Bonaventura wa Bagnoregio

(Elekezwa kutoka Bonaventura)

Mtakatifu Bonaventura (Bagnoregio, Italia, 1217 hivi – Lyon, Ufaransa, 15 Julai 1274) alikuwa mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo, halafu padri, askofu na kardinali, ambaye aling'aa kwa mafundisho, maisha matakatifu na matendo bora hasa katika kufanikisha Mtaguso wa pili wa Lyon.

Bonaventura alivyochorwa na Francisco de Zurbarán.

Kwa miaka mingi aliongoza kwa busara shirika lake lote kufuata roho ya mwanzilishi, Fransisko wa Asizi,

Mtu wa sala na utendaji, alitokeza wingi wa ujuzi na moyo wa ibada aliokuwanao hasa katika ufundishaji na uandishi akawa mmojawapo kati ya wale waliochangia zaidi ulinganifu wa imani na utamaduni katika karne XIII, ambapo Ukristo wa magharibi ulizaa matunda bora hata upande wa elimu na sanaa mbalimbali.

Kisha kufa alitangazwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa na Kanisa Katoliki kila mwaka tarehe 15 Julai[1].

Maisha yake kabla ya kuwa mtumishi mkuu wa shirika

hariri
 
Legenda maior, 1477

Mwaka aliozaliwa haujulikani kwa hakika, bali ni kati ya 1217 na 1221. Mahali ni Civita di Bagnoregio, karibu na Viterbo, leo katika mkoa wa Lazio, Italia ya Kati.

Wazazi wake walikuwa mganga Yohane Fidanza na Maria wa Ritello; kwanza aliitwa kwa jina la baba yake, lakini alipoingia utawani aliitwa Bonaventura (yaani Bahati Njema). Inasemekana jina hilo lilikuwa shangilio la Fransisko wa Asizi alipomuona bado mtoto kabla hajamponya kimuujiza ulemavu wake baada ya kufa na kutangazwa mtakatifu.

Alizidi kumfahamu Fransisko alipokwenda Paris (Ufaransa), kwa masomo (1235) na kukuta huko Ndugu Wadogo waliokuweko tangu mwaka 1219. Baada ya kupata stashahada ya Arts, aliamua kujiunga nao, kwa kutambua kazi ya Kristo ndani ya tapo lao, akavikwa kanzu ya shirika mwaka 1243.

“Nakiri mbele ya Mungu kwamba kilichonifanya zaidi nipende maisha ya mwenye heri Fransisko ni kuwa yalifanana na mwanzo na ustawi wa kwanza wa Kanisa. Kanisa lilianza na wavuvi sahili, halafu likatajirika na walimu maarufu na wenye hekima sana; utawa wa mwenye heri Fransisko haukuanzishwa na busara ya watu bali na Kristo”..

Aliendelea kusoma katika chuo kikuu cha Paris (Ufaransa), hadi mwaka 1253, akipata digrii ya Biblia na teolojia, halafu akafundisha huko (1253-1257) akifuata falsafa ya Plato na teolojia ya Agostino wa Hippo.

Mazingira ya chuo hicho yalimwezesha kufahamiana na walimu na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na kustawisha mtazamo wake wa pekee, uliokuwa na Kristo kama kiini.

Upinzani wa maaskofu na maparoko dhidi ya Ndugu Wadogo na ya Wadominiko ulipoungwa mkono na chuo hicho hazikupingwa tu ruhusa kadhaa walizopewa, na haki yao ya kufundisha chuoni, bali msingi wenyewe wa mtindo wa maisha wao. Upya ulioletwa na mashirika hayo mawili haukueleweka kwa urahisi wakati huo, lakini pia kulikuwa na kijicho na wivu.

Baada ya Bonaventura na Thoma wa Akwino kuutetea kwa kuonyesha ulivyolingana na Injili, Papa Aleksanda IV alilaani upinzani na kusifu sana mtindo huo wa maisha (1257).

Mwaka huohuo mwalimu huyo kuchaguliwa kuwa Mtumishi mkuu wa shirika lake kukawa ushindi mwingine mkubwa chuoni.

