Koloni za Ufaransa

Koloni za Ufaransa zilikuwa maeneo yaliyodhibitiwa na Ufaransa kutoka karne ya 17 hadi mwishoni mwa miaka ya 1960. Maeneo machache ambayo hayajapata uhuru yamekuwa sehemu za Jamhuri ya Ufaransa kama maeneo ya ng'ambo ya Ufaransa yenye hadhi ya mikoa na wananchi wana haki zote za raia wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya.

Koloni za Ufaransa; kijani: koloni za awamu ya kwanza; bluu: koloni za awamu ya pili

Wanahistoria hutofautisha mara nyingi awamu ya kwanza na awamu ya pili ya ukoloni wa Ufaransa.

Awamu ya kwanza

hariri

Awamu ya kwanza ilikuwa katika karne ya 17 na 18 ambako Ufaransa ilipata na kupoteza maeneo makubwa huko Amerika Kaskazini na Uhindi. Hasa koloni kwenye visiwa vya Karibi na visiwa kwenye Bahari Hindi zilitegemea kazi ya watumwa waliochukuliwa kutoka Afrika. [1]

Koloni ya kwanza ya Ufaransa ilianzishwa katika maeneo ya Kanada. Wafaransa walilenga hasa kufanya biashara na wazawa Waindio wakileta mwanzoni walowezi wachache tu. Kwa mikataba na makabila ya Waindio walijenga mtandao mkubwa wa vituo vya biashara na vya kijeshi ulioendelea hadi Louisiana na New Orleans kwenye Ghuba ya Meksiko kwa kufuata bonde la mto Missisippi.

Katika karne ya 18 waliongeza walowezi katika sehemu za Kanada ambao wamekuwa asili ya Wakanada wenye lugha ya Kifaransa katika Quebec ya leo.

Kuanzia mwaka 1624 waliunda koloni ya Guyana ya Kifaransa wakaendelea kwenye visiwa kama Guadeloupe, Martinique na Hispaniola kwenye Bahari ya Karibi.

Kuanzia mwaka 1664 walilenga pia biashara na Asia ya Kusini wakaunda koloni kwenye visiwa vya Bahari Hindi (Réunion, Morisi, Shelisheli) na Bara Hindi (Pondicherry, Chandernagore, Yanam, Mahe na Karikal.

Mnamo mwaka 1680 koloni za Ufaransa zilikuwa na eneo la kilomita za mraba 10,000,000 na hivyo kuwa himaya ya pili kwa ukubwa ulimwenguni wakati huo baada ya ile ya Hispania tu.

Vita dhidi ya Uingereza (Vita ya Miaka Saba, vita za Napoleoni) vilisababisha upotevu wa sehemu kubwa ya maeneo hayo. Ni Guyana pamoja na visiwa kadhaa kwenye Karibi na Bahari Hindi, pamoja na vituo vidogo katika Uhindi vilivyobaki.

Mapinduzi ya Haiti ilisababisha upotevu wa koloni kwenye kisiwa cha Hispaniola katika Karibi.

Ufaransa ilikuwa pia na Lousiana hadi mwaka 1803 ambapo Napoleon aliuza koloni hii pamoja na madai yote ya Ufaransa kwenye bonde la Missisippi kwa Marekani.

Awamu ya pili ukoloni ya Ufaransa (baada ya 1830)

hariri
 
Ramani iliyohuishwa inayoonyesha ukuaji na kupungua kwa himaya ya kwanza na ya pili ya Kifaransa ya kikoloni.

Mwisho wa vita za Napoleoni, koloni kadhaa za Ufaransa zilirudishwa kwake na Uingereza, hasa Visiwa vya Guadeloupe na Martinique huko Karibi, Guyana kwenye pwani ya Amerika Kusini, vituo vya biashara nchini Senegal (iliyopata hadhi ya peke kama Miji Minne (quatre communes), Île Bourbon yaani Réunion kwenye Bahari ya Hindi, na vituo vidogo vya Ufaransa katika Uhindi; hata hivyo, mwishowe Uingereza ilibaki na Saint Lucia, Tobago, Shelisheli, na Isle de France (sasa Morisi).

