Matendo ya Mitume

(Elekezwa kutoka Mdo.)

Matendo ya Mitume ni kitabu cha Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo chenye sura 28.

"Huduma za Mitume" katika picha takatifu ya Fyodor Zubov, 1660.
Agano Jipya

Katika orodha ya vitabu 27 vya Agano Jipya kinashika nafasi ya tano baada ya Injili nne.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Jina asilia la Kigiriki ni "Πράξεις των Αποστόλων" (praxeis toon apostoloon): maana yake ni sawa na jina la Kiswahili.

Kinajulikana kwa jina hilo, kwa kuwa kinawatokeza hasa watu wawili ambao mwandishi aliwafahamu na kupenda kuwaenzi, yaani Petro mpaka sura ya 12, halafu Paulo.

Kwa namna ya pekee alikuwa mwanafunzi wa Paulo akamfuata mpaka kifo chake: hivyo si ajabu kwamba alipenda kushuhudia kazi zake na mateso yake kwa ajili ya Yesu Kristo na uenezi wa imani.

Mbali ya hao wawili, kitabu kinataja mwanzoni majina ya mitume 11 waliobaki baada ya kifo cha Yuda Iskarioti, na kueleza jinsi Mtume Mathia alishika nafasi yake, lakini hakuna habari zaidi juu ya wengi wao.

Kumbe kuna habari juu ya Wakristo wengine wa kwanza, hasa Stefano na Filipo mwinjilisti.

Pamoja na hayo, Luka anasisitiza kuwa mhusika na mtendaji mkuu wa ustawi wa Kanisa si binadamu yeyote, hata kama ni shujaa, bali ni Mungu tu.

Mwandishi

hariri

Kitabu chenyewe hakitaji jina la mwandishi lakini mapokeo ya kale na wataalamu karibu wote wa leo hukubaliana kwamba kimeandikwa na Mwinjilisti Luka, mganga anayetajwa katika nyaraka za Paulo kwa Wakolosai 4,14, Filemoni 24 na 2Timotheo 4,11.

Kabla ya kitabu hicho yeye aliandika Injili ya Luka, lakini peke yake kati ya Wainjili wote, hakuishia kuandika habari za Yesu tu, bali alizikamilisha kwa kuandika kitabu cha pili chenye historia ya mwanzo wa Kanisa.

Mpangilio

hariri

Mpangilio wa kitabu hicho unaelezwa katika 1:8, yaani kuonyesha jinsi imani hiyo ilivyoshuhudiwa toka Yerusalemu, Yudea na Samaria hadi mwisho wa dunia upande wa magharibi.

Ndiyo sababu kitabu kinaishia na habari za Paulo kufikia Roma na kuanza utume huko miaka 61-63, ingawa kuandikwa kiliandikwa kama miaka 20 baadaye.

Kuanzia Injili yake, Luka anaonekana alivyojitahidi kuzingatia ukweli wa historia, lakini pia jiografia: katika Injili yake mambo yote yanaelekea Yerusalemu, ambapo Yesu alikwenda kufa na kufufuka, na katika Matendo ya Mitume mambo yote yanaanzia Yerusalemu, ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia.

Tukipenda kujua historia ya wokovu ilivyoendelea baadaye, hatuna budi kufuata kitabu hicho tukilinganisha habari zake na zile tunazozipata hasa katika barua za mitume. Kwa namna ya pekee zile za Paulo tunaweza kuzipanga kwa faida katika mfululizo wa habari za maisha yake alizotuachia Luka, ingawa kuna utatanishi fulani.

Kanisa la Yerusalemu

hariri

Kabla ya kusimulia uenezi wa Ukristo, Luka aliandika habari za Kanisa mama, yaani lile la Yerusalemu.

Katika msingi wake tunaona mitume wakiwa wanasali pamoja na mama wa Yesu na waamini wengine.