Ni kwamba Mtumishi mkuu aliyemtangulia, Yohane wa Parma (1247-1257), alipoamua kujiuzulu, ingawa mkutano mkuu ulitaka aendelee, hakurudi nyuma. Hatimaye walimuomba walau amchague mwandamizi wake, naye akamtaja Bonaventura, mtu wa Mungu na wa watu, mwema kwa wote na mwenye kipawa cha uongozi.

Kufuatana na tabia yake chanya, alikubali hali halisi ya shirika na kujitahidi kuliepusha na hatari za nje na za ndani alizoziona mapema kabla hajachaguliwa.

Akiwa mtumishi mkuu wa shirika

hariri

Kwa miaka 17 (1257-1274) alikuwa Mtumishi mkuu wa shirika, akatembelea na kuwaandikia barua ndugu zake za kiroho, waliokuwa tayari zaidi ya 30,000 na kuenea Ulaya, Afrika Kaskazini, Mashariki ya Kati na hata China, akijitahidi kudumisha umoja kwa kulinganisha misimamo tofauti ya watawa walioelekea zaidi sala na ufukara na ya wale walioelekea zaidi elimu na utume.

Chini yake mkutano mkuu wa Narbone (1260) ulitunga katiba maarufu ambayo ilikusanya na kusawazisha taratibu za maisha ya kila siku ikawa msingi wa katiba za karne zilizofuata. Lakini alijua kwamba sheria haziwezi kutosha zisipoendana na umoja wa vipeo na malengo.

Mzizi wa uongozi wake ulikuwa daima sala na tafakuri. Muungano na Kristo ulimfanya asiishie kuagiza, bali aangaze watawa na kuwaleta kwa Yesu. Hivyo vitabu mbalimbali vya [[maisha ya Kiroho ]] alivyoviandika vinatokeza namna yake ya kuongoza.

Kati yake, maarufu zaidi ni “Itinerarium Mentis in Deum” (yaani “Safari ya Akili kwa Mungu”), kinachoongoza kwa hatua sita kutoka ujuzi wa Mungu unaopatikana kwa kuchunguza ulimwengu na vipawa vya roho yetu hadi shibe ya muungano na Utatu kumpitia Kristo, kama alivyojaliwa Fransisko.

Sawa na huyo, Bonaventura alifurahia uzuri wa viumbe, alivyoandika mwanzoni mwa kitabu: “Asiyeangazwa na mng’ao huo wa vitu vilivyoumbwa ni kipofu; asiyeamshwa na kelele hiyo ni kiziwi; asiyemsifu Mungu kwa kazi hizo zote ni bubu; asiyegeukia Asili Kuu kutokana na maelekezo hayo ni mpumbavu”.

Ulimwengu wote unatangaza upendo wa Mungu mwema, na maisha ya binadamu ni safari ya kumuendea. Lakini hawawezi kupanda kwake kwa nguvu zao bila kuvutwa naye. Ndiyo sababu sala ni ya lazima kama mama na chanzo cha kwenda juu.

Karibu na mwisho aliandika: “Ukitaka kujua jinsi mambo hayo yote yanavyotokea, uiulize neema, si elimu; uiulize hamu, si akili; uuulize mlio wa sala, si juhudi ya kusoma; umuulize bwanaarusi, si mwalimu; umuulize Mungu, si mtu; uuulize ukungu, si weupe; usiulize mwanga, bali moto unaowasha nafsi yote na kuizamisha ndani ya Mungu kwa mpako wake tamu sana na mapendo motomoto zaidi”.

Mashambulizi ya kutisha yalitokea pia ndani ya shirika, upande wa ndugu “wa Kiroho” walioelekea kufuata uzushi wa abati Yohakimu wa Fiore, aliyefariki mwaka 1202, baada ya kutabiri umonaki mpya utakaoleta hali mpya katika Kanisa na jamii. Hao walidhani Ndugu Wadogo ndio waliotimiza utabiri huo wakajiona hawahitaji tena kuwa chini ya miundo ya zamani, wala chini ya uongozi wa shirika na wa Kanisa, kinyume cha utiifu mnyenyekevu wa Fransisko.

