Mgawanyo wa Afrika

Mgawanyo wa Afrika (kwa Kiingereza: Scramble for Africa) ulikuwa uvamizi wa bara hilo uliofanywa na baadhi ya nchi za Ulaya katika miaka 1881 - 1914. Kwa muda huo Wazungu kutoka asilimia 10 ya maeneo waliteka asilimia 90 na kuacha huru Ethiopia na Liberia tu.

Ramani ya tamaduni na falme za Afrika kabla ya ukoloni (500 KK - 1500 BK).
Kulinganisha Afrika miaka 1880 na 1913.

Malengo yao yalikuwa hasa utajiri wa malighafi na utaifa.

Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885 ulioitishwa na chansela Otto von Bismarck huko Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, ili kupanga mgawanyo unaohesabiwa kama chanzo cha ukoloni huo. Matokeo yake yalikuwa "Azimio la Berlin" (Kongoakte; General Act of the Berlin Conference) lililoweka msingi wa ugawaji wa Afrika kati ya madola ya Ulaya.

Kufifia kwa ukoloni mwanzo wa karne ya 19 hariri

Kwa sehemu kubwa ya karne ya 19 mataifa ya Ulaya hayakutafuta utawala katika Afrika. Vituo mbalimbali vilivyoanzishwa katika karne za 17 na 18 kwenye pwani za Afrika zilikwama tena kwa sababu gharama hazikulingana na faida.

Hasa kupigwa marufuku kwa utumwa katika milki ya Uingereza kulipunguza faida za makoloni hayo yailiyokuwa madogo na zaidi vituo vya kibiashara na vya kijeshi kwa ajili ya mawasiliano baharini. Biashara ya watumwa iliendelea bado kuelekea makoloni ya Kireno ya Brazil na nchi za Kiislamu.

Mataifa ya Ulaya hayakujaribu sana kupanua utawala wao barani. Sifa za koloni zilipungua kwa jumla kwa sababu nchi mbalimbali zilipoteza makoloni yao baada ya kuasi kwa walowezi huko Amerika ya Kaskazini dhidi ya Uingereza (ndio mwanzo wa Marekani), huko Amerika ya Kusini dhidi ya Hispania (ndio mwanzo wa mataifa mapya ya Amerika Kusini) na uasi wa watumwa wa Haiti dhidi ya Ufaransa.

Watu wengi waliuliza maswali juu ya faida ya kuwa na koloni kama wachache walitajirika lakini umma ilipaswa kugharimia vita na majeshi ya kutetea koloni.

Kuangalia upya Afrika hariri

Lakini katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Afrika ilianza kuvuta upya wafanyabiashara wa Ulaya kwa sababu mapinduzi ya viwandani yalihitaji mafuta yaliyotokana na mawese ya kutia grisi mashine za viwandani. Mafuta hayo yalipatikana katika nchi za Guinea hasa eneo la delta ya mto Niger.

Serikali za Ulaya zilijaribu kuhakikisha kipaumbele na faida kwa wafanyabiashara kutoka kwao. Hali hii ilianzisha mashindano kati ya nchi hizo.

Kuanzia mwaka 1869 mfereji wa Suez ulifunguliwa na kufupisha safari kati ya Ulaya na Asia. Uingereza, Ufaransa na Italia zilishindana kukamata vituo vya kijeshi kando la mlangobahari wa Bab el Mandeb kwa nia ya kuhakikisha athira yao juu ya njia hiyo ya mawasiliano.

Safari za Henry Morton Stanley katika beseni ya mto Kongo ziliondoa mabaka meupe kwenye ramani za Afrika. Mfalme Leopold II wa Ubelgiji alimwajiri Stanley aliyejenga misingi ya utawala wa Leopold huko Kongo. Wakati huohuo taarifa za Stanley juu ya eneo la Kongo iliwasha tamaa za kujipatia malighafi za eneo hili.

Mashindano juu ya utawala wa Afrika hariri

Katika miaka tangu 1880 nchi mbalimbali za Ulaya zilianza kuvamia sehemu za bara la Afrika kwa sababu tofautitofauti. Sababu muhimu ilikuwa maendeleo makubwa ya teknolojia katika nchi za viwandani yaliyosababisha uwezo wao wa kijeshi kupita uwezo wote wa jamii ambazo hazikufikia bado hali hii. Kwa lugha nyingine: gharama za kuvamia nchi isiyo ya viwandani zilipungua haraka. Mwendo huo ulisababisha mashindano kati ya nchi zilizoendelea na hofu ya nchi nyingine kupata kipaumbele.