Majina ya hao 11 yameorodheshwa tena, halafu pengo lililoachwa na msaliti Yuda Iskarioti likazibwa ili idadi muhimu ya 12 ikamilike tena.

Aliyeamua ifanyike hivyo ni Petro akitumia tayari mamlaka aliyoachiwa na Yesu, na akiweka masharti kwa mapendekezo ya watu, hasa kwamba mteule awe shahidi wa utume na ufufuko wa Yesu (Mdo 1).

Baada ya idadi hiyo kukamilika tena, Roho Mtakatifu akawashukia wote katika nafasi maalumu, yaani sikukuu ya Pentekoste, iliyotimiza Pasaka siku 50 baada yake (Mdo 2:1-41).

Safari hiyo alijitokeza kama upepo wa nguvu kubwa ajabu uliojaza nyumba nzima (yaani Kanisa lote) na kama ndimi za moto zilizowashukia mojamoja kila mwamini aliyekuwemo (kwa kuwa karama zake ni mbalimbali).

Hapo hao waoga, waliojifungia ndani kwa usalama, wakatoka nje na kuhubiria umati wa watu waliokusanyika kwa kufuata upepo.

Kwa kuwa siku hiyo ni ya hija walikuwepo Wayahudi na waongofu kutoka sehemu nyingi za ulimwengu, lakini kila mmoja aliwaelewa mitume kwa lugha yake mwenyewe.

Hivyo umoja wa binadamu uliovunjika Babeli katika kujenga mnara wa kiburi ukapatikana tena Yerusalemu kwa nguvu ya Yule aliye upendo wa Mungu.

Toka mwanzo Kanisa si la kabila la Yuda tu au la lugha ya Kiaramu tu, bali ni Kanisa Katoliki, yaani la mataifa yote na la lugha zote.

Bila shaka aliyesimama kwa niaba yake lote atoe hotuba ya kwanza na kufafanua matukio hayo pamoja na kumshuhudia Kristo mfufuka ni Petro: maneno yake yaliwachoma moyo wasikilizaji hata wakamuuliza wafanye nini.

Jibu likawa watubu na kubatizwa ili wapate msamaha na Roho Mtakatifu. Siku hiyo ya kwanza waamini wakawa hawapungui elfu tatu.

Luka ametuachia picha ya Kanisa mama hasa katika mihtasari mitatu (Mdo 2:42-47; 4:32-35; 5:12-16) ambayo inachora maisha ya Wakristo wa kwanza kama kielelezo kwa wale wote watakaofuata.

Kweli katika historia yote ya Kanisa wengi wakaja kujipima kwa kuangalia kielelezo hicho cha umoja katika roho na katika mali. Hasa watawa wengi wakaja kujaribu kutekeleza tena umoja huo mashirikani mwao na hivyo kuwachochea waamini wenzao wote. Umoja huo ndio sifa ya kwanza ya Kanisa na mpango wa Mungu kwa watu wote.

Mwanzoni umoja ulifanikiwa kwa namna ya pekee, ingawa hapo pia ulikuwa na kasoro tunavyosoma katika Mdo 5:1-11; 6:1 na katika vitabu vingine vyote vya Agano Jipya.

Kutokana na malalamiko ndani ya jumuia, mitume waliamua kuwashirikisha kazi yao katika ngazi ya chini watu saba: idadi hiyo katika Biblia inamaanisha mataifa, na kweli wote walikuwa na majina ya Kigiriki hata kama walikuwa Wayahudi (Mdo 6:2-6).

Tofauti za waamini hasa upande wa lugha na utamaduni zinadai daima ubunifu na nia njema zisije zikavuruga umoja.

Shida iliyotokea hapo ni utangulizi wa habari nyingine kuhusu Wakristo wa Kiyahudi kuwabana wenzao wenye asili ya Kipagani.

Katika Mdo 6-8 hao viongozi 7 wapya wanajitokeza kama mashujaa katika utume, ambao mwisho wake kwa Stefano ulikuwa ni kifodini.