Mwanzo wa awamu ya pili ya ukoloni wa Ufaransa ulianza mnamo 1830 na uvamizi wa Ufaransa katika Algeria, ambayo ilishindwa katika vita ya miaka 17 iliyofuata na kuwa na wahanga Waalgeria 825,000. [2]

Tangu mwaka 1838 jeshi la majini la Ufaransa lilianza kuingilia kati Ufalme wa Tahiti baada ya malalamiko ya wamisionari Wakatoliki Wafaransa. Malkia wa Tahiti alipaswa kukubali ulinzi wa Ufaransa na hatimaye nchi hiyo ya visiwa ilitangazwa kuwa koloni kamili mnamo mwaka 1880.

Napoleon III: 1852-1870

hariri

Napoleon III (mpwa wa Napoleon Bonaparte) alitaka kujenga upya ukuu wa Ufaransa akapanua jeshi la majini na kulifanya jeshi la pili duniani baada ya Uingereza. Alianzisha utawala wa Kifaransa huko Kaledonia Mpya katika Bahari Pasifiki. Wafaransa walikifanya kisiwa hicho kuwa koloni ya gereza, kuanzia miaka ya 1860 hadi 1897 watu 22,000 waliohukumiwa Ufaransa kutokana na sababu za kisheria au za kisiasa walipelekwa huko.[3]

Kusini mwa Vietnam (Cochinchina) Wafaransa walitumia madhulumu ya wamisionari Wakatoliki kuingilia kati kwa wanamaji wao wakamlazimisha mtawala wa kusini kuwakabidhi maeneo kadhaa katika kusini kabisa.

Mwaka 1863 mfalme wa Kamboja aliyekuwa katika mapambano na Uthai aliomba ulinzi wa Ufaransa. Mwaka 1867 Kamboja ilitangazwa rasmi kuwa nchi lindwa chini ya Ufaransa.

Mwaka 1860 Napoleon III aliamua kuingilia kati mapigano baina ya Wakristo Wamaroni na Wadruzi katika Lebanoni iliyokuwa sehemu ya Milki ya Osmani. Wakristo wengi walichinjwa, na serikali ya Waosmani ilishindwa kudhibiti mapigano yaliyoenea hadi Syria. Baada ya mawasiliano na Uingereza, iliyohofu athira kubwa mno ya Ufaransa, Napoleon III alituma wanajeshi Lebanoni na matokeo yake yalikuwa kwamba Lebanoni ilimpata gavana Mkristo aliyeteuliwa na sultani wa Osmani. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi wa madai ya baadaye ya Ufaransa juu ya Lebanoni iliyokuwa koloni yake kwa miaka kadhaa katika karne ya 20 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Jamhuri ya Tatu (1871-1940)

hariri

Baada ya kushindwa kwake katika Vita ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani ya 1870-1871 na kuanzishwa kwa Jamhuri ya Tatu (1871-1940) ndipo maeneo ya koloni za Ufaransa yaliongezwa sana. Wengi wanaona upanuzi huo kama njia mbadala ya kuonyesha umuhimu na ukuu wa Ufaransa baada ya aibu ya kushindwa na Ujerumani mwaka 1871.

Kutoka kituo chao huko Cochinchina, Wafaransa walichukua Tonkin (Vietnam ya kaskazinii) na Annam (Vietnam ya kati) mnamo 1884-1885. Pamoja na Kamboja na Cochinchina maeneo hayo yaliunda "Indochina ya Ufaransa" mnamo 1887 ambapo Laos iliongezwa mnamo 1893. [4]

Katika China, Ufaransa ilijipatia maeneo madogo katika Shanghai, Tientsin (sasa inaitwa Tianjin), Guangzhou na Hankou (sasa ni sehemu ya Wuhan) kwa njia ya mikataba iliyodumu hadi mwaka 1946.[5]

Katika Afrika, Ufaransa ilipanua maeneo yaliyokuwa chini ya mamlaka yake kutoka vituo katika Senegal ikielekea beseni la Ziwa Chad ambako vikosi vidogo vya Kifaransa vilivyofanywa na askari Waafrika walioongozwa na maafisa Wafaransa vilifaulu kupata kibali cha watawala wenyeji -ama kwa ahadi au kwa nguvu ya kijeshi- ya kutambua ukuu wa Ufaransa. Pierre Savorgnan de Brazza alifanya mikataba na watawala wenyeji katika Gabon na upande wa kaskazini wa mto Kongo.

Misafara ya kijeshi yalivuka jangwa la Sahara na kuunda madai ya Ufaransa juu ya maeneo kati ya pwani ya Mediteranea na ukanda wa Sahel. Ilhali Ufaransa ilijipatia pia kituo katika sehemu za Wasomalia (Jibuti) kulikuwa pia na jaribio la kuunda ukanda wa koloni za kuvuka Afrika kutoka magharibi hadi mashariki. Ilikuwa dhahiri kwamba mpango huo ulipigana na mpango wa Uingereza kutawala mstari kati ya Misri na Afrika Kusini (Cape - Cairo line). Mwaka 1896 Ufaransa ilituma kikosi cha askari Wasenegal chini ya maafisa Wafaransa kutoka Gabon kilichofuata mito Kongo, Ubangi, Bahr al-Arab na Bahr al-Ghazal hadi kufikia mto Naili kwenye mji wa Fashoda (leo Kodok, Sudan Kusini). Hapa kilitegemea kukutana na kikosi kingine kilichotoka Jibuti. Badala yake walikutana na kikosi cha Kimisri-Kiingereza chini ya jenerali Horatio Herbert Kitchener aliyewahi kushinda Mahdi wa Sudan. Baada ya kusubiri miezi miwili na mawasiliano mengi na serikali ya Paris, Ufaransa iliamua kuondoa wanajeshi na kupatana na Uingereza.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, ambako Ufaransa ilikuwa kati ya washindi juu ya Ujerumani na juu ya Milki ya Osmani, maeneo chini yake yaliongezeka tena kutokana na koloni za Kijerumani za Togo na Kamerun halafu na Syria na Lebanoni zilizowahi kuwa maeneo ya Waosmani. Hayo yote yaliwekwa chini ya Ufaransa kama maeneo ya kudhaminiwa na Shirikisho la Mataifa.

Itikadi ya ukoloni wa Kifaransa

hariri

Shabaha kuu ya ukoloni wa Ufaransa mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 ilitangazwa kuwa "uenezaji wa ustaarabu" (mission civilisatrice), kwa kufuata itikadi kwamba ilikuwa jukumu la Ulaya kuleta ustaarabu kwa watu wasionao. [6] Kwa hiyo, maafisa wa kikoloni walichukua sera ya Ufaransa na Ulaya katika koloni za Ufaransa, haswa Magharibi mwa Afrika na Madagaska. Wakati wa karne ya 19, uraia wa Ufaransa pamoja na haki ya kumchagua mwakilishi katika bunge la Ufaransa ilitolewa kwa koloni nne za zamani za Guadeloupe, Martinique, Guyanne na Réunion na pia kwa wakaazi wa "Jumuiya Nne" huko Senegal. Katika visa vingi, wabunge waliochaguliwa walikuwa Wafaransa Wazungu, ingawa kulikuwa pia na Waafrika, kama Msenegal Blaise Diagne, ambaye alichaguliwa mnamo 1914. [7]

Mahali pengine, katika koloni kubwa na yenye watu wengi, mgawanyiko mkali kati ya "sujets français" (wenyeji wote) na "citoyens français" (raia kamili wenye ukoo kutoka Ulaya) na haki na majukumu tofauti yalidumishwa hadi mwaka 1946. Kama ilivyodhihirishwa katika mkataba wa 1927 juu ya sheria ya koloni za Ufaransa, utoaji wa uraia wa Ufaransa kwa wenyeji "haikuwa haki, bali ni fursa". [8] Amri mbili za 1912 zinazoshughulikia Afrika ya Magharibi ya Kifaransa na Afrika ya Ikweta ya Kifaransa ziliorodhesha masharti ambayo mzawa alipaswa kutimiza ili apewe uraia wa Ufaransa (ni pamoja na kuzungumza na kuandika Kifaransa, kupata maisha bora na kuonyesha viwango bora vya maadili). Kuanzia mwaka 1830 hadi 1946, Waalgeria kati ya 3,000 na 6,000 pekee walipewa uraia wa Ufaransa. Katika Afrika Magharibi ya Kifaransa, nje ya Miji Minne, kulikuwa na "walioendelea" 2,500 kati ya idadi ya watu milioni 15. [9]

