Yesu

mtu mkuu wa Ukristo (6 au 4 KK - AD 30 au 33)
(Elekezwa kutoka Yesu katika Ukristo)

Yesu (kwa Kiebrania יֵשׁוּעַ, Yeshua, kifupisho cha יהושע‎, Yeoshua, yaani "Mungu anaokoa") alikuwa Myahudi mwanamume aliyeishi miaka 2000 hivi iliyopita (labda 6 KK - 30 BK).

Yesu Kristo.
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa


Yesu.

Alizaliwa na bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, huko Bethlehemu ya Uyahudi. Maisha yake yalikuwa ya pekee kwa kuwa alifahamu vitu vingi kwa mfano: sheria hata kuwazidi walimu wa sheria japokuwa hakusomea sheria. Alifanya pia maajabu mengi.

Ndiyo maana leo hii zaidi ya nusu ya wanadamu wote wanamuamini kuwa Mwana wa Mungu (ndio wanaoitwa Wakristo) au walau nabii (hasa Waislamu).

Kutokana na umuhimu wake katika historia ya binadamu, kwa kawaida miaka yote inahesabiwa kuanzia ujio wake (ulivyokadiriwa na Denis Mdogo kimakosa katika karne ya 6).

Misingi ya ujuzi wetu juu yake

hariri
 
Papyrus P52, iliyoandikwa kwa Kigiriki mwaka 125 hivi, inahesabika kuwa andiko la zamani zaidi kutufikia kuhusu Yesu. Ina sehemu za Injili ya Yohane; mbele 18:31-33, nyuma 18;37-38.

Yesu hakuacha maandiko yoyote. Habari zake zinapatikana hasa katika Biblia, kwa namna ya pekee katika Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.

Nje ya Ukristo kuna habari fupi kuhusu Yesu katika maandiko ya waandishi wa Roma, Wagiriki na Wayahudi. Habari hizo zinaangaliwa sana kwa sababu zimetungwa na watu wasiomwamini Yesu kidini. Kwa ujumla zinathibitisha ya kwamba Yesu alikuwepo, na kwamba wakati hao walipoandika alikuwa na wafuasi huko Roma na ya kwamba awali Waroma hawakuelewa tofauti kati ya wafuasi wake na Wayahudi.

Kati ya waandishi hao muhimu ni hasa:

1. Mtaalamu Myahudi Flavius Josephus: huyo aliandika mnamo 90 BK kitabu cha "Antiquitates Judaicae“ (Habari za historia ya Wayahudi) akitaja kifo cha "Yakobo ndugu wa Yesu“ (sura ya 20, 200).

2. Mwandishi Mroma Tacitus: huyo aliandika mnamo mwaka 117 ya kwamba Kaisari Nero alishtaki kikundi cha “Chrestiani” ya kuwa wamechoma moto mji wa Roma. Aliongeza: “Mtu ambaye ni asili ya jina hilo ni Chrestus aliyeuawa wakati wa Tiberio kwa amri ya Pontio Pilato” (Annales XV,44).

3. Mwandishi Mroma Svetonius: huyo alimtaja “Chrestos” katika kitabu chake juu ya maisha ya Kaisari Klaudio (25,4) ya kwamba huyu amesababisha fujo kati ya Wayahudi wa Roma hivyo Kaisari aliwafukuza wote mjini.

4. Mwanasiasa Mroma Gaius Plinius Caecilius Secundus: huyo aliacha barua kadhaa zinazotaja Wakristo mnamo mwaka 100 BK. Alimwuliza Kaisari Traianus jinsi ya kushughulikia Wakristo waliokataa kutoa sadaka mbele ya sanamu za Kaisari.

Mazingira yake

hariri

Nchi ambayo Yesu alizaliwa akafundisha ni nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu zamani za Abrahamu, ni nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile waliyoirudia kutoka utumwani Babeli.

Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani tangu Yesu alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa huru, bali chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji waliowekwa na wakoloni.

Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37 KK-4 KK) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya Uyahudi karne iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa madaraka na uzinifu wake.

Vilevile maliwali wa Kirumi waliowekwa pengine kutawala nchi au sehemu fulani walionyesha mara nyingi ukatili na dharau kwa Waisraeli na dini yao, hata kusababisha chuki na mapigano kati ya jeshi na wananchi. Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 BK.

Mbali na hayo, utawala wa Dola la Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya leo, kwa jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne za kwanza za Kanisa.

Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi wa mawasiliano kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa lugha ya kimataifa (Kiyunani, yaani Kigiriki cha zamani), ilichangia kasi ya uenezaji wa habari njema (Injili).

Lugha hiyo ndiyo iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili vitabu vyao viwafaidishe watu wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua vizuri.

Lugha mama ya Yesu na ya Mitume ilikuwa Kiaramu ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole kilishika nafasi yake kati ya Wayahudi kuanzia karne ya 6 KK.

Hao wote walitokea mkoa wa Galilaya, uliokuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na mataifa), kiasi kwamba huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za Kiyunani hata wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea).

Kati ya mikoa hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi baada ya uhamisho wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili la Yerusalemu.

Maisha yake

hariri

Dionisi Mdogo, mmonaki aliyeanzisha (mwaka 533 hivi) mtindo wa kuhesabu miaka tangu kuzaliwa Yesu kurudi nyuma (K.K.) au kwenda mbele (B.K.), alikosea hesabu zake. Leo tunakisia Yesu alizaliwa mwaka 6 hivi K.K. kwa sababu alizaliwa Bethlehemu chini ya Herode Mkuu aliyefariki tayari mwaka 4 K.K.

Huyo alipojaribu kumuua mtoto Yesu, familia takatifu ilikimbilia Misri mpaka baada ya kufa kwa Herode. Hapo ikarudi Galilaya hata Yesu akajulikana kwa jina la kijiji cha Nazareti kilichodharauliwa na Wagalilaya pia. Ndipo alipokulia na kuishi akifanya kazi ya ufundi.

Hivyo Yesu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kijijini akiwatii wazee wake Maria na Yosefu na kufanya kazi za mikono. “Alishuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii” (Lk 2:51). Kwa namna hiyo ametuachia kielelezo cha utakatifu katika maisha ya familia na ya kazi ambayo ndiyo njia ya kawaida ya kukomaa kiutu na kumtumikia Mungu. “Mnyenyekeane katika kicho cha Kristo” (Ef 5:21).

Mwaka 26 hivi BK ndugu yake Yohane Mbatizaji aliacha maisha ya jangwani alikokulia na kuanza kuhubiri toba kandokando ya mto Yordani. Kwa kuwa Waisraeli walikosa manabii kwa muda mrefu, na walitamani sana ukombozi, walimuendea kwa wingi hata wakamtia hofu Herode Antipa.

Ingawa huyo akamfunga mapema akamuua, kazi ya Yohane ilikuwa imetimia kwa sababu aliweza kuwaandaa Waisraeli wengi (hasa watu wadogo na wakosefu) wampokee Yesu aliyebatizwa naye. Katika nafasi hiyo Yohane alimtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.

Ndipo Yesu naye alipoanza kuhubiri, lakini pia kutenda miujiza ya kila aina, akapata haraka wafuasi wengi. Kati yao akachagua Mitume wake 12 kama msingi mpya wa taifa la Mungu badala ya Israeli ya kale.

Alifanya kazi hizo kuanzia Galilaya, akitangaza ujio wa ufalme wa Mungu, kwa maana ya kwamba ufalme uliotazamiwa na Wayahudi umewajia kwa njia yake.

Ingawa hakupitia shule yoyote ya Biblia, Yesu alionekana anafundisha vizuri kuliko walimu wa sheria wa kawaida, kama mtu mwenye mamlaka juu ya Torati.

Mafundisho yake yalilingana na yale ya Mafarisayo kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao wa kwanza.

Kijicho na upinzani vikazidi hasa Yerusalemu, walipoanza kufanya njama za kumuua. Ingawa Yesu alijua hayo, alijikaza kwenda katika huo mji mtakatifu autangazie habari njema na kufia huko.

Baada ya kupokewa kwa shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka 30 (au 33) akakamatwa na baraza la Israeli kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na Mungu, halafu akakabidhiwa kwa liwali wa Kirumi aliyekuwa na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo.

Baada ya kikao ambapo Wayahudi walitafuta kisingizio cha kisiasa, Ponsyo Pilato akalazimika kuagiza Yesu asulubiwe, na kisha kufa kwake kaburi lilindwe na askari.

Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza kuwatokea wanafunzi wake wa kike na wa kiume kwa muda wa siku arubaini, halafu akapaa mbinguni mbele ya macho yao.

Habari hizo zikatangazwa kwa sauti tu kwa miaka kadhaa, halafu zikaanza kuandikwa.

Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Mwinjili Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.

Ni muhimu kujua maisha ya Yesu kwa sababu matendo na maneno yake, pamoja na kimya na sala yake, na hasa kifo na ufufuko wake, yote yanatufunulia Baba na matakwa yake kwetu. “Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote” (Lk 24:19).

Baada ya kujua maisha ya Yesu tunapaswa kujilinganisha naye hadi aundwe na kuishi ndani mwetu akitushirikisha uhai, kifo na ufufuko wake. “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu, na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu… Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu!” (Gal 2:20; 4:19).

Sala zake

hariri

(Math 11:25-26)

Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako

(Yoh 11:41-42)

Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.

(Yoh 17:1-26)

Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako, na ulimwengu umewachukia, kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo, ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

(Mk 14:36)

Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.

(Mk 15:34)

Eloi, Eloi, lama sabakthani? (maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?)

(Lk 23:46)

Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

Imani juu yake

hariri

Waumini wake wanaunda Kanisa la Kikristo ambalo linapatikana leo katika madhehebu mengi. Karibu wote wanamwamini kuwa Mungu aliyechukua umbile la mwanadamu au, kwa lugha nyingine, kuwa Mwana wa Mungu.

Kwa imani hiyo, Yesu ni Mungu na mtu kwa pamoja, ndiyo sababu ni mshenga pekee kati ya Mungu na watu. “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu” (1Tim 2:5). “Katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9). Hivyo ni Mungu kweli na mtu kweli.

Umungu na utu wa Yesu vimeunganika katika nafsi moja visichanganyikane, kwa kuwa ndani yake hali hizo mbili zinatenda kila moja ya kwake. “Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, ‘Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu’” (Mk 15:39).

Mwana wa Mungu tangu atwae mwili ni mtu kamili mwenye akili na utashi wa kibinadamu. Katika umoja wa nafsi yake vipawa hivyo vinatenda kulingana na Umungu anaouchanga na Baba na Roho Mtakatifu milele. “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake” (Yoh 14:10).

Hapa duniani Yesu alizaliwa na Bikira Maria kama malaika alivyomuambia: “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo, hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Lk 1:35).

Hata hivyo Wakristo wachache wanaamini kuwa yeye ni mtume wa pekee wa Mungu ila si Mungu.

Katika dini ya Uislamu, Yesu anajulikana kama Nabii Isa. Waislamu wanaamini kuwa yeye alikuwa nabii wa Mungu ila hakuwa mwana wa Mungu wala Mungu.

Maadhimisho yake

hariri

Maisha yake yamekuwa msingi wa sikukuu mbalimbali zinazosheherekewa katika nchi nyingi duniani, kama vile Noeli au Krismasi (kuzaliwa kwake), Epifania (kuonekana kwake na kubatizwa kwake), Majilio (kuandaliwa kwa ujio wake wa kwanza na kutarajia ujio wa pili), Kwaresima (mafungo na mateso yake), Ijumaa Kuu (kifo chake); muhimu kuliko zote ni Pasaka (kufufuka kwake).

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri
      .
      . http://books.google.com/books?id=UCBBY_O88uYC&pg=PA113#v=onepage&q&f=false.
      . http://books.google.com/?id=37uJRUF6btAC&printsec=frontcover#v=onepage&q&f=false.

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Yesu kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.