Dhidi ya upotoshaji huo, Bonaventura alisoma kwa makini maandishi yote ya abati huyo, na hatimaye akawafafanulia wanashirika wa Paris teolojia ya historia kwa usahihi. Mafundisho yake hayakutimia ila yalikusanywa na wasikilizaji katika kitabu “Hexaëmeron”, yaani ufafanuzi wa uumbaji kwa siku sita ambazo toka zamani zilitazamwa kumaanisha vipindi sita vya historia.

Hata hivyo yeye alivitafsiri upya kwa kumuonyesha Kristo kama kiini cha historia, si mwisho wake. Ndiyo sababu karne XIII ilipiga hatua kubwa upande wa ujuzi, wa utakatifu na wa umisionari vilevile, hasa kwa njia ya mashirika mapya ya Ombaomba. Karama ya Fransisko ilithibitisha kwamba Kristo anaweza kusababisha daima hali mpya kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Basi, ndani ya Kanisa lilelile kuna maendeleo, na teolojia yenyewe haiwezi kuishia katika kurudiarudia tu mafundisho ya mababu wa Kanisa. Kwake teolojia inalenga hasa hekima, nayo inakumbatia kwanza ujuzi unaopatikana hasa kwa sala, halafu wema unaotokana na ujuzi huo kupitia matendo. “Imani imo akilini namna ambayo inasababisha mapendo".

Kwa mfano, ujuzi wa kwamba Kristo alikufa kwa ajili yetu haubaki ujuzi, bali unakuja kugeuka upendo. Ni upendo huo, si kiburi cha akili, unaotakiwa kuchochea teolojia kwa lengo la kuzidi kumjua Mpenzi. Hivyo kwa Bonaventura upendo unashika nafasi ya kwanza, kwa kuwa lengo la binadamu ni kuungana na Mungu katika upendo, na humo kupata heri.

Katika msimamo huo na katika teolojia yake yote aliathiriwa sana na Fransisko aliyechanganyikiwa na Yesu na kuwaka moto kama Serafi, aina bora ya malaika kadiri ya Pseudo-Denis. Katika maandishi ya Msiria huyo wa karne VI Bonaventura alichota hasa wazo la kwamba, katika kumuelekea Mungu, mtu anaweza akafikia hatua ambapo akili haioni tena, ila upendo unakwenda mbele na kupenya fumbo la Mungu. Hilo linalingana kabisa na karama ya Kifransisko inayopita michakato ya akili kwa kumpenda Kristo msulubiwa.

Katika uongozi wake Bonaventura alijipangia kulinganisha uaminifu kwa kanuni na mabadiliko shirikani, akionyesha hayo hayaendi kinyume cha nia ya mwanzilishi. Kwa ajili hiyo ilimpasa kuziondolea lawama za hao ndugu "wa Kiroho" msingi wowote kwa kupigania uaminifu kwa wito wa shirika. Mwenyewe alikubali kwa moyo matamko ya Mapapa juu ya kanuni kama ufafanuzi rasmi wa wachungaji wakuu wa Kanisa na wa shirika pia.

Kielelezo cha Fransisko wa Asizi kilitakiwa kuzingatiwa na wote kwa umoja, bila kupishana kuhusu namna ya kukitazama. Kwa ajili hiyo alitunga kitabu rasmi cha maisha yake kilichopitishwa na mkutano mkuu hata ukaagiza maandishi yote yaliyotangulia juu ya Fransisko yateketezwe. Ndivyo shirika lilivyopotewa kwa muda mrefu na habari nyingi muhimu juu ya mwanzilishi.

Bila kusema uongo, kitabu alichokiandika (“Legenda Maior”, kilichofupishwa katika “Legenda Minor”) kinaleta baadhi tu ya matendo na mafundisho ya Fransisko yaliyochaguliwa kwa makini ili kumchora kama mfano kamili wa Yesu msulubiwa na kusisitiza mang’amuzi yake bora ya kiroho, lakini kwa kuficha mambo fulanifulani kuhusu kipeo cha udogo.