 
Vikosi vya wakoloni wa Ufaransa, wakiongozwa na Kanali Alfred-Amédée Dodds, mulatto wa Senegal, walishinda na kutwaa Dahomey mnamo 1894.

Mnamo 1905, Wafaransa walikomesha utumwa katika sehemu nyingi za magharibi mwa Afrika. David P. Forsythe aliandika: "Kutoka Senegal na Mauritania magharibi hadi Niger mashariki (iliyokuwa Afrika ya Kifaransa), kulikuwa na mfululizo wa vita haribifu, na kusababisha idadi kubwa ya watu kuwa watumwa. Mwanzoni mwa karne ya 20 kunaweza kuwa na watumwa kati ya milioni 3 na 3.5, wanaowakilisha zaidi ya asilimia 30 ya idadi ya watu wote, katika eneo hili lenye watu wachache." [10]

Idadi ya watu

hariri

Takwimu za sensa ya Ufaransa kutoka mwaka 1931 zilionyesha idadi ya wakazi nje ya Ufaransa yenyewe walikuwa watu milioni 64.3 waliokalia kilomita za mraba milioni 11.9. Kati ya watu hao wote, milioni 39.1 waliishi Afrika na milioni 24.5 waliishi Asia; 700,000 waliishi katika eneo la Karibi au visiwa vya Pasifiki Kusini. Koloni kubwa zilikuwa Asia penye milioni 21.5 (katika koloni tano tofauti), Algeria ikiwa na milioni 6.6, Moroko yenye milioni 5.4, na Afrika Magharibi yenye milioni 14.6 katika koloni tisa.[11]

Mwisho wa ukoloni

hariri

Utawala wa Ufaransa juu ya kaloni zake ulianza kuporomoka wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Ufaransa yenyewe ilitwaliwa na Ujerumani mwaka 1940; katika sehemu ilitokea serikali ya jenerali Petain aliyepaswa kushirikiana na Ujerumani, katika Uingereza kanali Charles de Gaulle aliunda serikali ya "Ufaransa Huru". ilhali magavana wa koloni waligawiwa kati ya pande hizi mbili. Koloni mbalimbali zilivamiwa na nchi nyingine. Japani ilitwaa Indochina (Vietnam, Laos na Kamboja), Uingereza ulitwaa usimamizi juu ya Syria, Lebanon, na Madagaska. Marekani na Uingereza zilivamia Moroko na Algeria, Ujerumani na Italia zilitwaa Tunisia.

Baada ya vita serikali ya Charles de Gaulle ilijaribu kurudisha utawala juu ya koloni ikakuta mara moja upinzani.

Maandamano na mashambulio dhidi ya walowezi Wafaransa katika Algeria kwenye mwezi wa Mei 1945 yalikandamizwa na maelfu ya Waalgeria waliuawa[12]. Huko Hanoi wanamgambo Wakomunisti chini ya Ho Chi Minh waltangaza uhuru wa nchi na hivyo kuanzisha vita iliyoendelea hadi 1954. Kule Madagaska wenyeji walishambulia wanajeshi na walowezi Wafaransa katika mwaka 1947[13].