Katika kusimulia tukio hilo la mwaka 36 hivi, Luka alisisitiza kuwa mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Stefano ni yaleyale yaliyomhusu Yesu: yaani upinzani dhidi ya mwalimu unaendelea dhidi ya wanafunzi wake.

Vilevile Stefano akakabili mateso kama alivyofanya Yesu akimkabidhi Bwana roho yake na kuwaombea watesi wake.

Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wamedhulumiwa katika nafasi mbalimbali, lakini dhuluma hiyo ya tatu ikawa kubwa zaidi na kusababisha wengi wakimbie Yerusalemu.

Lakini kwa mpango wa Mungu mtawanyiko huo ulichangia kueneza Injili.

Ukristo ulivyoanza kuenea

hariri

Kufuatana na mpangilio wa kitabu, Mdo 8 inaeleza jinsi Mungu alivyoongoza uenezi wa Kanisa kwa watu wasiokubaliwa na Israeli, yaani kwanza kwa Wasamaria waliokuwa maadui wakuu wa taifa teule, halafu towashi (yaani mwanamume mbovu) toka Ethiopia.

Katika nafasi hizo zote mbili Luka alisisitiza furaha iliyotokea kama dalili ya wokovu.

Juhudi za Filipo mwinjilisti zikaja kuthibitishwa na mitume kwa kuwawekea mikono Wakristo wapya wa Samaria.

Wakati uleule likatukia jambo lingine, la ajabu kabisa, ambalo kwa umuhimu wake limesimuliwa na Luka mara tatu, yaani uongofu wa Saulo/Paulo aliyekuwa mtesi mkuu wa Stefano na Wakristo wengine.

Ndiye aliyechaguliwa na Mungu awe mwenezi mkuu wa imani ya Kikristo, mtetezi mkuu wa uhuru wa Wakristo wa mataifa kuhusu sheria za Kiyahudi, tena mwandishi mkuu wa Agano Jipya, mwenye kufafanua mafumbo ya imani kwa undani kabisa.

Mungu alimteua awe chombo chake kiteule ili kuleta jina lake kwa mataifa (Gal 1:13-24; Mdo 9:1-31; Mdo 22:17-21): katika historia yote ya Kanisa baada ya Pentekoste hadi leo hakuna tukio lingine muhimu kuliko uongofu wake.

Lakini, kabla Luka hajasimulia umisionari wake, aliandika habari nyingine ya ajabu ambayo pia inapatikana mara tatu katika Matendo ya Mitume, yaani uongofu wa Kornelio na nyumba yake (Mdo 10).

Wapagani hao walijaliwa Roho Mtakatifu kabla hawajabatizwa, wakimsikiliza tu mtume Petro.

Hivyo Mungu alimuonyesha mkuu wa mitume nia yake kuhusu wokovu wa mataifa, naye Petro akalitangazia Kanisa kwamba Wapagani wasilazimishwe kufuata sheria za Kiyahudi.

Uamuzi huo uliofuata hiyo Pentekoste ya mataifa ilimfungulia Paulo mlango wa umisionari wake unaotawala Mdo 13-28.

Ingawa Wakristo wenye msimamo mkali wa Kiyahudi walikubali maneno ya Petro (Mdo 11:1-18), hawakuweza kumuunga mkono Paulo aliposisitiza kwamba wokovu unategemea imani kuliko utekelezaji wa Torati.

Basi, mvutano juu ya suala hilo ukaendelea kuvuruga maisha ya Kanisa kwa miaka mingi ya mbele.

Ni baada tu ya Petro kufungua mlango kwamba Mdo 11:19-26 inasimulia jinsi waliotawanyika baada ya uuaji wa Stefano walivyoeneza Ukristo huko walikohamia nje ya nchi takatifu, wakiwahubiria kwanza Wayahudi wenzao, halafu Wapagani.