Chanzo cha Mkutano wa Berlin hariri

Chanzo cha mkutano ulikuwa fitina kati ya Ureno na Shirika la Kimataifa la Kongo la mfalme Leopold II wa Ubelgiji juu ya utawala wa mdomo wa mto Kongo.

Ureno ilikumbuka mkataba wake wa karne zilizopita na ufalme wa Kongo na kudai pwani yote pamoja na mdomo wa mto mkubwa ni yake. Leopold II alitegemea njia ya mto kwa mawasiliano yake, alihitaji kanda la eneo hadi baharini.

Uingereza ulisimama upande wa Ureno. Chansela Bismarck wa Ujerumani alikuwa tayari kupatanisha nchi hizo na kuongeza msimamo wake wa kidiplomasia.

Habari za mkutano ziliharakisha jitihada za kusimamisha bendera za Ulaya kwenye ardhi ya Afrika. Mwaka 1884 uliona wimbi la matangazo ya maeneo ya Afrika kuwa eneo lindwa la Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia. Mara nyingi sababu ya kutangaza madai au eneo lindwa ilikuwa hofu ya nchi nyingine kusimamisha bendera yake palepale.

Wapelelezi na wafanyabiashara walijitahidi kuweka msingi wa koloni kabla ya mkutano wa Berlin kwa tumaini la kwamba maazimio yake yatathibitisha madai yao.

Kati ya wapelelezi waliokazia jitihada alikuwa Mjerumani Karl Peters, aliyezunguka katika Afrika ya Mashariki[2]dhidi ya ushauri wa serikali yake, akikusanya sahihi za machifu waliotia sahihi mikataba naye bila kuelewa walichofanya.

Kabla ya mkutano na wakati wa mkutano wenyewe Peters aliweka msingi wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ya baadaye.

Washiriki wa Mkutano wa Berlin hariri

Nchi zifuatazo zilishiriki mkutano chini ya uenyekiti wa Chansella Bismark:

Agenda za Mkutano wa Berlin hariri

Agenda za mkutano zilikuwa na vipengele vifuatavyo:

  1. Uhuru wa biashara katika beseni la mto Kongo
  2. Biashara ya utumwa
  3. Azimio kuhusu nchi katika beseni ya Kongo kutokuwa upande wowote
  4. Usafiri kwa maji kwenye mto Kongo
  5. Usafiri kwa maji kwenye mto Niger
  6. Kanuni za kutwaa sehemu za Afrika kwa njia inayokubalika kati ya mataifa makubwa ya Ulaya

Maazimio ya Mkutano wa Berlin hariri

  1. Kuhusu uhuru wa biashara katika beseni la mto Kongo mkutano ulikubali mipaka ya eneo la beseni ya Kongo, uhuru kwa nchi zote kufanya biashara hapo na kuingiza bidhaa bila ushuru au malipo ya forodha. Haki za wananchi wenyeji zilitakiwa kulindwa. Kila taifa lenye mamlaka katika eneo hilo lilipewa wajibu wa kulinda haki za wenyeji na kufanya juhudi za kuboresha hali ya maisha yao, kuzuia biashara ya watumwa na kuhakikisha uhuru wa dini, hasa kwa wamisionari Wakristo lakini pia kwa dini zote zilizofuatwa katika eneo hili.
  2. Kuhusu biashara ya watumwa mataifa yote yalipaswa kuzuia biashara hiyo na kuadhibu wote waliotenda kinyume
  3. Kuhusu eneo la Kongo kutokuwa upande wowote mataifa yote yalitakiwa kuepukana na hatua za kivita kati yao ndani ya beseni ya Kongo.
  4. Kuhusu usafiri kwa maji washiriki walipatana kutumia kanuni za Mkutano wa Vienna 1815 zinazoipa meli za mataifa yote haki ya kupita na kutumia mito ambayo ni njia za kimataifa.
  5. Kuhusu kanuni kwa kutwaa sehemu za Afrika washiriki walipatana kuwa a) kila nchi inayotaka kutangaza mamlaka juu ya sehemu za pwani za Afrika inapaswa kuwaarifu mataifa mengine[3] na b) mamlaka inaweza kukubalika kuwa kama iko hali halisi yaani kama nchi inayodai mamlaka juu ya sehemu fulani inaweza kuhakikisha uhuru wa biashara na usalama wa kusafiri.