Mwaka 1946 Ufaransa ilipata katiba mpya ambako nchi hiyo pamoja na koloni na nchi lindwa chini yake yalitangazwa kuwa sehemu za "Umoja wa Kifaransa" ambako wakazi wote walikuwa na uraia mmoja. Maeneo ya "Ufaransa ya Ng'ambo" (yaani koloni) yalipewa pia idadi ya wabunge katika Bunge la Paris. Mwaka 1946 walikuwepo wabunge Waafrika 21 waliongezeka kuwa 30 mnamo mwaka 1955[14]. Viongozi mbalimbali wa nchi huru za baadaye walianza njia yao ya kisiasa kama wabunge katika Ufaransa, kwa mfano Félix Houphouët-Boigny (Cote d'Ivoire) na Léopold Sédar Senghor (Senegal). Lakini udhibiti mkuu ulibaki katika sehemu ya Ulaya. Kila eneo lilipata bunge lake lenye madaraka madogo. Waafrika waliopita vizuri kwenye mfumo wa elimu ya Kifaransa waliangaliwa kama "evolués" (walioendelea) na kupewa haki zote za kisiasa. [15] Hata hivyo, majaribio hayo yote ya kuunganisha koloni za awali na Ufaransa yalishindikana na kuanzia muongo wa 1950 polepole nchi zote ziliamua kuwa nchi huru.

Algeria iliyokuwa nchi pekee yenye walowezi wengi Wafaransa ilipita katika vita kali iliyoona umwagaji wa damu nyingi hadi kupata uhuru wake kwenye mwaka 1962.

Tanbihi

hariri
  1. "French Slave Trade". Slavery and Remembrance. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2020-10-30. Iliwekwa mnamo 2020-10-27.
  2. Warfare and Armed Conflicts: A Statistical Encyclopedia of Casualty and Other Figures, 1492–2015, 4th ed. McFarland. 9 Mei 2017. uk. 199.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. Robert Aldrich; John Connell (2006). France's Overseas Frontier: Départements et territoires d'outre-mer. Cambridge University Press. uk. 46. ISBN 978-0-521-03036-6.
  4. "Kwangchow Bay" .
  5. Paul French (2011). The Old Shanghai A-Z. Hong Kong University Press. uk. 215. ISBN 9789888028894.
  6. Betts, Raymond F. (2005). Assimilation and Association in French Colonial Theory, 1890–1914. University of Nebraska Press. uk. 10. ISBN 9780803262478.
  7. Segalla, Spencer. 2009, The Moroccan Soul: French Education, Colonial Ethnology, and Muslim Resistance, 1912–1956.
  8. Olivier Le Cour Grandmaison, De l'Indigénat.
  9. Le Cour Grandmaison, p. 60, note 9.
  10. David P. Forsythe (2009).
  11. Herbert Ingram Priestley, France overseas: a study of modern imperialism (1938) pp 440–41.
  12. Horne, Alistair (1977). A Savage War of Peace: Algeria 1954–1962. New York: The Viking Press. uk. 27.
  13. Anthony Clayton, The Wars of French Decolonization (1994) p 85
  14. Philippe Guiemin: Les élus d'Afrique noire à l'Assemblée nationale sous la Quatrième République, Revue française de science politique Année 1958 8-4 pp. 861-877
  15. Simpson, Alfred William Brian (2004). Human Rights and the End of Empire: Britain and the Genesis of the European Convention. Oxford University Press. ku. 285–86. ISBN 978-0199267897.

Marejeo

hariri
  • Langley, Michael. "Bizerta to the Bight: The French in Africa." History Today. (Oct 1972), pp 733–739. covers 1798 to 1900.
  • Hutton, Patrick H. ed. Historical Dictionary of the Third French Republic, 1870–1940 (2 vol 1986)
  • Northcutt, Wayne, ed. Historical Dictionary of the French Fourth and Fifth Republics, 1946– 1991 (1992)

Sera na makoloni

hariri
  • Aldrich, Robert. Greater France: A History of French Overseas Expansion (1996)
  • Aldrich, Robert. The French Presence in the South Pacific, 1842–1940 (1989).
  • Anderson, Fred. Crucible of War: The Seven Years' War and the Fate of Empire in British North America, 1754–1766 (2001), covers New France in Canada
  • Baumgart, Winfried. Imperialism: The Idea and Reality of British and French Colonial Expansion, 1880–1914 (1982)
  • Betts, Raymond. Tricouleur: The French Overseas Empire (1978), 174pp
  • Betts, Raymond. Assimilation and Association in French Colonial Theory, 1890–1914 (2005) excerpt and text search
  • Burrows, Mathew (1986). "'Mission civilisatrice': French Cultural Policy in the Middle East, 1860–1914". The Historical Journal. 29 (1): 109–135. doi:10.1017/S0018246X00018641..
  • Chafer, Tony (2002). The End of Empire in French West Africa: France's Successful Decolonization?. Berg. ISBN 9781859735572.
  • Clayton, Anthony. The Wars of French Decolonization (1995)
  • Conklin, Alice L. A Mission to Civilize: The Republican Idea of Empire in France and West Africa, 1895–1930 (1997) online Ilihifadhiwa 23 Novemba 2020 kwenye Wayback Machine.
  • Evans, Martin. "From colonialism to post-colonialism: the French empire since Napoleon." in Martin S. Alexander, ed., French History since Napoleon (1999) pp: 391–415.
  • Gamble, Harry. Contesting French West Africa: Battles over Schools and the Colonial Order, 1900–1950 (U of Nebraska Press, 2017). 378 pp. online review
  • Jennings, Eric T. Imperial Heights: Dalat and the Making and Undoing of French Indochina (2010).
  • Kang, Mathilde (2018). "II The affirmation of the French presence in Asia". Francophonie and the Orient: French-Asian Transcultural Crossings (1840-1940). Ilitafsiriwa na Martin Munro. Amsterdam University Press. doi:10.2307/j.ctv80cd6t. ISBN 9789048540273. JSTOR j.ctv80cd6t.
  • Lawrence, Adria. Imperial rule and the politics of nationalism: anti-colonial protest in the French empire (Cambridge UP, 2013).
  • Newbury, C. W.; Kanya-Forstner, A. S. (1969). "French Policy and the Origins of the Scramble for West Africa". The Journal of African History. 10 (2): 253–276. doi:10.1017/S0021853700009518. JSTOR 179514..
  • Klein, Martin A. Slavery and colonial rule in French West Africa (Cambridge University Press, 1998)
  • Manning, Patrick. Francophone Sub-Saharan Africa 1880-1995 (Cambridge UP, 1998). online Ilihifadhiwa 31 Agosti 2020 kwenye Wayback Machine.
  • Neres, Philip. French-speaking West Africa: From Colonial Status to Independence (1962) online Ilihifadhiwa 25 Novemba 2020 kwenye Wayback Machine.
  • Priestley, Herbert Ingram. France overseas: a study of modern imperialism (1938) 464pp.
  • Quinn, Frederick. The French Overseas Empire (2000) online Ilihifadhiwa 18 Juni 2020 kwenye Wayback Machine.
  • Pakenham, Thomas (1991). The Scramble for Africa, 1876–1912. New York: Random House. ISBN 978-0-394-51576-2..
  • Poddar, Prem, and Lars Jensen, eds., A historical companion to postcolonial literatures: Continental Europe and Its Empires (Edinburgh UP, 2008), excerpt also entire text online
  • Petringa, Maria (2006). Brazza, A Life for Africa. Bloomington, IN: AuthorHouse. ISBN 978-1-4259-1198-0..
  • Priestley, Herbert Ingram. (1938) France overseas;: A study of modern imperialism 463pp; encyclopedic coverage as of late 1930s
  • Roberts, Stephen H. History of French Colonial Policy (1870-1925) (2 vol 1929) vol 1 online also vol 2 online; Comprehensive scholarly history
  • Segalla, Spencer (2009). The Moroccan Soul: French Education, Colonial Ethnology, and Muslim Resistance, 1912–1956. Lincoln: Nebraska UP. ISBN 978-0-8032-1778-2..
  • Strother, Christian. "Waging War on Mosquitoes: Scientific Research and the Formation of Mosquito Brigades in French West Africa, 1899–1920." Journal of the history of medicine and allied sciences (2016): jrw005.
  • Thomas, Martin. The French Empire Between the Wars: Imperialism, Politics and Society (2007) covers 1919–1939
  • Thompson, Virginia, and Richard Adloff. French West Africa (Stanford UP, 1958).
  • Wellington, Donald C. French East India companies: A historical account and record of trade (Hamilton Books, 2006)
  • Wesseling, H.L. and Arnold J. Pomerans. Divide and rule: The partition of Africa, 1880–1914 (Praeger, 1996.) online Ilihifadhiwa 8 Novemba 2020 kwenye Wayback Machine.
  • Wesseling, H.L. The European Colonial Empires: 1815–1919 (Routledge, 2015).