Kitabu kizima kinafuata utaratibu huo: Paulo mwenyewe kila alipofika aliwaelekea Wapagani baada tu ya Wayahudi kukataa Injili.

Kati ya miji ambapo ilianzishwa jumuia ya waamini wengiwengi, muhimu zaidi ni Antiokia (mpakani kwa Siria na Uturuki wa leo): huko wafuasi wa Yesu walikuwa mchanganyiko mkubwa wa Wayahudi na mataifa, hivyo wakapewa jina jipya maalumu la Kiyunani (Wakristo).

Ndipo walipofanya kazi Barnaba aliyetumwa na mitume, Paulo aliyeitwa naye kumsaidia, pamoja na manabii na walimu wengine.

Wakati huohuo (mwaka 44 hivi) Herode Agripa alimuua Yakobo Mkubwa (mtume wa kwanza kumfia Yesu) akakusudia kumuua hata Petro, lakini huyo akahama Yerusalemu (Mdo 12:1-17) akafanya kazi huko na huko kabla hajahamia moja kwa moja Roma akiuletea mamlaka yake.

Safari za kimisionari za Paulo zilivyoanza (46-49)

hariri

Kanisa changa na motomoto la Antiokia likawa kituo cha umisionari kuanzia mwaka 46; kwa mara nyingine Roho Mtakatifu ndiye aliyechochea juhudi za kitume na kuteua watu wa kutumwa, yaani Barnaba na Paulo (Mdo 13:1-3).

Safari yao ya kwanza ilichukua miaka 3 katika kisiwa cha Kupro na mikoa ya kusini ya Uturuki wa leo (Mdo 13:16-51; 14:19-23).

Mtaguso wa Yerusalemu (49)

hariri

Waliporudi Antiokia walipaswa kupambana na Wakristo wa Kiyahudi kuhusu uwezekano wa mataifa kuokoka pasipo kutahiriwa.

Hatimaye suala likapelekwa Yerusalemu kwa Kanisa mama. Baada ya majadiliano marefu Petro akatoa neno la mwisho kwamba Wapagani wanaomuamini Yesu wasitwishwe mzigo usiobebeka wa kufuata sheria za Kiyahudi (Mdo 15:1-12).

Katika Gal 2:1-10 Paulo pia ametuachia kumbukumbu ya mtaguso huo akisisitiza kuwa mitume waliokuwepo (Yakobo, Petro na Yohane) walitambua rasmi karama ya kimisionari ya kwake na ya Barnaba na uhalali wake, wakiwaomba tu wachangishe pesa kati ya Wakristo wa mbali kwa ajili ya wenzao wa Yerusalemu wwnye hali ngumu.

Hiyo ilikuwa namna mpya ya kutekeleza upendo wa kidugu na kudumisha umoja wa Kanisa baada ya uenezi wake.

Masuala hayo yakadai uamuzi mwingine ili Wakristo wa Kiyahudi waweze kuendelea kushirikiana na wenzao wa mataifa pasipo kuogopa unajisi ambao ungewazuia wasifuate ibada zao.

Gal 2:11-14 inaeleza shida iliyotokea Antiokia: ingawa Paulo alimheshimu sana Petro, alipoona hafuati kwa unyofu uamuzi wa mtaguso hakusita kumkosoa kidugu hadharani ili aliepushe Kanisa na upotovu kuhusu suala la wokovu.

Basi, kadiri ya Mdo 15:13-35, Yakobo Mdogo aliyeachiwa uongozi wa Kanisa la Yerusalemu alichagua makatazo makuu manne kutoka Mambo ya Walawi akidai Wakristo wote wayashike kama mambo mazito kwa dhamiri ya Kiyahudi.

Uamuzi huo uliarifiwa kwa Wakristo wa Antiokia na mikoa ya jirani kwa wajumbe na barua.

Barua zikaendelea kuandikwa hata leo kwa lengo la kudumisha umoja na amani katika Kanisa, kwa kuwa ni kazi ngumu kuelewana kwa watu tofauti kama hao waliozoea kudharauliana kwa matusi kama “mbwa”.

Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)

hariri

Mdo 15:36-39 inasimulia ugomvi kati ya Paulo na Barnaba walipotaka kufunga safari tena (mwaka uleule 49).

Mungu hakuzuia ugomvi huo kusudi hao wawili waeneze zaidi neno lake wakienda sehemu tofauti.

Barnaba na Marko walielekea Kupro, kumbe Paulo alimchukua Sila na kufunga safari iliyodumu miaka mitatu, akielekea kwanza jumuia zile za bara alizoziunda miaka iliyopita (Mdo 15:40-16:5).

Paulo ni maarufu kwa juhudi zake za kueneza Ukristo mahali pengi palipokuwa bado, lakini pia tunajua upendo wake kwa watu aliowatangazia habari njema, na bidii zake kwa makanisa aliyoanzisha: alikuwa akiwaombea usiku na mchana, akiwaka hamu ya kuwatembelea, akiwaandikia barua za kusisimua ili kuwatia moyo au kuwakosoa, kutatua matatizo yao na kujibu maswali mbalimbali.

Pengine aliwatumia watu alioongozana nao: kati yao alimpendelea Timotheo akashirikiana naye mpaka kufa.

Kadiri ya Mdo 16:6-15, katika safari hiyohiyo kwenye mikoa mbalimbali ya Uturuki wa leo, huenda Luka pia akajiunga na msafara akifuatana na Paulo hadi kufa kwake.

Yeye anatia maanani uongozi wa Mungu ambaye kwanza aliwazuia mara mbili wasielekee walikokusudia, halafu kwa njozi alionyesha ni mapenzi yake wavukie Ulaya katika Ugiriki wa leo.

Inavyojulikana, Wagiriki walikuwa na hamu kubwa ya kupata maarifa kuliko wengine, halafu kubishana nao kwa ufasaha na kuwashinda. Katika mazingira hayo, falsafa na dini zilikuwa mada kuu na kuingiliana na hadithi za ajabuajabu kuhusu miungu, malaika na wengineo. Karibu barua zote za mitume zilikabili hatari hiyo, ambayo ikazidi kuwa kubwa na kuleta mafarakano katika Kanisa hasa katika karne II, ilipoitwa “Gnosis” (= ujuzi). Hasa Paulo alijitahidi kuishinda mapema iwezekanavyo.

Huko wakaanzisha Kanisa kwanza Filipi, halafu Thesalonike.

Kutokana na dhuluma za Wayahudi, Paulo alilazimika kuondoka akafika Athene, mji mkuu wa falsafa, akajaribu kutangaza Injili kwa ufasaha wa maneno ili kuwavuta hao watu wa elimu; kumbe akashindwa kabisa (Mdo 17).

Ndipo alipoelewa kuwa imani haitegemei akili na elimu, akaamua kuhubiri kwa unyofu tu mafumbo ya imani (1Kor 1:17-2:5).

Mdo 18:1-11 inasimulia mang’amuzi mengine aliyoyapata katika jiji la Korintho, lenye bandari mbili katika bahari tofauti zilizoleta urahisi wa kuvusha bidhaa toka moja hadi nyingine badala ya kuzisafirisha kwa meli kandokando ya rasi. Kutokana na umuhimu huo na wa kuwa makao makuu ya mkoa wa Akaya (Ugiriki kusini), pamoja na biashara kubwa, mchanganyiko wa watu, watumwa na makahaba wengi.

Huko alikaa mwaka mmoja na nusu kutokana na kufunuliwa na Yesu kwamba ana wateule wengi jijini.

Kweli utume wa Paulo ukazaa sana, ingawa kabla hajafika walikuwepo tayari Wakristo kadhaa kama Akula na Priska waliofukuzwa na mfalme Klaudio mwaka 49 watoke Roma pamoja na Wayahudi wote hasa kutokana na mabishano yao kuhusu Kristo.

