Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

milki ya zamani ya Wajerumani katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika kati ya 1884-1919
(Elekezwa kutoka DOA)

Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (au: ya Kidachi; kwa Kijerumani Deutsch-Ostafrika -DOA-; kwa Kiingereza German East Africa) ilikuwa jina la koloni la Ujerumani huko Afrika ya Mashariki kati ya miaka 1885 na 1918/1919.

Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Bendera ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Bendera ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Nembo ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mwanzo wa utawala wa kikoloni 1885
Makao ya serikali ya kikoloni Bagamoyo hadi 1891 halafu Dar es Salaam
Eneo km² 995,000
Wakazi 7,665,234 (1-1-1913)
Wakazi Wajerumani 4,100 (1913)
Pesa 1 Rupie= 64 Pesa,
kuanzia 1904
1 Rupie = 100 Heller
Nchi huru za leo 1961 Tanganyika, tangu 1964 Tanzania

Ruanda
Burundi

Ramani ya Kijerumani ionyeshayo Zanzibar na pwani (mnamo 1888)

Eneo lake lilijumlisha nchi za kisasa za Tanzania bara (yaani bila Zanzibar), Burundi na Rwanda. Ilikuwa koloni kubwa kabisa la Dola la Ujerumani.

Eneo, mipaka na wakazi

hariri

Eneo na mipaka

hariri

Eneo la koloni lilikuwa na kilomita za mraba 997,000 pamoja na sehemu za maziwa makubwa kama Ziwa Tanganyika na Ziwa Viktoria. Eneo hili lilikuwa karibu mara mbili kuliko eneo la Ujerumani wenyewe kabla ya mwaka 1914.

Mipaka iliamuliwa katika mapatano na Uingereza, Ubelgiji na Ureno zilizotawala makoloni ya jirani ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (leo Kenya na Uganda), Kongo ya Kibelgiji (leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Rhodesia (leo Zambia na Zimbabwe), Nyasaland (leo Malawi) na Msumbiji. Mipaka hii ni pia mipaka ya Tanzania, Rwanda na Burundi hadi leo hii.

Katika mapatano baina ya Uingereza na Ujerumani ya Novemba 1886 pande zote mbili ziliahidi kuheshimu utawala wa Sultani wa Zanzibar juu ya visiwa pamoja na kanda la maili 10 kwenye pwani baina ya mto Tana na Mto Minengani (Msumbiji). Pamoja na hayo walielewana kuhusu maeneo ya maslahi yao, wakipatana kuhusu mstari uliokuwa baadaye mpaka baina ya Tanzania na Kenya hadi leo.[1]

Katika mkataba wa 1890 kuhusu mipaka katika Afrika Uingereza iliahidi kumshawishi Sultani wa Zanzibar kuuza maeneo yake kwenye pwani la bara pamoja na kisiwa cha Mafia[2] kwa Ujerumani[3].

Upande wa Kenya mstari ulichorwa kuanzia Bahari Hindi kwa mdomo wa mto Umba hadi Ziwa Jipe, halafu kufuata mitelemko ya kaskazini ya mlima Kilimanjaro na kutoka hapa hadi Ziwa Viktoria. Mipaka na Uganda ilifuata latitudo ya kwanza ya kusini ya ikweta hadi mpaka na Kongo. Upande wa Kongo mpaka ulifuata sehemu za chini za bonde la Ufa na katikati ya maziwa kama Kivu na Tanganyika.

Upande wa kusini ulifuata mstari kati ya ncha ya kusini ya ziwa Tanganyika hadi mdomo wa Mto Songwe katika Ziwa Nyasa. Eneo lote la ziwa lenyewe lilibaki upande wa Nyasaland ya Kiingereza, halafu mstari kutoka Ziwa Nyasa kwa kufuata mto Ruvuma hadi Rasi ya Delgado kwenye Bahari Hindi.