Matokeo ya Mkutano wa Berlin hariri

Vipengele vingi vya mapatano ya Berlin havikutekelezwa. Lakini azimio la Berlin lilitambua Shirika la kimataifa la Kongo la mfalme Leopold II.

Mapatano yaliyotokea kando ya mkutano (bila kutajwa ndani ya azimio) yalipandisha cheo cha shirika hilo hadi kuwa kama serikali halisi. Uingereza ilitaka kuzuia upanuzi wa Ufaransa katika eneo la Kongo. Bismark aliona afadhali mfalme dhaifu wa Ubelgiji apate nafasi huko kuliko mataifa makubwa yaliyohofiwa kufunga mlango wa utajiri wa Kongo kwa wafanyabiashara toka nchi nyingine.

Hali hii ilifungulia nafasi kwa ujanja wa mfalme Leopold II aliyeendelea kutangaza maeneo ya shirika yake kuwa "Dola huru la Kongo" lililokuwa mali yake binafsi. Hii ilikuwa chanzo cha utawala wa kinyama na unyonyaji wa Kongo uliokuwa kipindi kibaya cha ukoloni kushinda nchi zote. Mamilioni ya wakazi wa Kongo walilazimishwa kukusanya malighafi, hasa mpira, na mamilioni walikufa.

Mengineyo ni kwamba mkutano ulisababisha kuongezeka kwa juhudi za mataifa ya Ulaya kugawa Afrika kati yao. Mnamo 1895 zilibaki nchi za kujitawala Ethiopia, Liberia pamoja na jamhuri za makaburu Dola Huru la Oranje na Transvaal pekee. Jamhuri mbili za makaburu zilitwaliwa na Uingereza kwa njia ya vita baina ya miaka 1899 na 1902. Miaka 15 baada ya mkutano Afrika yote iligawiwa tayari kati ya mataifa ya Ulaya isipokuwa nchi za Liberia na Ethiopia.

Makoloni yaliyokuweko Afrika hariri

Nchi za Afrika ziliwekwa rasmi chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya mara baada ya Mkutano wa Berlin.

Nchi zilizojenga ukoloni huo Afrika zilikuwa Uingereza, Ufaransa, Ureno, Ujerumani, Uhispania, Italia na Ubelgiji. Uholanzi karne za nyuma ilikuwa na Afrika Kusini.

1. Ubelgiji ilikuwa na maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda ya leo

2. Uingereza ilikuwa na Afrika Kusini, Botswana, Cameroon ya Kiingereza, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Misri, Nigeria, Shelisheli, Sierra Leone, Somaliland, Sudan, Swaziland, Tanganyika, Uganda, Zanzibar, Zambia, Zimbabwe na sehemu nyingine kwa muda.

3. Ufaransa ilikuwa na Algeria, Benin, Cameroon, Chad, Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jibuti, Komoro, Gabon, Guinea, Madagaska, Mali, Mauritania, Moroko, Niger, Senegal, Togo, Tunisia na sehemu nyingine kwa muda.

3. Ujerumani ilikuwa na Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (leo Namibia), Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (tangu 1922 Burundi, Rwanda na Tanganyika), Kamerun na Togo, lakini baada ya vita vikuu vya kwanza ilinyang'anywa kila mojawapo; zilikuwa maeneo ya kudhaminiwa kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa na kuweka chini ya Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Afrika Kusini.