Baada ya Sila na Timotheo kufika Korintho toka Thesalonike, walimpa Paulo ripoti kuhusu hali ya Kanisa la kule na kumuondolea wasiwasi: dhuluma zilikuwa zikiendelea lakini Wakristo wapya ni imara.

Kwa furaha Paulo akawaandikia barua tuliyonayo mpaka leo na ambayo ndiyo andiko la kwanza la Agano Jipya kwa kuwa ni wa mwaka 51 hivi.

Miezi michache baadaye akarudia kuwaandikia kutokana na taarifa nyingine zilizomtia tena wasiwasi.

Mwaka 52 Paulo aliondoka kwa hiari Korintho kuelekea Yerusalemu na Antiokia.

Njiani alihubiri kidogo Efeso, makao makuu ya mkoa wa Asia Ndogo (Uturuki Magharibi wa leo), lakini hakukubali kubaki muda mrefu zaidi, ila aliwaacha huko Priska na mumewe akiahidi kurudi, Mungu akipenda (Mdo 18:18-22).

Huo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya mseja na watu wa ndoa katika utume.

Mdo 18:24-28 inasimulia kwamba, baada ya Paulo kuondoka, alifika Myahudi wa Aleksandria, jina lake Apolo.

Kama vile wenzake wengi wa Misri alikuwa na elimu ya Kiyunani na ujuzi wa Biblia.

Tena alikuwa motomoto katika kufundisha habari za Yesu, ingawa hazijui sawasawa, hasa hana habari ya ubatizo wake mpya (kasoro hiyo ikaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa sababu baadhi ya wanafunzi wa Yohane Mbatizaji hawakumuamini Yesu, hivyo wakaendeleza ujumbe wa mwalimu wao).

Priska na mumewe wakamuelimisha zaidi, halafu wakampa barua ya kumtambulisha kwa Wakristo wa Korintho alipokwenda kuhubiri.

Wamisionari wa namna hiyo wakazidi kustawisha na kuvuruga makanisa walau mpaka mwisho wa wakati wa mitume.

Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)

hariri

Baada ya kukaa Antiokia mwaka mmoja na nusu Paulo akafunga tena safari akiyapitia makanisa ya Galatia na Frigia ili kuyathibitisha (Mdo 18:23).

Hatimaye akafika Efeso ambapo akabaki tangu mwaka 54 hadi 57, akifundisha kila siku na kueneza sana Injili katika mkoa mzima (Mdo 19:1-10).

Pamoja na hayo aliandika barua kadhaa, ambazo baadhi zimepotea, nyingine tunazo hadi leo (kwa Wagalatia, kwa Wafilipi, ile ya kwanza kwa Wakorintho, inawezekana Filemoni pia).

Luka hakusimulia mateso yote ya Paulo, kwa mfano alivyohukumiwa mwaka 56 hivi hukohuko Efeso (1Kor 15:32; 2Kor 1:8-9).

Akiwa kifungoni alifikiwa na mjumbe toka Filipi aliyemletea msaada wa pesa na wa huduma kwa niaba ya Wakristo wa mji huo.

Paulo kabla hajamrudisha alipenda kuwaandikia barua nzuri ya shukrani pamoja na kuwaeleza sababu ya kufungwa (Fil 4:10-20).

Humo tunaona wazi Paulo alivyokuwa na furaha hata kifungoni, kwa kuwa alizoea kuridhika na kila hali: kwake muhimu ilikuwa tu kumfikia Kristo.

Mdo 19:21-20:1 inasimulia alivyohama Efeso kutokana na matatizo kuzidi, akaelekea Makedonia na Ugiriki.

Toka huko alipata nafasi ya kuhubiri huko Iliriko, yaani Albania ya leo kwenda kaskazini (Rom 15:19).

Wakati huo alipata habari tofauti kabisa kuhusu Wakorintho, akawaandikia tena na tena kabla hajawaendea kwa mara ya tatu.