Jinsi ilivyo na mipaka ya kikoloni mistari hii ilikata mara nyingi maeneo ya makabila ya wenyeji.

Wakazi

hariri

Mwaka 1913 takwimu ya Wajerumani ilihesabu wakazi Waafrika 7,645,000, Waasia (Wahindi na Waarabu) 14,898 na Wazungu 5,336, kati yao Wajerumani 4,107. Nusu ya wakazi wote waliishi katika eneo la maziwa makubwa ambako serikali ya kikoloni iliacha maeneo ya Rwanda (wakazi 2,000,000), Burundi (1,500,000) na Bukoba (275,000) kama maeneo lindwa chini ya watawala wa kienyeji waliosimamiwa na afisa mkazi Mjerumani.[4]

Historia ya koloni

hariri
Historia ya Tanzania
 
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Koloni hilo halikuanzishwa kwa azimio la kisiasa upande wa serikali ya Ujerumani bali lilianzishwa kama mradi wa watu binafsi waliotafuta makoloni katika Afrika.

Historia ya koloni ilikuwa na awamu tatu:

  1. mwanzo kama maeneo yaliyotawanyika ambako kampuni binafsi (Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki) ilifaulu kushawishi watawala wa kienyeji kutia sahihi kwenye mikataba; kipindi hiki kilianza 1885 hadi kuporomoka kwa utawala wa kampuni mnamo 1890
  2. koloni la Dola la Ujerumani (kwa Kijerumani Deutsches Reich) lililoamua kuchukua mamlaka mkononi mwake kuanzia 1891, ambako Ujerumani iliweza kupanusha utawala wake juu ya maeneo yote
  3. mwisho wa utawala wa Kijerumani wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuanzia mwaka 1916 wakati jeshi kubwa la Uingereza na Afrika Kusini pamoja na Ubelgiji lilivamia, hadi kusalimu amri kwa jeshi la Schutztruppe kwenye Novemba 1918

Katika mapatano baada ya vita koloni liligawiwa kati ya Uingereza (iliyopata Tanganyika) na Ubelgiji (iliyopata Rwanda na Burundi). Kwa historia ya baadaye ilikuwa na maana ya kwamba walikabidhiwa maeneo ya koloni la Kijerumani la awali si kama mali kamili lakini kama maeneo ya kudhaminiwa kwa niaba ya shirikisho la Mataifa (mtangulizi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Utangulizi

hariri

Hadi mnamo mwaka 1880 serikali ya Ujerumani chini ya chansella Otto von Bismarck ilikataa kuanzisha makoloni. Sehemu ya wafanyabiashara Wajerumani walidai koloni. Walisikitika kuona faida za wenzao Waingereza waliopata mara nyingi msaada kutoka kwa wanajeshi na serikali za koloni za Uingereza hasa Asia. Waliona pia faida ya viwanda vya Uingereza vilivyokuwa na soko la kulindwa katika nchi kama Uhindi kwa sababu serikali ya kikoloni ilidai kodi kali kwa bidhaa zisizotoka Uingereza.

Bismarck hakuamini ya kwamba koloni lingeleta faida kwa taifa kulingana na gharama kubwa kwa serikali. Lakini wapigania koloni walikuwa na wabunge muhimu kwa serikali na polepole Bismarck alianza kukubali hatua za kwanza.

Mwenyewe aliamini mwanzoni ya kwamba itatosha kuwapa wafanyabiashara ulinzi kwa shughuli zao kwa kuwaruhusu matumizi ya bendera ya Ujerumani na kuwa na askari wao wa ulinzi kama wamepatana na viongozi wazalendo katika eneo fulani kuanzisha shughuli huko. Kwa njia hii alifungua mlango kwa harakati iliyoendelea kuwa mchango wa Ujerumani katika mbio wa kugawa dunia, hasa Afrika.

Juhudi za Karl Peters

hariri
 
Maeneo ya kwanza yaliyotwaliwa na Karl Peters.

Koloni hili lilianzishwa na kijana Mjerumani Karl Peters mwaka 1885 kwa niaba ya "Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki".

Peters, aliyewahi kusoma chuo Uingereza, aliona wivu juu ya ukoloni wa Uingereza, akiamini ya kwamba Ujerumani ungestahili nafasi hiyo pia. Hivyo alianza kudai koloni katika mikutano, akaanzisha "Shirika kwa Ukoloni wa Kijerumani" mwaka 1884 iliyokuwa kitangulizi cha kampuni.

Shirika hii ilimtuma pamoja na wenzake wawili kwenda Afrika na kutafuta nafasi ya kuanzisha koloni. Kiasili walilenga maeneo mpakani mwa Msumbiji na Zimbabwe ya leo lakini hatimaye waliamua kwenda Afrika ya Mashariki. Peters alifika Zanzibar alipoambiwa na konsuli ya Ujerumani ya kwamba hawezi kuendelea: serikali ya nyumbani iliogopa ugomvi na Uingereza ilikataa mipango yake. Aliamua kuvuka barani hata hivyo akafika Saadani tarehe 10 Novemba 1884 na kufuata njia kando ya mto Wami ili apite kanda la Kizanzibari kwenye pwani na kutembelea machifu na masultani ndani ya bara.

Hapo alifaulu kushawishi watawala wa maeneo yaliyojulikana kama Usagara, Nguru, Useguha na Ukami kutia sahihi kwenye mikataba iliyoandikwa kwa Kijerumani ambayo hawakuielewa. Mikataba hii ilisema ya kwamba mtawala alikabidhi kwa kampuni nchi yake pamoja na haki juu ya ardhi na mali yote.

Mwaka 1885 Peters alirudi Berlin na kuonyesha mikataba yake kwa magazeti na serikali. Chansela Bismarck alikataa, akacheka mikataba kama karatasi bila maana.

Peters alitumia mbinu: akatisha kupeleka mikataba yake kwa mfalme Leopold II wa Ubelgiji aliyekuwa kununua haki zake. Hapa Bismarck aliogopa kilio cha wapenda koloni akakubali kumpa Peters hati ya ulinzi ya tarehe 27 Februari 1885 kwa maeneo yaliyokuwa ya kampuni kufuatana na mikataba.

Upanuzi wa eneo la kampuni

hariri

Upanuzi na ugomvi na Zanzibar

hariri

Peters na wawakilishi wake walirudi wakaendelea kutafuta machifu waliokuwa tayari kutia saini mikataba yake. Sultani wa Zanzibar alipinga juhudi hizi. Zanzibar ilisimamia pwani ya Afrika ya Mashariki na tangu karne watu wa miji ya pwani walikuwa na mawali wa Sultani.

Zanzibar ilidai pia utawala ya bara hadi Ziwa Tanganyika na Kongo, ingawa hali halisi athira yake haikwenda mbali na njia za misafara ambako ndovu na watumwa walipelekwa pwani.

Tarehe 27 Aprili 1885 serikali ya Zanzibar ilituma barua Berlin kupinga kazi na madai ya kampuni na kutangaza maeneo ya Tanzania ya leo kama milki yake. Iliongeza pia wanajeshi wake barani zilizokuwa chini ya amri ya mwanajeshi mstaafu Mwingereza Matthews. Hapo serikali ya Berlin ilituma kikosi cha manowari kwenda Bahari Hindi.

Mwezi Agosti manowari za Kijerumani chini ya amri ya admirali Eduard von Knorr zilifika mbele ya Unguja zikalenga mizinga yao kwa ikulu ya sultani. Akishauriwa na balozi wa Uingereza, Sultani Bargash alipaswa kutoa tamko kuwa, "Kutokana na madai tunayopelekewa kwa matishio na Kaisari wa Ujerumani, tunatambua ulinzi wa Ujerumani juu ya nchi za Usagara, Nguru, Useguha, Ukami na juu ya wilaya ya Witu. Mipaka yake itaelezwa baadaye na sisi tunatambua ulinzi wa Kaisari juu ya mahali palipotajwa." [5].

Sultani alipaswa pia kutia sahihi mkataba wa biashara na Ujerumani alipokubali haki nyingi kwa Wajerumani katika milki yake.[6]

Mwaka 1886 Uingereza na Ujerumani walipatana juu ya "maeneo ya masilahi" yao katika Afrika ya Mashariki; hapa walielewana kuhusu mstari kati ya mdomo wa mto Umba (kati ya Tanga na Mombasa) hadi nukta ambako latitudo ya 1 kusini inakata mwambao wa Ziwa Viktoria Nyanza[7]. Sultani alipaswa kukubali tena. Katika mapatano hayo Sultani alibaki na visiwa vya Unguja, Pemba, Mafia na funguvisiwa ya Lamu pamoja na kanda la pwani barani lenye upana wa maili 10 kati ya mto Ruvuma upande wa Kusini na mto Tana upande wa Kaskazini, halafu miji ya Kismayu, Barawa, Merka na Mogadishu upande wa kaskazini zaidi. [8].

Mkataba kati ya Zanzibar na Kampuni juu ya kofo na pwani

hariri
 
Sarafu ya rupia 1 iliyotolewa kwa jina la "Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft" (Kampuni ya Kijerumani ya Afrika ya Mashariki); tangu 1904 zilitolewa kwa jina la koloni yenyewe bila kutaja kampuni tena

Mapatano ya 1886 yaliwapa Wajerumani nafasi ya kuendeleza upanuzi barani nyuma ya kanda la pwani la Kizanzibari na mstari wa mpaka ulichorwa kuanzia mdomo wa mto Umba kupitia mlima Kilimanjaro hadi Ziwa Viktoria. Lakini kwa ajili ya matumizi ya kibiashara suala la mabandari bado lilibaki wazi. Hapo Peters na kampuni yake walianza kujadiliana na Sultani Seyyed Bargash (alitawala 1870 hadi 1888) kuhusu utawala wa pwani katika sehemu ya Tanganyika.

Mnamo mwaka 1887 Bargash alikuwa amechoka: alitafuta pesa tu kwa ajili yake binafsi; alikuwa tayari kukodisha utawala wa kanda la pwani ya Tanganyika kwa Wajerumani. Wajerumani walidai kuongezeka haki na Bargash alikufa bila kumaliza mapatano.

Lakini mwandamizi wake Sultani Seyyed Khalifa aliwapa Wajerumani walichotaka. Tarehe 15 Agosti 1888 wawakilishi wa kampuni ya Kijerumani walifika kwenye mabandari yote wakatangaza utawala wao kwa niaba ya sultani.

Vita ya Abushiri na mwisho wa utawala wa Kampuni

hariri

tazama Vita ya Abushiri

Badiliko hili lilisababisha upinzani na hatimaye ghasia ya wenyeji. Vipengele vya mkataba vilisema mali isiyokuwa na hati za kimaandishi haiwezi kutambuliwa. Wenye mali kama mashamba walitakiwa kununua hati kutoka kwa watawala wapya. Hapo Waswahili wa pwani walijisikia wamesalitiwa na sultani asiyekuwa na haki ya kuchukua mali zao na kuzipa kwa wageni.

Mara baada ya kufika kwa Wajerumani kwenye miji ya pwani ghasia ilianza mjini Pangani na kuenea haraka kote pwani kati ya Tanga na Lindi.

Kampuni ilikuwa na Wajerumani wachache tu walioshindwa kujitetea. Walipaswa kukimbia au wakauawa. Bagamoyo pekee palikuwa na kikosi cha askari kutoka manowari ikatetewa.

Serikali ya Ujerumani iliona lazima kuingia kati na kutuma manowari pamoja na askari waliokandamiza ghasia. Bismarck alitumia mbinu wa kupata kura za bunge alizohitaji kwa ajili ya gharama ya vita hiyo. Alipeleka sheria bungeni kuwa Ujerumani unatoa mark milioni 2 kwa kupambana na biashara ya watumwa na ulinzi wa manufaa ya Kijerumani. Sasa alimtuma afisa wa jeshi mwenye maarifa ya Afrika, Hermann von Wissmann aliyeajiri maafisa na wanajeshi Wajerumani, kwa jumla watu 87 wakaelekea Afrika ya Mashariki. Njiani walipopita Misri waliajiri askari waliostaafishwa Wasudani 650; waliongeza baadaye askari Wazulu 350 kutoka Msumbiji na kuwaunganisha kuwa "kikosi cha Wissmann" kilichofaulu kushinda upinzani wote kwa msaada wa silaha za kisasa na manowari za Ujerumani[9].

Baada ya upinzani wa wenyeji wa pwani mwaka 1889/1890 wakiongozwa na Abushiri na Bwana Heri serikali ya Ujerumani iliamua kutwaa mamlaka kutoka kwa kampuni na kufanya eneo lote kuwa koloni la Dola la Ujerumani badala ya shirika.

Koloni la Dola la Ujerumani

hariri

Maeneo ya kampuni yalikuwa rasmi koloni la serikali tarehe 1 Januari 1891. Koloni lilisimamiwa na gavana.

Magavana wa Kijerumani walikuwa wafuatao:[10]

Utawala wa Kijerumani ulikwisha katika Vita Kuu ya Dunia ya Kwanza (1914 - 1918) kutokana na uvamizi wa Uingereza na Ubelgiji.

Katika Mkataba wa Versailles mwaka 1919 eneo la koloni la Kijerumani liligawiwa. Sehemu ya Tanganyika ilikabidhiwa kwa Uingereza na maeneo ya Rwanda na Burundi yaliwekwa chini ya Ubelgiji.

Utawala

hariri

Eneo lote la koloni liligawiwa katika mikoa 21 na maeneo matatu yaliyokuwa bado chini ya watawala wenyeji kwa mfumo wa maeneo lindwa. Hadi 1913 mikoa 19 ilikuwa chini ya utawala wa kiraia, yaani chini ya maafisa wa serikali ya kikoloni. Mikoa miwili ya Iringa na Mahenge ilikuwa bado chini ya utawala wa kijeshi yaani hapo walikuwa maafisa wa Schutztruppe waliotekeleza majukumu yote ya serikali.

Mikoa chini ya usamimizi wa maafisa Wajerumani wa kiraia ilikuwa:

1. Tanga (DOA)
2. Pangani (DOA) pamoja na ofisi ndogo Handeni
3. Bagamoyo (DOA) pamoja na ofisi ndogo Saadani
4. Daressalam pamoja na ofisi ndogo ya polisi Kisangire
5. Rufiji (DOA), makao makuu Utete
6. Kilwa (DOA) pamoja na ofisi ndogo za Kilindoni, Kibata na Liwale
7. Lindi (DOA) pamoja na ofisi ndogo za Mikindani, Newala und Tunduru
8. Langenburg (DOA) (Tukuyu) pamoja na ofisi ndogo Itaka na Mwakete na kituo cha polisi Muaja
9. Wilhelmstal (DOA) (Lushoto)
10. Morogoro (DOA) pamoja na ofisi ndogo za Kilossa na Kissaki
11. Songea (DOA) pamoja na ofisi ndogo Wiedhafen
12. Moshi (DOA)
13. Arusha (DOA) pamoja na ofisi ndogo Umbulu
14. Kondoa-Irangi (DOA) pamoja na ofisi ndogo Mkalama
15. Dodoma (DOA) pamoja na kituo cha polisi Mpapwa na kituo cha kijeshi Singida
16. Mwanza (DOA) pamoja na ofisi ndogo Shirati na kituo cha kijeshi Ikoma
17. Tabora (DOA) pamoja na ofisi ndogo za Shinyanga na Ushirombo
18. Ujiji (DOA) pamoja na kituo cha kijeshi Kasulo
19. Bismarckburg (DOA) (Kasanga (Ufipa)

Mikoa ya kijeshi (jer. Militärbezirke) chini ya usimamizi wa maafisa wa Kijerumani wa kijeshi:

21. Iringa (DOA) pamoja na kituo cha kijeshi Ubena
22. Mahenge (DOA)

Maeneo lindwa (jer. Residentur) chini ya watawala wenyeji waliopaswa kufuata ushauri wa afisa mkazi Mjerumani (jer. Resident):

Bukoba pamoja na vituo vya kijeshi Usuwi na Kifumbiro, kwa ajili ya watawala wa Wahaya
Rwanda, mji mkuu Kigali, kituo cha kijeshi Mruhengeri
Burundi, mji mkuu Gitega, pamoja na ofisi ndogo Usumbura (Bujumbura).

Tanbihi

hariri
  1. No. 123 Agreement between the British and German Governments, respecting the Sultanate of Zanzibar and the opposite East African Mainland, and their Spheres of Influence - 1st November, 1886 (in: Map of Africa by Treaty Vol II, p. 617 and p. 620) "3. Both powers agree to establish a delimitation of their respectives spheres of influence on this part of the East African Continent" "Line of Demarcation. The line of demarcation starts from the mouth of the River Wanga or Umbe, runs direct to Lake Jipe, passes thence along the eastern and round the northern side of the lake and crosses the Lumi River; After which it passes midway between the territories of Taveita and Chagga, skirts the northern base of the Kilimanjaro range, and thence is drawn direct to the point on the eastern side of Lake Victoria Nyanza which is intersected by the 1st degree of south latitude"
  2. "Great Britain shall bring to bear her full influence on the Sultan of Zanzibar to facilitate an amicable agreement by which the Sultan unconditionally cedes to Germany the Island of Mafia and his territories on the mainland (including dependencies) that are referred to in the existing concessions of the German East Africa Company. It is understood that His Highness shall receive fair compensation for the loss of revenue resulting from this cessation." (Anglo-German Treaty (Heligoland-Zanzibar Treaty), July 1, 1890 online hapa kwa http://germanhistorydocs.ghi-dc.org)
  3. Wakati ule bado kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki, kwa sababu serikali haikumaliza bado kutwaa haki au zaidi madai ya kampuni katika Afrika
  4. Kamusi ya Koloni za Kijerumani, makala "Deutsch-Ostafrika", fungu 9. Bevölkerungsstatistik.
  5. nukuu ya Kiingereza katika Franz Kotrba: William Astor Chanler (1867-1934) und Ludwig von Höhnel (1857-1942) und Afrika, Vienna 2008
  6. Mkataba wa urafiki na biashara kati Dola la Ujerumani na Sultani wa Zanzibar(Kijerumani + Kiingereza)
  7. Nukta hii ilisogezwa kidogo kusudi la kutokata rasi ya Muhuru inayoingia ziwani kwa umbo la pinde
  8. Februari 1887 Sultani aliendelea kupungukiwa maeneo alipopatana na Mwingereza William Mackinnon kumkodisha pwani ya Kenya pamoja na haki za utawala kwa malipo ya kila mwaka. Kisheria kanda hili lilibaki mali ya Zanzibar hadi uhuru wa Kenya mwaka 1964
  9. Makala "Araberaufstand" katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani, Berlin 1920
  10. A. J. Dietz. "A postal history of the First World War in Africa and its aftermath - German colonies: II Kamerun" (PDF). African Studies Centre, Repository, Leiden University. Iliwekwa mnamo 17 Januari 2018.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Marejeo

hariri
  • Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.