4. Italia ilikuwa na Eritrea, Libya na Somalia ya Kiitalia; pia Ethiopia kwa miaka mitano tu (1936-1941).

5. Ureno ilikuwa na Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau, Msumbiji, Sao Tome na Principe

6. Hispania ilikuwa na Guinea ya Ikweta, sehemu za Moroko na Sahara Magharibi.

Vyanzo hariri

Marejeo mengine hariri

  • Aldrich, Robert. Greater France: A History of French Overseas Expansion (1996)
  • Atkinson, David. "Constructing Italian Africa: Geography and Geopolitics." Italian colonialism (2005): 15–26.
  • Axelson, Eric. Portugal and the Scramble for Africa: 1875–1891 (Johannesburg, Witwatersrand UP, 1967)
  • Boddy-Evans, Alistair. "What Caused the Scramble for Africa?" African History (2012). online
  • Brantlinger, Patrick. "Victorians and Africans: The genealogy of the myth of the dark continent." Critical Inquiry (1985): 166–203. online
  • Chamberlain, Muriel Evelyn. The scramble for Africa (4th ed. Routledge, 2014) excerpt and text search
  • Curtin, Philip D. Disease and empire: The health of European Troops in the Conquest of Africa (Cambridge University Press, 1998)
  • Darwin, John. "Imperialism and the Victorians: The dynamics of territorial expansion." English Historical Review (1997) 112#447 pp. 614–42.
  • Finaldi, Giuseppe. Italian National Identity in the Scramble for Africa: Italy's African Wars in the Era of Nation-building, 1870–1900 (Peter Lang, 2009)
  • Förster, Stig, Wolfgang Justin Mommsen, and Ronald Edward Robinson, eds. Bismarck, Europe and Africa: The Berlin Africa conference 1884–1885 and the onset of partition (Oxford UP, 1988) online
  • Gifford, Prosser and William Roger Louis. France and Britain in Africa: Imperial Rivalry and Colonial Rule (1971)
  • Gifford, Prosser and William Roger Louis. Britain and Germany in Africa: Imperial rivalry and colonial rule (1967) online.
  • Gjersø, Jonas Fossli (2015). "The Scramble for East Africa: British Motives Reconsidered, 1884–95". Journal of Imperial and Commonwealth History 43 (5): 831–60. doi:10.1080/03086534.2015.1026131.  Unknown parameter |s2cid= ignored (help); Unknown parameter |doi-access= ignored (help)
  • Hammond, Richard James. Portugal and Africa, 1815–1910: a study in uneconomic imperialism (Stanford University Press, 1966) online
  • Henderson, W.O. The German Colonial Empire, 1884–1919 (London: Frank Cass, 1993)
  • Hinsley, F.H. ed. The New Cambridge Modern History, Vol. 11: Material Progress and World-Wide Problems, 1870–98 (1962) contents pp. 593–40.
  • Klein, Martin A. Slavery and colonial rule in French West Africa (Cambridge University Press, 1998)
  • Lovejoy, Paul E. Transformations in slavery: a history of slavery in Africa (Cambridge University Press, 2011)
  • Lloyd, Trevor Owen. Empire: the history of the British Empire (2001).
  • Mackenzie J.M. The Partition of Africa, 1880–1900, and European Imperialism in the Nineteenth Century (London 1983) online
  • Middleton, Lamar. The Rape Of Africa (London, 1936) online
  • Oliver, Roland, Sir Harry Johnston and the Scramble for Africa (1959)
  • Pakenham, Thomas (1992) [1991]. The Scramble for Africa. London: Abacus. ISBN 978-0-349-10449-2. 
  • Penrose E.F., ed. European Imperialism and the Partition of Africa (London 1975).
  • Perraudin, Michael, and Jürgen Zimmerer, eds. German colonialism and national identity (London: Taylor & Francis, 2010).
  • Porter, Andrew, ed. The Oxford history of the British Empire: The nineteenth century. Vol. 3 (1999) online pp 624–650.
  • Robinson Ronald, and John Gallagher. "The partition of Africa", in The New Cambridge Modern History vol XI, pp. 593–640 (Cambridge, 1962).
  • Robinson, Ronald, and John Gallagher. Africa and the Victorians: The official mind of imperialism (Macmillan, 1961). online
  • Rotberg, Robert I. The Founder: Cecil Rhodes and the Pursuit of Power (1988) excerpt and text search;
  • Sarr, Felwine and Savoy, Bénédicte, The Restitution of African Cultural Heritage, Toward a New Relational Ethics (2018) http://restitutionreport2018.com/sarr_savoy_en.pdf Archived 26 Machi 2021 at the Wayback Machine.
  • Sanderson G.N., "The European partition of Africa: Coincidence or conjuncture?" Journal of Imperial and Commonwealth History (1974) 3#1 pp. 1–54.
  • Stoecker, Helmut. German imperialism in Africa: From the beginnings until the Second World War (Hurst & Co., 1986.)
  • Thomas, Antony. Rhodes: The Race for Africa (1997) excerpt and text search
  • Thompson, Virginia, and Richard Adloff. French West Africa (Stanford UP, 1958)
  • Vandervort, Bruce. Wars of Imperial Conquest in Africa, 1830―1914 (Indiana UP, 2009).
  • Wesseling, H.L. and Arnold J. Pomerans. Divide and rule: The partition of Africa, 1880–1914 (Praeger, 1996.)

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mgawanyo wa Afrika kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. iliyokuwa baadaye Kongo ya Kifaransa, leo Jamhuri ya Kongo
  2. maeneo ya Tanzania bara ya leo
  3. kwa shabaha ya kuepukana na kugongana kwa madai ya mataifa tofauti juu ya eneo lilelile