Ingawa Paulo alikaa Efeso miaka mitatu, moyo wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka alivyotabiriwa atafanya kazi hata mbali zaidi.

Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya magharibi, yaani Roma na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia.

Ila kabla ya kwenda huko alipanga kuleta mchango kwa Wakristo wa Yerusalemu.

Basi, mwishoni mwa miezi mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) yaani mwanzoni mwa mwaka 58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo ambapo Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi huko ambao walibatizwa Yerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30.

Ukristo baada ya Paulo kufika Roma

hariri

Paulo kupeleka mchango Yerusalemu (Mdo 20:16-21:36) ndio mwisho wa kipindi cha utume wake mkubwa zaidi.

Sura tisa za mwisho za Matendo ya Mitume zinatusimulia kinaganaga habari zake kuanzia 58 hadi 63, ambapo karibu miaka yote alikaa kifungoni akisubiri kesi (Mdo 23:12-24; 24:22-25:22; 28:11-16,23:30).

Bila ya shaka ilikuwa ya majaribu makubwa kwake, lakini ilimpa nafasi ya kutafakari mafumbo ya wokovu kwa undani zaidi tena, na ya kumshuhudia Kristo mbele ya wafalme (Agripa II na nyumba ya Kaisari) alivyotabiriwa.

Kwa Luka ni muhimu sana kwamba Paulo alifika Roma na kuanza huko kazi yake ya utume, kiasi kwamba hakuendelea kuandika kilichofuata.

Hasa kwamba mwaka 64 mfalme Nero alianza dhuluma za serikali dhidi ya Wakristo zilizoendelea mpaka 313, ingawa si mfululizo.

Petro na Paulo waliuawa mjini Roma kati ya mwaka huo na mwaka 68, wakiliachia Kanisa la mji huo usimamizi wa makanisa yote.

Kuhusu kipindi hicho tuna ushahidi wa vitabu mbalimbali vya Kipagani, vya Kiyahudi na vya Kikristo.

Baadhi yake ni vile vya mwisho vya Agano Jipya ambavyo mkazo wake unaelekea miundo ya Kanisa (uchungaji) kuliko umisionari (uvuvi).

Katika hiyo miaka ya mwisho ya ufunuo, Wakristo wa mataifa wakazidi kuwapita wale wa Kiyahudi kwa idadi na kwa umuhimu.

Nafasi ya Yerusalemu katika Kanisa ulizidi kupungua kutokana na hali ya nchi, yaani vurugu kati ya Wayahudi, Wayunani na serikali ya kikoloni.

Mwaka 62 Yakobo, ndugu wa Bwana na kiongozi wa Kanisa la huko, aliuawa na Wayahudi.

Tangu mwaka 66 hadi 73 hao walipigania uhuru wakashindwa; mwaka 70 Yerusalemu ulitekwa tena na Waroma na kuteketezwa pamoja na hekalu lake.

Kuanzia hapo hadi leo dini ya Kiyahudi imebaki haina ukuhani wala sadaka; nguvu yake ni katika masinagogi inapofanyika ibada ya Neno la Mungu chini ya walimu wa sheria.

Maangamizi hayo yalizidi kutenganisha Wakristo na Wayahudi, hasa kwa sababu Wakristo wa Yerusalemu walikimbilia ng’ambo ya Yordani badala ya kupigania uhuru, halafu wakarudi mjini mpaka vita vya pili vya Kiyahudi (132-135) ambapo Waroma wakabomoa tena Yerusalemu na kuwafukuza Wayahudi wote wasiweze hata kuingia wilayani na kuona kwa mbali mlima wake.

Marejeo

hariri

Viungo vya nje

hariri

Tafsiri ya Kiswahili

hariri
  • [1] Agano Jipya kwa lugha ya Kiswahili.
  Makala hii kuhusu mambo ya Agano Jipya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Matendo ya Mitume kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.