Aliheshimu ufukara kama sifa kuu na utukufu wa shirika, ingawa alikubali mabadiliko yaliyotokea, yaani konventi kubwa mijini n.k. Kwake elimu pamoja na utume ni sehemu ya lazima ya utendaji wa Kifransisko. Kwa ajili hiyo alikubali ruhusa lilizopewa shirika, ingawa kwa udogo alipenda kupatana na Maaskofu na maparoko.

Basi, chini ya uongozi wake shirika likatulia, kwa jinsi alivyoweza kulinganisha upendo kwa Fransisko na furaha kwa mabadiliko, hamu ya kuishi upwekeni muda mrefu pamoja na ndugu “wa Kiroho” na utetezi wa konventi za mijini.

Akiwa kardinali askofu

hariri

Baada ya kuteuliwa na Papa Gregori X kuwa kardinali mnamo Mei 1273, akiwa askofu wa Albano Laziale, kwa agizo lake aliandaa kwa bidii Mtaguso wa pili wa Lyon ulioanza mwaka 1274 hasa kwa lengo la kurudisha umoja kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi, lakini katikati yake akafa na muungano uliofikiwa ukaja kuvunjika tena.

Kutukuzwa kwake baada ya kifo

hariri

Mwaka 1434 walipohamisha masalia yake, walikuta kichwa hakijaoza. Jambo hilo liliharakisha hatua ya kumtangaza mtakatifu iliyochukuliwa na Papa Sixtus IV tarehe 14 Aprili 1482.

Halafu tarehe 14 Mei 1588 akatangazwa na Papa Sixtus V kuwa mwalimu wa Kanisa kwa jina la Doctor Seraphicus, yaani Mwalimu wa Kiserafi. Hilo lilitokana na umotomoto wa upendo uliokuwa tunda la maisha yake ya sala ya dhati na unaojitokeza katika maandishi yake mengi.

Sala zake

hariri

Lo, uzuri usiosemeka wa Mungu mkuu, lo, mng’ao safi kabisa wa nuru ya milele!

Wewe ni uhai unaohuisha kila uhai, mwanga unaoangaza kila mwanga!


Bwana Yesu Kristo, unichome mpaka kiini cha moyo wangu kwa donda lile tamu la kuletea wokovu la upendo wako.

Unijaze kwa ule upendo motomoto, mnyofu na mtulivu uliomfanya mtume wako mtakatifu Paulo atamani kutengwa na mwili wake awe nawe.

Roho yangu ikuonee shauku, ikijaa daima hamu ya makao yako ya milele.

Vitabu alivyoviandika

hariri
  • Breviloquium
  • Collationes de decem praeceptis
  • Collationes de septem donis Spiritus Sanctis
  • Collationes in Hexaemeron
  • Commentaria in quattuor libros sententiarum Magistri Petri Lombardi
  • De mysterio Trinitatis
  • De perfectione vitae ad sorores
  • De reductione artium ad theologiam
  • De Regno Dei descripto in parabolis evangelicis
  • De scientia Christi et mysterio Trinitatis
  • De sex alis Seraphin
  • De triplici via
  • Itineriarium mentis in Deum
  • Legenda Sancti Francisci
  • Lignum vitae
  • Officium de passione Domini
  • Quaestiones de perfectione evangelica
  • Soliloquium
  • Summa theologiae
  • Vitis mystica

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri
  • LaNave, Gregory F. "Bonaventure," in Paul L. Gavrilyuk and Sarah Coakley (eds.), The Spiritual Senses: Perceiving God in Western Christianity, Cambridge: Cambridge, University of Cambridge, 2011, 159-173.
  • Quinn, John Francis. The Historical Constitution of St. Bonaventure's Philosophy, Toronto: Pontificial Institute of Mediaeval Studies, 1973.
  • Tavard, George Henry. From Bonaventure to the Reformers, Milwaukee: Marquette University Press, 2005 (Marquette Studies in Theology). ISBN 0-87462-695-1 ISBN 9780874626957.

Viungo vya nje

hariri
 
WikiMedia Commons