Mwisho wa ukoloni

hariri
  • Betts, Raymond F. Ukoloni (2 ed. 2004)
  • Betts, Raymond F. Ufaransa na Ukoloni, 1900-1960 (1991)
  • Chafer, Tony. Kumalizika kwa himaya katika Ufaransa Magharibi mwa Afrika: Mafanikio ya ukoloni wa Ufaransa (Bloomsbury Publishing, 2002).
  • Chamberlain, Muriel E. ed. Mshirika wa Longman kwa Ukoloni wa Ulaya katika karne ya ishirini (Routledge, 2014)
  • Clayton, Anthony. Vita vya ukoloni wa Ufaransa (Routledge, 2014).
  • Cooper, Frederick. "Afrika ya Ufaransa, 1947-48: Mageuzi, Vurugu, na Kutokuwa na uhakika katika Hali ya Kikoloni." Uchunguzi muhimu (2014) 40 # 4 pp: 466-478. huko JSTOR
  • Ikeda, Ryo. Ubeberu wa Ukoloni wa Kifaransa: Sera ya Ufaransa na Jibu la Anglo-American huko Tunisia na Moroko (Palgrave Macmillan, 2015)
  • Jansen, Jan C. & Jürgen Osterhammel. Ukomeshaji: Historia Fupi (princeton UP, 2017). mkondoni
  • Jones, Max, et al. "Kukomesha mashujaa wa kifalme: Uingereza na Ufaransa." Jarida la Historia ya Imperial na Jumuiya ya Madola 42 # 5 (2014): 787-825.
  • Lawrence, Adria K. Utawala wa Kifalme na Siasa za Utaifa: Maandamano ya Kupinga Ukoloni katika Dola ya Ufaransa (Cambridge UP, 2013) ukaguzi wa mkondoni
  • McDougall, James . "Haiwezekani Jamhuri: Reconquest ya Algeria na kumaliza ukoloni wa Ufaransa, 1945-1962," Journal of Modern History 89 # 4 (Desemba 2017) uk 772-811 dondoo
  • Rothermund, Dietmar. Kumbukumbu za Mataifa ya baada ya Kifalme: Matokeo ya Ukoloni, 1945-2013 (2015) kifungu ; Inalinganisha athari kwa Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Ufaransa, Ureno, Italia na Japan
  • Rothermund, Dietmar. Rafiki wa Routledge kwa ukoloni (Routledge, 2006), chanjo kamili ya ulimwengu; 365pp
  • Shepard, Todd. Uvumbuzi wa Ukoloni: Vita vya Algeria na Uwekaji upya wa Ufaransa (2006)
  • Simpson, Alfred William Brian. Haki za Binadamu na Mwisho wa Dola: Uingereza na Mwanzo wa Mkataba wa Uropa (Oxford University Press, 2004).
  • Smith, Tony. "Utafiti wa kulinganisha wa ukoloni wa Ufaransa na Uingereza." Mafunzo ya kulinganisha katika Jamii na Historia (1978) 20 # 1 pp: 70-102. mkondoni Ilihifadhiwa 14 Juni 2015 kwenye Wayback Machine.
  • Smith, Tony. "Makubaliano ya Kikoloni ya Ufaransa na Vita vya Watu, 1946-58." Jarida la Historia ya Kisasa (1974): 217-247. huko JSTOR
  • Thomas, Martin, Bob Moore, na Lawrence J. Butler. Shida za Dola: Ukoloni na majimbo ya kifalme ya Uropa (Bloomsbury Publishing, 2015)
  • Von Albertini, Rudolf. Ukoloni: Utawala na Baadaye ya Wakoloni, 1919-1960 (Doubleday, 1971), uchambuzi wa kitaalam wa sera za Ufaransa, ukurasa wa 265-469. .

Viungo vya Nje

hariri