mapokeo ya Kigiriki, wengine wale wa mapokeo ya Kiarmenia, wengine wale wa mapokeo ya Kikaldayo na wengine wale wa mapokeo ya Kiroma, hasa wahamiaji kutoka nchi nyingine.
Orodha
hariri- Makanisa sui iuris yanayofuata mapokeo ya Kigiriki (14):
- Kanisa Katoliki la Waalbania wa Italia (Italia), waamini 60,162.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Albania (Albania), waamini 1,000-4,000.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Belarus (Belarus), waamini 4,000-9,000.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Bulgaria (Bulgaria), waamini 6,000-10,000.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Korasya na Serbia (Croatia na Serbia), waamini 43,000.
- Kanisa Katoliki la Kibizanti la Ugiriki (Ugiriki na Uturuki), waamini 500-6,000.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Masedonia (Masedonia Kaskazini), waamini 11,374.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kimelkiti (Siria, Lebanon, Israel, Palestina, Jordan, Iraq, Kuwait, Misri, Sudan, Marekani, Kanada, Mexiko, Venezuela, Brazil, Argentina n.k.), waamini 1,568,239.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Romania (Romania, Marekani na Kanada), waamini 150,593.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kiruteni (Ukraina, Marekani, Ucheki), waamini 417,795.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Russia (Russia na China), waamini 30,000.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Slovakia (Slovakia, Kanada), waamini 211,208.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraina (Ukraina, Poland, Marekani, Kanada, Brazil, Argentina, Ufalme wa Muungano, Ujerumani na Skandinavia, Ufaransa, Australia, Italia n.k.), waamini 4,471,688.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Hungaria (Hungaria), waamini 262,484.
- Makanisa sui iuris yanayofuata mapokeo ya Aleksandria (2)
- Kanisa Katoliki la Wakopti (Misri), waamini 187,320.
- Kanisa Katoliki la Waethiopia (Ethiopia), waamini 70,832.
- Kanisa Katoliki la Waeritrea (Eritrea), waamini 167,722.
- Makanisa sui iuris yanayofuata mapokeo ya Antiokia (3)
- Kanisa la Wamaroni (Lebanon, Siria, Kupro, Israel, Palestina, Jordan, Misri, Afrika Magharibi na ya Kati, Argentina, Brazil, Marekani, Kanada, Mexiko, Australia n.k.), waamini 3,498,707.
- Kanisa Katoliki la Kisiria (Lebanon, Iraq, Jordan, Kuwait, Palestina, Misri, Sudan, Syria, Uturuki, Marekani, Kanada, Venezuela n.k.), waamini 195,765.
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malankara (India), waamini 458,015.
- Makanisa sui iuris yanayofuata mapokeo ya Mesopotamia (2)
- Kanisa Katoliki la Wakaldayo (Iraq, Iran, Lebanon, Jordan, Palestina, Misri, Siria, Uturuki, Marekani, Australia), waamini 628,405.
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar (India, Marekani), waamini 4,251,399.
- Kanisa sui iuris linalofuata mapokeo ya Armenia (1)
- Kanisa Katoliki la Armenia (Armenia, Georgia na nchi nyingine zilizokuwa zinaunda Urusi, Lebanon, Iran, Iraq, Misri, Syria, Uturuki, Israel, Palestina, Ugiriki, Romania, Ukraina, Ufaransa, Argentina na nchi nyingine za Amerika ya Kilatini, Marekani, Kanada n.k.), waamini 757,726.
Viungo vya nje
haririKwa jumla
hariri- Hati Orientalium Ecclesiarum ya Mtaguso wa pili wa Vatikano
- Hati Orientales omnes Ecclesias ya Papa Pius XII
- Codex Canonum Ecclesiarum Orientalium Ilihifadhiwa 5 Machi 2012 kwenye Wayback Machine. - Mkusanyo wa Sheria za Makanisa ya Mashariki (katika Kilatini pamoja na sehemu sambamba)
- Instruction for Applying the Liturgical Prescriptions of the Code of Canons of the Eastern Churches Ilihifadhiwa 25 Aprili 2009 kwenye Wayback Machine. - Hati ya Idara ya Papa kwa Makanisa ya Mashariki kuhusu liturujia
- Ujuzi wa msingi kuhusu Makanisa hayo Ilihifadhiwa 17 Mei 2011 kwenye Wayback Machine.
- Makanisa Katoliki ya Mashariki huko Marekani
- CNEWA Idara ya Papa inayosaidia Makanisa hayo
- Sura ya Idara ya Papa kwa Makanisa hayo
- Takwimu za Makanisa hayo Ilihifadhiwa 1 Februari 2014 kwenye Wayback Machine.
Moja moja
hariri- Kanisa la Wamaroni Ilihifadhiwa 29 Desemba 2016 kwenye Wayback Machine. Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malabar Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kibizanti nchini Marekani Tovuti isiyo rasmi
- Kanisa Katoliki la Waarmenia Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Romania Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Hungaria Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kimelkiti Ilihifadhiwa 11 Februari 2007 kwenye Wayback Machine. Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Ukraina Ilihifadhiwa 30 Julai 2008 kwenye Wayback Machine. Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malankara Ilihifadhiwa 25 Julai 2008 kwenye Wayback Machine. Tovuti rasmi
- Kanisa Katoliki la Kisiria la Malankara
- Jimbo kuu la Kibizanti la Pittsburgh Tovuti rasmi
- Kanisa la Kibizanti la Ugiriki Ilihifadhiwa 28 Septemba 2011 kwenye Wayback Machine.
- Kanisa Katoliki la Kigiriki la Romania
Makala hii kuhusu Kanisa Katoliki bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Makanisa Katoliki ya Mashariki kama historia yake au maelezo zaidi? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |