Uganda

nchi ya Afrika Mashariki ya Kati
(Elekezwa kutoka Jamhuri ya Uganda)
Jamhuri ya Uganda (Kiswahili)
Bendera ya Uganda Nembo ya Uganda
(Bendera ya Uganda) (Nembo ya Uganda)
Lugha rasmi Kiswahili Kiingereza
Mji Mkuu Kampala
Mji Mkubwa Kampala
Serikali Jamhuri
Rais Yoweri Museveni
Eneo km² 241,038
Idadi ya wakazi 42,729,036 (2018)
Wakazi kwa km² 177
Jumla la pato la taifa kinaganaga Bilioni $46.38[1]
Jumla la pato la taifa kwa kila mtu $1,060.43[1]
Pesa Shilingi ya Uganda
Kaulimbiu "kwa mungu na nchi yangu"
Wimbo wa Taifa Ewe Uganda, Ardhi ya Uzuri/Urembo
Uganda katika Afrika
Saa za Eneo UTC +3 (Wakati wa Afrika Mashariki)
Mtandao .ug
Kodi ya Simu +256

Uganda ni nchi ya Afrika ya Mashariki. Imepakana na Kenya upande wa mashariki, Sudan Kusini upande wa kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa magharibi, Rwanda na Tanzania upande wa kusini.

Uganda inamiliki sehemu ya ziwa la Viktoria Nyanza ikipakana huko na Kenya na Tanzania.

Uganda ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na wa miundo mingine mbalimbali ya kimataifa.

Jina

Jina Uganda lina asili yake katika ufalme wa Buganda ulioko kusini mwa nchi pamoja na mji mkuu, Kampala.

 
Ramani ya Uganda

Jiografia

Tazama piaː Orodha ya milima ya Uganda; Orodha ya maziwa ya Uganda; Orodha ya visiwa vya Uganda; Wilaya za Uganda

Uso wa nchi umepata tabia yake kutokana na maziwa makubwa, mito, milima ya juu na tambarare.

Upande wa kusini nchi imepakana na Ziwa Nyanza Viktoria ambalo kwa eneo ndilo ziwa kubwa kuliko yote ya Afrika. Maziwa makubwa mengine upande wa magharibi ni Ziwa Albert na Ziwa Edward.

Mto mkubwa ni Nile inayopita nchi yote kati ya Ziwa Viktoria hadi Ziwa Albert na kuendelea hadi mpaka wa Sudani ikiitwa mwanzoni Nile ya Viktoria na baadaye Nile ya Albert.

Milima ya Ruwenzori ni kati ya milima mikubwa kabisa ya Afrika baada ya Kilimanjaro na Mlima Kenya.

Kusini kuna ardhi yenye rutuba na kilimo kinastawi vizuri.

Historia

Makala kuu: Historia ya Uganda

Historia ya kale

Eneo la Uganda limeona uhamiaji wa vikundi vingi waliowazidi wenyeji asili (walioishi huko tangu miaka 50,000 kama si 100,000 KK).

Kusini liliingiliwa hasa na wakulima Wabantu. Kaskazini iliona kufika kwa Waniloti kwa mfano Waluo na baadaye Karimojong.

Tangu karne ya 15 himaya mbalimbali zilianza kujengwa na kati ya hizo ni hasa falme za Buganda, Ankole, Bunyoro Toro zilizoendelea kuwa muhimu hadi kuja kwa ukoloni na kwa kiasi fulani kama urithi wa kiutamaduni hata katika Uganda ya kisasa.

Ukoloni

Karne ya 19 iliona kufika kwanza kwa Waarabu na baadaye kwa Wazungu. Kila mmoja alileta dini yake yaani Uislamu na Ukristo wa Kikatoliki na wa Kianglikana.

Katika mashindano juu ya Afrika ya Kati Waingereza walifaulu katika kushindana na Waarabu, Wafaransa na Wajerumani. Walienea kwa mapatano na Buganda wakisaidiana kukomesha upinzani kutoka falme za jirani.

Baadaye Waingereza walikuwa na nguvu ya kutosha kuamua hata mambo ya ndani ya Buganda wakatangaza Uganda wote kuwa nchi lindwa tangu mwaka 1894.

Baada ya uhuru

Uganda ilipata uhuru wake tarehe 9 Oktoba 1962 kwa katiba ya jamhuri yenye serikali ya kibunge.

Rais wa kwanza alikuwa Kabaka Sir Edward Mutesa II na waziri mkuu Milton Obote.

Mwaka 1967 Obote alibadilisha katiba akamfukuza Kabaka nchini.

Serikali ya Obote ilipinduliwa na mkuu wa jeshi Idi Amini mwaka 1971. Utawala wake ulikuwa kipindi cha udikteta ulioharibu uchumi wa nchi na misingi ya dola. Takriban watu 300,000 waliuawa chini ya Amin ama wapinzani wa siasa yake ama watu wa makabila yaliyotazamwa kuwa maadui wa serikali. Raia wenye asili ya Asia walifukuzwa katika nchi na mali yao yote kutwaliwa na serikali.

Mwaka 1978 vikosi vya jeshi la Uganda viliingia Tanzania na kuvamia maeneo ya mpakani kaskazini kwa mto Kagera. Mwaka 1979 Tanzania ilijibu kwa njia ya vita na jeshi lake pamoja na wapinzani wa Uganda walishinda jeshi la Amin na kumfukuza dikteta nchini. Rais wa baadaye Yoweri Museveni alikuwako kati ya wanamgambo waliosaidiana na Watanzania.

Uchaguzi wa mwaka 1980 ulimrudisha madarakani Milton Obote aliyeanzisha upya udikteta na kuua watu ovyo. Wapinzani wake wakiongozwa na Museveni walirudi porini wakashika silaha. Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kundi la Museveni likashinda na kutwaa serikali tangu mwaka 1986.

Museveni alichaguliwa rais katika kura bila vyama vya upinzani za 1996 na 2001.

Mwaka 2005 ulikuwa na uchaguzi wa vyama vingi wa kwanza. Museveni alipata kibali cha bunge kwa badiliko la katiba lililomruhusu kugombea urais tena mwaka 2006 akachaguliwa mara ya tatu.

Miji ya Uganda

Watu

 
Ramani ya Uganda ikionyesha makabila na lugha.

Wakazi wa Uganda wameongezeka kutoka 9,500,000 (1969) hadi 34,634,650 (2014), hivyo wengi wao ni vijana kuliko nchi zote duniani. Umri wa wastani ni miaka 15 tu.

Makabila makubwa ni Waganda (16.9%), Wanyankole (8.5%), Wanyoro (7.7%), Wasoga (7.4%), Walangi (7.1%), Wakiga (6.9%), Wateso (6.4%), Waacholi (5.7%), Wagisu (4.6%), Walugbara (4.2%). Wengineo ni 33.6%.

Nchini kuna lugha asilia 40 hivi, ambazo zinagawanyika katika makundi makubwa mawili: lugha za Kibantu upande wa kusini na lugha za Kinilo-Sahara upande wa kaskazini. Pia kuna lugha za Kisudani na lugha za Kikuliak. Hata hivyo lugha rasmi ni Kiingereza na Kiswahili.

Upande wa dini, kadiri ya sensa ya mwaka 2014, 84.5% za wakazi wanafuata Ukristo, hasa katika madhehebu ya Kikatoliki (39.3%) na ya Kianglikana (32%), halafu Wapentekoste (11.1%) na mengineyo. Waislamu ni 13.7%, wengi wao wakiwa Wasuni. Wanaoendelea kufuata dini asilia za Kiafrika ni 0.1% tu.

Tanbihi

  1. 1.0 1.1 "World Economic Outlook database: April 2022". imf.org.

Tazama pia

Marejeo

Kamusi elezo
  • Appiah, Anthony and Henry Louis Gates (ed). Encyclopaedia of Africa (2010). Oxford University Press.
  • Middleton, John (ed). New encyclopaedia of Africa (2008). Detroit: Thompson-Gale.
  • Shillington, Kevin (ed). Encyclopedia of African history (2005). CRC Press.
Vitabu vingine muhimu

Viungo vya nje

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Kwa jumla
Ramani
Serikali na uchumi
Masuala ya kiutu
Biashara
Utalii


Nchi za Afrika  
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira